The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Kuwa Wenye Furaha?

Wataalamu wa malezi wanaamini kuwa, watoto wanaolelewa katika mazingira ya upendo wanakua na furaha na msingi imara wa kujiamini na mafanikio katika maisha.

subscribe to our newsletter!

Kuwalea na kuwakuza watoto wenye furaha ni mchakato unaohitaji upendo, uvumilivu, na maarifa. Wataalamu wa malezi wanaamini kuwa, watoto wanaolelewa katika mazingira ya upendo wanakua na furaha na msingi imara wa kujiamini na mafanikio katika maisha.

Lakini kama wazazi na walezi, tunawezaje kuwalea watoto wenye furaha? Kwanza kabisa tuepuke migogoro au makabiliano ya maneno na watoto wetu. Badala yake, tuwe na mazungumzo yanayowakuza kiroho na kihisia. 

Tuwaulize maswali na kuwapa nafasi ya kujielezea hata pale wakikosea na tuwape nafasi ya wao kutuuliza maswali na tuwape majibu.

Watoto hupenda kuwa na udhibiti fulani juu ya maisha yao. Hivyo, tunashauriwa kuwapa fursa za kuchagua vitu ambavyo vinawahusu, kama vile mavazi ya kuvaa, shughuli za kufanya, masomo ya kusoma, na kadhalika, huku tukiwapatia ushauri na muongozo juu ya tamaduni na tunu za jamii na familia zetu. 

Kufanya hivi kutawapa mwanya na uwezo wa kutumia akili zao, hali itakayohimiza ujuzi wa kujitegemea katika maisha yao ya sasa na baadaye. Muda tunaokuwa na watoto wetu pia ni muhimu mno katika furaha yao. Tujitahidi kupanga ratiba zitakazo husu kufanya mambo ya kufurahia pamoja kama familia. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Uwezo Thabiti Mabinti Zetu?

Tunaweza kutenga muda tukiwa nyumbani na watoto; kucheza nao, kusoma au kuwahadithia hadithi, kula pamoja, kufanya matembezi, au hata kutoka nje ya nyumba kutembelea sehemu mbalimbali kama mbuga za wanyama, kumbi za michezo, migahawa ya chakula, kuonesha ushirikiano wetu katika vipindi vya televisheni na michezo wanayoipenda, na kadhalika. 

Hii husaidia kujenga uhusiano wa familia na kujenga kumbukumbu nzuri za maisha na kumpa mzazi, au mlezi, kujua vipaumbele vya mtoto na maudhui anayopendelea ili kumshauri zaidi.

Kusifia

Jambo lingine ambalo linawajengea watoto furaha ni kusifia bidii, mafanikio na juhudi zao. Mara nyingi wazazi tunapenda kuangalia matukio ya watoto wetu bila kujali juhudi walizoziweka katika jambo hilo. 

Mtoto anaweza kufaulu masomo sita kati ya kumi, lakini tutaangalia masomo yale manne ambayo hakufanya vizuri kuliko yale sita. Hii siyo sawa, na tujitahidi kutambua juhudi za watoto na kuwasaidia kufikia viwango vya juu zaidi vya mafanikio na ari ya kujituma.

Watoto wanahitaji upendo na msaada kutoka kwa wazazi wao. Tuwaoneshe kwa maneno na vitendo kwa kuwakumbatia, kuwabusu na kuwaambia maneno ya kuwatia moyo mara kwa mara ili waendelee kuwa na uthubuti na juhudi katika nyanja mbalimbali za maisha yao.

SOMA ZAIDI: Dondoo Muhimu za Kuzingatia Katika Safari ya Malezi

Wataalamu wa makuzi ya watoto wanaamini kuwa lishe bora na mazoezi hujenga furaha kwa watoto na hata watu wazima. Ni kweli kwamba watoto wanahitaji lishe bora ili waweze kukua vizuri na kuwa na afya, lishe hii huhusisha mlo kamili wenye virutubisho vyote muhimu kama vile protini, vitamini, na madini muhimu. 

Pia, watoto wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga miili yenye nguvu. Tunaweza kushiriki nao katika michezo na shughuli mbalimbali za kuchangamsha mwili kama sehemu ya ratiba ya mida wetu nao.

Hisia na matamanio

Ni muhimu kuelewa hisia na matamanio ya watoto wetu na kuwasaidia kukabiliana nazo. Hii ni kwa sababu watoto wanahitaji kujifunza jinsi ya kudhibiti hisia zao na matamanio yao. 

Kama wazazi, au walezi, tunapaswa kuwaonesha watoto jinsi ya kudhibiti hisia kama hasira, majonzi, hofu na matamanio kama kupenda mtu, starehe, vitu vya thamani na aina fulani ya maisha, na kadhalika, kwa njia ya utulivu na ya majadiliano. 

Tujifunze jinsi ya kuwatia moyo na kuwapa msaada wa kihisia wanapokabiliana na changamoto mbalimbali na kuwasaidia kutambua hali halisi ya maisha.

SOMA ZAIDI: Fahamu Sehemu Watoto Wanaweza Kutoa Taarifa Kuhusu Vitendo vya Ukatili

Katika ngazi ya familia, furaha inakuwepo pale tunapoweka mipaka na sheria wazi kwa watoto wetu, ili wafahamu vitu gani wanapswa kufanya na vitu ambavyo hawapaswi kufanya pamoja na matarajio yetu kwao na yao kwetu. 

Mipaka hii inasaidia katika kujenga nidhamu na kuwafanya watoto wajue majukumu yao na majukumu ya wazazi wao kwao.

Kwa upande wa adhabu, tujitahidi kutokutumia adhabu kali katika kuwaadabisha watoto kwani adhabu kali huondoa furaha kwenye maisha ya watoto na hupunguza upendo baina ya mtoto na mzazi, au mlezi. 

Tutumie njia zinazojenga na kufundisha matokeo ya makosa yao, kama vile kupunguza muda wao wa kucheza au kuwapa kazi za nyumbani. Hii inasaidia watoto kujifunza kutokana na makosa yao bila kuumizwa au kudhalilika.

Juu ya yote, watoto wanajifunza kutoka kwetu. Kama tunataka kulea na kukuza watoto wenye furaha, sisi wenyewe tunapaswa kuwa watu wenye furaha. 

SOMA ZAIDI: Mzazi, Hakuna Ushahidi Kwamba Viboko Vinasaidia Katika Malezi ya Mtoto Wako

Changamoto za maisha haziepukiki, ila namna tunavyozikabili na kuzidhibiti ndiyo inatoa taswira halisi ya hali zetu za maisha. Tukiwa watu wenye hasira, hofu na manung’uniko kila mara basi watoto wetu watakua hivyo pia.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *