The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ilikuwa Ni Lazima CHADEMA Ipoteze, Suala Lilikua Ni Nini Wanapoteza

Kati ya kujikanganya katika misimamo na kupoteza baadhi ya wanachama wake shupavu, CHADEMA imechagua la pili kujitanzua na hali iliyotishia kukipasua chama hicho cha upinzani

subscribe to our newsletter!

Usiku wa Ijumaa ya Novemba 27, 2020, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe alitangaza kuwavua vyeo vyao pamoja na kuwafukuza uanachama wabunge 19 wa chama hicho walioamua kwenda kuapishwa Novemba 24, kinyume na maagizo, makubaliano, na baraka kutoka vyombo vikuu vya maamuzi vya chama, kama vile Kamati Kuu.

Waliokumbwa na fagio hilo la chuma ni pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Halima Mdee,  Esther Bulaya na Esther Matiko. Katibu Mkuu wa BAVICHA, Nusrat Hanje. Katibu Mkuu Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) Grace Tendega. Makamu Mwenyekiti BAWACHA, Hawa Mwaifunga. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu BAWACHA, Jesca Kishoa  na Katibu Mwenezi BAWACHA Agnesta Lambat. Wengine ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mtwara, Tunza Malapo. Wengine ni Ceciia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao. Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Itakumbukwa kwamba mapema mwezi huu wa Novemba CHADEMA, kikishirikiana na chama cha ACT-Wazalendo, kilitangaza kutoyatambua matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28, 2020, uliokipa Chama cha Mapinduzi (CCM) ushindi, wakidai mchakato mzima uligubikwa na kasoro lukuki kama vile uwepo wa kura feki, pamoja na vitendo vya kukamatwa na kuzuiliwa mawakala na wanachama wao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hata hivyo, imekanusha madai yote haya.

CHADEMA na Ubunge wa Viti Maalumu

Ingawa CHADEMA ilipata kiti kimoja tu cha ubunge, chama hicho kilikuwa na nafasi 19 za Ubunge wa Viti Maalum, kikiwa ni chama pekee cha upinzani kilichobahatika kuwa na nafasi hizo baada ya kukidhi matakwa ya kikatiba ya kupata asilimia tano ya kura zote za ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu. Lakini kwa kuzingatia hatua iliyoichukua awali, ya kutotambua matokeo ya uchaguzi na mamlaka za nchi zilizoundwa kutokana na uchaguzi huo, CHADEMA ilionekana kutokuwa tayari Kupeleka majina ya wanachama wake NEC kwa ajili ya kuteuliwa kuwa Wabunge wa Viti Maalumu.

Lakini wakati CHADEMA ikiendelea kutafakari suala hili, na mjadala ukiendelea nchi nzima juu ya kwamba je, chama hicho cha upinzani kipeleke majina NEC kwa ajili ya uteuzi au isipeleke, huku faida na hasara za kila uamuzi zikijadiliwa, ghafla baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho, wengi wao wakiwa ni viongozi wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) walionekana mjini Dodoma wakienda kuapishwa kama Wabunge halali wa Viti Maalumu wa Bunge la 12 kutoka CHADEMA.

Tetesi kwamba wanachama hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa BAWACHA Halima Mdee, watakwenda kula kiapo kuwa Wabunge wa Viti Maalumu zilishasambaa katika mitandao ya kijamii siku moja kabla ya wanachama hao kuapishwa. Baadhi ya wanachama hao wazikana taarifa hizo, wakisema si za kweli na za uzushi. Lakini licha ya ukanushaji wao, wanachama hao walifanya kile kile ambacho tetesi zilidai. Wakila kiapo mbele ya Spika wa Bunge Job Ndugai, wanachama hao walisisitiza kuwa taratibu zote za kisheria zilifuatwa na kuwa walipewa baraka zote na chama. “Tunakishukuru chama chetu Chadema kikiongozwa na [Mwenyekiti] Freeman Mbowe kwani kupitia wao, tumepata nafasi hii ya kukiwakilisha chama chetu,” alisema Mdee katika hotuba yake punde baada ya kula kiapo.

CHADEMA yawakana waapishwaji

Lakini siku moja baada ya wanachama hao kuapishwa, uongozi wa juu wa CHADEMA, kupitia msemaji wake mkuu, Katibu Mkuu John Mnyika, ulikanusha kuhusika na kitendo hicho, ukisema kwamba CHADEMA bado haijapeleka majina ya yoyote ya wanachama wake NEC kwa ajili ya uteuzi na kusema kilichofanywa na wanachama wake 19 ni usaliti na hujuma kwa chama wakishirikiana na vyombo vya dola. Mnyika alisema: “NEC ijitokeze hadharani, ieleze hiyo orodha iliwasilishwa na nani, nani aliyesaini eneo la Katibu Mkuu ikiwa mimi sikufanya hivyo [wala] naibu wangu.” Kufuatia hatua hiyo, CHADEMA iliitisha kikao maalumu cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam Novemba 27 na kuwaita wanachama wake 19 kuja kujibu tuhuma za kwenda kinyume na msimamo na taratibu za chama kwa kwenda kula kiapo cha kuwa Wabunge bila ya idhini ya chama.

Hii ilikuwa ni Novemba 25, na ndani ya siku mbili kabla ya kikao cha Kamati Kuu viongozi waandamizi kutoka Serikalini, wakiwemo Mwanasheria Mkuu Profesa Adelardus Kilangi na Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC Dk Wilson Mahera Charles, wakisema wabunge hao 19 kutoka CHADEMA wametueliwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria na kikatibu, huku Profesa Kilangi akiwaonya viongozi wa CHADEMA kuchukua uamuzi wowote dhidi ya wabunge hao, akisema kufanya hivyo itakuwa ni kuvunja sheria na Serikali haitasita kuchukua hatua. Profesa Kilangi aliliambia gazeti la CCM Uhuru kwamba: “Katiba haijawekwa kufurahisha utashi wa mtu au matakwa ya mtu na kwa kuwa inaelekeza haki hizo za msingi, hatutokuwa tayari kuona mtu au chama fulani kinaweza maslahi yake mbele kuwazuia wabunge hawa, watambue kufanya hivyo ni kuvunja katiba.”

Ijumaa ya Novemba 27, siku ambayo Kamati Kuu ya CHADEMA ilikuwa inakaa, Dk Charles wa NEC alisema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba orodha ya majina ya wanachama 19 wa CHADEMA walioteuliwa na NEC kama Wabunge wa Viti Maalum ilipelekwa NEC na Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika Novemba 19, 2020. Dk Charles alisema: “Tume ilitumia orodha iliyowasilishwa na CHADEMA kuteua Wabunge wa Viti [Maalumu]. Hivyo, Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu wa CHADEMA waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria na kikatiba.” Hata hivyo, kauli hiyo ya Dk Charles ilikinzana na hile aliyotoa Novemba 20, 2020, jijini Dodoma wakati wa kikao na wadau wa uchaguzi kutathmini namna zoezi zima la uchaguzi lilivyokwenda ambapo alisema mpaka kufikia muda huo, Novemba 20, CHADEMA bado ilikuwa haijapeleka orodha ya wanachama wake kwa ajili ya uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalumu. Hii imefanya wadadisi wengi kutilia shaka maelezo ya Dk Charles.

Washukiwa wasusia kikao

Lakini licha ya kupewa wito wa kufika katika Kamati Kuu ya chama kujibu tuhuma mbali mbali zilizokuwa zinawakabili, hakuna mtuhumiwa hata mmoja kati ya 19 waliofika kwenye kikao hicho jana, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Freeman Mbowe. Kwa mujibu wa Mbowe, wanachama hao waliandikiwa barua wakitakiwa kuja kutoa maelezo juu ya kile kilichotokea lakini waligoma kufanya hivyo huku wakitoa sababu mbali mbali ikiwemo kwamba muda uliokuwepo ulikuwa mchache sana kuwawezesha kujiandaa kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwao, wakiomba wapatiwe muda zaidi kufanya hivyo. Mbowe alidai kwamba barua zote zilionekana kuandikwa na mtu mmoja: “Kama chama, CHADEMA tumekwazwa na dada zetu ambao wengine walikuwa wagombea wetu [wa] ubunge. Wameacha wanachama na wapiga kura zaidi ya 450 wakiwa gerezani wao wanakwenda kuapa.” Mbowe alisema CHADEMA kinapitia wakati mgumu kwa sasa na kisingemvumilia yoyote anayetaka kukihujumu kutokea ndani. Mbali na kuwavua nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama, CHADEMA pia iliwavua wanachama hao uanachama  na kuwataka wasijihusishe na kitu chochote kinachohusu chama. Mbowe alisema kwamba kama kutakuwa na yoyote ambaye hakuridhika na uamuzi huo anaweza kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama.

Kupoteza ilikuwa lazima, ila nini upoteze?

Matukio ya wiki za hivi karibuni yanaonesha kwamba CHADEMA kilikuwa katika mtanziko mkubwa ambao bila shaka ulikiweka chama hicho katika njia panda. Kama CHADEMA wangewaacha wanachama wake 19 bila ya kuwachukulia hatua yoyote wasingekuwa tu wameruhusu watu kujiamulia wanavyotaka ndani ya chama kila wanapoona inawafaa lakini pia ingewaondolea uhalali wa kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28. Kwa mantiki hii malalamiko yao yote ya mwanzo kuhusu uchaguzi yasingekuwa na mashiko,na ingeweza kupelekea CHADEMA kupoteza kuaminika mbele ya wanachama na wasiokuwa wanachama, hasa kwa kuonekana kukosa msimamo. Pia namna sakata zima lilivyotokea ikiwemo sintofahamu kati ya mamlaka mbalimbali na CHADEMA zinaacha maswali kwamba kama CHADEMA  wangekubali hali iliyokuwepo iendelee, je uaminifu wa wanachama wake 19 ungekuwa kwa nani, kwa chama au mamlaka? Kwa upande wa pili, CHADEMA kuamua kuwavua vyeo na kuwafukuza uanachama wanachama hao ilikuwa inakwenda kupoteza watu waliokipigania chama kwa hali na mali, na wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa Watanzania walio wengi. Mwisho wa siku, inaonekana kama vile hakukua na namna yoyote ile CHADEMA ingezuia kupoteza. Hii ndiyo sababu baadhi ya wachambuzi wanadhani suala la msingi ni namna chama hicho kimeamua kupoteza kwa kuangalia uamuzi upi ungepunguza hasara ambayo kama chama wangepata.

Kwa mujibu wa Katiba, Mbunge anapovuliwa uanachama ndani ya kilichokuwa chama chake au kuacha uanachama wa chama alichopatia ubunge basi  na ubunge hukoma. Hata hivyo, kuna ushahidi kwamba hali haiwi hivyo mara zote. Kwa mfano, wakati wa Bunge la Kumi na Moja ambapo baadhi ya wabunge wa upinzani, kama vile Cecil Mwambe, waliweza kuendelea na Ubunge hata baada kukoma kwa uanachama wao ndani ya vyama vyao. Kutokana na kuwa Wabunge hawa 19 ndio kwanza wameanza ngwe yao ya uongozi, inategemewa wanaweza kwenda mahakamani katika kupinga kufukuzwa uanachama.

Mpaka wakati wa kuandika makala haya hakuna yoyote kati ya wanachama hao wa zamani wa CHADEMA waliotoa maoni yao kuhusiana na kile kilichotokea usiku huo wa Ijumaa Novemba 27, 2020. Ni moja kati ya vitu vinavyosubiriwa kwa hamu kubwa sana kwa sasa na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini Tanzania. Je, watakubaliana na uamuzi wa CHADEMA wa kuwafukuza uanachama au wataupinga uamuzi huo? Na nini hatma yao kama Wabunge wa Viti Maalumu katika mazingira ambayo chama walichodai kuwapendekeza kwa nyadhifa hiyo kimewakana na kuwatosa?

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Spika anajaribu kukigawa chama cha CHADEMA
    Katiba inasemaje? Ni nani anayependekeza wabunge hao kama si chama chao? Hiyo barua ya chama ilikuwa halali au ya kugushi? Hili ndio suali la msingi. Acha chama kiteuwe wabunge wake wa viti maalum

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *