The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Samia Ataka Usawa Katika Mashirikiano ya Kiuchumi, Kisiasa ya Kimataifa

Aihakikishia BRICS kuwa Tanzania itaendelea kuwa muungaji mkono wake mkubwa na rafiki wa kweli. 

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezitaka Jumuiya za Kimataifa kuongeza juhudi katika kuondoa mgawanyiko wa kiuchumi uliopo miongoni mwa mataifa ili kuongeza ushirikiano wenye kulenga kufungua fursa katika utekelezaji wa Ajenda ya Afrika ya Mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu duniani.

Hayo ameyaeleza Agosti 24, 2023, wakati wa mjadala uliojumuisha viongozi wa nchi za Afrika, Amerika ya Kusini, Asia na nchi wanachama wa BRICS wakati wa mkutano wa 15 wa nchi wananchama wa BRICS uliofanyika kwa siku tatu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

“Moja ya kipengele muhimu wakati wa mazungumzo haya ni wito wa kuongeza juhudi na kuchukua hatua kamilifu kushughulikia mgawanyiko kati ya kaskazini na kusini,” alisema Rais Samia. “[Hii ni muhimu] ili kuimarisha biashara ya kimkakati ya kifedha, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kwa kuzingatia utaratibu wa kiuchumi wa kimataifa.”

BRICS ni kifupi cha ushirika wa kiuchumi ambao unaundwa na mataifa ya Brazil, Urusi, India, China pamoja na Afrika Kusini. Ushirika huu ulianza mwaka 2009 kwa lengo la kutafuta njia za kuleta mageuzi ya uwakilishi katika taasisi za fedha za kimataifa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

“Ushirikiano kati ya BRICS na Afrika unahitaji kulenga katika kufungua fursa muhimu barani Afrika kuelekea utekelezaji wa Ajenda 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu,” alisema Samia.

Nchi wanachama wa BRICS kwa sasa zina jumla ya pato la taifa la Dola za Kimarekani Trilioni 26 kwa pamoja, sawa na asilimia 26 ya uchumi wa dunia, huku idadi ya watu wakiwa bilioni 3.23 sawa na takribani asilimia 40 ya watu wote duniani.

“Tanzania inatazamia ushirikiano kati ya BRICS na Afrika ambao unaunga mkono juhudi za Afrika katika kukuza na kuimarisha mnyororo wa thamani wa kikanda na ushirikiano ambao unaweza kukuza au kusaidia wazalishaji wa Kiafrika kuweza kupata masoko mapana ya nje,” alisisitiza Samia.

Mwaka 2022 Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 14.2 kutoka nchi za BRICS, huku mauzo katika nchi hizo yakiwa na thamani ya dola za Kimarekani bilioni 7.

Kiongozi huyo mkuu wa Tanzania ametoa wito pia wa kufanyika kwa mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liweze kushughulikia changamoto za kidunia kwa ufanisi kwani hicho ndiyo chombo pekee kinachowakutanisha pamoja mataifa yote duniani.

“Katika mwaka wa 78 wa kuwepo [kwa Umoja wa Mataifa], kinabakia kuwa chombo pekee chenye uanachama wa wote,” alisema.

“Na kwa hivyo, Tanzania katika hatua hii ingependa kusisitiza kwa sauti kubwa haja ya kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kulifanya liwe lenye uwakilishi wa haki, lenye kuakisi hali halisi ya kijiografia na kisiasa,” Rais Samia amesisitiza.

Akifunga hotuba yake, Samia ameyapongeza mataifa wanachama wa BRICS kwa jitihada zao za kuziendeleza nchi zinazoendelea pamoja kwa kuzingatia ajenda yao Afrika ya maendeleo.

Hivyo, ameihakikishia jumuiya ya BRICS kuwa Tanzania itaendelea kuwa muungaji mkono wake mkubwa na rafiki wa kweli katika kufanikisha jitihada zake za kuyaletea mataifa maendeleo.

Katika mkutano huu, mataifa  ya Irani, Saudi Arabia, Misri, Argentina, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu yametangazwa kuwa wanachama wapya wa BRICS kuanzia mwezi Januari 2024.

Biashara kati ya Tanzania na mataifa ya BRICS| The Chanzo

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts