The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali za Majimbo na Ajenda ya Utaifa

Kilicho cha muhimu ni kuhakikisha kuwa wananchi kupitia vyombo vyao vya kidemokrasia wanakuwa na mamlaka ya kujiamulia na kujisimamia katika shughuli zao za kujiletea maendeleo.

subscribe to our newsletter!

Wakati hekaheka za Uchaguzi Mkuu zikiendelea kushika kasi, hivi karibuni kumejitokeza malumbano juu ya sera ya uundaji wa serikali za majimbo. Malumbano hayo yameibuka hususani baina ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hii ni baada ya mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA Tundu Lissu kuinadi sera ya muda mrefu ya CHADEMA ya uundaji wa Serikali za Majimbo. Sera hiyo ipo katika ilani ya CHADEMA. Lissu alizungumzia sera hiyo kwa mara ya kwanza wakati akihutubia wananchi mjini Mpanda, Mkoani Katavi.

Katika mkutano huo wa kampeni Lissu alieleza azma ya chama chake kutaka kuunda serikali za majimbo endapo watapewa ridhaa na Wananchi Oktoba 28. Mtizamo wa Lissu katika hotuba hiyo na nyingine zilizofuata ni kwamba serikali za majimbo zenye mamlaka juu ya mambo kadhaa yanayohusu ustawi wa wananchi ndio njia pekee itakayowawezesha wananchi wa maeneo husika kujiletea maendeleo kutokana na jitihada zao wenyewe.

Kwa mujibu wa Lissu, mfumo huo utawawezesha wananchi kuwawajibisha viongozi wao waliowachagua kuwaongoza katika ngazi mbalimbali kama vile majimbo, mikoa, wilaya na halmashauri kwa kuwa mamlaka yao hao viongozi yatatokana na wananchi kwa kuchaguliwa na sio kuteuliwa. Hivyo, utaratibu huo utapunguza uhodhi wa mamlaka ya wananchi ambao kwa sasa yapo chini ya Serikali Kuu (au Rais).

Hata hivyo, hoja hizo za Lissu zilianza kujibiwa punde tu ndani ya masaa 24 na Katibu Mkuu wa CCM ndugu Bashiru kwa kusema: “Wale wote waliofilisika kisiasa wanapanga kuikata kata Tanzania vipande vipande viitwavyo majimbo na kila jimbo liwe na mtawala anaitwa Gavana. Gavana ni neno la kikoloni, washindwe na walegee.” Kudhihirisha kuwa CCM haikubaliani kabisa na hoja ya mfumo wa serikali za majimbo mgombea wa kiti cha urais kupitia CCM naye, ambaye ndio Rais aliyepo madarakani Raisi John Magufuli akihutubia moja ya mikutano yake ya kampeni mkoani Tabora alisema: “Kuna chama kina sera yake hiyo ya kuigawanya Tanzania katika majimbo ya utawala. Ukishatengeneza majimbo katika nchi huo ndio mwanzo wa mfarakano. Kwa sababu kila jimbo litajitegemea lenyewe kama lilikuwa maskini litakuwa maskini la kutupwa.”

Wapo wachambuzi wengine wa siasa ambao wamejitanabaisha na CCM kama vile Thomas Kibwana wamepinga mfumo wa Serikali za Majimbo. Hoja ya kibwana aliyoitoa wakati wa mazungumzo kati yangu na yeye ni kwamba mfumo unaopendekezwa na CHADEMA hauwezekani Tanzania. Sababu kubwa, kwa mujibu wa mchambuzi huyu, ni kwamba Tanzania, tofauti na Nigeria, Agrika Kusini na Ethiopia, kwa mfano,  haina utambulisho mkubwa wa kikabila (strong tribal identity) katika maeneo mbalimbali ya nchi. Kwa mtazamo wa mchambuzi huyu, serikali za majimbo zitachochea kuibuka na kukuza utambulisho wa kikabila na utengano katika taifa la Tanzania. Mbali na kwamba mfumo huo utaongeza mzigo wa kodi kwa wananchi bali pia unaweza kuleta mkanganyiko zaidi kwa kuwa tayari Tanzania ni Jamhuri ya Muungano ambayo ndani yake kuna serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Ukiangalia hoja kubwa inayotolewa na upande wa CCM kupinga mfumo wa serikali za majimbo ni kwamba mfumo huu utapelekea ubaguzi na utengano baina ya watu wa maeneo tofauti tofauti ya nchi. Kwamba serikali za majimbo zitaondoa utaifa wetu. Hii hofu inatokana na nini? Je, gharama pekee ya kuhifadhi hali ya kujiona wamoja kama taifa ni kurundika mamlaka ya wananchi sehemu moja (Serikali Kuu)? Na je, jitihada yoyote ya dola kugatua madaraka yake itahatarisha utaifa wetu?

Mfumo wa kiutawala uliopo hivi sasa katika nchi yetu umekuwa ni ule uliolimbikiza madaraka kwa Serikali Kuu ambayo inaongozwa na rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa mujibu wa Katiba. Katika historia ya nchi yetu yamewahi fanyika majaribio kadhaa kwa lengo la kurudisha madaraka kwa wananchi ili kuwawezesha kujipangia na kujiamulia wenyewe mustakabli wa maendeleo yao. Sera kama ‘Madaraka Mikoani’ ya miaka 1970s ilikuwa na lengo hilo japo matokeo yake ikawa ni jambo tu la uhawirishaji wa madaraka toka kwa warasimu wa Serikali Kuu kwenda kwa warasimu wa serikali katika ngazi za mikoa na wilaya, na sio wanachi wenyewe.

Serikali hii hii inayongozwa na CCM mwaka 1998 ilitoa Andiko la Kisera ambalo ndilo linatumika kama mwongozo wa utekelezaji wa Sera ya Ugatuzi wa madaraka nchini kwa lengo la kuboresha mfumo wa Serikali za Mitaa ambazo zipo kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1977. Muongozo huo una miaka 22 sasa, je, muongozo huo umewezaje kufanikisha azma ya Serikali Kuu kurudisha mamlaka ya wananchi kupitia Mamlaka za Serikali za mitaa (MSM)? Uzoefu wa hivi karibuni unaonesha kuwa serikali za mitaa zimeendelea kupunguziwa madaraka na hivyo kubaki kama vyombo vya utoaji/upitishaji huduma (service delivery) za Serikali Kuu na sio kama ilivyokusudiwa kuwa kitovu cha wananchi katika kujipangia na kusimamia shughuli zao za kimaendeleo. Pamoja na ukweli huo bado suala la ugatuzi limeendelea kuelezwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020 kama njia ya kuimarisha na kuzipa nguvu Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Sera ya mfumo wa serikali za majimbo inayonadiwa na CHADEMA licha ya kwamba imeshawahi kuwepo katika Ilani za CHADEMA huko nyuma, ilipewa nguvu na muongozo ya Kisera wa Chama hicho uliozinduliwa Septemba 25, 2018 na kujulikana kama ‘Sera Mbadala.’ Sura ya Pili, ukurasa wa 12 wa sera hiyo inazungumzia ugatuzi wa madaraka kwa mfumo wa majimbo. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ya mwaka 2020 pia, Sura 3 kipengele cha 1 kinazungumzia ugatuzi wa madaraka. Maana ya ugatuzi inayoelezwa na ilani hiyo ni: “Mfumo wa serikali ambao mamlaka ya dola inatokana na wananchi, kupitia serikali za shirikisho zilizochaguliwa, huku masuala ya jumla ya kitaifa yakibaki chini ya Serikali Kuu.” Ilani hiyo inaendelea kufafanua namna ambayo ugatuzi huo wa madaraka ambao utahakikisha tawala za majimbo, mikoa, wilaya na serikali za mitaa kwa ujumla zinapaswa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na serikali kuu.

Lakini jambo moja linaloibuka kwenye mjadala huu wa serikali za majimbo na faida na hasara zake ni kwamba suala la ugatuzi wa madaraka kwa namna yoyote ile, iwe kwa njia ya uundaji wa serikali za majimbo au kupitia tawala za mikoa na serikali za mitaa, huwezi tu kusema mojawapo ni mbaya au nzuri. Ikumbukwe kuwa kitendo chenyewe cha ugatuzi sio lengo. Lengo haswa ni kuhakikisha kuwa wananchi kupitia vyombo vyao vya kidemokrasia wanakuwa na mamlaka ya kujiamulia, kujipangia na kujisimamia katika shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo bila kuathiri hali yao ya umoja.

 

Hivyo basi ugatuzi wa madaraka unaweza kuleta tija iliyokusudiwa kwa umma endapo tu madaraka yaliyohodhiwa na Serikali Kuu yatahaulishwa kwa wananchi. Kama wananchi katika Mikutano yao ya kijiji/mtaa, mabaraza yao ya ngazi za wilaya , vyama vya wafanyakazi vilivyoundwa na wao wenyewe, ushirika na jumuiya za kijamii za wananchi  wenyewe wataweza kujiamulia mambo yao wenyewe.

Joel Ntile ni mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia barua pepe yake ya mwankina1993@gmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @NtileJoel. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na hayawakilishi msimamo wa The Chanzo Initiative.

 

 

 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *