The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uchaguzi Mkuu 2020: Je, Watanzania Watapiga Kura?

Jumla ya wapiga kura milioni 29.19 wamejiandikisha kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu 2020. Je, watajitokeza kufanya hivyo ifikapo Octoba 28?

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mwamko wa Watanzania wanaopiga kura umeonekana kupungua katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, huku taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zikionesha kwamba tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 chini ya asilimia 70 ya wananchi wanaojiandikisha kupiga kura ndio hutimiza takwa hilo la kidemokrasia.

Kwa maneno mengine, hii inaonesha kwamba zaidi ya watu watatu katika kila watu kumi hawakupiga kura katika Chaguzi Kuu za miaka 2005, 2010 na 2015. Hali hii ni tofauti na ilivyokua miaka ya 1985 mpaka 2000.

Katika matokeo ya hivi karibuni, taarifa ya NEC inaonesha watu wawili kati ya watatu waliojiandikisha mwaka 2015 walipiga kura. Hii ina maana kuwa asilimia 67 ya Watanzania waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu walipiga kura.

Hili ni ongezeko kidogo ukilinganisha na asilimia 43 pekee ya waliopiga kura mwaka 2010. Tathmini inaoneshwa kwamba mwaka huo pia ndio uliokuwa na uwiano wa watu wachache zaidi waliojitokeza kupiga kura kati ya waliojiandikisha katika historia ya Uchaguzi Mkuu nchini. Kwa mujibu wa NEC, hakujawahi kutokea mwaka mwingine wa Uchaguzi Mkuu ambao zaidi ya nusu ya waliojiandikisha hawakupiga kura.

Mwaka 2000 ndio uliweka historia kwa watu wengi kupiga kura ikiwa ni asilimia 84. Hii inamaana kuwa watu 21 kati ya 25 waliojiandisha walipiga kura. Katika miaka ya 1985 mpaka 1995 zaidi ya asilimia 70 ya watanzania walipiga kura.

Kwanini watu hawapigi kura?

Kuna sababu mbali mbali zinazowafanya watu wasipige kura. Kwa mfano, kwa Thomas Mpinga, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, zoezi hilo halina maana yoyote isipokuwa kupoteza muda tu. Anasema: “Ni kupoteza muda kwa sababu kuna viashiria vingi vinavyoonyesha uchaguzi hautokuwa wa huru na haki.”

Hii ni hoja ambayo inaungwa mkono na Dk Muhidin Shangwe kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye ameiambia The Chanzo hivi karibuni kwamba wananchi wamekosa imani na tume ya uchaguzi na wanaamini kuwa hakuna uwanja sawa wa kisiasa kwa vyama vyote katika mchakato wa upigaji wa kura. Dk Shangwe anasema:

Sababu kubwa ni kukosa imani na mchakato wa uchaguzi, watu wanakua hawana imani, hawavutiwi (they are not excited) na mchakato kutokana na mambo mengi kuna ile kama hata tukipiga kura mtu anaona kama kura yake haiwezi kuleta mabadiliko.”

Akizungumzia uchaguzi uliopita, Dk Shangwe ameeleza kuwa mwaka 2015 muamko ulikuwa mkubwa kwasababu ya umaarufu wa mgombea wa upinzani wa wakati huo ndio ulisababisha watu wengi wakajitokeza kupiga kura.

Wadau wengine walitaja sababu kama wagombea kutokua na hoja zinazowagusa wananchi pamoja na watu wengi kukosa imani na mchakato wa uchaguzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, kwa mfano, anasema uamuzi wa watu kupiga kura ama kutokupiga unatokana na uzito wa hoja wanazotoa wagombea. Wakati wa mahojiano ya simu na The Chanzo, Profesa Mpangala alisema: “Kama hoja haziwashawishi watu hawawezi kupiga kura. Sera za wagombea ndio zinaamua watu wapige kura ama wasipige, unakuta watu wanaona sera hawajazipenda ndio wanaghairi kupiga kura.”

Waliojiandikisha kupiga kura 2020

NEC inasema kwamba baada ya mazoezi mawili ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura kukamilika, kwa sasa daftari hilo lina wapiga kura milioni 29.19. Mazoezi haya yalifanyika katika vipindi tofauti ikiwemo mwanzoni mwa mwaka huu, 2020.

Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 20 ukilinganisha na walioandikishwa mwaka 2015 ambao ni wapigakura milioni 23.25.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa makadirio ya wapigakura uliofanywa na The Chanzo, mkoa wa Dar es Salaam uliokuwa na wapigakura wengi mwaka 2015 (asilimia 11.9 ya wapiga kura wote) unakadiriwa kuwa na wapigakura milioni 3.48 mwaka 2020 ukilinganisha na wapigakura milioni 2.78 mwaka 2019.

Mkoa wa Mwanza unaokadiriwa kuwa na wapiga kura milioni 1.82 ukifuatiwa na Mbeya wenye wapiga kura milioni 1.75.

Mikoa mingine tisa inakadiriwa kuwa na wapiga kura zaidi ya milioni moja. Hii inafanya kuwa na mikoa 13 itakayokuwa na wapigakuza zaidi ya milioni moja ikiwa ni ongezeko la mikoa minne ukilinganisha na mikoa tisa pekee mwaka 2015.

Mikoa miwili pekee inatarajiwa kuwa na wapigakura chini ya laki tano (Katavi wapigakura 404,333 na Njombe 481,200).

Mikoa mingine mitatu inatarajiwa kuwa na wapigakura chini ya laki saba wakati visiwani Zanzibar kutakuwa na wapiga kura 692,085 ukilinganisha na 551,375 mwaka 2015).

NBS na idadi ya wapigakura

Miongoni mwa sifa za mtu kupiga kura ni kufikisha umri wa miaka 18 au zaidi. Hii inamaanisha idadi ya wapigakura walioainishwa na NEC ni Watanzania wenye miaka 18 au zaidi ambapo wapo milioni 29.19.

Licha ya hivyo taarifa ya Makadirio ya Idadi ya watu (2013 – 2035) iliyotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) 2018 inakadiria uwepo wa watanzania milioni 57.64 mwaka 2020.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo idadi ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi ni milioni 28.86.

Hii inamaanisha makadirio ya Watanzania wenye uwezo wa kupiga kura ni milioni 28.86 ikiwa ni wachache kidogo ukilinganisha na takwimu za NEC.

Hata hivyo, jambo la muhimu kufahamu ni kuwa haya ni makadirio ya watu na sio idadi kamili.

Je, watu  watakwenda kupiga kura? 

“Siwezi kusema moja kwa moja itakuwaje lakini kuingia kwa [Tundu] Lissu katika mchakato kumeleta mabadilikio na kuna uwezekano wa kuongezeka kwa wapigaji kura ukuilinganisha na kama Lissu asingekuwepo” alisema Dk Shangwe.

Lissu ni mgombea wa uraisi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na viongozi waandamizi wa chama kingine cha upinzani cha ACT-Wazalendo, akiwemo mgombea wa uraisi wa Zanzibar kupitia tiketi ya chama hicho Seif Sharif Hamad.

Kwa upande wake, Profesa Mpangala anasema kuwa ili angalau watu wapige kura kuna haja ya wagombea kuimaridha hoja zao ziwe ni zenye kuwagusa wananchi

“Wagombea wahakikishe sera zao ziaingizie katikia matatizo ya wananchi, ili washawishike kupiga kura na kumchagua kiongozi atakayetatua matatizo yao,” alisema Mpangala.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

 1. Nimeyasoma makala haya, hakika ni kazi nzuri sana Sana Sana imefanyika. Mizani iko sawa na takwimu zimekaa vizuri. Uzuri zaidi ni hoja inayojengwa ni kwanini watu hawapigi kura; wakati fulani nimewahi kuwasikia baadhi ya watu mkoani Dar es salaam wakidai zoezi la kupiga kura linawapotezea muda wa kujali mihangaiko yao ya kujipatia pato. Inawezekana hawapo sahihi lakini namna gani tutalishawishi kundi hilo kupiga kura? Hapo ndipo penye mtihani sababu sio kwamba hawaelewi umuhimu wa ushawishi wa hoja lakini wanaelekea kupuuza. Ndio maana hata uandishikishaji wanaojitokeza wanataka kadi/vitambulisho tu kwa matumizi mengine.
  Ni changamoto yetu kutoa elimu ya uraia.

  Kongole waandaaji wa tovuti hii.

  Markus Mpangala
  Safarini Nyanda za Juu Kusini
  Oktoba 19/2020.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *