Dar es Salaam. Katika jitihada za kupambana na magonjwa mbali mbali ya wanyama nchini, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa pamoja wamekuja na programu inayofanya kazi kwenye simu janja ambayo inarahisisha ukusanyaji na uhabarishaji wa taarifa wa papo kwa papo kuhusu maradhi ya wanyama, hivyo kurahisisha ufuatiliaji na uchukuaji wa tahadhari za mapema.
Programu hiyo inayojulikana kwa kimombo kama Event Mobile Application (EMA-i) ilitengenezwa na FAO kwa ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) na ilianza kufanya kazi kwa majaribio mnamo mwaka 2017 kwa kuanzia na watumiaji 13 kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo na Mamlaka ya Maabara ya Veterinari Tanzania kabla ya kujaribiwa kwa watumiaji wengine 23 kutoka wilaya 20 za Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FAO Alhamisi, Oktoba 7, 2021, jumla ya matukio 9,273 yanayohusu magonjwa mbali mbali ya wanyama yaliripotiwa kupitia EMA-i kati ya kipindi cha Juni 2017 programu hiyo ilipoanza kutumika na Agosti 2021. Hii ni tofauti na matukio 283 yaliyoripotiwa kati ya kipindi cha Desemba 2016 na Novemba 2017 kabla programu hiyo haijaanza kutumika.
“Kabla ya [programu hii ya] EMA-i haijaanza kutumika ilikuwa inachukua zaidi ya siku saba kwa ripoti zinazohusiana na magonjwa ya wanyama kuchakatwa,” Cainan Kiswaga, afisa mtoa taarifa na mtumiaji wa EMA-i, amenukuliwa na taarifa hiyo akisema.
Kwa mujibu wa FAO, programu hiyo imewezesha kuimarika kwa kwa utolewaji wa tahadhari za mapema kuhusiana na magonjwa ya wanyama katika ngazi ya kitaifa nchini Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba programu hiyo imeimarisha uwezo wa uangalizi na mifumo ya mawasiliano kati ya wadau husika.
“Teknolojia za habari ni nzuri sana katika kuboresha na kuimarisha uangalizi na utoaji wa taarifa,” Mkuu wa Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Teknolojia kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Baltazary Kibola amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema. “EMA-i imerahisisha na kuimarisha usimamizi na utoaji wa mapema wa taarifa zinazohusiana na tahadhari za miripuko ya magonjwa ya wanyama Tanzania.”
Lengo la FAO ni kuhakikisha kwamba asilimia 80 ya wilaya zote Tanzania zinatumia programu hii ya EMA-i katika usimamizi na utoaji wa taarifa zinazohusiana na magonjwa ya wanyama.
“Ili nchi iweze kuwa na mfumo imara na madhubuti wa uangalizi wa maradhi ya wanyama,” anasema Mkurugenzi wa Huduma za Veterinari kutoka Wizara ya Uvuvi na Mifugo, “Wadau wote, hususani maafisa waliopo field, lazima wahakikishe kwamba taarifa zinazohusiana na magonjwa ya wanyama zinakusanywa vizuri kulingana na dalili na ishara zinazoonekana na kuripotiwa kwa wakati.”