The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Afya ya Akili: Ushuhuda wa Mhanga na Mapambano ya Kupata Matibabu

Uelewa wa tatizo la afya ya akili Tanzania bado ni mdogo, wengi huhusisha tatizo hilo na imani za kishirikina.

subscribe to our newsletter!

Kwa majina naitwa Monica Isaya, ni mzaliwa wa Dodoma. Mimi nilizaliwa mwaka 1984 nikiwa mzima wa afya lakini nipofikisha umri wa miaka 19, wakati huo nikiwa kidato cha tatu, ghafla nilipatwa na matatizo ya afya ya akili. Hali hii ya matatizo ya afya ya akili ilinisababishia mimi kushindwa kumaliza elimu yangu ya kidato cha nne.

Nakumbuka siku ambayo nilipatwa na matatizo ya afya ya akili nilikuwa darasani, wenzangu wakashangaa tu baada ya mimi kudondoka kutoka kwenye kiti na kuanguka chini, nikiwa najipiga kichwa changu chini kwenye sakafu, unaweza kusema ilikuwa nikama nimepatwa na kifafa hivi. Waliwaita walimu kuja kuniangalia. Walimu walichokifanya waliita gari la wagonjwa kwa ajili ya kunipeleka hospitali kwa matibabu zaidi.

Nilipofika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambako ndiko nilikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu, nikafanyiwa vipimo kama kawaida lakini chaajabu ni kwamba madaktari walisema sina tatizo lolote.

Baada ya kuambiwa kuwa sina matatizo yoyote, nikaruhusiwa kurudi nyumbani. Lakini hali yangu iliendelea kuwa vilevile. Mimi nilikuwa najiona kabisa siko sawa halafu hospitali wanasema sina tatizo. Kwani licha ya kwamba nilikuwa na tatizo, muda mwengine akili zangu zilikuwa zinanirudia kwani nilikuwa natumia madawa.

Safari ya kwenda mirembe

Kutokana na hali yangu kuendelea kuwa mbaya, baadaye madaktari waliwashauri wazazi wangu wanipeleke Hospital ya Taifa ya Mirembe iliyopo hapa Dodoma kwa ajili ya kupata matibabu zaidi. Ni kweli walinipeleka Mirembe ila kukawa na changamoto kubwa kwa upande wangu, kwa sababu mbali na kuwa nilikuwa nikitumia dawa za hospitali wazazi wangu, na wale waliokuwa wanakuja kuniona, waliniambia kwamba ni bora niende kwa waganga wa kienyeji.

Wakati mwingine wananiambia niende kuombewa. Unajua tena mtu ukiwa na shida yaani unakosa cha kufanya, unakuwa huna maamuzi binafsi namaanisha. Inakuwa ni kusikiliza tu kile ambacho unaambiwa kwa wakati huo ili tu upone.

Wakati huo haikuwa rahisi kwa mimi kujua cha kufanya, hivyo familia  yangu iliamua kunipeleka  kwa waganga wa kienyeji ili nipone tatizo ambalo lilikuwa linanisumbua. Nilikuwa nikianza kupata nafuu wanasema nikaombewe. Nikija tena hospitalini wananiambia haya madawa yanasababisha uwe zezeta zaidi. 

Wakati mwingine walikuwa wakiniambia kuwa dawa ambazo nilikuwa natumia niachane nazo kwa sababu nitakuwa chizi zaidi, nitaanza kutembea uchi na nitakuwa sitamaniki. Walivyoniambia hivyo nikawa natumia dawa za hospitali kidogo huku natumia dawa zinazotoka kwa waganga wa kienyeji kwa wingi.

Kama unavyojua ukianza kuchanganya dawa mara huku za hospitali mara za kwa waganga wa kinyeji kiukweli huwezi kupona na ikawa inanipa wakati mgumu zaidi mimi mwenyewe. Pamoja na kwamba hali yangu ya kiafya iko imara lakini bado naendelea kutumia dawa.

Kuharibika kwa mahusiano

Watu wenye matatizo ya afya ya akili tunakumbana na changamoto nyingi sana. Mimi ni mama mwenye watoto watatu. Nakumbuka katika kipindi kirefu cha hali yangu nilikuwa nikiishi na mume wangu, lakini baada ya kuona hali yangu ya matatizo yamezidi alinikimbia akaniacha nikiwa na watoto wawili huku na mimba.

Mume wangu alinioa nikiwa na matatizo haya ya akili lakini sasa ilifika mahali alishindwa kunivumilia akaamua kuniacha. Maana hata ndugu zake walianza kumwambia kwamba mwanamke mwenyewe ana matatizo ya akili. Nikawa nashindwa sasa nifanyaje na tangu wakati huo alivyoondoka sijawahi kuwa na hamu ya kuwa na mwanaume yeyote yule nilimuomba Mungu anisaide.

Nilipambana na mengi sababu pamoja na kwamba nilikuwa na matatizo hayo mama yangu mzazi ilifikia mahali alikuwa akininyanyapaa. Alikuwa akiniona mimi kama si chochote na sina mchango wowote ule.

Nakumbuka wakati niko nyumbani mama yangu alikuwa akirithisha viwanja. Sasa kutokana na hali yangu ile aliamua kumrithisha kaka yangu mimi akaniacha.  Nilipojaribu kumuambia kwa nini mama unafanya hivyo unampa mtoto mmoja, akaniambia mimi ni chizi wa Mirembe.

Kuna changamoto nyingine ambayo tunakutana nayo watu wenye matatizo ya afya ya akili. Dharau na kunyanyapaliwa ni vitu ambavyo vinatukumba. Inafikia wakati unanyimwa hata nafasi ya kuonana na viongozi wakubwa. Nakumbuka mwaka jana [2020] watu wenye matatizo ya afya ya akili tuliomba mkopo lakini wakasema hawa machizi nao tukiwapa mkopo watarejesha. Kwa hiyo, ikawa shida.

Kitu kinachoniumiza zaidi ni ile hali ya kutengwa na jamii kutokana na hali  yangu, yaani wakati mwingine jamii inawaona watu wenye matatizo haya ni kama watu tusiofaa na tuliokosa thamani. Niseme tu watu ambao wako vizuri na hawana matatizo haya wanapaswa  kutambua kuwa sisi ni kama wao.

Ombi langu kwa Serikali ni tukipata dawa, dawa zikawa zinagawiwa bure, zikawa zinapatikana kila sehemu itasaidia sana. Maana dawa zikipatikana kila sehemu sisi ambao tumeshapona tutawashawishi wale wenzetu kwamba wakitumia dawa watapona. 

Monica Isaya amesimulia kisa hiki kwa mwandishi wa The Chanzo mkoani Dodoma Jackline Kuwanda. Unaweza kumfikia Jackline kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na simulizi hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *