Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla amesema kuwa hadi zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM linakamilika siku ya jana Julai 2, 2025 wanachama 5,475 walichukua fomu za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Akizungumza leo makao makuu ndogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam amesema kuwa kwa nafasi ya wabunge wa majimbo 272 ya uchaguzi nchini, watia 3,585 wamechukua upande wa bara na 524 wamechukua upande wa Zanzibar. Kati ya watia nia hao 4,109 walioenda majimboni wanawake ni 263. Uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu ni 503.
Kwa upande wa viti maalum ubunge kwenye jumuiya za chama 623 wamechukua kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Tanzania Bara ikiwemo 91 wa makundi maalum, huku kwa upande wa Zanzibar wamechukua 8 na viti maalum Baraza la Wawakilishi ni 9.
Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara ni 55 huku Zanzibar ni watatu na wanne wamejitokeza katika viti maalum uwakilishi, hivyo kufanya jumla ni 62.
Wanachama 161 wamejitokeza katika kinyang’anyiro cha ubunge wa viti maalum kupitia Umoja wa Vijana wa CCM, ambapo kati yao 154 ni kwa upande wa Tanzania Bara na saba upande wa Zanzibar.
Makalla amesema kwa upande wa ngazi ya udiwani ambapo takribani kuna kata 3,960 bado hawajafanya majumuisho japo wanatarajia kuwa na watia nia takribani 15,000 nchi nzima katika nafasi hiyo, inayojumuisha madiwani na madiwani wa viti maalum.
“Uchukuaji wa fomu safari hii umevunja rekodi, na hamasa ni kubwa,” amesema Makalla, “tumefurahishwa na hamasa kubwa ya makada wetu”
Gharama za uchukuaji fomu kwa ngazi ya ubunge ilikuwa shilingi 500,000 huku kwa nafasi ya udiwani ikiwa ni shilingi 50,000. Hivyo kwa takwimu hizi kwa ngazi ya ubunge, CCM imeingiza shilingi bilioni 2.7 kutokana na ada za fomu.
SOMA ZAIDI: Mchakato Uchukuaji Fomu CCM Washika Kasi: Vijana CCM Wajitosa Majimbo ya Mawaziri
Makalla amesema kuwa baada ya zoezi hili kukamilika vikao vya mchujo ngazi ya kata vitaanza siku ya Ijumaa, Julai 4, 2025 ambapo kamati za siasa ngazi ya kata zinatoa mapendekezo ya waliotia nia ngazi ya udiwani na udiwani wa viti maalum.
Vikao hivyo vitafuatia na kamati za siasa za wilaya na baadaye kamati za siasa za mkoa ambazo zitafanya uteuzi wa majina matatu ya madiwani watakaopigiwa kura na wajumbe. Kamati hizo za mkoa zitafanya utezi Julai 9, 2025.
Ameeleza kuwa kamati za mkoa zitafanya majukumu mawili ya uteuzi wa majina matatu ya madiwani, pamoja na kutoa mapendekezo ya majina ya wabunge kwa kamati kuu ya CCM itakayofanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wabunge na wawakilishi watakaoenda kupigiwa kura na wajumbe.
Makalla amewataka wanachama na wafuasi wa chama hiko kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mchujo, na kutoa wito wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutaka zoezi la mchujo katika ngazi zote litendeke kwa haki bila ya fitina na majungu.
“Vikao vya uchujaji vitende haki, visionee watu na haki ionekane ikitendeka,”amesisitiza Makalla.