Mtanzania Afariki Marekani Baada ya Kushambuliwa na Risasi

Familia inafanya utaratibu wa kumsafirisha kuja Tanzania kwa ajili ya mazishi.
Na Mwandishi Wetu20 October 20213 min

Dar es Salaam. Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Humphrey Magwira ameuwawa huko Marekani katika mjini wa Houstan, Texas baada ya kushambuliwa na risasi kufuatia kile polisi jijini humo wamesema ni shambulio la risasi baada ya kijana huyo aliyehamia Marekani akitokea nchini Tanzania na familia yake kusababisha ajali ya barabarani.  

Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Fort Bend amenukuliwa na tovuti ya habari ya Tri-City Herald akisema kwamba Mghwira, 20, alifariki katika hospitali iliyokuwa karibu na eneo la tukio baada ya kupata mashambulizi mengi ya risasi mwilini mwake.

Humphrey Magwira, Mtanzania aliyeuwawa na risasi katika mji wa Houston, Texas nchini Marekani.

Tayari polisi katika mji wa Houston wanamshikilia mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Ramon Vasquez anayedaiwa kuhusika na mashambulizi ya risasi dhidi ya Maghwira na kusababisha kifo chake. Polisi wanadai kwamba Vasquez alitoka kwenye gari yake na kwenda kumshambulia Magwira.

Vasquez anadaiwa alikimbia kutoka kwenye eneo mauaji lakini polisi walifanikiwa kumkamata Jumamosi, Oktoba 16, 2021, Fort Bend polisi walisema.

“Tukio hili la kusikitisha la mauaji ya holela lilitokana na gari kugongana kwa bahati mbaya,” Mkuu wa Polisi Eric Fagan ameiambia Tri-City Herald. “Dua zetu zinaenda kwa familia ya mhanga na polisi wetu wanaendelea na kazi yao kwenye kesi hii.”

Ramon Vasquez, kijana wa miaka 19 anayeshukiwa kumuua Humphrey Magwira kwa kumpiga risasi. PICHA | ABC13

Magwira alikuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya uhandisi wa kompyuta katika Chuo Kikuu cha Houston. Familia yake ilihamia Marekani wakati yeye akiwa na umri wa miaka 11 tu.

Akimueleza mtoto wake kwa tovuti ya habari ya Click2Houston, mama mzazi wa Maghwira Josephine Kuyangana amesema mtoto wake huyo alikuwa “mtoto mzuri.” Kuyangana amesema: “Siamini kama ametutoka. Alikuwa rafiki yangu. Imekuwa ni ngumu sana kwa familia, kama mama, unajua [kukubaliana na ukweli kwamba ametutoka].”

Baba mzazi wa Magwira, Exuperius Magwira, ameiambia Click2Houston kwamba kijana wake alikuwa hodari na mwenye bidii. Amesema: “Tulidhani ni wazo zuri kuhamia [Marekani] kwa ajili ya kuwapatia vijana wetu elimu iliyo bora. Lakini [kutokana na tukio hili] hali haiko hivyo sasa.”

Exuperius amesema imekuwa ngumu sana kwake kukubaliana na ukweli kwamba kijana wake amefariki, akisema: “Imekuwa ngumu sana kwangu. Sijaweza kula tangu nipate taarifa za tukio lenyewe. Ni ngumu kwa mimi kula kitu chochote. Ni ngumu kwangu hata kulala.”

Kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha usafirishwaji wa Humphrey Magwira kuja Tanzania kwa ajili ya mazishi. PICHA | SCREENSHOT YA UKURASA WA GOFUNDME

Familia ya Maghwira imepanga kumsafirisha marehemu kuja Tanzania kwa ajili ya shughuli za mazishi. Tayari kampeni ya uchangishaji fedha kwa ajili ya mchakato huo imeanza kwenye mtandao wa GoFundMe ambapo mpaka kufikia majira ya 4:41 leo, Oktoba 20, 2021, jumla ya dola za Kimarekani 24,488, ambazo ni sawa na Sh56,444,840, zimekusanywa.

Kampeni hiyo pia inaendeshwa kwa njia ya mitandao ya simu kwa ajili ya watu wanaoishi Tanzania ambapo mtu anayejisikia kuchangia anaweza kufanya hivyo kupitia TigoPesa 0715 447 436 na M-Pesa 0754 447 436. Jina ni Janet Kuyangana.

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved