The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ubashiri Hatma ya Samatta Stars Haukutakiwa Kuwepo

Kutotoa maelezo kumuhusu nyota na kipenzi cha mashabiki ni kufungua mlango wa ubashiri usiotakiwa na usio na umuhimu wowote.

subscribe to our newsletter!

Kumeibuka ubashiri tofauti baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, kutotangazwa katika orodha ya wachezaji wa timu ya taifa walioingia kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Ethiopia kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Baadhi walimtaka kocha wa Taifa Stars, Hemed Morocco, kutomuacha mchezaji huyo, wakisema bado ni muhimu kwa taifa, wengine wakidhani kuwa ameachwa pengine kwa sababu kiwango chake kinashuka kutokana na umri.

Na baadhi walisema kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Aston Villa ya England alikataa kujumuishwa kwenye kikosi hicho kitakachoicheza mechi mbili. Ni haki yao mashabiki kuwa na hisia tofauti kuhusu mshambuliaji huyo ambaye aliandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England.

Kwa nini? Kwa sababu taarifa ya Shirikisho la Soka (TFF) halikuwa na maelezo yoyote kuhusu kutojumuishwa kwa Samatta kwenye kikosi hicho, akiwa ndiye nahodha wa taifa.

Kwa kuona mjadala umekuwa mkubwa, TFF ililazimika kutoa maelezo kuwa Samatta aliomba asijumuishwe kwenye kikosi hicho kwa sababu binafsi na si kwamba aliachwa kutokana na utashi wa kocha mkuu wa Stars.

Ni maelezo sahihi kabisa yaliyotolewa wakati ambao si sahihi.

Kwa mchezaji kama huyo ambaye amekuwa muhimili wa timu na nahodha, si busara kutangaza kikosi cha Stars bila ya kuwaambia wananchi sababu za kutokuwepo kwake. Kutotoa maelezo kumuhusu nyota na kipenzi cha mashabiki ni kufungua mlango wa ubashiri usiotakiwa na usio na umuhimu wowote.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Iondoe Hisia Hasi za Udhamini

Na hii ni kwa sababu ya kutangaza kikosi hicho kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari badala ya jopo la ufundi likiongozwa na kocha kutangaza lenyewe mbele ya waandishi wa habari na kujibu maswali yanayohusu timu hiyo ili kuondoa sintofahamu na kuonyesha kuwajibika kwa mashabiki na taifa kwa ujumla.

Pamoja na kuonyesha kuwajibika kwa umma, pia ni fursa ya kuwapa thamani wadhamini wa timu ya taifa ambao huwa wanataka wahusishwe na kila taarifa inayohusu timu wanayoidhamini ili wanufaike na habari hiyo.

Kawaida

Imekuwa ni kawaida kwa makocha katika siku za karibu kutangaza timu kwa mtindo huo, hata pale inapotangazwa timu ambayo inakwenda fainali za Mataifa ya Afrika na hivyo kuwepo na maswali mengi kuhusu wachezaji walioitwa na walioachwa.

Ingawa makocha wengi huwa hawapendelei kuzungumzia wachezaji ambao hawajawateua kwa kuwa ni wengi kulinganisha na wateule wachache, ni muhimu sana kuzungumzia wachezaji wachache muhimu, hasa nahodha kama Samatta na wale walioitumikia timu kwa muda mrefu na kwa mafanikio.

Hii ni kuonyesha kuwajali, kuthamini mchango wao na kutoa fundisho kwa wengine waone kuwa kuichezea Stars kwa muda mrefu na kwa mafanikio kuna kitu cha thamani unaweza kupata, hasa heshima kama hiyo ya kuzungumziwa unapokuwa haumo au unapoelekea mwishoni mwa uwezo wake na hivyo kuagwa kwa heshima.

SOMA ZAIDI: Olimpiki Itupe Mtazamo Mpya Kwenye Michezo

Ni muhimu kujenga utamaduni huu ili kuipa thamani timu yetu na kujenga imani kwa wachezaji ambao wanaitwa kubeba bendera ya taifa lao. Kama thamani hiyo hawaioni, kuitwa au kutoitwa hakutakuwa na thamani yoyote kwao na hivyo kulipigania taifa lao kwa nguvu zote kunakuwa kwa kiwango cha kawaida.

Kuheshimisha wachezaji

Pengine Mohamed Chuma, ambaye alikuwa beki wa timu ya taifa, angekuwa bado yuko, angekuwa kila mara akihadithia jinsi chama cha soka cha wakati huo, FAT, kilivyomuheshimu alipoamua kustaafu soka.

Chuma aliagwa kwa heshima zote katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru, na mwishoni mwa mchezo alichukua bendera ya taifa na kukimbia nayo kuzunguka uwanja kuwaaga mashabiki.

Hakupewa mamilioni ya fedha kuonyesha kuthamini mchango wake, bali heshima ya kuagwa rasmi mbele ya mashabiki aliowatumikia kwa muda mrefu ilimtosha kujua kuwa FAT iliona thamani katika kile alichokuwa akikifanya.

Ni kwa jinsi hiyo, TFF haina budi kuweka kanuni ya kulazimisha makocha wa timu ya taifa kuwa na utaratibu wa kuwajibika kwa mashabiki na wananchi kwa ujumla katika mambo ambayo ni makubwa na si kuyarusha kwa wananchi kwa taarifa za maandishi kwa kisingizio kwamba teknolojia ya sasa inaruhusu. 

SOMA ZAIDI: Kulihitaji Utafiti Ligi Kuu Kutumia Uwanja wa Amaan

Teknolojia hiyohiyo ndiyo inayoruhusu pia kocha kutangaza timu kwa njia ya mtandao na kuwa tayari kujibu maswali wakati huohuo.

Pia, TFF haina budi sasa kuandaa tuzo tofauti kwa wachezaji waliotumikia Stars kwa muda mrefu. Yaani, wachezaji waliotumikia kwa miaka kumi na kuendelea wawe wanatambuliwa kwa tuzo fulani ambayo watapewa wakati wanastaafu na waliotumikia kwa miaka mitano na kuendelea wawe na tuzo yao.

Hivi ndivyo vitu vinaweka thamani kwenye makabati yao au kwenye kuta za sebule zao kuonyesha kuheshimiwa kwa mchango wao kwa taifa. Ndiyo maana huwa kuna tuzo kama ya dhahabu, shaba na fedha kuonyesha mafanikio tofauti ya wanamichezo.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *