The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Askofu Bagonza: Jicho Langu Mahali Penye Dhuluma Linapaona Haraka Sana

Dk Bagonza anataja sababu tatu kwa nini anaamini viongozi wa dini Tanzania wameshindwa kutimiza ipasavyo wajibu wao wa kupigania taifa la haki nchini.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Dini ina mchango mkubwa sana katika uendeshaji wa nchi. Mbali na kushuhudia shule, vituo vya afya na hospital na vyuo vikuu vinavyojengwa na kuendeshwa na taasisi mbali mbali za dini nchini Tanzania, tumekuwa tukishuhudia pia namna ambavyo viongozi wa dini wamekuwa wakipaza sauti zao kutoa muelekeo wa kisiasa, kiuchumi, na hata kidiplomasia ambao Tanzania inapaswa kuufuata.

Jukumu hili la pili limekuwa likiuweka uhusiano kati ya dini na dola, au Serikali, katika hali ya mashaka, na muda mwengine hufikia hata hatua ya Serikali kutishia kuyafutia baadhi ya mashirika ya kidini leseni zao za usajili huku yakiyashutumu kwa kile inachokiita kuchanganya dini na siasa.

Kuweza kujadili mambo haya kwa ujumla na nini mchango wa taasisi ya dini katika kujenga taifa la haki na kidemokrasia, tunayofuraha kubwa sana kuungana na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza. Pamoja na mambo mengine, Askofu Bagonza anasema kwamba hadhani kwamba viongozi wa dini wanatimiza wajibu wao ipasavyo katika kutoa mchango wa uendeshaji wa nchi. Endelea …

The Chanzo: Nataka kuongea na wewe kupata maoni yako kuhusiana na mchango wa dini, au viongozi wa dini, katika ujenzi wa taifa la haki na la kidemokrasia. Na nakuuliza hili pamoja na kutambua kwamba Tanzania, kikatiba, ni nchi isiyokuwa na dini lakini tunafahamu kwamba Watanzania wako na dini zao, na nataka kufahamu kama katika juhudi zinazoendelea nchini za kuhakikisha kwamba Tanzania linakuwa taifa la kidemokrasia, namaanisha kwamba kunakuwepo na ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi kwenye uendeshaji wa nchi na uwepo wa uwajibikaji kwa wale waliopewa dhamana ya uongozi wa nchi, ikiwemo wajibu wao wa kuheshimu Katiba na sheria nyingine za nchi. Unatathimini vipi mchango wenu kama viongozi wa dini kwenye mchakato huu?

Askofu Bagonza: Mchango wa dini na mchango wa viongozi wa dini katika kujenga taifa la haki na la kidemokrasia, mchango huo ni wa muhimu sana. Wakati mwingine mchango wa dini unaweza kuwa tofauti na mchango wa viongozi dini na hasa unaposema taifa letu ni taifa lisilokuwa na dini, Serikali yetu haina dini lakini watu wake wana dini.

Kwa hiyo, hakuna dini ya Serikali lakini hao wananchi wenye dini ndio wanao unda Serikali. Wananchi wenye dini ndio viongozi wa Serikali. Kwa hiyo, mchango upo. Mchango wa moja kwa moja ambao kwamba wananchi wenye dini na viongozi wenye dini wanaongozwa na dini katika maisha yao ndio wanaoliongoza taifa na ndio wanaongozwa na taifa. Kwa hiyo, huwezi kuitenga dini na taifa.

Jambo la pili ni kwamba unaposema neno haki, unagusa vionjo vya kiroho vya kila mwanadamu. Pamoja na kwamba zipo taasisi zinazojihusisha na utoaji haki kama mahakama, lakini neno haki, [yaani] justice [au] righteousness, ni jambo la kiroho na mahali sahihi pakupata mambo ya kiroho ni kwenye dini. Mungu wetu ni Mungu wa haki, ni Mungu asiyependa dhuluma.  Kwa hiyo, suala la haki huwezi kulitenga na dini.

Kwa mara nyingine tena dini ina mchango mkubwa sana katika kuzungumzia masuala ya haki kwa sababu haki kabla halijawa suala la kisheria, haki ni suala la kiroho. Kwa hiyo, kwa mara nyingine tena, dini na viongozi wa dini wananafasi kubwa sana katika kujenga taifa linaloheshimu haki, linaloheshimu utu, na linalojali kwamba demokrasia iwepo kwa sababu huwezi kuongoza wanadamu kama unavyoongoza wanyama.

[Binadamu] ni watu wenye ufahamu na sisi Wakristo tunasema wanadamu wameumbwa katika mfano na sura ya Mungu. Kwa hiyo, watu hawa wana hitaji kuwaheshimu, kuwapa nafasi ya kufanya maamuzi kwa sababu nafasi hiyo wamepewa na Mwenyezi Mungu wakati wa uumbaji. Kwa hiyo, demokrasia [na] haki havitenganishwi na dini. 

The Chanzo: Umezungumza vizuri sana Askofu na ningependa kupata mtazamo wako labda au tathmini yako kwa sababu kusema ukweli ulivyozungumzia ni kinadharia zaidi tukija pengine kiuhalisia labda kwa hapa kama nchini kwetu, tunafahamu tuna dini nyingi, tuna jumuiya nyingi za kidini, unautathimini vipi mchango wenu nyinyi kama viongozi wa dini katika kusimamia ujenzi wa taifa la haki hapa Tanzania?

Askofu Bagonza: Mchango wa dini katika kujenga taifa, tathmini yangu, kwa kweli, naweza kusema hatujafanya vya kutosha na mchango wetu unatakiwa uwe katika hatua tatu na zote ninahisi hatujafanya vya kutosha.

Hatua ya kwanza tunahitaji kufundisha na kuhubiri masuala ya haki katika mafundisho yetu ya kuhamasisha umma na waumini wetu. Hatua ya pili tunahitaji tuchukue hatua tunapoona haki inapotoshwa, ama kwa kukemea ama kwa kujitenga na vitendo vinavyofanywa na kukiuka haki za msingi za watu. Hatua ya tatu, tukishindwa [hizo hatua mbili] basi angalau tuoneshe kwamba tumekerwa, tunune [na] tukasirike kwa kuonesha kwamba hatuungi mkono vitendo hivi.

Sasa, hatua zote tatu, kwa tathimini — umeniuliza juu ya tathimini — hatua zote tatu hatujafanya vya kutosha. Hatujafundisha masuala ya haki na kuyafanya sehemu ya mafundisho yetu ya kila wakati. Hatujakemea ipasavyo vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika taifa letu na katika jamii yetu. Baadhi ya vitendo vinatendwa ndani ya taasisi zetu za kidini. Kwa hiyo, hatujakemea kiasi cha kutosha na tatu, kwa kweli, hatujaonekana kununa na kukasirishwa na vitendo hivi. Kwa hiyo, kama ni tathimini yangu ndiyo hiyo. 

The Chanzo: Asante, sasa labda mtu anaweza akajiuliza labda hiyo itakuwa imesababishwa na nini? Au hali hiyo, kwa mfano, ya kutokufanya vya kutosha unadhani inaweza ikawa imetokana na kitu gani labda, kuna kitu gani kinafanya viongozi wa dini au dini kwa ujumla ishindwe kutimiza hayo uliyoyasema?

Askofu Bagonza: Sababu ziko nyingi sana na zinatofautiana kutoka dini moja kwenda nyingine. Ziko sababu chache za jumla zinazounganisha madhehebu yote ya dini, ni chache, lakini kila dhehebu la dini katika taifa hili lina sababu zake za kutokufanya vya kutosha katika maeneo niliyoyataja.

Labda nijitahidi kutaja sababu kubwa tatu ambazo ninaamini zinaunganisha madhehebu yote kutofanya vya kutosha. Sababu ya kwanza, viongozi wa dini, kimuundo, sisi ni sehemu ya uongozi wa kitaifa. Kwenye ile kitu inaitwa superstructure na sisi tupo huko kwenye msonge. Kwa hiyo, tuko sambamba, [na] tuko sawa na uongozi wa kitaifa kwa hiyo hatuwezi kujipinga. Sisi ni sehemu ya mfumo unao tawala kwa hiyo kusema sema na kupinga pinga na kukosoa kosoa wakati sisi ni sehemu ya ule mfumo unaotawala.

Viongozi wengine wa dini hawataki kuwa wanafiki tuseme, kwamba wao ni sehemu ya tatizo halafu wajifanye wanakemea tatizo hilo hilo. Hiyo [ni] sababu ya kwanza. Sisi ni sehemu ya mfumo, kwa hiyo hatuguswi moja kwa moja na yale ambayo yanawaumiza wananchi wengine wa kawaida, hiyo sababu ya kwanza.

Sababu ya pili ningeweza kusema ni malezi ya kidini tuliyoyapata katika maandalizi ya kuwa viongozi, inaitwa ministerial formation. Liko sisitizo kubwa katika maandalizi [ambapo] wengine maandalizi yao yanachukua muda mrefu miaka mpaka kumi ndipo unakuja kuwa kiongozi. Sasa uko msisitizo wa utii usiohojiwa, kwa hiyo mtu baada ya kuambiwa kutii, kutii, kutii miaka yote unalemaa, unapoteza uwezo wa kuhoji unakuwa ni mtu wa kutii.

Kwa hiyo, baadhi ya malezi yetu katika maandalizi ya kuwa viongozi wa kidini yametulemaza kiasi cha kutotuachia mwanya wakuhoji sisi ni watu wa kukubali, watu wa kutii, ni watu wa kukaa kimya, ni watu wa kuomba kwa kweli ukiona jambo limekuudhi nenda kaombe usipige pige kelele barabarani wala kwenye majukwaa. Hiyo sio nafasi yako ni nafasi ya watu wengine. Kwa hiyo, malezi na maandalizi ya sisi kuwa viongozi wa dini ni sehemu inayotufanya tusifanye sawa sawa kama nilivyosema katika swali lako la awali.

 

Sababu ya tatu elimu. Elimu, haya masuala ya utawala, masuala ya uongozi masuala ya jamii na hasa nyakati hizi za utandawazi wakati mwingine yanahitaji elimu dunia iwe imepanda kidogo. Kuelewa mifumo ya dunia inakwendaje, mifumo ya kitaifa inakwendaje. Kwa hiyo, uweze kuwa na maoni uweze kujenga ufahamu wa kuona kwamba hili jambo ni baya na hili ni zuri.

Kwa hiyo, nafikiri madhehebu yote bado tunao viongozi ambao, sio dhambi, lakini ufahamu wao wakuifahamu miundombinu na mifumo ya utawala uwezo wetu na ufahamu wetu ni mdogo sana. Kwa hiyo, hatuwezi kuwa na mchango sahihi unaoweza kusaidia katika kujenga jamii ya haki na demokrasia katika taifa letu. Sababu hizo tatu, kwa kweli, unaweza ukawa ni mchango wangu wa kueleza kwa nini hatujafanya vya kutosha kama nilivyoeleza katika swali jingine. 

The Chanzo: Nataka kwenye kuongezea hapo hapo kwenye sababu ulizozitaja hudhani kwamba woga, hudhani kwamba woga wa mamlaka, kwa mfano, unaweza ukawa unasababisha hali hiyo? 

Askofu Bagonza: Ukiamua kuchukua woga kama sababu ya pekee inayojitegemea siwezi kukupinga uko sawa sawa. Lakini mimi woga ningeuweka katika sababu yangu ya pili niliyoitaja, malezi na makuzi tuliyopewa katika kuandaliwa kuwa viongozi wa dini yanatufanya tulemae [na] tuwe watiifu wakati mwingine unatii uovu bila kujua na woga ni sehemu ya hiyo sababu. Lakini nakukubali, nakubaliana na sababu yako, unaweza ukaifanya isimame peke yake badala ya kuitenga. 

The Chanzo: Na kwenye hilo hilo Askofu tunafahamu kwamba wewe, kusema kweli, ni mtu ambaye una nafasi kijamii na ni mtu ambaye kusema kweli una maisha ambayo kwa wastani ni bora kuliko Watanzania walio wengi sana — kiustawi namaanisha. Ukiamua leo unaweza kuacha hizi harakati kwa sababu tunafahamu kwamba wewe ni moja kati ya watu ambao mpo mstari wa mbele katika kupigania masuala ya haki kwenye hili taifa, na ukiamua leo unaweza kuacha na kuendelea na maisha yako na hili lisiwe na athari yeyote kwenye maisha yako. Labda nataka unieleze kwa nini wewe unafanya hivyo, kwa nini unadhani sauti na nafasi yako inahitajika katika vuguvugu la mageuzi ya kisiasa kwenye nchi hii ya kujenga taifa lenye haki, lenye demokrasia. Nini nini kinakusukuma wewe binafsi kufanya hivyo?

Askofu Bagonza: Ninaweza kutaja sababu tatu. Sababu ya kwanza mimi si kweli nisipofanya ninachofanya sitaathirika. Nitaathirika kwa sababu kuongoza watu wasiokuwa na furaha, kuongoza watu ambao hawatendewi haki, kuongoza watu ambao wanadhulumiwa, sioni kama ni sawa sawa. [Wanakuja ibadani] halafu nawaambia, mwishoni mwa ibada, nendeni kwa amani, nendeni kwa amani ya bwana na kesho mrudi tuendelee na mafundisho yetu.

Biblia ninayoitumia inazuia [kufanya hivyo]. Katika waraka wa Yakobo [imeandikwa] “Kumuona mwenye njaa ukamwambia nenda kaote moto” sio sawa sawa, sio sawa sawa. Kwa hiyo, kwangu mimi kwa dhamiri yangu safi na kiapo nilichokiweka kumtumikia Mwenyezi Mungu na mwana wake mpendwa Yesu Kristo ambaye alipenda haki ili niwe mwaminifu kwa wito wangu ninafikiri ninahitaji kufanya ninayofanya. Nikiacha nitakuwa sio mwaminifu kwa wito wangu, sababu ya kwanza.

Sababu ya pili ninaweza kusema kwa namna ya pekee viongozi walionilea kidini, kijamii naweza kusema kisiasa waliniandaa. Waliniandaa kuwa mkweli [na] kutetea haki na nimeliona hili tangu nikiwa mtoto. Shule ya msingi, shule za sekondari nilikosoma, vyuo vikuu nilivyosoma hapa ndani na nje ya nchi, kote imekuwa sehemu ya maisha yangu [kupigania haki].

Kwa hiyo, kuniambia niache haya ni sawa sawa na kuniambia niache kuwa Benson Bagonza nitakuwa ni mtu mwingine. Nimekuwa hivi kwa sababu kuna viongozi walichukua nafasi kuniandaa na kunitengeneza hivi nilivyo na ndio role models wangu, moja wapo ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa hiyo, hiyo ni sababu ya pili.

Sababu ya tatu, mimi ninadhani, hata kwa Kanisa ninaloliongoza [la KKKT], likiacha kutetea haki litakuwa sio kanisa lile la Yesu Kristo Mnazareth aliyezaliwa katika maisha ya dhuluma lakini akatoa sauti kukataa dhuluma na kufundisha watu wengine kuukataa ufalme unaoanzia mbinguni. [Yesu] alisema ufalme unaanzia hapa hapa duniani. Kwa hiyo, mimi nitakosa cha kufundisha kama nikiacha haya, nitakosa cha kufundisha! 

The Chanzo: Na hapo umezungumzia vizuri kwamba hiki unachokifanya sasa hivi si kwamba umekianza jana na wala juzi ni sehemu ya maisha yako. Labda unaweza ukafafanua zaidi ya hapo labda?

Askofu Bagonza: Ni sehemu ya maisha yangu. Hivi sasa naandika kitabu. Nimeamua kuelezea historia yangu mwenyewe ninavyoifahanu kitakapotoka mtaona. Lakini, naweza kukwambia, mimi tayari nikiwa darasa la sita nilifukuzwa shule nikakaa nyumbani mwaka mzima kwa sababu tu niliandika barua kuhoji kwa nini wanafunzi wanalazimishwa kuwachotea maji walimu, kuwachanjia kuni, kuwapikia, kuwafulia, kuwalelea watoto wao.

Na nilipoandika barua [hiyo] wazazi wakaniunga mkono wakapiga marufuku lakini badae wakanigeuzia kibao mimi kwamba nimesababisha mgomo nikafukuzwa shule. Nikaendesha kesi mwaka mzima toka kijijini ilikuja kuamuliwa na Afisa Elimu wa Mkoa [na] nikarudishwa shuleni. Lakini mwaka mzima sikusoma nikiwa nimefukuzwa kwa sababu ya kutetea wanafunzi [wakati nipo] darasa la sita.

Kwa hiyo, na mengine mengi yako maushuhuda mengi sana ya maisha yangu. Lakini nilikuwa wakati ule nayafanya nikiwa tayari ni kamanda wa chipukizi wa Umoja wa Vijana wa Chama  Cha Mapinduzi (CCM) kwa ngazi ya kata mpaka wilaya na mafundisho niliyoyapata wakati ule ya uwanaharakati ndani ya Chama Cha Mapinduzi ndio yaliyonifanya nione kwamba watoto wale wenzangu walikuwa wananyanyaswa kwa hiyo nikasimama kuwatetea.

The Chanzo: Na hiyo ilikuwa mwaka gani, Askofu? 

Askofu Bagonza: Ilikuwa mwaka wa 1977 Chama Cha Mapinduzi kikiwa [bado] kichanga. Mwaka 1977 kikiwa na mwaka mmoja kikiwa kimezaliwa.

The Chanzo: Sawa sawa lakini badae ukafanikiwa kurudi shule na kuendelea na masomo?

Askofu Bagonza: Ehee badae nikarudi shule na kuendelea na masomo yangu, lakini jicho langu mahali penye dhuluma linapaona haraka sana.

The Chanzo: Asante sana Askofu, unajua katika nchi kama yetu ya Tanzania ambayo kusema kweli Serikali na chama vinakuwa na nguvu na mamlaka nyingi kuliko wananchi, kunakuwa na hatari nyingi zinazohusiana na suala zima la kusimama na wananchi na kupigania maslahi yao. Unajua tunafahamu kuna watu wamepoteza maisha kwa kufanya kazi hii, wengine wametekwa na kuteswa na kupotezwa kabisa na hatujawaona mpaka leo. Wengine wamelazimika kukimbia nchi na kwenda nchi za mbali. Nilikuwa nataka kupata uzoefu wako, kwa sababu wewe ni moja kati ya watu ambao wanafanya hiyo kazi, kwamba unaamua kusimama, na wananchi na kama ulivyozungumza mwenyewe kwamba jicho lako linaona sehemu ambapo haki ina ikakandamizwa kwa haraka sana. Ni kwa kiasi gani, kwa mfano, harakati zako zimekuathiri wewe binafsi au labda kazi au labda familia? Nafahamu kwamba kipindi fulani mwaka 2020 kuna ripoti ziliibuka, sasa sijui kama ni kweli au uongo labda utatwambia, kwamba kulikuwa kuna watu wanatishia maisha yako. Unazungumiaje athari ambazo pengine zinaweza zikawa zinatokana na msimamo wako wewe wa kupigania haki nchini hapa?

Askofu Bagonza: Unajua mwandishi labda nikueleze kitu hiki ili kiweze kukupa mtazamo wa nini kinachoendelea. Mimi nimekua na kulelewa chini ya mfumo wa chama kimoja na wakati wote wa mfumo ule chama kilishika hatamu, chama kiliisimamia Serikali, chama kilitoa maelekezo kwa Serikali na Serikali ilitii. Na katika kipindi hicho chama chetu kingesikia dhuluma mahali popote sauti yake ilikuwa inatoka haraka sana.

Kuna mtu kadhulumiwa mifugo yake, kuna mtu kanyang’anywa urithi, kuna mtu kaonewa, kuna mtu kapigwa na polisi, chama kilikuwa kinasimama haraka sana, tena kinasimama haraka sana si kwa mambo ya ndani tu hata ya nje. Mimi nimeshuhudia nikiwa kijana watu waliokuwa kidogo enzi hizo wana vihela hela wamenunua vigari wanapeleka gari kwenye ofisi ya Chama Cha Mapinduzi ilale kwamba ipo salama lakini hawawezi kulilaza hilo gari kanisani.

Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa inaaminika kuliko hata kanisa kwa msimamo wake wakutetea haki za wanyonge. Sasa mambo yamebadilika badala ya chama kuiongoza Serikali, Serikali sasa inakiongiza chama. Kwa hiyo, Serikali imeshika hatamu [na] chama kimeshikwa, chama kinachotawala. Kimsingi, mimi ninaweza kusema chama kinaitwa chama tawala hakitawali chochote kinatawaliwa na Serikali. Serikali inasauti kubwa kuliko chama kiasi kwamba chama kinakwenda kushtaki kwa Serikali kwamba jamani tunaonewa huku, mje mtusaidie.

Sasa mabadiliko hayo ni makubwa sana kisera. Ni mabadiliko makubwa sana kimfumo. Kwa hiyo, unapoanza kunieleza habari za watu sijui kutekwa, watu kuondoka nchini, zama zile chama kilikuwa kinapiga kelele kwa watu kuonewa mpaka wafikie hatua ya kutaka kufikiria kuondoka, yaani wewe ukiona Rais mstaafu [Ally Hassan] Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alilazimika kujiuzulu kwa sababu tu wafungwa fulani walikuwa kule Shinyanga wamekufa wakiwa chini ya ulinzi wa Polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani akaondoka!

Sasa, kwa hiyo, unaponieleza haya yote sijui ya watu wamepotea na nimesikia kelele za watu wengi kuhusu watu hao kupotea sijawahi kusikia sauti ya Chama Cha Mapinduzi wakisema jamani huyu ni Mtanzania mwenzetu [na] haonekani, hajulikani alipo tunataka maelezo. Serikali itupe maelezo. Kwa hiyo, kama kuna mtu kalazimika kukimbia nchi, kuna mtu kapotea haonekani, kuna mtu sijui kanyanyaswa chama tawala kinatakiwa kisimame kuihoji Serikali itoe maelezo wananchi waelewe watu hawa waliopotea wana wazazi, wana watoto, wana ndugu wanahitaji kupata maelezo.

Ni jukumu la chama tawala kiibane Serikali itoe maelezo vinginevyo kama chama hakiamini kama kweli wamepotea basi na chenyewe kidai hao wanaosema kwamba watu wamepotea wawajibishwe, wasimamishwe hapa hadharani watueleze wao wameona wapi mtu anapotea, wameona wapi mtu anatekwa, hiyo ndio haki.

The Chanzo: Na hapo hapo umegusia kwamba zamani chama ndio kilikuwa kimeshika hatamu, kwamba kulikuwa na chama tawala kweli kinachoiongoza Serikali, lakini saa hivi Serikali inakiongoza chama.

Askofu Bagonza: Kwa maoni yangu, [hayo] ni maoni yangu.

The Chanzo: Sawa sawa, na labda pengine hapa kati itakuwa kumetokezea nini mpaka hali ikawa hivyo kukatokezea hayo mabadiliko kwa mtazamo wako?

Askofu Bagonza: Mabadiliko yanaweza kuwa yapo ya aina mbalimbali lakini nafikiri badiliko kubwa lililotokea ni kwamba chama tawala, Chama cha Mapinduzi, kiliacha kuwa chama cha siasa kikawa chama dola, badae dola ikakigeuka ikaanza kukiongoza badala ya chenyewe kuiongoza. Ndio badiliko kubwa lililotokea.

The Chanzo: Na hilo lilitokea vipi labda, samahani lakini nataka tu kufahamu hilo lilitokezea vipi? 

Askofu Bagonza: Sasa ndugu yangu kwa mahojiano kama haya huwezi kupata jibu kwa sababu hilo ni suala la sayansi ya siasa. Nahitaji nipate nafasi ya kutoa muhadhara wa sayansi ya siasa nieleze jinsi ilivyotokea.

The Chanzo: Nakuelewa Askofu, nakueelewa.

Askofu Bagonza: CCM iliachaje kuwa chama cha siasa ikawa chama dola?

The Chanzo: Inabidi uje utuandalie huo mhadhara siku moja na mimi bila shaka nitashiriki.

Askofu Bagonza: Kabisa. Mimi niko tayari kujitolea kutoa mhadhara kitaifa unaoeleza mnyumbuliko huo ulioifanya CCM kutoka kuwa chama cha siasa kikawa chama dola. 

The Chanzo: Sasa labda tuendelee na hoja nyingine ili tukijaribu kumalizia malizia. Serikali kusema kweli, zaidi ya mara moja, imekuwa ikiwaonya viongozi wa dini kutokuchanganya dini na siasa. Lakini hii tunaona inatokezea pale tu viongozi wa dini wanapoonekana kupigania mambo yenye maslahi mapana kwa nchi. Kwa mfano, kama vile kuhimiza utii wa sheria na Katiba kwa viongozi, kupinga uonevu wa vyombo vya dola kwa raia wasio kuwa na nguvu nakadhalika. Lakini Serikali haioni shida kuwatumia viongozi wa dini kwenye shughuli zake, kama vile kuwaita Ikulu wakati wa hafla mbalimbali au kuwatumia kwenye kuhamasisha ile Serikali inaita amani na utulivu ambayo kimsingi ni shughuli za kisiasa. Unazungumziaje huu uwili huu wa Serikali linapokuja suala la kuchanganya dini na siasa?

Askofu Bagonza: Huo kwangu mimi umekuwa ni wimbo ambao unachosha masikio, hauna uhalisia. Kwa sababu, viongozi hawa unaosema wasiseme [au] wasijihusishe au wasitoe maoni yao juu ya mambo ya kisiasa viongozi hao hao wanatoa maoni au kufanya mambo mengine yasiyo ya dini lakini hamuwakemei.

Kwa mfano, viongozi wa dini unapotokea ukame Serikali inawaomba viongozi wa dini wakaombee mvua, mbona hamsemi viongozi wa dini wanachanganya dini na hali ya hewa? Au viongozi wa dini hawa wanajenga shule mpaka vyuo vikuu, mbona hamsemi viongozi wa dini waache kuchanganya dini na elimu? Wanajenga mahospitali mbona hamsemi viongozi wa dini hawa wanachanganya dini na afya? Viongozi wa dini hawa wakati wa balaa la njaa wanaleta misaada ya chakula kuwapa watu waliopata shida mbona hamuwaambii kwamba viongozi wa dini wanachanganya chakula na dini?

Kwa hiyo, mimi nasema ni kusema kweli ni mgongano wa kimantiki usio kuwa na faida yeyote. Siasa ni maisha ya ujumla ya watu. Ukivaa nguo umeshiriki siasa. Ukienda kulala jioni badala ya kuanza kufanya kazi umeshiriki siasa. Kwa sababu, wanasiasa hawa hawa wanaweza kuamka asubuhi wakasema kuanzia sasa watu mtalala mchana na kufanya kazi usiku na tutatii!

Kwa nini tunakwenda msikitini Ijumaa na kanisani Jumapili? Ni maamuzi ya wanasiasa. Vinginevyo wangeweza kusema kwamba kuanzia sasa siku ya kusali ni moja Alhamisi na tutatii. Kwa hiyo, tunashiriki maamuzi ya kisiasa. Tunaishi maisha ya kisiasa ukila ni siasa ukivaa ni siasa. Ukiamua kutovaa pia umeshiriki siasa!

The Chanzo: Unadhani hii, kwa mfano, hilo suala la Serikali kutaka watu wasichanganye dini na siasa linatokana na nini? 

Askofu Bagonza: Ahaaa ni kujitetea tu na kujitetea inaruhusiwa mahali popote. Hata sisi [viongozi wa dini] tukisemwa mambo yetu mara nyingi tunakimbilia kusema, “Ninyi watu, msianze kuingilia mambo ya dini fanyeni kazi yenu ya siasa.” Kwa sababu tu tumeguswa mambo yetu. Mimi naiona huwa ni uamuzi wa kawaida wala huwa hainikwazi. 

The Chanzo: Haikukwazi kabisa? 

Askofu Bagonza: Hata sisi [viongozi wa dini] huwa tuna namna zetu za kujitetea.

The Chanzo: Na unadhani haikuzuii wewe kufanya shughuli zako, unadhani haikuzuii wewe kufanya shughuli zako za kupigania haki? 

Askofu Bagonza: Hapana, hainizuii. Kwanza sio kosa la jinai kuniambia hivyo [kwamba nisichanganye dini na siasa]. Kwa hiyo, hajanitukana mtu kuniambia usichanganye dini na siasa. Hujanitukana, ni maoni yako. 

The Chanzo: Lakini muda mwingine iaenda mbali zaidi, kwa mfano kuandikiwa barua za onyo [na] kutishiwa kufungiwa.

Askofu Bagonza: Iko hivyo, inashangaza kuifanya kwa sababu haya tuliyajua wakati wa ukoloni nchi ikiwa chini ya ukoloni. Hizo ndio zilikuwa barua zinazotoka kwa Gavana kwenda kwa viongozi wa dini. Lakini sasa taifa huru miaka sitini bado tunaandikiwa barua za namna hiyo. Kwangu ni msiba wa kitaifa!

The Chanzo: Askofu nataka kukuuliza kama ambavyo binadamu tumezaliwa ni wazi kwamba kuna siku moja tutakufa na naamini kabisa kwamba kila mmoja wetu, au angalau wengi wetu, kuna vitu tungependa kuvifanikisha au kuviona vinatokea kabla ya siku zetu hazijatufikia. Nataka kufahamu kwa upande wako kama mtu ambaye, na umeeleza hapo kwenye haya mazungumzo ambayo tumekuwa nayo mpaka sasa, unapigania masuala ya haki, uko mstari wa mbele kuwasemea wananchi wanyonge na ambao hawana nguvu. Ni mageuzi gani ya msingi katika uendeshaji wa nchi ungependa kuyaona yanatokezea Tanzania wakati wa uhai wako?

Askofu Bagonza: Kwa kweli hilo swali, [ni] swali moja gumu sana. Nina tamani kabla ya kufa kwangu, kama ningefanikiwa kuona tunapata kizazi cha viongozi wanaoamini kwamba viongozi ni watumishi wa wananchi, wameajiriwa na wananchi na sio kwamba wao wamewaajiri wananchi. Kwa hiyo, natamani kuona siku viongozi wa nchi wakiwachezea wananchi ngoma na kuwashukuru na kuwaimbia shairi kuwashukuru kwamba tunawashukuru sana kwa kutupa kazi ya ajira inayotusaidia na sisi kupata ugali na watoto wetu.

Kwa hiyo, nina tamani kuona taifa langu la Tanzania kwamba tunakuwa na mfumo wa uongozi unaojali na kutetea wanyonge na ninaposema unyonge si kutetea unyonge kama ajira ya kujipatia kipato, bali kwamba msimamo wa viongozi ni kuona kwamba watu wote wanahaki sawa mbele ya sheria ndani ya taifa lao. 

The Chanzo: Asante sana Askofu, tumalizie kwa kuzungumzia kuhusu hatua yako ya kuamua kuandika kitabu kuhusu maisha yako. Kwa nini umeona hatua hiyo ni muhimu, umeona ni jambo muhimu kuandika kitabu kuhusu historia maisha yako?

Askofu Bagonza: Katika uhai wangu nimesoma vitabu vya historia za maisha ya watu ninaowafahamu na nikagundua vilivyopotoshwa, jinsi vilivyopotoshwa. Kwa hiyo, mimi natamani Mungu anipe afya niandike kitabu hiki nikimalize mwenyewe kusudi wasije watu wengine wakapotosha baadae.

The Chanzo: Wasije wakapotosha historia ya maisha yako maana yake? 

Askofu Bagonza: Ndio ndio. 

The Chanzo: Na mchakato umefikia wapi labda? 

Askofu Bagonza: Ninapanga kuchukua likizo ya miezi miwili ili nione kama naweza kukisogeza. Tayari nina sura kama mbili hivi. 

The Chanzo: Kwa hiyo, mpaka mwakani mwishoni labda itakuwa umekikamilisha?

Askofu Bagonza: Labda naweza kuwa nimekimaliza ndio na unajua watu mtu akifa wanakuwa wanafiki, wanasema mambo mazuri [tu]. Kwa hiyo, ningetamani hata mabaya yangu niandike mimi mwenyewe.

The Chanzo: Askofu Dk Benson Bagonza mimi nakushukuru sana kwa muda wako, imekuwa faraja sana kwetu sisi hapa The Chanzo kupata fursa hii ya kuzungumza na wewe na tunakutakia kila la kheri katika mchakato wako wa kuandika kitabu cha historia ya maisha yako.

Askofu Bagonza: Ahsante sana!

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *