The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wasomi Watofautiana Hoja ya Rais Samia Kubadilisha Baraza la Mawaziri

Ni kuhusiana na matakwa ya kikatiba na kisiasa ya hatua hiyo.

subscribe to our newsletter!

Hoja kwamba endapo Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuunda baraza jipya la mawaziri au la imeendelea kuumiza vichwa vya wafuatiliaji wengi wa siasa za Tanzania, huku wanasheria, wanadiplomasia na wachambuzi wengine wengi wa masuala ya kisiasa na kiutawala wakiendelea kutofautiana juu ya jambo hilo linaloendelea kujadiliwa na kufuatiliwa kwa shauku kubwa na Watanzania walio wengi.

Wakati baadhi ya wadadisi wanatoa hoja za kisheria na kisiasa za kwa nini Rais Samia anapaswa kuunda baraza jipya la mawaziri, wakisema kwamba baraza lililopo halikidhi matakwa ya kikatiba na kwamba utii wake hauko kwa Rais Samia bali kwa hayati Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021, wengine wanasema hakuna ibara ya Katiba iliyovunjwa mpaka sasa na si mawaziri tu waliopishwa na Rais Magufuli bali mpaka wakuu wa idara, mihimili na mashirika mengine ya Serikali, wakiuliza kama na hao watapaswa kuteuliwa wapya.

Hoja ya uundwaji wa baraza jipya la mawaziri iliibuliwa kwa mara ya kwanza na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) ambao katika tamko lao la Machi 19, 2021, siku ambayo Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania, walisema kwamba baada ya usomaji wa pamoja wa ibara ya 51(2) na ibara ya 57(2)(e) za Katiba, imewafanya waseme “kwa kujiamini” kwamba mara tu baada ya Rais kuapishwa anatakiwa kumteua Waziri Mkuu ndani ya siku 14 tokea kuwa kwake Rais. Ibara ya 51(2) inazungumzia uteuzi wa Waziri Mkuu na ibara ya 57(2)(e) inahusu kiti cha Waziri Mkuu kuwa wazi kutokana na kujiuzulu au kwa sababu nyengine yoyote ile. Kwa mujibu wa Baraza la Uongozi la TLS, ‘sababu nyengine yoyote’ katika muktadha wa sasa ni kufariki kwa Rais aliyekuwepo madarakani na kusimikwa kwa aliyekuwa makamu wake.

Mjadala huu hata hivyo ulichukua sura nyengine pana zaidi kufuatia hatua ya Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba kuingilia kati kwa ajili ya kutolea ufafanuzi suala hili. Akiandika katika ukurasa wake binafsi wa Instagram Machi 20, 2021, Dk Nchemba alisema kwamba hakuna ibara yeyote ya Katiba iliyokiukwa mpaka sasa, na kwamba Ibara ya 57(2)(e) ya Katiba haiwezi kutumika katika muktadha huo.

Ni lazima kubadilisha Baraza la Mawaziri?

Lakini wakati wa mahojiano na The Chanzo, Hardson Mchau, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Mchau and Co. Advocates, anaeleza kwamba ni kitu cha lazima kwa Rais mpya anapoingia madarakani kuunda upya Baraza la Mawaziri. Mchau anasema hii ni kwa mujibu wa sheria, na si kwa utashi wa mtu binafsi.

“Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais kamili wa Tanzania, hivyo ana mamlaka kamili na ukiangalia Katiba imempa mamlaka kwamba anapoingia madarakani anatakiwa kuunda serikali yake. Kwamba Rais mpya atavunja Baraza la Mawaziri na kumteua Waziri Mkuu ndani ya siku 14 baada ya kuapishwa,” anasema wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya kwa njia ya simu.

“Pale [Rais Samia] alipoapishwa tu, sheria inamtaka kuunda Serikali yake. Hivyo, asipovunja watabaki Makatibu Wakuu kwa sababu nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, utawala bora na haki za binadamu hivyo asipovunja ni kinyume cha sheria. Tunatarajia wiki ijayo [Rais Samia] atafanya hivyo na inatakiwa Waziri Mkuu kuteuliwa ndani ya siku 14 hivyo pengine tunategemea sura mpya katika Baraza la Mawaziri.”

Hata hivyo, si wanasheria wote wana mtazamo kama wa Wakili Mchau kwani Wakili Justine  Kaleb kutoka Moriah Law Chamber anasema kwaba sheria haijatoa maelekezo kuwa ni lazima Rais mpya atengue uteuzi wa Waziri Mkuu hivyo hakuna ulazima wa Rais Samia kuunda upya Baraza la Mawaziri.

“Kwanza ni muhimu kutambua kuwa Rais alipatikanaje. Na Rais Samia alipatikana baada ya kifo cha hayati Dk Magufuli kulingana na ibara ya 37(5), na kwa mujibu wa ibara ya 42(5) kabla ya kushika nafasi hiyo ataapa kiapo cha uaminifu na kiapo chochote.

“Na akiapa anakuwa Rais kamili sawa na aliyechaguliwa na wananchi lakini sheria haijatoa maelekezo kuwa lazima atengue uteuzi wa Waziri Mkuu kwa sababu akifanya hivyo atakuwa amevunja Baraza la Mawaziri. Katiba haijatoa maelekezo ya moja kwa moja kwamba Rais lazima avunje Baraza la Mawaziri, hivyo anaweza kuamua kuvunja au asivunje na akaendelea nalo.”

Hoja za kisiasa, kiungwana

Hoja za kisheria ni upande mmoja tu wa shilingi kuhusiana na suala hili ya uundwaji wa baraza jipya la mawaziri. Upande mwingine wa shilingi ni hoja za kisiasa kwani baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kwamba kuna umuhimu wa Rais Samia kuunda timu yake mpya ya uongozi kutokana na ukweli kwamba timu iliyopo sasa si ya kwake bali ya mtangulizi wake Rais John Magufuli.

Katika andiko lake la Machi 24, 2021, lililochopishwa na The Chanzo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Richard Mbunda anasema kwamba kumteua mtu katika nafasi ya uongozi kuna maana juu ya falsafa na haiba kwa mamlaka ya uteuzi, kwa kuwa wateule hawa wanakuwa wawakilishi wake.

“Sasa kama falsafa ya kiutawala ya Rais mtangulizi haiendani na ile ya Rais mpya, Rais mpya atahitaji watu wapya wa kubeba falsafa hiyo,” anaandika Dk Mbunda. “Kwa mfano, kama kiongozi analenga kuja na falsafa ya maridhiano, uongozi jumuishi, na kushirikisha wanajamii katika kuyafikia malengo ya maendeleo kama Mama Samia alivyodokeza punde baada ya kula kiapo, ni dhahiri kuwa atahitaji wasaidizi wanaoendana na falsafa hiyo.”

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania wamebainisha kwamba huu si muda muafaka wa kujadili endapo ni muhimu kubadilisha Baraza la Mawaziri au la. Wadau hawa wamebainisha kwamba kitendo cha kujadili mambo haya wakati ambapo hata Rais Magufuli hajazikwa si kitendo cha kiungwana.

“Nchi ipo katika maombolezo [na] wanasheria wanatakiwa kutambua kuwa uzalendo ni kitu muhimu kwa sababu kwanza familia na Watanzania wanapitia katika kipindi kigumu cha majonzi, huu sio muda wa kuhoji,” anasema Ibrahim Sostheness, mchambuzi huru wa masuala ya diplomasia na ushirikiano wa Kimataifa kutoka Dar es Salaam.

Aveline Kitomary ni mwandishi wa habari za kisiasa kutokea Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: avekitomary@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, unaweza kuwasiliana na mhrariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *