Ninafurahia sana mijadala kuhusu elimu kwenye mitandao ya kijamii, ingawa, kwa bahati mbaya, sioni kwamba mijadala hiyo inashirikisha wenye maamuzi juu ya elimu yetu, au labda wanaona kwamba tunabwata tu. Sisi ni akina nani kuhoji? Lakini wengine tumekuwa na bahati ya kushiriki katika elimu kwa miaka karibu hamsini. Sikatai kwamba mawazo yetu yanaweza kuwa batili au hayafai lakini ingefaa angalau tuoneshwe tumefyatuka wapi na kwa vipi.
Nimeamua kuandika makala hii kwa sababu nina wasiwasi kwamba katika kukataa mapengo ya mitaala ya sasa kuna hatari ya kuingia kwenye mapengo upande wa pili, tena mapengo yaleyale.
Hebu nijaribu kufafanua. Kwa jinsi masomo yaliyo mengi yanavyofundishwa katika shule za sekondari siku hizi, sina budi kukubaliana na wakosoaji kwamba masomo kama historia, na fasihi katika Kiswahili na Kiingereza hayana maana. Hayapanui uelewa wala kuchokoza tafakuri.
Hapo ni dhahiri kwamba suala la lugha ya kufundishia linachangia sana. Kama huelewi lugha, utawezaje kutafakari kwa kina? Huwezi kutambua mawazo yanayokinzana, kuchambua kwa nini yanakinzana, kuelewa mitazamo ya watu na makundi mbalimbali na kwa nini na kujaribu kupima wazo lipi linaelekea zaidi kwa faida ya mustakabali wao na wa jamii yetu.
Mitaala inayofinya badala ya kuzichokoza fikra
Lakini suala la lugha si tatizo peke yake. Sasa tuna mitaala ambayo hufinya fikra badala ya kuzichokoza. Linalotakiwa ni kujua ‘jibu sahihi’ ili kuweza kulitapikia kwenye mtihani. Katika hali hii, ni kweli historia, fasihi na masomo mengine yenye malengo ya kufikirisha, ya kupanua mawazo, ya kuleta mijadala ili kuelewa zaidi, masomo kama haya hayana maana tena. Mtu anaelimika vipi kwa kukariri vitu badala ya kujadili masuala?
Shida yangu ni kwamba walioona hivi wameona kwamba tatizo ni somo lenyewe si jinsi linavyofundishwa. Hivyo, wako tayari kufuta masomo kama haya ili kuleta masomo ya ufundi na mengine ya kuwaandaa watoto wetu kwa kuwapatia stadi za kazi ili waweze kuajiriwa au kujiajiri baadaye. Ninakubali kwamba masuala ya stadi za kazi ni muhimu sana pia lakini naamini wanataka kutupa jongoo na mti wake. Bila kuwa na masomo ya kuchokoza fikra na ubunifu, hata stadi za kazi hazitafanikiwa. Pia nchi yetu haitaweza kuendelea.
Naomba niongelee uzoefu wangu kidogo. Nilikuwa na bahati sana ya kuanza kufundisha Shule ya Sekondari ya Milambo mwaka 1973. Wakati huo, Tanzania ilikuwa imejitoa kwenye baraza la mitihani la Afrika ya Mashariki na kutengeneza mitaala na mitihani ya Kitanzania. Maana yake ilikuwa kwamba historia ilifundishwa kwa mtazamo wa kiafrika badala na wa kizungu. Wanafunzi walifundishwa siasa na katika masomo yangu ya Kiingereza na fasihi katika Kiingereza kulikuwa na mabadiliko makubwa. Hata katika kufundisha lugha, wanafunzi walitakiwa kusoma vitabu vya fasihi angalau 12 juu ya dhamira mbalimbali, kama vile Mila na Familia, Kupinga (naam KUPINGA, wanafunzi walifundishwa kupinga maovu mahali popote), kujifahamu, migogoro na kujenga maisha ya baadaye.
Wanafunzi walitakiwa kusoma nguli wote wa fasihi katika Kiingereza enzi zile, kama vile Chinua Achebe, Wole Soyinka, Ngũgĩ wa Thiong’o, Okot p’Bitek, Camara Laye, na wengineo wengi. Aidha, walitakiwa kufanya kazi maalum katika vikundi. Hizi kazi maalum ziliwalazimisha wanafunzi kushirikiana kufanya utafiti, kutafakari na kutumia ubunifu kutengeneza kazi za kwao. Hivyo kazi zao maalum ziliwafundisha wanafunzi kushirikiana, kufikia lengo kwa pamoja, badala ya kushindana tu. Na kazi maalum zilikuwa sehemu ya maksi za mtihani wa taifa pamoja na kazi zingine za darasani. Bila shaka walikariri pia lakini mitaala na mfumo wa tathmini uliwalazimisha kufanya zaidi ya hivyo.
Lakini kiboko chake kilikuwa mitaala ya Kidato cha Sita ya Kiingereza. Kulikuwa hakuna mambo ya sarufi. Badala yake walitakiwa kusoma angalau vitabu 12 tena, juu ya dhamira ya Mapambano ya Waliokandamizwa, Mkengeuko (Alienation) na Kujenga Mustakabali. Upande wa vitabu kulikuwa na mchanganyiko maalum wa nguli wa Afrika pamoja na wa kila mahali duniani, kuanzia Enemy of the People hadi hadithi za Kichina na mchanganyiko wa riwaya, tamthiliya, mashairi, pamoja na hotuba na kazi nyingine za siasa kuanzia za Mwalimu Julius Nyerere hadi Frantz Fanon, Samora Machel na Nelson Mandela.
Uwezo wa kupima ni wa kuchambua, siyo wa kukumbuka
Wanafunzi waliiva katika kusoma na kujadili vitabu vile. Tena hawakuwa na haja ya kukariri kwa sababu waliruhusiwa kuingia kwenye mtihani na vitabu vyao. Tulichopima si uwezo wa kukumbuka bali uwezo wa kutafakari na kuchambua. Na si hivyo tu. Kila mwanafunzi alitakiwa kufanya kazi maalum mbili: Kazi binafsi ya ubunifu (mashairi, tamthiliya, au hadithi) na kazi ya vikundi ya uchambuzi wa vitabu vya fasihi (pamoja na vitabu ambavyo havikuwepo kwenye mitaala).
Kazi maalum hizi zilichangia sana kuiva kwa wanafunzi, kiitikadi na kiubunifu pamoja na kuendeleza Kiingereza chao bila hata kujua (by osmosis ha ha ha). Matokeo yake yalionekana. Kazi binafsi za ubunifu zilizaa vitabu vya fasihi kama Zaka la Damu kilichoandikwa na mbunge na waziri mstaafu Harrison Mkwakyembe. Aidha wanafunzi wangu wengi wakawa waandishi, kama vile Pepo ya Mabwege ya Mwakyembe na Machozi ya Mwanamke na Ushuhuda wa Mifupa zote za Hayati Ibrahim Ngozi ambaye alifariki mapema mno kutokana na ajali ya gari. Aidha Summons, Poems from Tanzania ni zao la mitaala hii maana waandishi ni wanafunzi wangu pamoja na marafiki zao wa shule nyingine. Waandishi wengine walitoka pia kwenye shule nyingine kama vile Freddy Macha na Hayati Seth Chachage kutoka Sekondari ya Mzumbe. Somo la Fasihi lilitajirisha fasihi ya Tanzania katika Kiingereza na Kiswahili.
Si hivyo tu, wanasheria bora wengi sana waliandaliwa na somo la Fasihi. Wakati fulani niliwalalamikia wanafunzi wangu, nikisema: “Nyinyi jamani, kwa nini wote mnaingia sheria? Nitang’atuka vipi wakati wote hamtaki kuwa walimu na nyinyi?” Hayati Jwani Mwaikusa akanijibu kwa kusema: “Kosa lako mwalimu. Umetufundisha kuchambua. Sasa sheria ni sehemu ya uchambuzi hasa.” Na kweli. Walitajirisha sana tasnia ya sheria!
Sasa ni matumaini yangu kwamba mnaona tofauti kati ya enzi zile na enzi za sasa. Enzi zile, hata katika kusahihisha mitihani, wasahihishaji walifurahi sana kupata shule zenye wanafunzi ambao kila mmoja alijibu kivyake. La muhimu lilikuwa jinsi wanavyotoa hoja na kuitetea kwa mifano mizuri. Iwapo waliona wanafunzi wote wanatoa majibu yanayofanana, wasahihishaji walihisi labda shule imeiba mtihani. Kukariri ‘jibu sahihi’ hakukutakiwa!
Umuhimu wa uwezo wa kutafakari, kubuni
Ndiyo maana walipoenda chuo kikuu na sehemu nyingine, walimu wao walifurahia. Na wao waliingia na kushiriki katika mijadala mizito enzi za ‘Dar es Salaam School of Thought’, enzi ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilivuma duniani kutokana na malumbano ya hoja nzito siku hadi siku na wanafunzi waliiva, waliiva kweli na huko walikoenda kufanya kazi, ilionekana.
Hapo narudi kwenye hoja yangu ya awali. Hata kutaka kutumia stadi za kazi, uwezo wa kutafakari, kuchambua na kubuni una umuhimu mkubwa. Hivyo, sambamba na kurudisha stadi za kazi kwa nguvu zaidi (inayofanana kidogo na michepuo ya zamani lakini kwa kuiboresha) ni muhimu sana kurudisha mitaala inayochochea fikra na ubunifu. Tuachane na wazo kwamba kwa kila suala au tukio lina jibu moja sahihi. Hakuna!
Mtu yeyote atayakesoma Wasifu mpya ya Mwalimu Nyerere iliyoandikwa na Issa Shivji, Saida Yahya-Othman na Ng’wanza Kamata atatambua kwamba kila tukio la historia, hata katika nchi yetu, lina mitazamo na mikinzano mingi. Ni katika kuelewa na kutafakari juu ya mitazamo na mikinzano hiyo tunapata vijana wale wajeuri ambao Mwalimu Nyerere aliwataka.
Au siku hizi hatutaki vijana wenye uwezo wa kutafakari, kuchambua, kubuni na kushirikiana kama mitaala ya zamani ilivyofanya? Hayati Mwaikusa alitabiri hivyo katika shairi lake: ‘Thinking is Prohibited’ (Kutafakari Mwiko). Alitabiri sawasawa? Kwa nini?
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu mbali mbali ikiwemo Mabala the Farmer na Hawa the Bus Driver. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni rmabala@yahoo.com au kupitia ukurasa wake wa Twitter @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative.
3 responses
Bila Shaka nakubaliana na wew Kwenye dhana ya kurejesha mitaala ya zamani kwasababu nimetafakari na kuona kuwa mitaala ya Sasa haimuandai mwanafunzi kuwa mbunifu na mwenye kuhoji,hivyo imepelekea kuwa ni wakupokea chochote kile wanachofundishwa bila kuruhusu kufikiri kwa kina katika kitu wanachofundishwa.
Pia maoni yangu na mtazamo wangu pamoja na kurudisha stadi za kazi katika mitaala ya sasa pia wangerudisha mitaala ambayo inamtaka mwanafunzi asome vitabu vya kutosha vinavyohusu nyanja zote kama vile kiuchumi,kisiasa,kijamii,Afya, technologia ili tuweze kuvumbua vitu vyakutosha kwa manufaa ya taifa na jamii inayo tuzunguka
Umesema vizuri sana. Kwa Sasa ubunifu hakuna kabisa. Wanafunzi wanakaririshwa vitu ambavyo haviko hata kwenye uhalisia wa maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano katika somo la Uraia(civics) wanafundishwa “principles of democracy” kwamba Ni pamoja na free and fair election, freedom of expression, etc. Lakini wanapoenda mtaani ndiyo wanakuwa wahanga wa kutoa maoni ambayo watawala wanayaona hayafai kutolewa. Si Bora wabadili mitaala inayoendana na matakwa yao?. Mwandishi Mimi nionavyo elimu yetu ya Sasa haina tofauti na ile ya kikoloni. Mambo wanayokaririshwa watoto wetu hayawasaidii wanapohitimu na kuishi maisha ya mtaani. Ndiyo maana mhitimu wa chuo kikuu unamkuta analalamika mtaani kuwa hana ajira wakati ufaulu wake unakuta Ni wa juu sana.
Kwa Tanzania mitaala inahitaji marekebisho makubwa ili elimu inayotolewa iendane na mahitaji ya wakati tulionao. Hivi sasa wahitimu wengi wanarudi mitaani wakiwa na taarifa badala ya maarifa na kujikuta hawana uwezo wa kuziona fursa lakini pia hawana ujasiri wala uthubutu kwa sababu wamejaza nadharia tupu vichwani mwao.
Kikwazo kimojawapo ni lugha ya kufundishia ambayo imekuwa kikwazo kikubwa katika uhawilishaji wa maarifa. Wanafunzi na walimu hawaelewani wakati wa ufundishaji na ujifunzaji.
Masomo yanayofundishwa yamebebwa maarifa yaliyopitwa na wakati kwa kiasi kikubwa na kufanya maarifa yanayotolewa yawe ni marudio na upotezaji wa muda bure. Kwa mfano katika somo la Kiswahili mada zinajirudiarudia bila ulazima. Kama tungefundisha mambo ya msingi basi miaka saba shule ya msingi isingekuwa na ulazima.
Mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia huchangia ugumu katika utekelezaji wa malengo ya elimu. Mathalan, ukosefu wa vifaa vya maabara, madawati na walimu kukosa motisha.
Kimsingi mitaala ni sehemu moja katika kufikia malengo ya elimu tunayoitaka.