Jee, ‘Kupiga Nyungu’ Kunatibu COVID-19?

Mtaalamu wa tiba asili kutoka MUHAS anaiambia The Chanzo kwamba ‘kupiga nyungu’ hakutibu COVID-19, ingawaje inasaidia kuboresha mfumo wa upumuaji wa mwanadamu

subscribe to our newsletter!

Hatua ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ya kuweka mitambo kwa ajili ya watu kujifukiza, au maarufu kama ‘kupiga nyungu,’ kwa ada ya Sh5,000, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, imezua mjadala mkubwa hususani kwenye mitandao ya kijamii. Ukiachana na mjadala juu ya ada, wadadisi wengi wanahoji inakuwaje MNH, inayoongozwa na mabingwa wa sayansi na tiba, wanaweza kuwataka watu watumie tiba ambayo Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema haitibu ugonjwa huo unaoendelea kutesa mataifa mengi ulimwenguni.

Kati ya mitambo hiyo minne, mitatu imefungwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Upanga, na mmoja umefungwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila. Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Profesa Lawrence Museru aliwaambia waandishi wa habari mnamo Machi 5, 2021, kwamba sababu za kufungwa kwa mitambo hiyo iliyotengenezwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ni kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa COVID-19.

“Sababu ya kuzifunga [hizi mashine] ni kwa sababu hii ni njia moja wapo ya kupambana na magonjwa ya kupumua, ikiwemo COVID-19, ambayo tunaambiwa kwamba njia ya kujifukiza inasaidia,” alisema Profesa Museru wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. “[Hatua hii] inaenda sambamba na utumiaji wa dawa za asili ambazo pia zimekuwa zinatumiwa na kuna ushuhuda kwamba zinasaidia.”

Vifo vitokanavyo na changamoto za upumuaji

Hatua ya MNH kufunga mitambo ya kujifukiza inakuja wakati ambao kumekuwa na wimbi kubwa nchini Tanzania la vifo vitokanavyo na changamoto za upumuaji, huku Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Dk Charles Kitima akisema kwamba ndani ya kipindi cha miezi miwili, kuanzia katikati ya mwezi Disemba na Februari, jumla ya mapadri 25 na masista 60 wamefariki kwa changamoto za upumuaji.

Baada ya miezi kadhaa ya kukanusha uwepo wa COVID-19 Tanzania, mnamo Januari2021, Rais John Magufuli alitaadharisha juu ya uwepo wa virusi hivyo nchini na kutaka watu wachukue tahadhari. Njia kubwa ya kujikinga na ugonjwa huu ambayo imepigiwa chapuo na Serikali mpaka sasa ni kutumia tiba za asili, ikiwemo hiyo ya kujifukiza, huku Waziri wa Afya Dk Dorothy Gwajima akiwa mstari wa mbele kuwaonesha wananchi kwamba tiba hizo ni sahihi kwa yeye na mumewe kujifukiza mbele ya waandishi wa habari.

Kufuatia hatua hizi, pamoja na tamko la WHO kwamba kujifukiza hakutibu COVID-19 na kuonya kwamba inaweza kumletea mtu anayejifukiza athari kubwa, The Chanzo ilifanya mahojiano na Dk Joseph Otieno, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Dawa Asili kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Kishiriki cha Muhimbili (MUHAS). Na hapa Dk Otieni anaanza kwa kueleza namna kujifukiza imekuwa ikitumika kupambana na magonjwa ya mfumo wa hewa.

“Ufukizaji ni njia moja wapo ya kujikinga na magonjwa ya mfumo wa hewa, na hii inajulikana kabisa kisayansi tangu miaka mingi  hivyo tunaiamini. Tunajukumu la kuhakikisha kwamba  tiba asili, kama inavyotolewa na waganga wa asili, zinafanyiwa utafiti kuhakikisha ubora wake na zile zinazofanya kazi zinaingia katika mfumo ambao unasaidia wananchi kunufaika na dawa hizi.

“Tiba asili kwa muda mrefu zimenyanyapaliwa na kutafsiriwa vibaya kama ni tiba inayohusishwa na uchawi na ushirikina.  Lakini kadiri watu wanavyobadilika na watu wanavyokuwa na uelewa  imekuja kugundulika kwamba tiba asili ni mfumo ambao ukifanyika vizuri  unaweza kuwa bora kama mfumo mwingine wa utoaji huduma wa tiba za kimagharibi.

“Tiba asili inajumuisha kulala mapema kama inavyotakiwa, kufanya mzoezi, kutumia mwanga wa jua vizuri, kunywa maji na mambo mengi. Ukiruhusu mwili kuwa hivyo unaweza kuwa na  afya njema na inawezekana  hata usihitaji matibabu ya kuweka dawa za kisasa katika mwili wako. Na sio tu kutumia tiba asili lakini pia tunasisitiza sana watu wafanye mazoezi hasa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na matatizo ya mfumo wa kupumua ambapo kila  nchi inatumia mfumo ambao unahisi utasaidia  wananchi wake.

“Tanzania  pamoja na kufuata maelekezo yote ya kiafya  kama inavyotakiwa kulingana na mwongozo wa WHO kama  kukaa mbali, kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na njia zingine zote ambazo zimependekezwa pia inaona kwamba itumie tiba asili.”

Kujifukiza si dawa ya COVID-19

Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Otieno, kujifukiza haipaswi kuchukulia kama tiba ya COVID-19, bali kama moja kati ya jitihada za kisayansi zinazohakikisha kuwa mfumo wa upumuaji una afya njema.

“Mfumo wa upumuaji unapokuwa katika afya njema unasaidia mwili kupambana na maradhi ikiwa ni pamoja na COVID-19 na maradhi mengine ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza,” Dk Otieni anaendelea kufafanua.

“Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kwamba tunatumia mimea au mfumo wa ufukizaji ambao utafanya mapafu kufanya kazi vizuri na ninapendekeza mimea mitatu. Wa kwanza ni kashwagara, ambao una mafuta ambayo ukiweka katika maji moto na kujifukiza  inasaidia  kuhakikisha  inatoa malendalenda na makamasi ambayo yamekaa katika mfumo wa upumuaji. Lakini mmea mwingine ni mchaichai, ambao unalimwa kila sehemu na mwingine ni makaratusi. Chukua majani ya mimea hii weka katika maji ya moto funua halafu baadae ujifunike kwa shuka safi  au kanga.

“Lakini njia nyingine ni kutumia  vinywaji  vya moto. Tunajua mvuke huwa unafika hata sehemu ambayo maji ya moto hayawezi kufika.  Kwa hiyo tunashauri mtu watumie maji ya moto ambayo yana tangawizi, mdalasini, na pilipili manga. Sio lazima uweke sukari, unaweka ndimu kidogo kwa sababu ndimu ikiwekwa nyingi inatabia ya kukwangua mfumo wa chakula  na utumbo.

“Wakati mwingine  unaweza kuchukua tangawizi iliyosagwa, mdalasini, na pilipili manga unachanganya na asali halafu unalamba.  Lakini pia unaweza kuchukua  vitunguu maji na vitunguu swaumu na pilipili ukakatakata inasaidia mfumo wa upumuaji.

“Kwanza  unapotumia tangawizi pamoja na kitunguu swaumu, damu hazigandi, kwa hiyo zinafaya kazi. Asprin, ambayo inasaida damu isigande, unaweza kutumia hii. Kama umepangiwa kufanyiwa upasuaji si vyema kutumia kitunguu swaumu  au tangawizi kwa sababu damu inakuwa laini  hata kuganda inakuwa ngumu.

“Na pia mmea kama yukaliptas unaweza kujifukiza  na wala sio ya kunywa  ila kashwagara na mchaichai unaweza kujifukiza na ukanywa.”

Kujifukiza siyo kwa kila mtu

Dk Otieni anaonya kwamba kujifukiza si kwa kila mtu, kwani inaweza kuwa na madhara kwa baadhi ya watu. Anaendelea: “Unapojifukiza hewa  inapata joto na inapanuka hivyo kufanya oksijeni kuwa kidogo na inapokuwa kidogo inaweza kuwa na athari kwa watu wenye presha, wajawazito au watoto wadogo. Kwa hiyo huwa  tunashauri wanapojifukiza watumie maji ya moto ambayo yamewekewa mimea kama chai.

“Watakuwa wanakunywa  kupitia  kikombe na wasijifunike kichwa. Hii inawapa nafasi ya kufaidi mvuke na pia kuvuta hewa ambayo inatoka nje na ifanyike kwa muda mrefu  kwa sababu dozi inayoingia kwenye mapafu inakuwa kidogo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts