The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

A-Z ya Alichokisema Majaliwa Kuhusu Afya ya Rais Magufuli

Asema tetesi za kuugua dhidi ya Rais Magufuli zinaenezwa na watu wasioitakia mema Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema leo Ijumaa, Machi 12, 2021, kwamba Rais John Magufuli anaendelea vizuri, akikanusha habari zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa kwamba kiongozi huyo mkuu wa nchi anasumbuliwa na matatizo ya kiafya, huku wengine wakidai kwamba amepelekwa nchini Kenya kwa ajili ya matibabu.

Kauli hiyo ya Majaliwa ni kauli ya kwanza kutolewa na kiongozi wa ngazi ya juu ya Serikali tangu minong’ono juu ya afya ya Rais Magufuli ianze kusambaa takribani wiki moja iliyopita huku vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiripoti habari hiyo vikibainisha kwamba kila vilipokuwa vikiwatafuta wasemaji wa Ikulu na Serikali hawakuwa wakipata majibu yoyote kutoka kwao.

Majaliwa pia ametoa kauli hiyo ikiwa ni baada ya masaa kadhaa tu tangu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika kuitaka Serikali itoe kauli kuhusiana na afya ya Rais Magufuli, akidai kwamba ukimywa wa Serikali kuhusiana na jambo hilo unaacha maswali ambayo wananchi wanahitaji kupatiwa majibu.

“Watanzania muwe na amani,” Majaliwa amewaasa wananchi katika hotuba yake aliyoitoa baada ya kushiriki ibada ya sala ya Ijumma mkoani Njombe. “Raisi wenu yupo timamu, anachapa kazi na sisi wasaidizi wake tunatembea kufuatilia miradi iliyoletewa fedha za Serikali kwa ajili yenu.”

Majaliwa aliwalaumu Watanzania waishio nje ya nchi kuhusika na kusambaza uvumi kuhusiana na afya ya Rais Magufuli, akisema kwamba kuna baadhi ya Watanzania hawapendi maendeleo ya taifa hilo la Afrika ya Mashariki. Alisema: “Nataka nioneshe masikitiko yangu kwa baadhi ya Watazania ambao hawapendi maendeleo yetu. Wamejawa na chuki tu. Wamejawa na husda tu, na kutaka kushuhudia taifa hili likiporomoka, wakiwa hawapo ndani [ya nchi], wako nje huko, na kutamani kuwachonganisha Watanzania.”

Kwa mujibu wa Mbunge huyo jimbo la Ruangwa kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hakuna msukumo mwengine wowote wa watu waliomzushia Rais Magufuli ugonjwa isipokuwa chuki.

“Kumzushia [Rais Magufuli] ugonjwa ni chuki tu,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa sura yake ikionesha kusikitishwa na kukasirishwa na habari zinazoendelea kusambaa kama moto wa nyika kuhusu kuumwa kwa Rais Magufuli. “Yaani ni sawa na mimi niseme wewe unaumwa halafu nikafurahi sana na kulazimisha watu wengine waamini kama wewe unaumwa. Nina lengo zuri mimi kwako? Inasaidia nini atoke, aende wapi, aje nje, aje afanye nini? Ushamkuta asubuhi anazunguka Kariakoo? Raisi ushamkuta magomeni yupo anazunguka?”

Awali akiongea na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema kwamba kitu kilichopelekea chama hicho kikuu cha upinzani kukaa kikao na kujadili jambo hilo ni imani ya chama hicho kwamba, “Jambo hili linauzito mkubwa, taarifa zilizopo zinauzito, zinahitaji majibu,” kwa mujibu wa Mnyika.

Lakini kwa mujibu wa Majaliwa, Rais, kama kiongozi mkuu wa nchi, ana mpango wake wa kazi na sio mtu wa kuzurura. “Lakini itifaki ya Serikali wote mnaijua,” aliendelea. “Baada ya Raisi kuna msaidizi wake [ambaye ni] Makamu wa Raisi. Ana Waziri Mkuu. Kuna mawaziri. Kuna Wakuu wa Mikoa [na] Wakuu wa Wilaya. [Kuna] maafisa tarafa, watendaji wa kata, mpaka kijijini kuna maafisa watendaji wa kata.”

Serikali iko kazini 

Katika kuwahakikishia Watanzania kwamba anacho kisema kuhusu Rais Magufuli ni cha kweli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alibainisha kwenye hotuba yake hiyo kwamba amekua na maongezi na Rais Magufuli tangu juzi, Machi 10, 2021, wakati Majaliwa alipokuwa na ziara ya kikazi Njombe. Majaliwa alisisitiza kwamba hata asubuhi ya leo, Ijumaa, Machi 12, 2021, aliweza kuongea na Rais Magufuli kama sehemu ya utaratibu wake wa kikazi.

“Hata asubuhi nilivyokua natoka Dodoma nilimpigia na kumjulisha ratiba yangu,” alisema Majaliwa kwa sauti iliyojaa mamlaka na uhakika. “Hata juzi alikua anajua nakuja, akanituma niwasalimie Wananjombe na mimi nilitoa salamu. Kwahiyo nimeona niliseme neno hili ili kuwatia faraja Watanzania. Mheshimiwa Raisi [Magufuli] yupo. Kwamba mimi nimezungumza naye asubuhi hii. [Sasa kama] angekuwa mgonjwa mimi ningezungumza naye kwa simu?

“Watanzania lazima kwanza tuipende nchi yetu. Pili, tuwapende viongozi tuliowaweka wenyewe ili waiongoze nchi yetu. Tatu, sisi wenyewe huku lazima tuzungumze lugha ya upendo. Lazima tuhamasishane mshikamano. Lazima tuondoe chuki ya mtu mmoja mmoja na wote ambao wenye chuki hawafai hawatufai kwenye jamii yetu.”

Kauli ya Majaliwa ilitanguliwa na kauli nyengine kutoka kwa viongozi wa Serikali waliokanusha kile wamekiita “uzushi” na kusisitiza kwamba afya ya Rais Magufuli ipo vizuri, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ambaye amenukuliwa akisema kwamba hata yeye aliongea na Rais Magufuli asubuhi ya leo, Ijumaa, Machi 12, 2021. Naye Balozi wa Namibia, ambaye pia alikuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Modestus Francis Kapilimba alinukuliwa akisema kwamba hali ya Raisi ni shwari na anaendelea na majukumu yake ya kila siku Tanzania.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *