The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bodi ya Ligi Iondoe Hisia Hasi za Udhamini

Hatuwezi kuinamisha vichwa na kusubiri neema ya Mungu itujie tujikute tuna kanuni nzuri za kudhibiti matumizi ya fedha na uwezekano wa kuwepo michezo michafu katika mpira wa miguu.

subscribe to our newsletter!

Kumekuwepo na mjadala kuhusu udhamini wa kampuni moja ya biashara kwa klabu zaidi ya moja kwenye Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara. Mjadala huo umejaa hofu kuwa udhamini huo unaweza kusababisha klabu moja kunufaika na matokeo ya uwanjani na hakuna kanuni inayozuia suala hilo.

Wanaohoji wanasema mbona suala hilo haliko katika nchi nyingine, hasa zile tunazoziangalia sana za barani Ulaya ambako mchezo wa mpira wa miguu umeendelea kwa kiwango kikubwa na klabu zinanufaika na udhamini wa kampuni kubwa na za kimataifa za kibiashara?

Ni kweli kwamba hatuna kanuni zozote zinazoongoza na kudhibiti masuala ya udhamini kwa klabu za soka na ndiyo maana kampuni kubwa za kibiashara zimekuwa zikielekeza fedha zake pale zinapoona panaweza kusaidia kutangaza bidhaa zao.

Awali kulikuwa na udhamini ambao haukuwa kamilifu. Kampuni iliyoona inaweza kununua jezi za klabu, ndiyo hiyo iliyopewa nafasi kifuani kuweka jina la bidhaa yake au nembo. Na kwa utamaduni huo, kampuni hizo ziliweza kuingia ndani zaidi ya klabu kwa kuwa wamiliki walikuwa na mapenzi na klabu hizo.

Iko mifano kama ya Bobby Soap iliyoivalisha Yanga jina la sabuni zake, Mohamed Enterprises Limited iliyotumia nembo ya MeTL katika jezi za Simba, klabu ya Bilicanas iliyoivalisha Yanga jezi zenye jina hilo na nyingine chache.

Wakati huo jezi zilikuwa ni bidhaa adimu na wale wafadhaili waliitisha hata mikutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kukabidhi msaada wa jezi.

Kubadili sura

Lakini ujio wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ulianza kubadili sura ya udhamini. TBL, kwa kutumia bia yake ya Safari Lager, iliamua kudhamini Ligi Kuu ya Bara, huku ikiweka fedha nzuri kwa washiriki. Hali ikabadilika zaidi pale kampuni ya Vodacom ilipoingia na kudhamini ligi yote na sasa ni NBC.

SOMA ZAIDI: Olimpiki Itupe Mtazamo Mpya Kwenye Michezo

Hapo ndipo kampuni kama Serengeti Breweries ziliingia kwa nguvu kwa kuidhamini timu ya taifa, huku TBL ikirudi kwa mlango mwingine ilipoamua kuzidhamini klabu kubwa za Yanga na Simba kwa kutumia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager. Baadaye SportsPesa ikazichukua timu hizo.

Hapo kampuni nyingine kama Bin Slum, Puma Energy, Mofaya, GF Trucl and Equipment, GSM na M-Bet zikaingia kwa nguvu kudhamini klabu za Ligi Kuu.

Wakati Kilimanjaro Premieum Lager walipokuwa wadhamini wa Simba na Yanga, hakukuwepo na gumzo la uwezekano wa upendeleo kwa moja ya klabu hizo. Hali kadhalika SportsPesa walipokuwa wakizidhamini klabu hizo mbili. 

Na malalamiko pia hayakuwepo wakati Bin Slum inazidhamini Coastal Union na Mbeya City, wala wakati MeTL inazidhamini Simba na Namungo, na wala mjadala huu haujaelekezwa kwa udhamini wa sasa wa Azam TV Max kwa Namungo FC na Azam FC.

GSM 

Mjadala mkubwa upo katika udhamini wa jezi wa kampuni ya GSM na kampuni nyingine zilizo chini ya mwamvuli huo kwa klabu tofauti za Ligi Kuu, huku mkurugenzi wa miradi wa kampuni hiyo, Hersi Said, pia akiwa ni rais wa Yanga.

GSM ndiye mdhamini jezi wa Yanga na wa pili kwa ukubwa baada ya SportsPesa, lakini kampuni hiyo yenye biashara tofauti za bidhaa na huduma, inaonekana zaidi kwa kuwa mmiliki wake, Gharib Said Mohamed, pia ni mfadhili wa vigogo hao wa Kariakoo, mfanyakazi wake, Hersi ndio rais.

SOMA ZAIDI: Kulihitaji Utafiti Ligi Kuu Kutumia Uwanja wa Amaan

GSM pia ndiyo mdhamini wa jezi wa Pamba, Namungo, Coastal Union, Mashujaa, Singida Fountain Gate na Singida Black Stars, hali inayowatia hofu wajenga hoja kuwa udhamini huo unaweza kutumiwa kama fimbo ya ushawishi kuiwezesha Yanga kupata matokeo mazuri uwanjani, matokeo ambayo imekuwa ikiyapata hata kwa timu ambazo hazina udhamini wa GSM.

Inawezekana kabisa kwamba hakuna uhusiano wowote wa matokeo ya uwanjani na udhamini wa klabu zaidi ya moja, na inawezekana kabisa kwamba hakuna mbinu zozote za kutumia udhamini kurubuni matokeo, lakini kwa sababu kuna kilio hicho, Bodi ya Ligi Kuu haitakiwi ikalie kimya suala hilo bila ya kuchukua hatua.

Viongozi wa bodi wanatakiwa kulichukulia suala hilo kwa urefu na mapana yake na kulifanyia kazi kwa kadri inavyostahili na si kwa fikra na hisia zilizotawala mijadala na ambazo hazitaki kabisa kuhusisha udhamini kama huo uliofanywa na kampuni nyingine kama MeTL, Bin Slum na Azam TV Max.

Nimejaribu kuperuzi kanuni zinazodhibiti udhamini kwenye ligi za nchi nyingine, nikaona ni China pekee ambako suala hilo liko wazi. Nchini China, klabu mbili tofauti haziruhusiwi kuwa na mdhamini mmoja kuhofia maslahi binafsi kuchukua mkondo wake.

Mambo yalivyo ulaya

Lakini ni kitu ambacho hakifikiriki barani Ulaya. Pamoja na kwamba kampuni kubwa ni nyingi zinazoweza kutoa hadi Pauni milioni 67 katika udhamini, bado hawajazibana taasisi hizo kiudhamini, ndio maana bidhaa kama Cardbury zinaonekana katika orodha ya wadhamini wa klabu tofauti.

Pia, suala la udhamini wa jezi kwa Waingereza na nchi nyingine duniani, si tatizo. Umbro inadhamini klabu tano, Adidas (nne), Nike (nne), Castore (3) na nyingine kama Errea, Hummel, Puma na Macron zina timu mojamoja.

SOMA ZAIDI: Hongera TFF kwa Tuzo, Lakini Bado Maboresho Yanahitajika

Udhamini kama huu ndio ambao GSM anaufanya kwa klabu nyingine, ukiondoa zile zilizopata udhamini mkuu kutoka moja ya kampuni tanzu za GSM. Lakini Waingereza hawajakaa kimya tu. Mwaka huu waliboresha kanuni yao inayoitwa “Associated Party Transaction” ambayo itaanza kutumika msimu ujao.

Katika kanuni hiyo, fedha zinazotolewa na mdhamini au associated party, zitatakiwa ziendane na thamani halisi ya sokoni. Yaani, si kusema zinazotolewa Pauni milioni 20 kwa ajili ya kununua wachezaji watatu, wakati thamani ya kila mmoja ni Pauni milioni tatu.

Kwa hiyo, inapovunjwa kanuni hiyo ofisi ya mratibu imepewa mamlaka ya kutoa adhabu. Hii imewekwa kwa ajili ya kuwepo na ushindani sawa. Yawezekana mchezaji akawa ananununliwa kutoka klabu nyingine ambayo mmoja wa wamiliki wake pia anahusishwa na mmiliki wa klabu husika na hivyo kuweka bei chini ya thamani ya soko wakati akitakiwa nje ya wigo huo anakuwa bei juu.

Kwa hiyo, wenzetu wameamua kuweka kanuni hiyo ya APT kudhibiti malipo ambayo yanaweza kuwa yanalenga kuweka ushawishi wa kupanga matokeo. Kwa kanuni hiyo kuwepo katika ile ya Financial Fair Play, kunazidisha udhibiti wa miamala kutoka kwa wadhamini au wamiliki na hivyo fedha inayotumika katika mpira wa miguu inakuwa ni ile inayotokana na shughuli za mchezo huo pekee.

Hiyo kwa kwa Ligi Kuu ya England. Pamoja na kwamba hatujafikia kiwango hicho cha maendeleo, hatuwezi kuinamisha vichwa na kusubiri neema ya Mungu itujie tujikute tuna kanuni nzuri za kudhibiti matumizi ya fedha na uwezekano wa kuwepo michezo michafu katika mpira wa miguu.

Kama ambavyo mashabiki, pamoja na kutokuwa na hoja za msingi, wanaona kuna uwezekano wa mpira kuchezwa nje ya uwanja, ndivyo ambavyo TPBL inatakiwa kuanza kuwaza nje ya uwanja jinsi ya kuwa na kanuni ambazo zitapunguza mijadala isiyokuwa na umuhimu wowote, lakini pia kuzuia uwezekano wa upuuzi huo kuwepo.

SOMA ZAIDI: Kutumia Takwimu Pekee Tuzo za TFF ni Usumbufu

Na hilo haliwezi kufanyika kwa kwenda kuchukua kitabu kizima cha Financial Fair Play na kukidurufisha na kusema hizi ni kanuni zetu kama tulivyofanya kwenye Leseni za Klabu. Ni lazima tuchambue vipengele vinavyolingana na hali halisi ilivyo hapa Tanzania. Vinaweza kuwa vichache lakini vikasaidia sana kurejesha Imani kwa mashabiki.

Watu wa sheria, fedha, teknolojia ya mawasiliano, wakaguzi na wataalamu wa benki wanaweza kuwa msaada mkubwa katika kutengeneza kanuni hizo zitakazowezesha TPLB kuwa na uwezo wa kuratibu masuala ya kifedha ya klabu, kitu ambacho ni muhimu kwa sasa kuliko vingine vyote.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *