The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Namna Kuzimwa Kwa Intaneti Kulivyoathiri Wafanyabiashara  Wanawake 

Wafanyabiashara wengi wanasema kuzimwa kwa intaneti kipindi cha Uchaguzi Mkuu kuliathiri biashara zao. Wakati baadhi waliweza kupunguza makali ya madhara hayo kwa kutumia teknolojia ya VPN, wengine hata hiyo VPN hawakuweza kuitumia.

subscribe to our newsletter!

Rebeca Minza ni moja kati ya wafanyabiashara wadogo wengi waliokumbwa na athari za kuzimwa kwa mtandao wa intaneti nchini Tanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Octoba 28, 2020, ambao John Magufuli, mgombea wa uraisi kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuchukua hatua hiyo ambayo tayari ilishaanza kushika kasi katika baadhi ya nchi, hususani za Afrika ambazo maendeleo yao ya kidemekrasia na kisiasa kwa ujumla yamekuwa yakisuasua. Hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuzima mtandao wa intaneti ilikuja licha ya kwamba tayari kulikuwa na kampeni ya kuzuia kitu hicho kutokea Tanzania. Pia, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya haki za mtandao walishaanza kuhoji endapo kama Serikali ingeruhusu matumizi ya intaneti kipindi cha uchaguzi ukizingatia mienendo ya uvunjifu wa haki za kiraia uliokuwa unaripotiwa nchini.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambayo inajukumu la kusimamia mawasiliano yote ya kielektroniki nchini, haikuwahi kutoa tamko lolote kuhusiana na kadhia hiyo ambayo mbali na kuwasababishia akina Minza hasara kubwa kwa biashara zao pia ilikosolewa vikali na watetezi wa haki za mtandao wakisema kwamba inaminya uhuru wa watu kujieleza na kutumia intaneti. TCRA pia imeshindwa kujibu maswali kadhaa ya The Chanzo licha ya juhudi za kuwatafuta wasemaji wake zaidi ya mara moja.

Wafanya biashara wanena

“Siku mtandao [wa intaneti] ulivyozimwa nilikuwa na oda ya Sh.500,000 kutoka kwa wateja wangu wa Arusha, hivyo wakati  wanaendelea kuchagua rangi kupitia picha nilizowatumia  [kupitia WhatsApp] ghafla mtandao ukakata, tukakaa siku nzima haukurudi hivyo ikala kwangu,” Rebeca, mkazi wa Kimara Baruti, Dar es Salaam,  anayefanya biashara ya viatu na magauni kwa njia ya mtandao anaeleza jinsi hatua hiyo ilivyoathiri biashara zake.

Kwa mujibu wa Rebeca, hali hiyo ilimuingizia hasara ya Sh.600, 000 kwa sababu wakati tukio hilo linatokea alikwisha lipia mzigo wa Sh.500,000 kwenye duka la jumla ambayo haikurudishwa na Sh.100,000 ni faida aliyotegemea kuipata.

Akielezea namna biashara yake inavyofanya kazi, Rebeca anasema: “Mteja anapotaka nguo za aina fulani huwa tunakwenda kuzilipia kabisa kwenye maduka ya jumla ili zisiuzwe. Halafu unasubiri mteja achague rangi anazopenda  ndio unakwenda kuchukua. Mteja akishachagua rangi ndipo analipia nguo na mimi ninapata faida kati ya Sh. 5,000 hadi Sh. 10,000 kwa kila nguo. Kwa hiyo, mteja asipochukua hiyo nguo napata hasara mara mbili, nakosa faida na ile hela ambayo nimeishailipia.”

Si Rebeca tu aliyeshuhudia biashara zake zikivurugwa na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti. Rhoda Nyambuya,  anayeuza pochi na viatu katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam ni mfanyabiashara mwengine mdogo aliyeonja joto la jiwe la kuzimwa kwa intaneti. Wakati wa mahojiano na The Chanzo, Rhoda anasema kuwa kusitishwa kwa mtandao kulimrudisha nyuma kimaendeleo kutokana na mauzo yake kupungua kwa kasi kwa siku takribani saba.

Ingawa Rhoda ana meza ya biashara Kariakoo, Dar es Salaam amewekeza nguvu kubwa kwenye mtandao kutokana na watu kupunguza safari za kwenda Kariakoo kuepuka kupata maambukizi ya Corona. Anaeleza: “Unajua tangu kuingia kwa janga la COVID-19 nchini wateja wengi wamehamia mtandaoni. Kwa hiyo, kulipozimwa ule mtandao kwa kweli biashara ilisimama. Kwa mfano, kabla ya mtandao kuzimwa nilikuwa nauza sana, mauzo madogo sana yalikuwa ni Sh100,000. Lakini baada ya mtandao kuzimwa, nikipata Sh20,000 nilikuwa nashukuru. Muda mwengine unaishia kuuza Sh5,000 tu.”

Kwa upande wake, Tuma Ifran, mfanyabiashara wa vyombo vya mtumba kutoka Zanzibar, anasema hawezi kusahau namna alivyowahi kukaa takribani wiki nzima bila kufanya biashara kutokana na kutopatikana kwa huduma ya mtandao. Asilimia 80 ya mauzo ya mama huyu hutegemea wateja kutoka Tanzania Bara ambao huchagua bidhaa kupitia mtandao wa Instagram na Facebook kisha kutuma hela na kusafirishiwa bidhaa zao.

“Nilikaa wiki nzima bila kufanya biashara mpaka mtandao uliporudi ndipo nikaanza kukusanya oda tena, kilichoniumiza zaidi ni kwamba siku mtandao ulipozimwa nilikuwa nafungua mzigo mpya hivyo nilitegemea mauzo mengi kutoka kwa wateja wangu wa jumla,” anasema Tuma. Wastani wa mauzo  ya Tuma kwa siku ni Sh.100,000 hadi Sh.200,000 hivyo kwa siku ambazo mtandao ulizima alipata hasara ya Sh.500,000 hadi 1,000,000 kwa makadirio.

VPN yaokoa jahazi

Lakini mtandao haukurudi baada ya wiki moja kama Tuma anavyobainisha. Anachomaanisha ni kwamba ilimchukua yeye takribani wiki moja mpaka kuja kufahamu namna ya kurudi mtandaoni kwa kutumia teknolojia inayojulikana kama Mtandao wa Kibinafsi wa Kidijitali, au Virtual Private Network (VPN) kwa kimombo. Kwa mujibu wa mtandao wa Tanzania Tech ambao huchapisha habari na chambuzi za masuala ya kiteknolojia, VPN ni programu maalum ambayo inaweka ulinzi kati ya mtumiaji wa intaneti na kampuni inayompa huduma ya intaneti. VPN, pamoja na mambo mengine, humuwezesha mtumiaji kutumia tovuti ambazo hazipatikani katika nchi yake au zimezuiliwa.

Licha ya ukweli kwamba sheria za Tanzania zinazuia matumizi ya VPN, wafanyabiashara wa mtandaoni, kama ilivyo kwa maelfu ya Watanzania wanaotumia mtandao wa intaneti kwa shughuli mbali mbali, hawakuwa nyuma katika kutumia teknoloja hiyo ili kuepusha athari zaidi ya kuzimwa kwa intaneti kwenye biashara zao.

Moja kati ya wafanyabiashara hawa ni Bertha Mmari anayeeleza kuwa mwanzoni alipata shida kama wafanyabiashara wengine wa mtandaoni lakini baada ya kuelekezwa kutumia huduma ya VPN mambo yalikuwa shwari. Anaeleza: “Mwanzoni hata mimi nilipata shida sana. Mimi ni mfanyabiashara wa jumla na wateja wangu wengi wapo mikoani na njia pekee ya kuwasiliana ni kutumia Facebook na WhatsApp.”

Bertha anasema alilazimika kurejesha Sh. milioni tatu kwa wateja ndani ya siku tatu za kuzimwa kwa intaneti kitu ambacho anakiona kama hasara kwa biashara yake. Ili kukabiliana na hasara kama hizo, ndipo Bertha, anayefanya biashara ya nguo, viatu na pochi, alipoelekezwa kutumia huduma ya VPN na rafiki yake aliyepo nchini China. Tangu hapo akapata unafuu wa mauzo yake. Anasema: “Baada ya kuona mafanikio, nami nikawaelekeza wateja wangu wa mikoani na hapa Kariakoo na tukaendelea na biashara. Lakini hapo zilishapita siku tatu bila kufanya biashara ya maana.”

Lakini siyo wote walielewa teknolojia hii na wapo ambao waliendelea kupata hasara na athari za kuzimwa kwa mtandao wa intaneti. Mmoja wao ni Ashura Selemani anayekiri kwamba hakufanukiwa kutumia huduma ya VPN hali iliyomsababishia biashara yake kuzorota.

Mfanyabiashara huyo wa  saluni ya kike na magauni ya harusi katika eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam anasema alikuwa akisikia tu kuhusu VPN lakini hakupata mtu wa kumuelekeza jinsi ya kutumia.  Ashura anailalamikia kadhia ya kutopatikana mtandao kumsababishia kupoteza wateja wake kwa kuwa walihamia kwa wafanyabiashara wengine ambao walikuwa wanaendelea na huduma hiyo kupitia VPN.

Wadau wa haki za mtandao, ujasiriamali watia neno

Mpaka sasa, hakuna tathmini rasmi iliyofanywa ya gharama iliyopatikana kutokana na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti nchini Tanzania. Hata hivyo, wadau kadhaa wa masuala ya haki za mitandao wamejaribu kuonesha namna hatua hiyo ilivyoathiri shughuli za watu mbalimbali. Moja kati ya wadau hawa ni shirika lisilo la kiserikali la Access Now linalojihusisha na masuala ya haki za mtandao. Kwenye taarifa yao ya Disemba 16, 2020, Access Now waliwasilisha jumla ya simulizi 11 kutoka kwa Watanzania wanaojihusisha na shughuli mbalimbali wakielezea athari za kuzimwa kwa mtandao kwenye shughuli hizo.

Zaituni Njovu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Zaina Foundation ni moja kati ya wadau wanaokiri kwamba kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kumerudisha nyuma maendeleo ya wanawake wengi wajasiriamali, akisema: “Kuzimwa kwa mtandao kunaathiri wanawake wajasiriamali nchini kwa sababu wengi wanategemea mtandao huo kuwasiliana na wateja wao hasa katika kipindi cha mlipuko wa COVID-19.”

Shirika lake za Zaina Foundation limejikita katika kuhamasisha wanawake juu ya matumizi salama ya mtandao likiamini kwamba matumizi ya intaneti ni haki  ya msingi ya binadamu. Ni moja kati ya wadau wachache walioishauri Serikali kutozima mtandao wa intaneti, likiendesha kampeni ya #KeepItOnTZ kufikisha ujumbe wake. Kwenye ripoti yake ya Septemba 9, 2020, Zaina Foundation iliitaka Serikali kufanya tahmini ya hasara zitakazotokana na kuzimwa kwa intaneti kabla ya kuchukua uamuzi huo.

Karen Alfred ambaye ni mhamasishaji wa wanawake wafanyabiashara kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao kupita Mradi wa Uthubutu wa Mwanamke anasema kuzimwa kwa mtandao kuliyumbisha harakati zao kwa muda.

“Tangu ilivyotokea ile hali [ya kuzimwa kwa intaneti] wanawake wanaoneka wamepoteza hamu ya kutumia mitandao kwa biashara,” anasema Karen. “Hoja kuu wanayotoa ni kuwa ukitegemea mtandao siku ukija kuzimwa ghafla hasara unayopata ni kubwa. Lakini bado tunaendelea kuhamasisha tukiamini kuwa jambo kama hili haliwezi kujirudia tena.”

Jenifer Gilla ni mwandishi wa kujitegemea wa habari za kijamii, wanawake na vijana anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, unaweza kuwasiliana na mwandishi kupitia jenifergilla2@gmail.com au mhariri wa The Chanzo kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *