“Fedha si kila kitu” ndiyo kauli inayoweza kuelezea kwa muhtasari kilichoikumba Azam FC katika michuano miwili ya mwanzoni mwa msimu baada ya kushindwa kufanya vizuri katika mechi za Ngao ya Hisani, ambayo kwa mara ya kwanza ilishirikisha timu nne, na kuondolewa mapema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya kufanya usajili wa kishindo msimu uliopita kwa kununua wachezaji nyota kwenye ligi tofauti barani Afrika msimu uliopita, na kuongeza wengine mwanzoni mwa msimu huu, matarajio yalikuwa ni kuimarika zaidi kwa matajiri hao wa Chamazi wilayani Temeke.
Huku mmoja wa wakurugenzi akionekana kwa mara ya kwanza kushiriki kununua wachezaji, Azam ilisajili nyota kama Kipre Junior kutoka Ivory Coast, Abdul Sopu (Tanzania), Tape Edinho (Ivory Coast), Ali Ahamada (Andorra), Malickou Ndoye (Senegal), Issa Ndala (Nigeria), Cleophace Mkandala (Tanzania) na Nathan Chilambo (Tanzania).
Usajili huu ulitarajiwa kufanya makubwa msimu uliopita na pengine kulikuwa na mafanikio kiasi baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya NBC na kufika fainali ya Kombe la Azam.
Kutibu udhaifu
Ni dhahiri kuwa kulionekana udhaifu kidogo ambao ungepata tiba katika kipindi cha usajili. Ndivyo walivyofanya. Azam walimsajili kiungo nyota kutoka Yanga, Feisal Salum. Wakamsajili Cheikh Tidiane Sidibe, Gibril Sila, Alasane Diallo na Bangala, akitokea klabu ya Yanga, ambako habari zinasema aliachwa.
Mbali na usajili huo, Azam ikaachana na baadhi ya wachezaji wake iliowasajili kwa mbwembwe na ambao uwanjani hawakuonyesha thamani ya usajili wao.
Bila shaka kikosi hicho kipya cha Azam kilimfanya kila shabiki wa soka aitabirie makubwa timu hiyo inayomilikiwa na kampuni za Said Salim Bakhresa. Ikaweka kambi ya kujiandaa kwa msimu mpya nchini Tunisia, ambako ilicheza mechi za kirafiki na vigogo, ikiwemo mechi ambayo matajiri hao wa Chamazi walisusia kuendelea na mchezo.
SOMA ZAIDI: Kanuni Mpya TFF Inaua Uchumi wa Wachezaji
Mtihani wao wa kwanza ukawa Ngao ya Hisani, ambako walifeli. Walifungwa 2-0 na Yanga katika mechi ya nusu fainali na baadaye kuishinda Sindida Fountain Gate katika kutafuta mshindi wa tatu.
Haikuwa na tatizo katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya kukutana na timu mpya ya Kitayose kutoka Tabora, ambayo haikuwa imekamilisha usajili na hivyo kulazimika kuingia uwanjani na wachezaji wanane tu huku katika benchi kukiwa hakuna mchezaji hata mmoja.
Mechi ilivunjika kikanuni baada ya wachezaji wawili kuumia na hivyo kubakiwa na wachezaji sita tu kinyume cha sheria. Wakati huo, Kitayose ilishacharazwa mabao 4-0, huku Fei Toto akifunga kilaini mabao matatu.
Katika mechi za raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam imetolewa na Bahir dar Kenema ya Ethiopia baada ya mechi mbili kuisha kwa ushindi wa mabao 2-1 kwa kila mmoja nyumbani kwake.
Azam haikuwa na bahati katika mikwaju ya penati. Licha ya kipa Mghana, Idrissou Abdilai, kuokoa penati mbili, Sospeter Bajana, Idris Mbombo na Djibril Sylla walishindwa kuenzi jitihada za kipa huyo walipopoteza mikwaju yao na hivyo Kenema kushinda kwa mikwaju 4-3.
Matokeo hayo yanamfanya kila mmoja ahoji kuna nini Azam Football Club?
Kama ni usajili, imesajili kila iliyemtaka; kama ni fedha ndiyo klabu tajiri kuliko zote Tanzania na ikiwezekana Afrika Mashariki na Kati.
Kama ni ukaribu wa wamiliki, basi Yusuf Bakhresa ameonyesha hilo kufanya kila liwezekanalo kusajili mchezaji anayetakiwa, akiwemo kipenzi cha mashabiki Fei Toto.
Tatizo ni nini?
Tatizo la kwanza inawezekana kuwa ni kukosa uvumilivu na mipango ya muda mrefu. Hadi inaelekea mwishoni mwa msimu uliopita, Azam ilikuwa na kocha wa muda, Kally Ongara, aliyekaimu nafasi ya mkuu wa benchi la ufundi baada ya kutimuliwa kwa kocha mkuu.
Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Mfaransa Denis Lavagne kutoka Septemba 7 mwaka jana hadi Oktoba 22, miezi miwili tu. Alitimuliwa baada ya Azam kutolewa Kombe la Shirikisho.
SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka
Baada ya Mfaransa huyo kuifikisha JS Kybilie ya Algeria fainali ya Kombe la Shirikisho, ilitegemewa angepewa muda zaidi Azam aipike timu kulingana na viwango vyake, lakini baada ya mwezi tu alitimuliwa.
Kabla ya hapo, Azam ilikuwa inanolewa na kocha Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdi Hamim Moalin, ambaye awali aliajiriwa kama mkurugenzi wa ufundi lakini baada ya kutimuliwa kwa Mzambia George Lwandamina alipandishwa na kupewa mkataba wa miaka miwili.
Aliutumikia mkataba huo kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja alipofikia makubaliano ya kuachia ngazi kwa hiari yake, lakini ikiaminika baada ya timu hiyo kufungwa na Yanga.
Kwa hiyo, katika kipindi kifupi cha kuanzia Januari 2022 hadi Mei mwaka huu, Azam imefundishwa na Lwandamina, Abdihamid Moalin, Daniel Cadena, Lavagne, Ongara na sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Youssouph Dabo ambaye ametokea klabu ya Jaraaf ya Senegal.
Msenegali huyo amekuwa na mafanikio katika klabu na timu za taifa za vijana nchini Cameroon, lakini mwanzo wake mbaya katika klabu ya Azam na utamaduni wa kukosa uvumilivu katika klabu hiyo unaweza kuashiria mwanzo wa safari yake nje ya Chamazi.
Tatizo kubwa
Uvumilivu katika masuala ya kiufundi ndiyo imeonekana tatizo kubwa kwa Azam, kiasi kwamba makocha wanashindwa kupata muda wa kutulia kujenga kikosi ambacho kinaweza kuweka ushindani wa kweli mbele ya vigogo nchini, Simba na Yanga na sasa Singida Fountain Gate.
Viongozi wamekuwa wakiona kasoro katika benchi la ufundi, lakini hawajichunguzi kuona wao wanakosea wapi. Klabu imeshindwa kujenga jeshi la mashabiki ambalo lingekuwa linaweza shinikizo la ziada kwa wachezaji ili wafanye vizuri.
Ukiachana na mashabiki ambao Azam huwakomba wanapocheza dhidi ya Simba au Yanga, klabu hiyo ina kikundi kidogo cha ushangiliaji kisicho na nguvu ya ziada zaidi ya ile ya kuimba na kupiga ngoma wakati wote wa mechi.
SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa
Imeshindwa kutengeneza kizazi kipya cha mashabiki, hasa kutoka eneo lake kubwa la Chamazi na Mbagala, kisicho na chembechembe za Simba na Yanga licha ya klabu hiyo kuwa na muda mrefu kwenye Ligi Kuu.
Hata muundo wa uongozi wake hauonyeshi kuwa ni klabu ya kisasa. Ungetegemea iwe na bodi, ambayo ingekuwa inawawekea viongozi malengo na kuwahoji kila baada ya robo mwaka, lakini kunaonekana kuna kikundi kidogo cha watu ambacho kinafanya kazi chini ya mmoja wa watoto wa mmiliki.
Ushirikishwaji mashabiki
Ungetegemea iwe na idara ya ushirikishwaji mashabiki, ambayo ni muhimu katika klabu za kisasa hivi sasa, lakini idara yake ya mawasiliano na habari inapoteza muda mwingi kuiga staili za wasemaji wa Simba na Yanga badala ya kujikita katika kuhamasisha mashabiki na kuwapamba nyota wake.
Inafikia wakati hadi watendaji wa idara hiyo wanatumia muda mwingi kujaribu kuonyesha mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, si mchezaji mkubwa, wakati kitendo hicho kinasaidia kuwatangaza vigogo hao wa Jangwani.
Kwa nini idara hiyo isingetumia muda mwingi kuonyesha mashabiki kuwa Prince Dube ni nyota anayeendelea kujinoa aonyeshe maajabu zaidi na hivyo kuvuta hisia za mashabiki?
Kwa muhtasari, utaona kwanza Azam haina uvumilivu kwa waajiriwa wa benchi la ufundi. Pili, uongozi kutojitathmini na badala yake kuona makosa upande mwingine.
Pia, kutokuwa na muundo mzuri wa uongozi ambao ungewawajibisha viongozi waajiriwa na kutokuwa na idara inayohusika na ushirikishaji mashabiki ambayo ingesaidia kujenga jeshi ambalo lingelazimisha uwajibikaji kwa wachezaji na hata uongozi.
Fedha pekee haziwezi kuihakikishia Azam mafanikio, bali mipango madhubuti na kusikiliza maoni kutoka nje ya kikundi kidogo cha watu.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.