Malezi huzingatia mambo mengi, lakini ushirikishwaji wa mtoto katika maamuzi ya kifamilia na kijamii kwa ujumla ni jambo la muhimu katika kumjengea mtoto uwezo wa kutatua changamoto katika maisha.
Tukitafakari kweli, ushirikishwaji wa mtoto katika maamuzi, hasa maamuzi yanayohusu maslahi yake, ni suala linalosahaulika na wazazi au walezi wengi.
Mara nyingi tunafikiri kwamba watoto ni viumbe wadogo wasioelewa na wenye kufikiri mambo madogo madogo ya kitoto, kwa hiyo kuwapa fursa hii ni kuwajengea kiburi, kitu ambacho siyo kweli!
Fursa hii haimjengei mtoto kiburi na jeuri bali inajenga uwezo wake wa kufikiri, kudadisi, kuwa mbunifu, na kujieleza. Pia, fursa hii humsaidia mtoto kukuza uelewa wake, kuondoa uoga na kujiamini.
Kumshirikisha mtoto kunapaswa kuanza mtoto akiwa na umri mdogo kabisa kwa kujitahidi kujenga ukaribu naye na kuwa rafiki yake ili kumfanya kuwa huru kukueleza kile anachokifikiria au masuala anayokumbana nayo katika maisha yake ya kila siku.
SOMA ZAIDI: Fahamu Maadili Mema Yanavyojenga Mwenendo Mzuri wa Maisha ya Mtoto
Kama huzungumzi na mwanao kuhusu mambo madogo madogo, vipi huko mbeleni akifikia umri wa kubalehe?
Unaweza kumpatia mtoto wako fursa ya kushiriki katika kufanya maamuzi kwenye mambo yanayohusu maslahi yake na yale yanayohusu jamii kwa kumpa uhuru wa kutoa maoni, mtazamo, na mawazo yake juu ya jambo husika.
Hata Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 hapa Tanzania, inatambua umuhimu wa uhuru wa mtoto kusikilizwa, ikisema: “Mtoto atakuwa na haki ya kutoa maoni na mtu yeyote hatamnyima mtoto mwenye uwezo wa kutoa maoni haki hiyo ya kusikilizwa na kushiriki katika maamuzi yatakayohusu maisha yake.”
Tunaishi katika jamii inayoadhibu udadisi. Mwanafunzi akimkosoa mwalimu dasarani kwa kuuliza maswali-dodosa inachukuliwa kama utovu wa nidhamu.
Hii itokea hata katika familia kwa mfano mtoto wako anaweza kukuuliza swali na badala ya kumjibu, unamwambia asikusumbue. Hapo unakua unamnyima fursa ya kudadisi na ubunifu na kumjengea uoga wa kuuliza maswali kwa mtu yeyote hadi darasani.
SOMA ZAIDI: Tujadili Kuhusu Upakiaji Picha za Watoto Mitandaoni
Tafiti mbalimbali ulimwenguni zinaonyesha kuwa watoto wanaonyimwa fursa hii huwa hawafurahii kwenda shule, hawajibu wala kuuliza maswali darasani kwa kuogopa watakosea, nakadhalika.
Tabia hizi za uoga zinaweza kuwafuata hadi vyuo vikuu, kamwe hawakai mstari wa mbele na wanajificha nyuma ya migongo ya watu wengine. Hawawezi hata siku moja kuwasilisha mada mbele ya darasa.
Je, kwa kuwanyima haki ya kushirikishwa na kutoa maoni yao, tunajenga viongozi wa aina gani?
Faida za kumshirikisha mtoto kwa kifupi zipo katika makundi mapana mawili. Kundi la kwanza ni faida wanazopata watoto na faida wanazopata wazazi zikiwa katika kundi la pili.
Kuwapa watoto fursa hizi kunasaidia kukuza na kuendeleza ujuzi wao wa mawasiliano, kujenga hoja zenye nguvu na kumudu vyema mawasiliano kwa lugha husika.
Watoto wa aina hii hujiamini na kuamini uwezo wao katika kutatua changamoto mbalimbali. Watoto hawa si rahisi kutendewa vitendo vya kikatili kwani mara nyingi watashitaki punde tu wapatapo nafasi ya kufanya hivyo.
SOMA ZAIDI: Tuongee Kuhusu Matumizi ya Simu, TV na Mitandao kwa Watoto
Kuwasiliana mara kwa mara husaidia kujenga mahusiano ya kirafiki na kuaminiana kati yako mzazi na mtoto wako, uhusiano ambao ni muhimu mno katika malezi. Mara nyingi tumeona wazazi wakilalamika gharama za malezi na mahitaji ya watoto.
Kama huko karibu na mtoto wako, hajui una kipato kikubwa kiasi gani, hivyo usimlaumu akiomba huduma za gharama usiyoimudu, mshirikishe.
Watalaamu pia wanasisitiza kwamba mtoto hupata fursa ya kujifunza taaluma na biashara za familia au jamii akishirikishwa katika miradi ya familia. Mfano hai ni Watanzania wenye asili ya Asia wanaowafunda watoto wao biashara na taaluma za familia. Mafanikio yao tunayaona, tunayajua!
Faida wanazopata wazazi pia ziko nyingi, ikiwemo kujua nini vipaumbele vya watoto wako kimahitaji. Pia, ushirikishwaji wa mtoto utakusaidia kujenga tabia ya kusema na kutoa ahadi za kweli na za kiuhalisia.
Wazazi bila ya kujua huumiza hisia za watoto kwa hutoa ahadi za kuwanunulia vitu ama kuwapeleka sehemu za michezo bila kuzifanikisha. Mara nyingi hudhani watoto wanasahau na hivyo hupotezea, jua kwamba watoto hawasahau kirahisi hivyo.
SOMA ZAIDI: Je, Wazazi Tunajua Watoto Wetu Wanashinda, Kucheza Wapi?
Mwisho, inatupasa tutambue kuwa watoto wetu wanaweza kutushangaza katika kutatua changamoto zetu, hasa kama tumewashirikisha. Watafiti wanasema watoto wadogo wanazo bongo zinazofikiri kwa ubora na haraka pengine kuliko watu wazima.
Bongo zao zinaweza kuona njia palipo na changamoto. Amini kwamba watoto wetu wanao uwezo mkubwa wa kufikiri na kuamua juu ya namna ya malezi na mambo mengine yanayoendelea kwenye familia.
Tuwaongoze na tuwatumie, ni wabunifu. Kila mzazi ana mikakati na malengo juu ya maisha ya baadaye ya mtoto wake. Hivyo, tusikilize mawazo ya watoto wetu kwa makini, tathmini faida na hasara zake ili tuweze kuwpatia miongozo na ushauri kwa lengo la kumsaidia kufanya maamuzi sahihi.
Tukumbuke kumpatia mtoto wako uhuru wa kushiriki katika kutoa mawazo yao ni muhimu mno, kwa sababu itamjengea uwezo atakaouhitaji katika kupambana na kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa kwa kujiamini na kuthubutu!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.