Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imesema kwamba haitegemei kuona ongezeko la bei ya vifurushi kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano kwani kanuni mpya za vifurushi zinataka watoa huduma hao kuomba idhini kwa mamlaka hiyo kwanza kabla ya kubadili vifurushi, na pia TCRA imeweka bei ya chini na ya juu ya vifurushi ambazo zinawalinda wote mtoa huduma na mteja na wote wanatakiwa kuzifuata.
Hayo yalibainishwa Ijumaa, Machi 5, 2020, na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa TCRA Dk Emmanuel Masasseh wakati wa mkutano na vyombo vya habari vya mtandaoni kupitia Zoom. Kikao hicho kilichohudhuriwa na waandishi wa habari za mtandaoni kama vile bloggers na waendeshaji wa TV za mtandaoni, maarufu kama online TV, kilihusu kanuni mpya zilizotolewa na TCRA zinazolenga kutatua kero mbalimbali kuhusu huduma za vifurushi.
Kanuni hizo mpya ambazo utekelazaji wake unategemewa kuanza April 2, 2021, ili kuwawezesha watoa huduma kujiandaa vyema, zinakuja miezi takribani mitatu baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Faustine Ndungulile kuitaka TCRA imalize changamoto za bando na vifurushi zinazotolewa na kampuni za simu kwa wananchi.
“Hivi karibuni kumekuwa na ushindani usio na tija ambao umesababisha watoa huduma wengi kuuza huduma za ndani ya vifurushi hasa data kwa bei zisizo na uhalisia,” alisema Dk Manasseh akielezea sababu za kupanda kwa bei ya vifurushi ambapo alisema hali hiyo ilisababishwa na ushindani usio na tija toka kwa watoa huduma. “Pamoja na ukweli kwamba hali hii ilikuwa ikiwanufaisha watumiaji wa huduma, utaratibu huu uliwafanya baadhi ya watoa huduma kushindwa kufikia viwango vya ubora wa huduma vinavyostahili na hivyo kuleta kero kubwa kwa watumiaji.”
Kuisha haraka kwa data
Akizungumzia malalamiko ambayo TCRA huyapokea kutoka kwa watumiaji kuhusiana na kuisha haraka kwa vifurushi, saa nyingine hata bila wao kutumia, Dk Manasseh alieleza kwamba kanuni zimewataka watoa huduma kuweka application maalum zitakazo wawezesha watumiaji kufuatilia matumizi yao ya data. Kwa mujibu wa Dk Manasseh, TCRA hufanya tafiti za mara kwa mara juu ya vifurushi huku akiwaasa watumiaji kuwa na mipangilio maalumu itakayowawezesha kukusanya velelezo vingi juu ya mienendo ya data ili TCRA iweze kufanyia kazi.
Dk Manasseh pia aligusia namna kanuni mpya zinavyomzuia mtoa huduma kupunguza kasi ya data kwenye kifurushi cha mteja ndani ya muda wa kifurushi husika. Kwa siku za hivi karibuni, watumiaji wengi wamekuwa wakilalamika kwamba baada ya kununua vifurushi wengi wao hushindwa kufurahia huduma kwa kupungua kwa kasi au kutokuwepo kabisa kwa mtandao. Dk Manasseh amesema kwamba katika kuhakikisha watoa huduma wanatoa huduma zilizo bora, TCRA imekuwa ikifanya mashauriano na watoa huduma hao ikiwemo kuwapiga faini pale inapobidi.
Changamoto nyingine ambayo iliibuliwa na washiriki wengi wa kikao hicho cha takribani masaa miwili ni suala la wateja kutoa bei kamili kununua vifurushi lakini mtoa huduma hukikata baada ya muda kuisha, hata kama mteja hajamaliza kifurushi chake.
Akifafanua kadhia hii, Dk Manasseh alisema hiyo inatokana hasa na muundo wa biashara ya mawasiliano na si jambo geni katika biashara kuwa na vifurushi vya muda fulani. Alisema jambo hilo pia linaonekana pia kwenye biashara zingine kama mahoteli, usafiri na kadhalika.
Masharti yatokanyo na kanuni mpya
Katika kutoa ahueni ya jambo hili, kanuni mpya zinamtaka mtoa huduma kuweka utaratibu wa kumwezesha aliyejiunga na kifurushi chochote kuendelea kutumia muda au uniti za kifurushi ambazo zitakuwa zimesalia ndani ya muda wa matumizi uliowekwa kwa kununua tena kifurushi hicho hicho kabla ya kumalizika kwa muda wake.
Ili kuhakikisha mteja kajiandaa kabla kifurushi hakijaisha, kanuni zimetaka watoa huduma kutoa taarifa kila wakati matumizi ya kifurushi yatakapofikia asilimia 75 na 100 kwa vifurushi vya muda wa maongezi, data na SMS. Pia kanuni zimetoa mwanya kwa mteja kuweza kuhamisha kuanzia MB 250 kwenda kwa watumiaji wengine wasiozidi wawili, hii inatoa wigo wa mtumiaji kumaliza kifurushi chake pale anapoona kinakaribia kuisha na hatakuwa na mpango wa kununua kingine cha aina hiyo.
Ili kudhibiti salio la kawaida kutumika pale kifurushi kinapoisha, kanuni hizi zimewataka watoa huduma kuweka utaratibu unaomuwezesha anayejiunga na huduma za vifurushi kuchagua na kukubali kutozwa gharama zisizokuwa kwenye vifurushi mara muda wa vifurushi alichojiunga nacho au uniti za kifurushi husika kumalizika.