Summary
Live Reporting
- 5:31 pm
- December 4, 2023
Mtwara: Watu 6 Wafariki Kwa Radi Wakiwa Kwenye Sherehe, Mmoja Ajinyonga Ofisi ya CWT

Mtwara. Watu 6 wamefariki na wengine watano wamejeruhiwa baada ya kupigwa na radi wakiwa kwenye sherehe ya kumpongeza kijana wao kuhitimu elimu ya kidato cha nne.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo inaeleza kuwa tukio hilo limetokea Disemba 3, 2023 majira ya saa 12 jioni katika kijiji cha Maparagwe kata ya Chikukwe wilayani Masasi.
Aidha taarifa nyingine inaeleza kuwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Angelus Mwinyuku mwenye umri wa miaka 49, Mratibu wa Elimu Kata ya Matawale na mkazi wa Jida wilaya ya Masasi amejinyonga mpaka kufa siku ya Disemba 3, 2023, majira ya saa 12 jioni.
Mwinyuku anadaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila ambayo aliifunga kwenye dirisha la bafu la Ofisi ya Chama cha Walimu (CWT) wilaya iliyopo mtaa wa Wapi Wapi.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema linaendela kufanya uchunguzi kujua chanzo cha tukio hilo kwa kuwa mpaka sasa bado hakijulikana
- 5:00 pm
- December 4, 2023
Hanang Vifo Vimefika 57, Serikali Yaahidi Kugharamia Mazishi, Matibabu na Misaada

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza Serikali kugharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha na majeruhi kutokana na mafuriko na kutiririka kwa udongo kwenye makazi ya watu wilayani Hanang, mkoa wa Manyara.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu hadi sasa vifo vilivyoripotiwa ni 57 na majeruhi 85 wamefikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Maafa haya yameathiri mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na pia vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi.
Idadi ya kaya zilizoathirika ni takribani 1,150 zenye watu takribani 5,600 na mashamba yenye ukubwa wa ekari 750 yameharibiwa.
Rais Samia pia ameagiza Serikali kuhakikisha wananchi walioharibiwa makazi yao kuwa wanasitiriwa mahali pazuri katika kipindi hiki.
Bado mamlaka za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na shughuli za uokoaji.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia kurasa za The Chanzo
- 2:26 pm
- December 4, 2023
Daraja Lakwamisha Usafiri Musoma, Walazimika Kusubiri Zaidi ya Saa Tisa

Mara. Wasafiri wanaopita barabara ya Musoma-Majita wilaya ya Musoma vijijini wamekwama kwa takribani saa 9 kutokana na maji kujaa kwenye mto Suguti.
Kujaa kwa mto huo kumetokana na mvua zinazoendelea kunyesha mikoa ya Manyara na Arusha ambayo humwaga maji katika mito Mara na Suguti.
Hii siyo mara ya kwanza kwa watumiaji wa barabara hii kukwama kutokana na mto Suguti kujaa pindi mvua zinapokuwa nyingi katika mikoa ya Manyara kupelekea kukatika kwa mawasiliano katika barabara hii.
Wananchi waliokwama katika eneo hilo wanaomba mamlaka inayohusika na barabara ya Musoma-Majita kuangalia sehemu ya daraja la Suguti kwa kuwa ni korofi Ili waweze kupunguza kero Kwa wananchi.
Hali imekuwa ikisababisha nauli kupanda na kutumia gharama kubwa kutafuta njia mbadala.
- 7:22 pm
- December 1, 2023
Kesi ya Mauaji Inayowakabili Askari Saba Mtwara, Mahakama Yaagiza Vielelezo Vya Mabaki ya Mwili Kutunzwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu

Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara imeagiza vielelezo vya mabaki ya mwili wa Mussa Hamis anayedaiwa kuuliwa na Polisi saba kuendelea kutunzwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Uamuzi huo umekuja kufuatia ombi la wakili wa upande wa mashitaka Maternus Marandu aliyeomba Mahakama kutoa maagizo maalum juu ya namna ya kutunza vielelezo namba sita, saba na nane vya kesi hiyo ambavyo ni mabaki ya mwili yanayodhaniwa kuwa ya Mussa Hamis.
Mabaki hayo ni mifupa nane ya mbavu, mifupa miwili inayodaiwa kuwa ni ya mguu wa kulia pamoja na suruali iliyookotwa kwenye eneo walilokuta mabaki.
Wakili Marandu ameiambia Mahakama kuwa mabaki hayo bado yanaweza kuendelea kutumika katika ushahidi wa kesi hiyo licha ya Hawa Bakari ambaye ni mama mzazi wa marehemu Mussa Hamis kuiomba Mahakama mabaki hayo kwa ajili ya mazishi kama yamethibitishwa kuwa ni ya mwanaye.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa vinasaba kutoka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyosalishwa Mahakamani hapo na shahidi namba tisa inaonyesha kuwa uwezekano wa vinasaba hivyo kuwa na uhusiano na sampuli ya mate iliyochukuliwa kwa Hawa Bakari ni asilimia 99.9.
Kufuatia uamuzi huu, kesi hii ambayo imesikilizwa mfululizo kwa siku 14 kuanzia Novemba 13, 2023 hadi Disemba 1, 2023, imehairishwa mpaka itakapopangiwa kikao kingine.
Hadi sasa tayari mashahidi 10 kati ya 72 upande wa mashitaka wameshawasilisha ushahidi wao mbele ya Jaji Ediwini Kakolaki.
- 6:20 pm
- November 30, 2023
Miaka 20 ya ZAFELA Yatajwa Kuwa Ni Ukombozi Kwa Jamii Visiwani Zanzibar

Zanzibar. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwepo kwa wanasheria wanawake Zanzibar ni msaada tosha wa upatikanaji wa haki kwa jamii inayokabiliwa na changamoto mbalimbali.
Ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la siku 3 la maadhimisho ya miaka 20 ya Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA).
“Kuwasaidia wanawake na watoto kwenye kupata haki bila ya malipo ni suala ambalo linahitaji kujitoa kwa moyo na huku mkiwa hamtarajii malipo” amesema Hemed.
Katika kipindi kifupi cha Julai hadi Septemba Jumuiya hiyo imepokea mashauri 395 yanayohusu talaka, matunzo na madai ya mali kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria.
ZAFELA ilianzishwa mwaka 2003 kwa lengo la kuwasaidia wanawake kupata haki na kutoa msaada wa kisheria visiwani hapa.
- 1:14 pm
- November 30, 2023
TAKUKURU Dodoma Yabaini Wazabuni Kulipwa Fedha Nje ya Mikataba

Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Dodoma imebaini kuwepo kwa mapungufu katika miradi ya maendeleo 28 iliyofanyiwa ufuatiliaji ikiwemo wazabuni kulipwa fedha nyingi nje ya mikataba na kulipwa fedha kabla ya kuwasilisha vifaa.
Haya yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Dodoma, John Joseph wakati akitoa taarifa ya utendaji katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2023.
“Mapungufu haya yamepelea kufunguliwa kwa majadala ya uchunguzi kwa baadhi ya miradi” amesema Joseph “Aidha, elimu na ushauri umetolewa kwa baadhi ya miradi.”
Mapungufu mengine ya miradi hii ambayo ina thamani ya zaidi ya bilioni 5 ni pamoja na uezekaji wa majengo kwa kutumia mabati yaliyochini ya kiwango, wazabuni kulipwa fedha na kuwasilisha vifaa pungufu, fedha za zuio kukatwa kwa wakandarasi na kutowasilisha katika mamlaka husika