Search
Close this search box.

Tusiruhusu Binadamu Atenganishwe Na Afya Yake

Watanzania masikini hawana shida na bima ya afya bali mfumo imara wa taifa wa afya ya jamii ambao utasukumwa na utoaji  huduma na sio utafutaji wa faida. 

subscribe to our newsletter!

Ni muhimu kujua kuwa mwanadamu na afya yake ni vitu ambavyo havitengani, hata kidogo. Kwa sababu afya ndiyo maisha ya binadamu, ndiyo uhai wake, na ndiyo inamfanya afanye kazi, ndiyo kazi hiyo hiyo inayomfanya pia aimarishe hiyo afya. Huo ndiyo mzunguko wa binadamu. Afya na maisha ya binadamu ni vitu vinavyoenda sambamba. Ukitoa kitu afya kwa mwanadamu basi pia utakuwa umeondoa na maisha yake. Anaweza akawa kama jiwe tu, ukiliweka hapo chini halifanyi kazi, kwa sababu halina kitu kiitwacho afya.

Hiki kitu afya kipo ndani yake mwanadamu, ndicho kinafanya ubinadamu wake utambulike. Lakini kitu hiki kinategemea sana mazingira ya jamii kukiendeleza kwa sababu kinahitaji chakula. Ndiyo, kwa sababu chenyewe ni kama mashine inayohitaji mafuta ili iweze kufanya kazi. Ndivyo afya nayo inahitaji chakula ili iendelee kufanya kazi. Hili si suala la hiari. Halina mjadala. Na suala la chakula nitalizungumzia siku nyingine, maana nalo limebeba sura mpya baina yake na fedha. Na mambo kadhaa ambayo nayo tunashuhudia yakitenganishwa na binadamu, kama vile maji, elimu, misitu, makazi, na kadhalika.

Lakini sasa tunaona yapo mambo ambayo yanataka kufanya binadamu huyu atengwe na hiyo afya yake. Mambo hayo yanataka kuharibu kabisa ubinadamu, kwa sababu yanalenga kufanya afya kuwa ni kitu mbali na binadamu, kama ilivyo gari au nyumba au hata simu. Unaweza kuishi bila ya simu au gari lakini huwezi kuishi bila afya. Sasa, kuna kitu kinaitwa bima katika mfumo wa kibepari ambacho nadhani kinamtenga huyu mtu na afya yake, kwa sababu sasa tunaambiwa tuikinge afya yetu kama vile nyumba au gari/simu wakati tunajua kabisa kwamba afya ni kitu kilichopo ndani yetu na wala sio nje kama ilivyo kwa vitu hivyo. Kimsingi ukifanya afya iwe kama gari na kuweza kuikatia bima, maana yake tumekubali kuifanya afya kuwa ni kitu ambacho kipo mbali kabisa na mwanadamu kama ilivyo gari au simu. Hapo tutakuwa tumekubali kwamba tunaweza kuishi bila ya kitu afya. Kitu ambacho sio kweli!

Suala la kila mtu awe na bima ya afya kama njia ya kumuwezesha kila mtu apate huduma za matibabu, ndiyo hoja kuu kwa sasa. Tuliona hapa nchini Tanzania kampeni za wagombea mbalimbali, wale wa chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) na upinzani, kama CHADEMA na ACT-Wazalendo, wakinadi suala hili wakati wakinadi sera zao kipindi cha kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2020. Sasa pia, baada ya uchaguzi, ahadi hii itaenda kutekelezwa kwamba kila mtu awe na bima ya afya.  Kwa ujumla, Serikali ipo mbioni kupitisha sheria ya bima ya Afya kwa wote, ili kila mtu awe ameingia kwenye mfumo wa bima ya afya. Hoja inayotolewa kwa hatua hii ni kwamba Serikali inalenga kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wengi, hususani wale wa vijijini na wanaoishi katika mazingira magumu.

Bima isiwe kigezo cha mtu kupata tiba

Suala hili, hata hivyo, linahitaji mjadala wa kina. Hii hatua ina maana gani? Je, huu si muendelezo wa kufanya kitu afya kuonekana kama kitu baki? Cha pembeni ya mtu? Kuwa jambo la ziada kwa mwanadamu? Na kama mtu hana pesa ya kukata bima je, huyu mtu asipate matibabu? Maswali haya yanaweza yakaonesha kwamba tumekubali bima iwe kigezo cha watu kupata tiba. Hii ina maanisha hicho  kitu afya kimekuwa hiari na siyo lazima kukipata. Kama jambo hili la bima ya afya kwa wote litakuwa la lazima, na kama ni hivyo maana yake watu lazima wachangie pesa, vipi watu ambao hawana uwezo wa kifedha na ambao watashindwa kuchangia? Hii inadhihirisha kwamba katika uchumi wa soko afya siyo ya lazima. Mwenye pesa ndiyo atapata afya nzuri zaidi. Na ukweli mchungu ni kwamba hivyo ndivyo hali ilivyo.

Suala hili la bima ya afya lina uhusiano mkubwa sana na dhana ya kupata faida. Kwa kuwa mfumo wa uchumi wa soko unasukumwa zaidi na faida kuliko kutatua shida za watu, kwa hiyo bima ni mwendelezo wa kubidhaifisha afya, kuifanya iwe bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa sokoni wakati ukweli ni kwamba afya ni haki ya asili ya kila mtu. Ndiyo maana nirahisi unapokwenda hospitalini kutafuta matibabu kusikia, “Ndugu, bima yako haikingi (covering).” Au unaambiwa kuwa bima yako haiwezi kutibu tatizo fulani au huu ugonjwa. Ukitaka huduma hiyo ongeza fedha zaidi na katika soko ndiyo maana tunaona bima nyingi na kila bima ikinadi vitu gani itatoa (packages) kwa mgonjwa.

Hili unaweza kumwambia mtu menye gari au nyumba kwamba bima yake haiwezi kutatua tatizo hili au lile. Kwake, itakuwa sawa tu na akaenda kuishi bila gari au hata nyumba. Huwezi kumwambia binadamu kwamba bima yako haiwezi kutibu ugonjwa huu. Hiyo inaweza kumfanya ashindwe kuendelea kuishi. Hii inatuonesha kuwa kuna shida katika kuifanya afya kuwa kitu cha kuwekewa bima. Ingawa inazungumzwa kwamba bima itasaidia mtu kutotumia pesa yake kutoka mfukoni bado utaratibu wa bima ya afya unatenganisha mtu na afya yake. Suala la kutibiwa lisingepaswa kuwa suala la pesa. Ilipaswa mtu akiumwa atibiwe kwa sababu ndiyo maisha. Ndiyo uhai. Sasa kuweka kitu kingine juu ya afya inapunguza uhusiano wa mtu na afya yake.

Utengenezaji wa matabaka

Nchini Marekeni waliona bima ndiyo suluhu ya matatizo yao ya kiafya. Lakini ikawa ndivyo sivyo. Watu wana bima lakini suala la watu kushindwa kugharamia hizo bima katika kupata matibabu limekuwa kubwa na wengi hushindwa kumudu gharama za matibabu. Sasa imekuwa ni mkanganyiko, mara Obamacare au Trumpcare! Ni jambo la kujifunza hili. Ni kwa kiasi gani tutafanya afya iwe kwa watu wote kwa usawa kwa kuwa lengo ni kutoa tiba kwa watu ili wapone na si vinginevyo. Na tunalo la kujifunza hata wakati huu. Bima zilizopo zinalenga kiasi gani kutoa huduma? Na je, zimefanya vya kutosha kuweka hali sawa kwa watu katika upatikanaji wa matibabu? Maana si jambo jipya kusikia maneno kama ‘bima kubwa’ na ‘bima ndogo.’ Na zipo kwenye mafungu, yaani wazee, watoto nakadhalika. Aina hizi za bima zinatokana na uwezo wa mtu kulipia hizo bima zenyewe.

Moja ya athari kubwa ya utaratibu huu ni kwamba unakuza matabaka katika upatikanaji wa huduma za afya na kuweka mbali zaidi watu na afya zao. Mwaka 2019, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuja na vifurushi vya bima ya afya — Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya — ambavyo vimegawanya watu kwa mafungu. Na kwa mujibu wa vile vifurushi, kadri mtu anavyozeeka ndivyo gharama zinazidi kuwa kubwa zaidi. Haishangazi kuona wananchi wakivipinga vifurushi hivi. Uzoefu unaonesha kuwa inafika wakati mtu hata ukienda hospitali na bima anaambiwa hii bima yako weka pembeni, toa pesa taslim ili ndugu yako atibiwe haraka! Hali hii inadhihirisha tatizo kubwa lililopo kwenye mfumo wetu wa afya kama taifa.

Watanzania masikini hawana shida na bima bali mfumo wa taifa wa afya ya jamii ambao utasukumwa na kutoa huduma na wala siyo faida. Ni muhimu kurudi katika mfumo wa afya wa taifa kwa wote, mbali na bima. Hii itasaidia kwanza kuwekeza zaidi kwenye afya za watu na kujikinga na magonjwa badala ya kusubiri watu waumwe ndiyo tuwatibu kwa bima. Pili, hii itapunguza idadi ya wanao umwa na hata wakiumwa matibabu yatakuwa bure kwao. Kwa sababu, mfumo wa jamii wa kibepari unaendeleza kufanya kila kitu kiwe kina uzwa au kununuliwa kwa lengo la kujipatia faida. Sasa ndiyo tunaona hata vile vitu ambavyo mtu alipaswa apate bure leo vinalipiwa pesa na vinawekewa vikwazo. Mfano mzuri ni hilo suala la afya.

Kumtibu mtu ni ubinadamu na ndiyo ilikuwa hivyo kabla ya pesa na kitu kinachoitwa ubepari. Mtu anatibiwa ili aweze kupona aendeleze ujenzi wa taifa kwa sababu afya ni utu na ndiyo uhai. Lakini sasa hayo yote yamebadilishwa na yamepewa tafsiri ya uchumi na si ya utu tena.

Nassoro Kitunda ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni nassorokitunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.

3 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *