The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tito Magoti Amdadisi Jenerali Ulimwengu Nafasi ya Wananchi Kudhibiti Viongozi Wao

Ulimwengu anasema Katiba Mpya ni muhimu kwani itawaokoa watu na upigaji ramli katika uendeshaji wa nchi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mnamo Oktoba 16, 2021, wanaharakati, wanasiasa, na wananchi wengine wa kawaida kutoka maeneo mbali mbali nchini Tanzania walikusanyika jijini Mbeya kusikiliza mhadhara kutoka kwa mwanaharakati, mwandishi wa habari, na wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Jenerali Ulimwengu, ambaye yuko katika ziara maalum ya kutangaza kitabu chake kipya cha Rai ya Jenerali kilichotoka Septemba 2021. 

Mhadhara huo ambao ulifanyika chini ya mwavuli wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ulijikita katika kuangazia suala zima la madai ya wananchi juu ya Katiba Mpya katika muktadha wa nini wananchi wanaweza kufanya kushinikiza Serikali yao kuwapatia nyaraka hiyo muhimu katika uongozaji wa nchi pamoja na suala zima la wananchi kusimamia na kuwawajibisha viongozi wao.

Mhadhara huu uliendeshwa kwa njia ya maswali na majibu ambapo Tito Magoti, Afisa Programu kutoka LHRC, ambaye mnamo Disemba 2019, akiwa na mwenzake Theodory Gian, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na kuachiwa mnamo January 2021, alikuwa akimuuliza Ulimwengu, mbunge na mkuu wa wilaya mstaafu, kuhusiana na masuali mbalimbali. The Chanzo ilikuwepo wakati wa mazungumzo kati ya watu hawa wawili, na ifuatayo ni sehemu ya mazungumzo hayo:

Tito Magoti: Tuko hapa [Mbeya] kwa ajili ya [kuitambulisha] Rai ya Jenerali na nimekwisha kutambulisha [kwenye utangulizi wangu]. [Lakini] mtu ambaye hajui chochote kuhusu Rai ya Jenerali, mtu ambaye hajui chochote ama hajui kitu chochote ategemee nini akisikia Rai ya Jenerali kwamba kuna rai gani? Kuna mwito gani? Ama ni nini? Ni nini ambacho ni shabaha ya Rai ya Jenerali

Jenerali Ulimwengu: Asante sana wakili Tito Magoti na asanteni ndugu zangu wa Mbeya kwa kunipokea leo hii na kunipa nguvu kwa kutaka nije kuongea nanyi kuhusu hiki kinachoitwa Rai ya Jenerali. Napenda kuwashukuru sana na nadhani mmeelezwa nini kilitokea mpaka kazi iliyokuwa ifanyike asubuhi inafanyika mchana kwa kadri ambavyo waandaaji wa shughuli hii walivyoitengeneza. 

Nimetakiwa nieleze Rai ya Jenerali ni nini? Jenerali ni mimi, kwa hiyo Rai ya Jenerali maana yake ni rai yangu mimi, ambayo ni safu ya maandiko yaliyojitokeza ikiwa mimi mwenyewe ndio mwandishi katika miaka tangu mwaka 1993 hadi miaka michache iliyopita katika magazeti, kwanza katika gazeti la Rai, Nguvu ya Hoja na baadae katika gazeti la Raia Mwema.

Haya ni maandiko ambayo niliyafanya tangu wakati huo nilioutaja, kila wiki takribani. Kuna siku nilikuwa nimeugua, kuna wiki nilikuwa nimesafiri, na intaneti ilikuwa bado haijatufikia sisi ikawa ni vigumu lakini takribani kila mwaka tangu mwaka 1993 hadi mwaka nadhani 2016 hadi mwaka 2017 nilikuwa na utamaduni na mazoea na shughuli ya kuandika makala moja ya Kiswahili, mengine katika Kiingereza, lakini kwa Kiswahili angalau jina la makala hiyo, jina la safu hiyo katika Kiswahili ilikuwa ni Rai ya Jenerali, na ya kwanza ilitoka mwaka Novemba 4, 1993, kama sijasahau.

Na hii ilikuwa ni safu ambayo ilikuwa ni sehemu ya gazeti hilo nililolitaja la Rai, Nguvu ya Hoja ambayo nilitaka kuwapa huduma Watanzania [kupitia] gazeti la Kiswahili ambalo linajichukulia kwamba lenyewe ni gazeti makini, linaandika mambo makini, kwa ajili ya wasomaji makini. Tukakataa kimsingi dhana ya kwamba katika shughuli hii ya magazeti unaweza vilevile ukachagua [au] ukateua kuwa ni gazeti la kufurahisha watu, la kupiga gumzo, la kusogoa na kuandika mambo ya umbea, sio umbeya kama wa mji huu, [hadhira inacheka] lakini umbea tu na udaku na vitu kama hivyo. Maana yake awe anauza sana.

Yaani magazeti [ya udaku] yanauza sana na kwa bahati mbaya watu wengi katika nchi hii wanapenda magazeti hayo ambayo hayamfanyi mtu afikiri sana, yatachekesha labda yataliwaza watu fulani na kuwaumiza wengine, lakini tukajikita katika kuandika gazeti ambalo ni makini tulidhani, na linaandika mambo makini, waandishi wake ni makini na yanaelekezwa kwa watu na wasomaji ambao ni makini, ambao wanaweza kufikiri kwa kina juu ya masuala wanayoandikiwa na labda kuchukua hatua kama raia, wananchi na wanajamii kurekebisha na kuboresha maisha yao kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kadhalika.

Sasa hizi ni makala hizo. Sasa hizi makala zinazoonekana katika kitabu hiki ambayo imeandikwa juzuu ya tatu, ni makala zilizochapwa mwaka 1996 tu, maana yake ni makala za mwaka mmoja tu, tangu Januari mpaka Disemba. Na kwa sababu kwamba zilitoka mwaka 1996 ilikuwa hakuna njia ya kuepuka kwamba lazima zingekuwa zimejadili Uchaguzi Mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi vya siasa mwaka 1995.

Kwa hiyo, makala zote hizi mwanzoni kabisa ukiangalia zinazungumzia mwaka jana tumefanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi baada ya kuwa kuna chama kimoja tu cha siasa je, hali ilikuwaje mwaka jana? Tulifanya uchaguzi, tulijiandaa vipi na shughuli za kampeni na kadhalika ziliendeshwa vipi? Je, tunaridhika nazo? Au haturidhiki nazo na kama kuna maboresho basi yafanyike katika maeneo gani, lazima hayo maboresho yafanyike, wiki hadi wiki kwa mwaka mzima 1996.

Hiyo ndio Ilikuwa mada kuu ya makala zilizoandikwa chini ya hiyo safu Rai ya Jenerali, ikiwa na maana kwamba hizi ni rai zangu mimi, Jenerali Ulimwengu, na haya mawazo ni ya kwangu, ingawaje sikuyabuni mimi mwenyewe, lazima nilijifunza mahali lakini mimi ndio nachukua uwajibikaji wote. Kama kuna makosa katika fikra zangu au katika uandishi wangu, kuna udhaifu, basi ndio nakubali kwamba ni yangu.

Sasa ukiacha masuala ya uchaguzi wa mwaka 1995, vilevile kuna makala fulani ni chache zaidi zinazohusu masuala kadhaa. Kwa mfano, masuala ya elimu tunayowapa watoto wetu na vijana wetu. Kwa mfano, masuala ya Kiswahili na umuhimu wa kuwa na lugha ambayo inafundisha maarifa kwa watoto wetu ambayo wao watoto na walimu wanaowafundisha wanaielewa dhidi ya hii hali ambapo tunatumia lugha katika kufundisha watoto wetu ambayo watoto wao hawaijui, hawaielewi, baba zao na mama zao hawaijui, hawaielewi, hata walimu wanaowafundisha hao watoto hawaijui hiyo lugha na wala hawaielewi, lakini tumeing’ang’ania tu lazima wasome kwa Kiingereza. Kiingereza hakitutaki lakini sisi tunakipenda sana.

Ukiacha hilo sasa kuna mambo yalijitokeza hapa mwaka 1996, lingine ni mwaka huo huo ilizama meli ya MV Bukoba na hiyo ilinikuta njiani nilikuwa naandika ilivyotokea. Kwa hiyo, kwa kila wiki kuandika makala ile ile, safu ile ile lazima utagusia MV Bukoba, kwa hiyo kuna makala mbili au tatu ambazo zinahusiana na MV Bukoba.

Lakini kwa ujumla wake wote hizi makala na hiki kitabu na hii rai ya mwaka 1996 ilijikita sana katika suala la Katiba. Wala hatuzungumzii Katiba Mpya. Mimi sitaki kuzungumzia Katiba Mpya. [Ninazungumziaa] Katiba tu kama utaratibu ambao umeweka sheria, kanuni, kinachoruhusiwa, kisichoruhusiwa, makatazo yake, nini kinatakiwa kifanyike kama utaratibu wa kuendesha nchi.

Na ninasema katika utangulizi [wa kitabu hiki] kwamba umuhimu wa Katiba ni kwamba ukiwa na Katiba ambayo wananchi wamechangia katika kuizungumza na kupata maudhui yake unaondokana na ulazima wa kupiga ramli. Sijui kama tunaelewana. Maana hapa [ukumbini] kuna Wanyakyusa, Wasafwa [na] watu chungu nzima kutoka maeneo haya [ya Mbeya]. Ramli ni kama-, nadhani hata Kinyakyusa-, [kwenye] Kinyakyusa inaitwaje ramli? Mnyakyusa safi nani hapa? Ramli kinyakyusa ni nini? [Hadhira inasema,] “Alagwile.”

Kwa hiyo, ukiwa na Katiba, ukiwa na utaratibu ambao unajulikana na wananchi wote kwamba hivi ndivyo huwa tunafanya mambo yetu, huna haja ya kwenda kupiga ramli. Unajua, yaani nafasi imetokea mahala fulani labda ya uongozi wa kijiji, sio mnakwenda tena kupiga madogoli na kucheza na kuimba usiku kucha, [mkiwa na Katiba] mnajua nini mnafanya. La si hivyo mtapiga ramli kila siku ili kujua sasa miungu wanasema nini? Na mizimu yenu inakwambieni nini?

Na suala hili nadhani kwamba limekuwa na miangwi mingi sana nchini [Tanzania] na wakati mwingine miangwi hii haina siha, haina afya njema kwa taifa kwa sababu inakuwa kidogo ni yenye sumu mpaka imefika mahala mtu akitaka kuzungumza juu ya Katiba watu wanasema utakamatwa, unazungumza juu ya Katiba [utakamatwa]. Sasa hivi nazungumza juu ya Katiba kwa sababu najua kwamba hiyo ndio njia peke yake ambayo inakufanya uwe na uhakika mambo yako yatakwenda vizuri kwa sababu hutegemei kwenda kupiga ramli ndio ujue nini kitatokea. Asante sana, comrade Tito. 

Tito Magoti: Asante sana kwa utangulizi mpana na bila shaka tumejua sasa Rai ya Jenerali ni nini hasa. Umezungumza mambo kama manne ambayo yamekaa kichwani kwangu, umezungumza watu, kwa maana ya wananchi …

Jenerali Ulimwengu: Sikuamua kuandika hizi makala kwa sababu nilipenda tu kuandika. Ni kwa sababu kuna mambo ambayo bila shaka tunavyoishi katika jamii tunajifunza, tunayaona na tungependa kuyajadili ili tupate maoni ya watu wengine. Inawezekana hilo ninalolifikiri mimi leo hilo hilo ninalolifikiriwa na watu wengine na labda nikitoa maoni yangu, nikitoa mawazo yangu inaweza nikaibua mijadala na watu wakanisaidia kwa kunikosoa [au] kwa kuniunga mkono. Lakini tuchangie kwa pamoja hali ya nchi yetu au jamii yetu hapo hapo tulipo.

Hata kama ni kijijini, hivi tulime kwa mtindo gani inawezekana wewe unavyofikiri kwamba ni kilimo bora sivyo anavyofikiri mwenzako. Kwa hiyo, ni bora mawazo yako juu ya shughuli hiyo ya kilimo kama ni kilimo yajulikane kwa wengine na wao waweze kuchangia hayo mawazo yako. Wanaweza kuwa na mawazo mbadala au wakaboresha mawazo yako. Hali ya kisiasa, kama nilivyosema, ni kwamba mwaka uliotangulia, mwaka 1995, tulikuwa tumekuwa na uchaguzi wa kwanza, Uchaguzi Mkuu wenye kushirikisha vyama vingi vya siasa, baada ya uamuzi uliopitishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukubali mapendekezo yaliyokuwa ndani ya Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali.

Sasa ilikuwa ni kuondoka katika mfumo mmoja wa kisiasa kuingia katika mfumo mpya wa kisiasa ambao tulikuwa tumeusahau kabisa na jinsi gani ambavyo tulichakarika kufanya kazi ili mfumo huo uweze kufanya kazi. Hali katika Afrika ilikuwa imebadilika, nchi nyingi ndani ya Afrika zilikuwa zimeona umuhimu wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi wakati ambapo zamani walikuwa wamezoea mfumo kama sisi mfumo wa chama kimoja, chama kimoja ambacho ndicho kinaelekeza kila kitu kwa wanawake, kwa vijana, kwa watoto wa shule, kwa timu za mpira, kwa vyama vya wafanyakazi na kadhalika, ni chama kimoja.

Sasa kuondoka huko na kuingia katika mfumo mpya mwaka 1992 kuendelea mpaka 1996 ambayo ndio naiandika hii haikuwa kazi rahisi na hata leo haijawa kazi rahisi kwa sababu mazoea wanasema Waswahili yana tabu. Kwa hiyo, kukawa kuna kusuguana kwingi, kuna kutoelewana kwingi, kuna kusukumana sukumana kuna kukataa kwa wana CCM waliokuwa wengi wanasema hivi wanataka kuleta vyama vingi halafu sisi tuende wapi?

Ikasaidia kwamba alikuwepo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, [alikuwa] bado yupo hai na akasaidia sana kwa uzito aliokuwa nao na sauti nzito aliyokuwa nayo kusukuma sukuma ili watu wakubali kwamba bora alivyosema kwamba ukiona mwenzako ananyolewa [kichwa] chako tia maji la si hivyo utanyolewa kavu kavu. Kwa hiyo, kulikuwa kuna ukinzani, kuna ugumu wa kukubali dhana ya kuwa na vyama vingi.

Mimi katika kitabu hiki nakosoa dhana ya vyama vingi kwa sababu nadhani kwamba tunachohitaji si wingi wa vyama ila ni ubora wa fikra za wananchi wote zilizopewa uhuru wakusambaa na kuzungumzwa na wananchi walio wengi. Lakini, tukakubali mfumo wa vyama vingi na tukaanza kuutekeleza vivyo hivyo wakati mwingine shingo upande kwa sababu kuna wakuu ndani ya CCM hawakupenda kabisa dhana ya vyama vingi lakini wakalazimishwa waende vivyo hivyo tu.

Sasa hali haijabadilika sana. Kwa wale ambao wanajua mwaka jana tulikuwa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020. Huu ulikuwa ni Uchaguzi Mkuu nadhani wa nne tangu mwaka 1995, wanajua jinsi ambavyo uchaguzi ulivyofanyika hata hapa mjini Mbeya au kwingineko na matatizo ambayo yalijitokeza ambayo bila shaka yatakuwa ni sehemu ya majadiliano yatakayokuja katika vikao vingine vya huko mbele, sasa tumekuwa tukijadili Rai ya Jenerali ya mwaka 2020 au 2021.

Kwa hiyo, hali ipo hiyo ni tete bado kwa sababu kuna kitu kinaitwa mfumo wa vyama vingi lakini kiuhalisia hakuna lolote linalofanyika linaloonesha kwamba kuna mfumo wa uhuru, kuna uhuru wa kisiasa wa kujadili namna gani tujiendeshe sisi wenyewe kama ni wanasiasa ama, ni akina mama, ama ni vijana, ama ni wasanii, ama ni wafanyakazi na kadhalika. Kwa hiyo, hayo mapambano bado yanaendelea, hiyo misuguano bado inaendelea na sidhani kwamba itaisha hivi karibuni. 

Tito Magoti: Lakini kwa nini unafikiri kwamba tumekuwa hatupigi hatua, kwa maana kama tunaendelea kusuguana labda hatupigi hatua ama tumekuwa tukisuasua kukubaliana katika mambo yanayotuhusu, hususani hayo yanayotugawa ama yanayogawa fikra zetu. Kwa nini? 

Jenerali Ulimwengu: Ni kwa sababu mifumo ya kijamii haiendi kama unavyowasha taa na kuzima. Unaposema kwamba twende hivi na watu wakakusikia kuna wengine ndani ya hao watu wanaokusikia wanasema kwamba kwa nini twende hivi, kwa nini tusiende hivi? Katika kubishana na kulumbana ndipo unapopata mwelekeo wa kuchukua. Nadhani kwamba kama huna uongozi ulio thabiti mnaweza mkakwama hapo hapo mlipo wala msipige hatua.

Kwa mfano, mwaka 1992 mtu aliyekuweko katika uongozi wa nchi alikuwa wala hana cheo cha Serikali, Julius Kambarage Nyerere wakati ule alishastaafu kama Rais wa Jamuhuri tangu mwaka 1985 na mwaka 1990 alishastaafu kama Mwenyekiti wa CCM. Lakini akathibitisha jambo jingine kubwa kwamba uongozi sio ofisi wala sio cheo. Unaweza kuwa ni kiongozi bila kuwa na cheo chochote na bila kukalia kiti chochote katika ofisi. Kwa ile nguvu yake na uzito wake tu kama mtu wa kihistoria wa nchi hii ulikuwa unampa nguvu ya uongozi Julius Nyerere ambayo hata Rais wa Jamuhuri alikuwa hana.

Na hiyo ndio inathibitisha kwamba kuwa kiongozi ni wewe mwenyewe hulka yako, haiba yako, ushawishi wako si lazima uwe na ofisi. Uongozi ni wewe mwenyewe maono yako, sifa zako, haiba yako, kukubalika kwako miongoni mwa jamii. Na kwa bahati mbaya, tumekuwa na nakisi kubwa sana ya sifa hizo za uongozi. Tuna watu ambao badala ya kuwaita viongozi ni maofisa tu wanashika ofisi kwa sababu ama wamechaguliwa na wananchi wakawakabidhi ofisi, ama wameajiriwa bila kuchaguliwa, wameteuliwa na wakawa wanakalia ofisi.

Lakini ni wachache miongoni mwao ni viongozi wa kweli kwa maana ya kwamba ni watu wenye maono na wako tayari kujitolea kuonesha njia. Maana yake uongozi ni kuonesha njia. Sasa, haiwezekani kwamba kiongozi yeye mwenyewe bado anatafuta njia hiyo ya kuwaonesheni hajaipata halafu mmeshambandika cheo cha uongozi. Kwa hiyo, anakubabaisheni na mwisho mnajikuta mmekwama. Tumekwama mpaka leo na ukiangalia ukisoma makala zilizomo katika kitabu hiki [cha Rai ya Jenerali] utaona kwamba mambo ambayo nilikuwa nikiyazungumza mwaka 1996 bado ni yale yale wala hatujapata mwanga mkali zaidi kuliko tuliokuwa nao katika kipindi hicho. Hii ndiyo nakisi ya uongozi [ninayoizungumzia]. Tuna watawala wengi lakini viongozi ni wachache na walio wengi ni dhaifu. 

Tito Magoti: Unasema kwamba tumebaki tukisigana, tumebaki tukiwa hatukubaliani katika kutengeneza mifumo ambayo itatengeneza muskatabali mzuri wetu kama taifa na umesema kwamba pamoja na mambo mengine kuna shida ya uongozi tumekuwa na watawala kuliko viongozi, tumekuwa na nakisi, [ya] uongozi. Unapima vipi nafasi ya wananchi wakati huo na wakati huu kwamba unaweza ukahusianisha vipi kwamba kama wakati ule tulikuwa na- …

Jenerali Ulimwengu: Wananchi matarajio yao ni makubwa sana na kila wakati wanapoitwa wafanye maamuzi huwa wanapata ari mpya kwamba labda sasa hivi tutapata nafuu katika mambo yanayotusibu na matatizo yaliyotuelemea na hapa leo tunapata tamaa kwamba tukimchagua huyu kama diwani wetu, au huyu kama mbunge wetu au huyu kama Rais wetu, mambo yetu yatakwenda vizuri zaidi kuliko yalivyokuwa yanakwenda kwa muda wa miaka thelathini au thelathini na tano iliyopita.

Na kila siku tunajikuta kwamba tunarudi pale pale. Wananchi wanakatishwa tama, wanavunjika moyo kwa sababu kila wanapokwenda kuchagua mambo ni yale yale. Hao wanaoitwa viongozi wanakuwa ni kundi jingine tena la watawala ambalo halijui linafanya nini na wengi wao wanawapotosha wananchi kwa kuingia madarakani au katika uwakilishi kama ni wabunge au madiwani au hata marais kwa kuwaambia wananchi kwamba nichagueni mimi nitakuleteeni maendeleo, ambayo ni uongo na wananchi kweli wanapiga kura wakiamini kwamba huyo wanayempigia kura atawaletea maendeleo.

Sasa, kama vile maendeleo labda ni karanga hivi [au] njugu unanunua sokoni unapeleka nyumbani au ni maharage au ni mchele umekwenda Kyela ukanunua mchele mzuri ukaleta nyumbani ili wapike. Maendeleo si bidhaa. Maendeleo hayawezi kuletwa na mtu au kikundi kimoja kidogo cha watu kuwaletea wananchi. Maendeleo ni mchakato ambao wananchi wenyewe wanajifanyia kwa kuongozwa na kushauriwa labda na viongozi mahiri wenye maono na mawazo ya kisasa na yaliyokuwa na nishati ya kutosha kuwasukuma wananchi ili wao wenyewe, kwa kushirikiana, wajiletee maendeleo.

Haiwezekani kwamba mtu ni mimi ndiyo naomba nichagueni [nikisema] nitakuleteeni maendeleo kama vile atakuja na mafurushi kama kumi hivi ya maendeleo halafu awe anawagawia, haiwezekani kabisa. Na ndio umuhimu sasa suala hili la Katiba tunalolizungumza. Wala sizungumzii juu ya mgawanyo wa madaraka kati ya Rais na Bunge na Mahakama na nini. Nasema katika mchakato mzima wa wananchi kujiletea maendeleo wao wenyewe ni namna gani watakuwa wamejipanga ili mawazo yao yachakatwe kusababisha maendeleo yatokee katika jamii yao. Na [wanasiasa] waache huu wimbo wa kuwaletea maendeleo [watu] kwamba mimi mkinichagua nitakuleteeni maendeleo.

Halafu kuna kichekesho kimoja ambacho ni kichekesho ambacho wala hakihitaji kucheka kwa sababu kinaumiza. Kwamba huyo huyo anayesema nichague nikuletee maendeleo huyo huyo anakuja na hela za kukuhonga wewe ili umchague akuletee maendeleo ambapo anakufanya kama zuzu wa aina fulani. Hivi akija kijana nyumbani kwako akasema, “Mzee nimesikia kwamba hapa una bustani nzuri na mimi ni hodari katika kutengeneza bustani, nitaitengeneza itang’aa kuliko bustani zote za mji wa Mbeya.” Ukasema, “Sawa hebu nitengenezee bustani hiyo.” Halafu, akarudi mchana huyo kijana ambaye anakuja kuifanyia kazi ya kulima bustani akakupa Sh50,000, akakuambia, “Mzee kabla sijaanza kufanya kazi yako Sh50,000 hii kapate soda mahala.” Utamuajiri bado huyo kijana? Sasa mbona wale wale wanakuja wanasema niajirini mimi nikuleteeni maendeleo bado wanakuhongeni hela na mnapokea hizo hela ili muwaruhusu wakufanyieni kazi? Nyie ni wendawazimu!

Tito Magoti: Lakini Mzee Ulimwengu, umetusema sana wananchi tunahongwa ahadi na maneno na sisi tunaingia kingi [au] tunaingia mkenge. Mimi nilitaka tuangalie kidogo hawa wananchi ambao wanahadaika katika maamuzi, wanahadaika wanaingia mkenge na baadae tunakuwa na viongozi ambao ni dhaifu. Kuna nafasi gani, ama hakikishio gani, la kikatiba – kwa sababu wewe ni mwanasheria pia ni wakili, ni mwandishi mkongwe [na] umekuwa kiongozi, mbunge, umekuwa mkuu wa wilaya, wewe ni raia mashuhuri wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania – kuna fursa gani za kikatiba za wananchi kuamua kujisimamia na kuhakikisha kwamba kile wanachoamua, ama kile wanachokipenda, ndicho kinachotokea? 

Ukichukulia mfano ushiriki wa wananchi katika uchaguzi, kwa maoni yangu mimi, chaguzi nyingi zimekuwa geresha – ukiachana na mazingira magumu ya upatikanaji wa viongozi, namaanisha ukiachana na hizo hadaa wanasiasa wanazozifanya – mimi naamini chaguzi nyingi zimekuwa geresha kutokana na mifumo iliyopo. Yapi ni maoni yako kuhusu nafasi ya wananchi kushadadia kile wanachokitaka? 

Jenerali Ulimwengu: Wananchi nafasi yao wala haijabadilika, wananchi wanatakiwa wao ndio wawe chimbuko la uongozi. Ubora wa huo uongozi lazima utokane na ubora wa tafakuri ya wananchi wenyewe na ubora wa uelewa wa wananchi wenyewe wanataka nini kama wanataka kupewa mchele [na] mafuta ya kupikia kila miaka mitano wale kwa wiki moja basi ndio wamechangua watapewa.

Lakini wajue kwamba hao wanaowapa hivyo hawawezi kuwa viongozi. Sana sana ni matapeli ambao wananunua dhamana ya kuwawakilisha wananchi na hawawezi kuwawakilisha wananchi kwa sababu huo uongozi umekuwa sio uongozi ni geresha tupu. Ni uongo. Ni utapeli. Kwa hiyo, wananchi lazima wajifunze  wao wenyewe kufikiri kabla ya kupiga kura kwa huyu au yule.

Huwa natoa mfano mmoja. Dar es salaam kuna soko kubwa sana la mbuzi Vingunguti. Sasa mswahili anayekwenda kununua mbuzi wakuchinja siku ya Idd au siku ya Pasaka anatumia muda mrefu zaidi kumkagua yule mbuzi anayekwenda kumchinja kesho yake kuliko muda anaotumia kumteua kiongozi atakaye mtumikia kwa muda wa miaka mitano.  Na huyu mbuzi anachinjwa kesho yake lakini anamuangalia pembe kama zimekaa sawa sawa. Kwato – sijui zinahusu nini kwato hizo – lakini ataangalia hata zile sufi za manyoya ya mbuzi wake kama zimenyooka, anakwenda kumchinja kesho yake.

Lakini yule mtu ambaye anamtumainia kwamba atakuja kumuendeshea shughuli zake kwa miaka mitano amletee eti maendeleo hana muda wa kumkagua hivyo. Sasa ni utaahira wa akili ulioletwa ma wanasiasa uchwara wa nchi hii na wananchi wanaubeba wote bila hata kuuchekecha. Wananchi wamemezeshwa sumu ya uzuzu na wamekubali kuimeza hiyo sumu na wanaiendesha hivyo hivyo na hiyo sumu ndio inawaendesha.

Sasa wananchi ni wengi. Wananchi hawana uwezo kama nilionao mimi au ulionao wewe. Lazima wawepo watu wenye utashi [wa kuleta mabadiliko] Lazima kuwepo na utashi fulani. Lazima [wananchi] wapate utashi ndani ya jamii yenyewe kwa sababu kuna watu, kuna vijana wamekwenda shule kidogo wamepata mwanga, wengine wamesafiri kama hapa Mbeya watakuwa tangu zamani wakienda Johannesburg [Afrika Kusini] kwenye migodi miaka ya 1940 na 1950 na miaka ya karibuni hivi walikuwa wakienda Malawi wakienda kwingine kupata maarifa na maarifa yote hayo yanakuja yakirudi hapa inabidi wasambaze hayo maarifa kupitia vyama vyao vya hiari na kadhalika.

Baadae atazungumza ndugu yangu hapa [Mwalimu Meshack Kapange, mwanaharakati wa haki za wafanyakazi] kuhusu uhuru wa watu kuunganika pamoja kutetea maslahi yao ambapo kwenye hayo maslahi moja wapo ya maslahi hayo ni kuwa na uchaguzi ambao una maana, si uchaguzi ambao eti wananchi wanatumia muda mrefu kuchagua mbuzi wa kuchinja kuliko kutafakari huyo anayesimama na kuwaambia kwamba, “Mimi nataka kuwaletea maendeleo lakini chukueni hizi kanga za bure na kofia za bure na mafuta ya kupikia ya bure ili mnichague.

Sasa, hii haina maana hata kidogo kwa sababu kama wewe unakuja kutufanyia kazi basi sisi ndio tungekuwa tuna kulipa wewe kwa sababu unakuja kutufanyia kazi. Sisi ndio tunakulipa hiki kianzio cha mshahara mwisho wa mwezi tutakulipa mshahara ndani ya miaka yote utayokuwa unatutumikia tutakulipa. Lakini huyo huyo anakuja kukutumikia ndio huyo huyo anakuletea na hela na wewe unakubali. Ina maana kwamba akili yako haifanyi kazi sawa sawa. Wewe ni taahira na una aina fulani ya kichaa ambayo kwa kawaida ilipaswa ikuzuie wewe usipate ruhusa ya kupiga kura. 

Tito Magoti: Lakini Mzee, comrade Jenerali utashi wa wananchi, kuwa na utashi ni jambo moja, kwa maoni yangu, kuwa na dhamira ya kufanya jambo fulani ni jambo moja lakini kuhakikishiwa, kwa maana kuwa na ulinzi wa kile ninachotaka kukifanya, ni jambo lingine. Katiba yetu, ama mifumo yetu, imelegea vipi katika kuhakikisha ushiriki wa utashi wa wananchi, ulinzi wa maslahi ya wananchi, ulinzi wa mawazo ya wananchi, kwa mfano tumekuwa na uzoefu mbaya sana katika chaguzi zetu karibu zote hakuna uchaguzi ambao haujalalamikiwa na malalamiko ni juu ya heshima, juu ya ulinzi wa heshima na hadhi ya maamuzi ya wananchi, juu ya ulinzi wa heshima na hadhi ya kura ya wananchi. 

Kwa maana hiyo, kuna wananchi wanautashi wa kufanya jambo fulani lakini bado hakuna ulinzi stahiki wa maamuzi yao, wananchi wananuia kufanya kitu fulani lakini bado hakuna ulinzi, hakuna hakikishio la ulinzi wa maamuzi yao. Tunalegalega wapi katika Katiba iliyopo, lakini pengine pia katika kufikiri ni namna gani tunaweza kuwa na mifumo itakayo tusaidia sisi kuhakikishiwa ulinzi wa maamuzi yetu? Hhida ipo wapi hapo? 

Jenerali Ulimwengu: Ulinzi wa maamuzi yetu, hivi ulinzi wa mazao ya wananchi unafanywa na nani? 

Tito Magoti: Wananchi. 

Jenerali Ulimwengu: Sasa, je, maamuzi yenu ya kisiasa, ya kiuchumi, ya kijamii, ya kiutamaduni si mazao yenu? Kwa nini ukiweka mazao yako yaliyoiva shambani hujaenda kumuuliza mkuu wa kijiji vipi nitalinda mazao yangu, lakini upo tayari kwamba mazao yako yanayohusu haki yako ya kujiamulia mambo yako wewe mwenyewe unataka mtu mwingine aje akulindie? Kama ile ni haki yako, basi nenda kaichukue na hakuna haki ambayo mwananchi anaipata bila ya yeye mwenyewe kuihangaikia.

Hakuna kitu kama hicho. Hata unapopewa ukiambiwa haki hii umepewa na mkuu wa mkoa, ujue sio [haki] yako kwa sababu aliyekupa anaweza akakunyang’anya kesho. Lazima iwe ni haki yako mwenyewe kwa sababu umeichukua kwa mkono wako mwenyewe na unailinda kwa wivu mkuu hiyo haki yako la si hivyo sio yako. Chochote kile ambacho hujakichukua kwa mkono wako mwenyewe hakiwezi kuwa haki yako, ni fadhila uliyopewa.

Kuifanya haki iwe ya kwako ni lazima uwe na nguvu ya kuilinda na kusema atakayepitisha ng’ombe, kwa mfano, malisho ya ng’ombe yakiwa ni sehemu ya mazao ya wananchi na wakulima na ikawa ndivyo hivyo ilivyokubalika basi wale wenye ng’ombe watakuwa wanapitisha kwenye mashamba ya watu mpaka ifike wakati watu wanasema kwamba hapa ng’ombe hapiti, nyasi zipo kule sio mihogo yangu wala sio mpunga wangu.

Kwa hiyo, wananchi wajifunze, wafundishwe na wasaidiwe kuelewa kwamba kuna haki nyingi ambazo hawawezi kuzipata kwa sababu wamekuwa ama wanababaishwa, ama wamedhoofishwa katika ule utashi wa kweli wa kusema hii ni haki yangu na hakuna mtu atakaye ninyang’anya na ukitaka kuninyang’anya hili tutavutana mashati, tutapigana mieleka.

Kwa hiyo, na huu utashi kwamba wale vijana na watu wengine wazima ambao wanauelewa mkubwa wa masuala haya lazima wawe mstari wa mbele kuwaeleza wananchi wao haki zao ni nini na ni namna gani ya kuzipigania hizo hata mtu atakayekuwa na nguvu kiasi gani anaweza akapora haki hizi mara ya kwanza mara ya pili hata mara ya kumi hata mara ya kumi na tano lakini itafika mahala mara ya kumi na nane atakutana na wananchi wanasema hapana hapa hupati kitu. Na akifika pale na yule mwenye mabavu akianza kuona kwamba mabavu yake yanaanza kudhoofika, yanaanza kufifia yakilinganishwa na mabavu ya wananchi, yeye mwenyewe atarudi nyuma.

Hii yote maana yake ni kwamba mtu atakuonea, atakupiga, atakudunda, atakudhalilisha kwa muda mrefu kwa sababu anaamini kwamba wewe huwezi kujibu. Akipata dalili hata kidogo kwamba sasa unaanza kuonekana kama vile unao uwezo wa kujibu, atanywea na atarudi nyuma na hapo ndio unasimama kwenye nafasi yako. Kutoka pale ulipokuwa, umeongeza kidogo nafasi kama kama mita ishirini hadi tena wanakoita kule.

Lakini hii lazima wananchi wapiganie. Ni lazima waipiganie. Tumeona katika chaguzi zilizopita vituo ambavyo wananchi walisema, wacha mwaka jana, sijui mwaka jana kilitokea nini, labda waheshimiwa waliomo ndani humu wanaweza wakatwambia, lakini ilivyofika mahala wanawaambia ama tangaza matokeo kama tulivyopiga kura, ama hutoki humo ndani na wakatangaza matokeo. Hiyo ndio njia peke yake ya kulinda haki zetu kama wananchi.

Labda nidokeze tu kidogo. Mwaka 1961 tulipopata uhuru Serikali ya Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa wakoloni, kutoka kwenye ule utawala wa kikoloni. Wanazuoni wanaonesha kwamba utawala wa kikoloni uliondoka mara moja ukaacha utawala wa watu weusi ambao walivaa viatu na suti na kofia za wakoloni. Ukiangalia vizuri, na ningependa hili lichukuliwe kwa makini, ni kwamba hakuna mchakato uliofanyika kuislimisha-, hapa nazungumza kama mtu niliyelelewa kama Muislamu, kuislimisha hiyo Serikali iliyokuwa ya kikoloni ikawa Serikali ya wananchi.

Ile Serikali [iliyoundwa baada ya uhuru] na miundo yake kwa kweli ilibaki ni Serikali ya kikoloni ila inaendeshwa na watu weusi na matumaini yetu yalikuwa ni kwamba hiyo Serikali kwa sababu ndani yake kuna baba zetu, kaka zetu, ndugu zetu itaslimishwa taratibu iwe Serikali ya wananchi. Hatujafanikiwa sana katika hilo. Kwa hiyo, tabia za kikoloni bado zipo nyingi.

Leo nazungumza hili miaka sitini baada ya [uhuru] tabia zile za kikoloni bado zipo kwa sababu bwana mkubwa akiletwa kuwa mkuu wa mkoa anadhani amepewa shamba kubwa linaitwa Mbeya. Akipelekwa mahala pengine amepewa na yeye mkoa mmoja unaitwa Kigoma [unaona] ni shamba moja kubwa na vitu vilivyomo ndani, wananchi waliomo ndani na ng’ombe na mbuzi ni mali yake anaweza kufanya anavyotaka. Lazima hiyo ibadilike.

Na [mabadiliko haya] ni mchakato ambao bado lazima uendelee leo kukomboa nchi isiwe tena kama ilivyokuwa mwaka 1961 wakati watawala waliokuwepo hapa wakimfanyia kazi Malkia, sasa hivi tunao watawala weusi lakini kama vile kuna Malkia mahala fulani wanamfanyia kazi. Lazima ibadilike na haijabadilika hata kidogo.

Kuna mahala fulani tulifanya mabadiliko kidogo. [Kuandikwa kwa] Azimio la Arusha mwaka 1967. [Kutolewa kwa] Muongozo wa TANU mwaka 1971 [ambapo] ibara ya 15, sijui kama mnaijua hii, [inatamka kwamba], “Kitendo chochote kinachompa mwananchi uwezo mkubwa zaidi wa kuamua mambo yake mwenyewe ni kitendo cha maendeleo, hata kama hakikuongezei shibe wala afya.” [Hiyo ni] ibara ya 15 ya Muongozo wa TANU [uliotolewa] mwaka 1971. Wengi wamesahau hilo. Wengi. Na leo inawezekana mahala ningesema mambo kama haya ningekamatwa kwamba mimi ni mchochezi. Kitendo chochote, anasemaje? Kwenye hii ibara ya Muongozo wa TANU wa mwaka 1971.

Na huo ndio msingi kwamba daima ule uwezo anaoupata mwananchi kuamua mambo yake mwenyewe na kusimamia maendeleo yake yeye mwenyewe ni kitendo cha maendeleo hata kama hiyo tu haimuongezei afya wala shibe. Hiyo afya na shibe itakuja baadae kwa yeye kuweza kukitumia hicho kitendo alichokianza kwa kuijiamulia yeye mwenyewe kama ni ameamua vibaya akalima wakati mvua hazijanyesha ni kitendo cha maendeleo. 

Lakini utashi wa kuchukua maisha yako ndani ya maisha yako ndani ya mikono yako na kusema nitayafanyia kitu, nitafanya kitu na kitatokea kwa sababu mimi mwenyewe nimeamua kukifanya, si kwa sababu nimepigwa mijeledi na bwana mkubwa juu yangu mpaka nifanye kitu. Hiki nakifanya mimi mwenyewe nikiwashirikisha wenzangu katika kijiji, nikishirikisha familia yangu, tunajaribu kufanya hivi kwa niaba yetu sisi wenyewe. Hicho ni kitendo cha maendeleo. 

Tito Magoti: Lakini Mzee, comrade Jenerali, umewaelezea sana wananchi na sisi tungetaka sana kusikia kwamba, kusikia uhusiano wa wananchi na mifumo ya maamuzi, ama mifumo inayoratibu maamuzi yao, kwamba katika Katiba yetu kuna mambo mengi sana ambayo yametengeneza uhusiano ama yanasidia wananchi kuhusiana kwa maana kwamba kunakuwa na Serikali, kunakuwa na taasisi za umma ambazo zinaratibu mahusiano ya wananchi na tukienda kwenye mantiki ya Katiba, kwa mujibu wa mwanazuoni mmoja, ni mkataba kati ya wananchi na viongozi wao, namaanisha Serikali, ni mkataba kati ya wananchi na viongozi wao na ndio maana pia ya Katiba. Ni mkataba pia ama makubaliano ya watu kwa ajili ya kuratibu mahusiano yao.

Kumekuwa na taasisi ambazo zimeanzishwa na Katiba kwa ajili ya kusimamia na kuratibu maamuzi ya wananchi na kwenye muktadha huu umewashtumu sana wananchi kwa kutokusimamia maamuzi yao ama kwa kutokudai ulinzi wa maamuzi yao. Taasisi zinazoratibu maamuzi ya wananchi, hususani Tume ya Taifa Uchaguzi, zimekuwa na changamoto nyingi sana ambazo zinalalamikiwa mara kwa mara na hii imekuwepo tangu tunapopokea mfumo wa vyama vingi.

Katika mfumo wa [sasa] wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi uliopo sasa hivi unafikiri kwamba ni rahisi wananchi kujihesabu kwamba ni wanaamua kwa utashi wao na je, unafikiri kwamba kwa muundo wa tume ulivyo sasa hivi na mienendo ya Tume ya uchaguzi iliyopo sasa hivi unafikiri kwamba wananchi wanaweza kujisikia huru kushiriki maamuzi, kushiriki katika Serikali? Kwa sababu licha ya kuwa na taasisi ambazo mimi binafsi nazishtumu, mimi naishtumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba haipo huru, wewe utatwambia maoni yako, kumekuwa na jitihada nyingi sana za kuwatenganisha wananchi na Serikali lakini pia kumekuwa na jitihada nyingi sana za kuzuia maamuzi ya wananchi angalau kwa miaka mitano iliyopita mimi nimeshuhudia.

Tuna Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambacho ni kikao cha chama kimoja, lakini pia tumekuwa na viongozi wengi ambao ni wateule wa viongozi ambao pia wametokana na uchaguzi unaotiliwa shaka. Lakini hawa watu tunawategemea wasimamimamie maamuzi ya wananchi, ama waratibu maamuzi ya wananchi. Unazungumiaje hizi taasisi katika muktadha wa Katiba, kwamba hizi taasisi zina maana yoyote, zinahitaji maboresho ama shida ni wananchi wenyewe ambao wameshindwa kuzibadilisha taasisi hizo ili zifanye kazi kwa matakwa yao. Karibu. 

Jenerali Ulimwengu: Swali gumu sana. Kwanza, nirejee nilichosema hapo awali kwamba chochote kile ambacho unaweza kukihesabu kwamba ni chako ni kile ambacho umekichukulia hatua na kukimiliki kwamba ni chako hata ungekuwa na nini. Inaitwa nini hii, hatimiliki. Unayo [hatimiliki] kwenye briefcase yako umeifungia nyumbani. Lakini hicho kiwanja au shamba ambalo umepewa hatimiliki juu yake hujaenda kuiangalia, si chako kiwanja hicho wala si shamba lako hilo. Utakwenda kule utakuta nyumba imeshajengwa imekamilika na mtu anaishi wewe bado una hatimiliki kwenye briefcase yako kwa sababu huja exercise authority juu ya ile ardhi. [Yaani], hujaitumikia. Huja ipiga mhuri kwamba hii hapa ni ya kwangu na mtu anapoleta kifusi kumwaga pale unapambana nae unamwambia, “Usimwage mawe wala matofali hapa kwa sababu hii ni mali yangu.”

Wananchi wakishindwa kufanya hivyo na kudai haki yao basi wajue kwamba hiyo haki hawataipata, hawataipata hata siku moja kwa sababu hakuna mtu ambaye, kwa mfano katika masuala ya madaraka, hakuna mtawala ambaye ana madaraka makubwa sana ambaye siku moja ataamka asubuhi kwa sababu kapata maono na malaika Gabriel au malaika Jibril kamtokea katika ndoto zake akamwambia, “Bwana mkubwa, mamlaka uliyonayo ni makubwa sana ni vizuri kama ungeweza kuyagawa kwa wananchi wako na wao wakapata nguvu kidogo katika kuamua masuala ambayo yanawahusu.” Hakuna kitu kama hicho.

Watawala wa namna hiyo walikuwepo zamani akina Nabii Suleiman na wengine, lakini siku hizi hatuwaoni kwa sababu utawala unakuja pamoja na chakula. Sasa nani mmeona anaweza kukaa kwenye meza akawagawia watu, hata watoto wadogo, kwamba na wewe mtoto kula hii? Watoto wetu wenyewe tunawanyima chakula ambapo ingetakiwa mtoto apewe kipaumbele katika kula lakini baba au mama ndio anakula zaidi kuliko mtoto. Sasa katika madaraka ambayo yanaleta na mlo ndani yake nani atakubali kutoa hicho chakula?

Lazima walazimishwe, ni budi walazimishwe na watawala wajue kwamba tusipokubali madai ya hawa watu itafika mahali hata hiki tunachopata sasa hivi wanaweza wakatunya’ng’anya kabisa. Na waogope, na kuogopa si kwamba mchukue bunduki wala mishale au mikuki. Hapana. Kelele tu. Kuzidisha kelele na kuwaambia watu, “Jamani mnatuumiza. Nyie mnatuumiza na wanaotuumiza ni hawa wafuatao.” Kwa mfano, kama ni Mkuu wa Polisi katika maeneo fulani fulani anafanya udhalimu mnamtaja. Sio mnasema polisi wanatuonea. Hapana. [Mnasema], polisi wakiongozwa na Inspekta wa Polisi Jenerali Ulimwengu na sijui inaitwa nini polisi namba hii hii mnaitaja kabisa wajulikane.

Polisi wadhalimu [na] waonevu wa watu ni hawa. Majina yao wakatangazwa. Hakimu mla rushwa, maana yake ananyima haki ya wananchi, au mkuu wa wilaya anayechukua na anayevamia mashamba ya watu na kujimilikisha au muovu yoyote yule mtajeni. Wanasema wazungu mtu anayetenda maovu huhisi usalama kwa sababu jina lake halijulikani. [Wananchi] wanasema Serikali imefanya makosa hapa, imetudhulumu. Hapana. Sema ni Masanja, ni John na Ibrahim na fulani ndio hawa watu waovu katika wilaya yetu ndio wamefanya moja, mbili, tatu, nne na watajwe kila mara inapowezekana kuwataja.

Wataogopa na baadae itakuja kujitokeza tabia moja kwamba [kabla mtu] hajafanya kitu, atafikiri mara mbili, akisema, “Hivi si watanitaja kama walivyomtaja bwana Salum, bora nisijihusishe na suala kama hili.” Usipo wataja unawapa kinga ya kutojulikana. Ndio hao mnasema watu wasiojulikana. Lakini hawa watu wasiojulikana mnawajua nyinyi, wako mitaani kwenu. Mngesema, “Sio watu wasiojulikana. Hapa kwenye mtaa wetu tunawajua hapa kuna Aloyce, kuna Elias, kuna Abdallah. Hawa ndio watu wanaoitwa ‘wasiojulikana’ lakini kwetu sisi wanajulikana.”

Ukifikia nafasi hiyo ya kujulikana sasa mnawataja wazi wazi, hususan hawa polisi ambao mna namba zao wanavaa kifuani na majina yao mnayajua na mnajua kwamba wanafamilia. Mbona wanatishia. Wakitajwa sawa sawa na madhambi yao yakitajwa sawa sawa wataacha. Jana kuna mtu [aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya] amehukumiwa miaka mingapi? Thelathini. Si juzi juzi tu miezi michache alikuwa anafanya anavyotaka,? Hata mwaka haujapita, anafanya anavyotaka na inaonekana kama vile Serikali haina nguvu ya kumdhibiti.

Amepoteza maisha ya watu, amewaumiza watu, amechukua mali za watu vibaya tu na haya mambo yalijulikana lakini imekwenda mpaka watu, kelele za watu zikafikia mahala zikachukuliwa hatua na huyu bwana yuko ndani miaka 30 na bado kwa sababu kesi nyingine bado hazijasikilizwa, inawezekana hiyo 30 ni kianziao tu kuna mambo mengine yanakuja badae. Lakini kama wananchi wa huko alikokuwa wangeketi kimya wangesema ni amri ya Mwenyezi Mungu, bwana aliyempa ndio kaninyima mimi, aliye juu mngoje chini, mpanda ngazi hushuka, mpaka kesho angekuwa anaendelea kupanda ngazi tu.

Lakini kelele za wananchi [zimesaidia Sabaya kuhukumiwa] miaka 30. Nasema na hiyo ni kianziao. Kuna uwezekano kukawa na mambo mengine makubwa zaidi. Lakini, hii itupe nafasi ya kusema kwamba tukipaza sauti zetu hata kama mnyonge, mimi [naweza] kujihisi mnyonge, lakini hatuwezi kuwa wanyonge watu milioni 60, watu wanyonge, wanyonge gani? Unyonge wa kuku huo kwamba wanaweza kuwa kuku 2,000 au 10,000 ndani ya banda anakuja mtoto mdogo tu wa miaka 12 anawachinja wote, anamaliza hawalalamiki, sana sana wanapiga koko koko koko! lakini wakiwa wanachinjwa wanakwisha. Lazima binadamu wajifunze kuwa tofauti na kuku au kondoo. [Binadamu ni lazima] aweze kuinua sauti yake na kusema, “Unaniumiza na hii si nzuri na ole wako siku moja nikipata nguvu ya kukuondoa, nitakuadabisha wewe.”

Tito Magoti: Lakini comrade Jenerali, mara kwa mara tumeona athari za kufurukuta, ama athari za kujaribu kutumia nafasi ya kiraia kujieleza, kukosoa, wakati mwingine hata kuwa tajiri imekuwa ni mambo ambayo yanaletea watu shida. Na wakati mwingine hata kujaribu kushiriki moja kwa moja katika masuala kama ya uongozi kutaka kugombea nafasi za kisiasa, kufadhili ama kumuunga mkono mtu fulani tumeona watu wakijaribu kushiriki katika Serikali ama katika maamuzi ama katika mambo yanayowahusu katika nchi yao lakini watu hawa ambao wamefanya hivyo mara kwa mara tumeona wakipata athari, kwa maana kwamba wengine wanashtakiwa, wengine wanaumizwa wengine wanatokomea kusikojulikana, tuna mifano mingi tu ya watu ambao wamepata shida kutokana na kujaribu kujieleza ama kujaribu kuelezea fikra zao.

Unahusisha vipi haya na kurudi nyuma kwa wananchi, lakini pia unahusisha vipi hili la hofu inayo inayotufanya sisi kuendelea kubaki pale pale tulipokuwa kwa sababu umeandika katika kitabu chako makala ambazo uliziandika mwaka 1996 na bado hali imekuwa ni ile ile au imekuwa mbaya zaidi. Sasa, unahisisha vipi suala la hofu na wananchi kurudi nyuma, lakini pia unahusisha vipi suala la watawala kutumia nafasi zao kuzuia shauku ya wananchi kuleta mabadiliko katika nchi yao. Kwa mfano, sasa hivi imekuwa-, juzi moja nilienda kumtembelea bwana mmoja gerezani na baadae akaja kijana mmoja ambaye alikuwa amevaa fulana nje ndani, nikamuuliza kwamba wewe hii fulana mbona umeigeuza au ni mtindo, akasema bwana wameniambia pale niigeuze hii fulana, nikamwambia kwa nini, akasema kwa sababu ina maneno yameandikwa Katiba Mpya.

Sasa matendo ya namna hii unafikiri zinawanyima wananchi fursa kiasi gani ya kushiriki katika Serikali yao moja kwa moja na huo ni mfano mmoja. Lakini pili, unafikiri kwamba kuna nafasi gani ya wananchi na watawala wenyewe kubadilisha hayo matendo ama kubadilisha hiyo mienendo? Lakini tatu, unaona kuna fursa ipi kikatiba ya sasa ama ijayo kuondoa uharamia huu na kutengeneza mazingira ambayo wananchi watakuwa huru kuelezea fikra zao na kushiriki moja kwa moja katika Serikali yao? 

Jenerali Ulimwengu: Hakuna formula. Hakuna kikokotoo cha mapambano. Kikokotoo pekee ni kutumia ujuzi, werevu, weledi, ujasiri na hata nguvu vyote hivi nilivyovitaja vinavyofanana na mazingira uliyonayo hapo ulipo na wakati mwingine hujui namna gani ya kupima huo uwezo kiasi gani cha werevu, kiasi gani cha weledi, kiasi gani cha ujasiri, kiasi gani cha akili na kadhalika na ujanja unahitajika katika hali hii uliyonayo na kiasi gani cha nguvu mahala fulani.

Kwa mfano, kama tulivyoona yule nani, anaitwa George Floyd alikuwa ni Floyd yule wa Marekani. Ni kiwango gani cha nguvu inayotumika kukuumiza wewe, huwezi kuivumilia tena kwa jinsi mtu alivyokukanyaga na buti lake kwenye shingo yako na lazima uiondoe kama unaweza iondoe kwa nguvu hata kama ni kwa kumsukuma. Hayo yote yanakuja katika kujaribu kujiepusha na usumbufu na uonevu na kuumizwa na huyo ambaye anakufanya maisha yako yawe magumu. Sasa ile haina kikokotoo, ingekuwa na kikokotoo tungesema hili kwamba kwa kila makofi matatu uliyopigwa na wewe piga moja, inawezekana wakati mwingine inabidi uvumilie makofi mia moja kabla hujapiga lako moja.

Bwana Yesu anasema kwamba ukipigwa shavu moja geuza la pili. Kuna wengine wanasema ukiona mtu anakuja vibaya usisubiri upigwe shavu moja mpige kwanza wewe, muwahi kabla hajapiga hata shavu moja. Yote hii nataka kusema kwamba hakuna kikokotoo. Hali yako uliyonayo wakati ule unapokuwa katika mapambano ndio itakuonesha, litakuongoza uchukue hatua gani na wakati mwingine inabidi ujirekebishe uache mbinu uliyokuwa ukitumia zamani na uchukue mbinu mpya kwa sababu sasa hali imebadilika, ilikuwa kwenye kiwango hiki imefika kiwango hiki cha juu na kila mahala kama wananchi wanashauriana, kama wanajadili kama wanashauriana namna ya kumtega nguruwe anayekuja shambani kula mihogo ya watu, itapatikana namna ya kumtega simba ambaye anakula ng’ombe au mbuzi za watu itajulikana na itakuwa ni kichekesho uweke kikokotoo hicho hicho cha kuua nguruwe na cha kuua simba hapana hata kidogo.

Itakuwa lazima kwa nguruwe utumie vitu kama mihogo kumtega huyo nguruwe lakini kwa simba itabidi labda uning’inize vikuku vilivyokufa au wanyama wanyama wadogo wadogo ambao watavutia simba. Kwa hiyo, ujanja wako utategemeana na hali ya mapambano uliyonayo, na yanaweza kuwa yanabadilika kila siku. Kwa mfano, najua kwamba mnalalamika sana juu ya uchaguzi, kilichoitwa uchaguzi mwaka jana [2020]. Hapa kuna watu nimewasikia wakisema kwamba hakukuwepo na uchaguzi wowote. Sasa mbinu za mwaka jana za kupambana na unyang’anyi kama mlivyoona ni unyang’anyi au ni udanganyifu au ni uonevu wa mwaka jana inawezekana hizo mbinu mlizo jaribu kutumia mwaka 2020 hazitawafaa mwaka 2025.

Lakini, hakuna mtu wa kutoka nje anayeweza kuja kuwaambia kwamba sasa mwaka 2025 tufanye moja, mbili, tatu, nne, tano. Hapana, itabidi ni kila eneo litakuwa na watu wake ambao wataamua kwamba safari hii tutafanya hivi na hivi na hivi na hivi kwa sababu tumeshajifunza, tumeshajifunza kutokana na miaka iliyopita na vipindi vya uchaguzi vilivyopita kwamba mbinu moja, mbili, tatu, nne hazifai tena na tuchukue mbinu mbili tatu ambazo ni tofauti na zile ambazo tulizokuwanazo miaka mitano iliyopita. 

Tito Magoti: Kabla sijahitimisha mazungumzo yangu na wewe kwa n’ngwe ya kwanza, ningependa kukuuliza swali moja la mwisho. Kumekuwa na kigugumizi miongoni mwa viongozi wetu, ikiwemo viongozi wa juu kabisa, akiwemo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kuruhusu wananchi, ama kuruhusu matakwa fulani fulani ya wananchi, ikiwemo suala la kuandika Katiba Mpya, ametoa sababu nyingi sana ambazo mimi kwa kumuheshimu kabisa, nafikiri ni visingizio vyake na watu wanomzunguka.

Suala la kigugumizi hichi ambalo limekuwepo sasa tangu mchakato uvurugwe miaka karibu saba iliyopita, hichi kikugumizi unafikiri kinaathiri vipi kutengeneza taifa bora kwenye ustawi imara, taifa lenye watu wanaofikiri, taifa ambalo maamuzi ya wananchi yanalindwa? Kwa sababu, mimi naamini Katiba bora itasaidia kuliunda upya taifa na watu wengine pia wanaamini hivyo. Sasa kigugumizi cha watawala kuruhusu suala la Katiba wewe unafikiri kinatokana na nini na ni kwa kiasi gani kigugumizi hiki kinatofautiana na utashi wa wananchi?

Vile vile, kigugumizi hiki cha viongozi wetu kinavunja kinavunja misingi ya uanzishwaji wa nchi kwa maana ukisoma utangulizi wa Katiba ambayo ndio inaongoza nchi, Katiba ni maafikiano ya wananchi, wananchi tumeafikiana hivi, wananchi tumeafikiana tutajenga kwenye nchi yetu jamii ya watu waliostarabika na kadhalika na kadhalika. Sasa kigugumizi cha kuruhusu haya mambo unafikiri kinaleta shida kiasi gani na kinawaumiza wananchi kiasi gani na je, unafikiri ni muda muafaka kuandika Katiba Mpya? 

Jenerali Ulimwengu: Hilo swali lina masuala ambayo yanapeana matoleo kama vile unavyojenga nyumba. Lakini muhimu ni hivi hakuna mtu, sidhani kama kuna mtu amefanya hivyo na wala sidhani kama kuna mtu anadhubutu kufanya hilo yaani kusema kwamba kuzuia wananchi wasizungumze masuala yanayohusu Katiba, sidhani. Hilo halijafanyika na sidhani kama kuna mtu anaweza kukifanya hilo, au kujaribu kulitekeleza, unalitekelezaje?

Wananchi kufikiria mambo yanayohusu Katiba hapa tulipo watu kama 80, 90 hapa humu ndani kila mtu najua kuna mchakato ndani ya kichwa chake hapa tulipoketi sote kuna michakato takribani 80 au 90 inafikiria Katiba. Nadhani kama wengine labda wamepitiwa na usingizi lakini kwenye usingizi ndio kabisa na katika ndoto zetu wako watu wanoota kabisa masuala ya kikatiba na yako yanaendelea kichwani mwao, mtu anayejaribu kufanya hivyo lazima awe na uwezo.

Kuna watu ni wendawazimu kidogo lakini hawajafikia uwendawazimu wa kiwango hicho kwa kudhani kwamba wanaweza wakafumua ubongo wetu, [ubongo] wa kila mtu na wakaona ndani unafikiri nini. Inabidi wawe na majeshi makubwa sana ya polisi fikra, sio tu polisi, [bali] polisi waliofundishwa mahususi kushughulikia fikra. Hawa inabidi wawe wana uwezo wa kuingia ndani ya bongo za watu na kuangalia na kukamata watu na kwenda kutoa ripoti kwamba, “Afande tumemkamata huyu kwa sababu tumeona fikra zake mbovu.” Bado hatujafika huko.

Kama ni kweli hatujafika huko hakuna mtu aliyewahi kuniita mimi kituo cha polisi kuniuliza kwamba jana waliangalia kwenye fikra zangu wakaona mambo ninayofikiri hayafai. Kama hiyo ni kweli hatujafika hapo tusifanye kama vile tunadhani kwamba tunatakiwa tufike huko. Tuendelee kufikiri kwa pamoja, na tukafikiri tuendelee kuongea na wenzetu ambao labda wanafikra kama zetu au zimetofautiana kidogo lakini tunaweza kujaribu kushawishiana na baada ya hapo tuendelee kutoa mawazo yetu hadharani ili wenzetu nao waseme, “Nilikuwa nafikiria kama wewe au nilikuwa na mawazo tofauti na ya kwako.”

Tubadilishane mawazo, kitu ambacho ni msingi wa kujenga uelewa mkubwa zaidi huku mkielimishana na baadae unakuwa na mjadala mpana zaidi wa masuala ambayo yanahusu Katiba. Sasa hivi mimi sioni mjadala huo. Ninachoona zaidi ni turuhusiwe kuandika Katiba Mpya au tusiruhusiwe. Mimi nasema hilo wala halina tija kubwa sana. Kikubwa ni unataka nini ndani ya Katiba hiyo? Kwa mfano, mimi kuna mambo ambayo nayasema kila siku, watu wa eneo wachague wakuu wa eneo hilo. Full stop! Kama ni watu wa Mbeya mjini, wachague viongozi wa wa Mbeya mjini. Kama ni wa wilaya gani, Kyela sijui wapi huko, wachague watu wa Kyela. Mimi naamini hilo.

Naamini kwamba ni kosa kubwa sana kumchukua mtu amezaliwa na amekuwa maisha yake yote Karagwe kesho unamfanya yeye ndio mkuu wa wilaya ya Tunduma, ambayo anafanya kazi kama mamluki miaka 20, 25 na anapostaafu anarudi zake Karagwe wala hataki kuuliza kule Tunduma nilikofanya kazi miaka 20 iliyopita kuna nini? Hakumhusu tena wala bibi yake na shangazi zake na wajomba zake walioko Karagwe hawana uhusiano wowote na Tunduma na hawatakaa siku moja wakawa na uhusiano na Tunduma.

Nadhani huo ni aina ya ukoloni ambao tumeuvumilia kwa miaka mingi lakini lazima uishe. Hayo ni mawazo yangu ya kikatiba. Sijasema mtu ayaandike. Ni mawazo yangu je, tunaweza kubadilishana mawazo sasa hivi? Kuandika Katiba ni kitu kingine. Ni hatua ya mwisho kabisa. Humu ndani [ya kitabu] mtaona hili kuna sura, kuna makala moja imeandikwa, ‘Sasa Katiba na Iandikwe’ na inasema hivyo kwa sababu mmeshapitia masuala mengi ndani ya kitabu hiki wiki moja baada ya nyingine namna gani mipango yetu iende masuala yenye makuu yaangaliwe katika  kujadili katiba yote ikifika mwisho kabisa kuhusu katiba ukurasa wa 139 Katiba na iandikwe.

Lakini kabla ya hayo, hizi makala [zilizomo kwenye kitabu hiki] zinasema nini kwanza? Kuna makala moja inasema, ‘Sasa Tugange Yajayo’ kwa sababu mwanzoni nimesema tugange yaliyopita kwa sababu na hayo vilevile ni ndwele. Msemo wa Kiswahili unasema kwamba, yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Naukataa mimi [mimi huu msemo] kwa sababu baadhi ya ndwele, baadhi ya magonjwa tuliyonayo leo chanzo chake ni magonjwa yaliyopita halafu hapa nasema nini?

Kuna mkutano wa kitaifa mjadala mpana, ushiriki mpana wengine wanazungumza kwamba huo mjadala lazima uwe mpana na mpana maana yake sio kwamba kiwe kikao kikubwa kwa sababu Rais Samia katoa idhini kwamba iwepo mikutano ya Katiba. Hapana. Sisi wenyewe tunavyozungumza hapa huu ni mjadala. Sasa mjadala ukiwa mpana maana yake utakuwa uko Dodoma, uko Lindi, uko Mtwara uko Kilimanjaro uko Arusha uko Kagera, uko kila mahala. Mjadala mpana na ushiriki uwe mpana.

Nadhani kwamba Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu [LHRC] ndio maana yake hii kusambaza huu mjadala uwepo kila mahali. Ndio maana hiyo makala inasema mjadala mpana, ushiriki mpana sio kikundi cha watu ndio wajuaji, ndio mafundi, ndio mabingwa wanaketi katika vyumba vilivyopigwa na viyoyozi mpaka vinatetemeka kwa baridi halafu wanasema kwamba tumesha fikiri, tumetafakari kwa niaba yenu na sasa hivi haya ndio mapendekezo tunayoyatoa. Hapana.

Baada ya mjadala mpana na ushiriki mpana tunapendekeza mkutano wa kitaifa ambao ulipendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992. Haujafanyika mpaka leo na tunasema kwamba katika mkutano huo wa kitaifa basi tuweke vipaumbele vya kitaifa ambavyo vitakuwa vinaonesha mipango ambayo inatokana na muafaka wa wananchi. Je, wananchi wa Rungwe na wananchi wa Kyela maslahi yao yanaendana hatua kwa hatua kwa kila kitu? Je, si kweli kwamba wananchi wa Kyela labda kuna sehemu fulani ya maisha yao inahusu zaidi uvuvi kuliko kilimo au tukiwaangalia hasa wananchi wa mikoa yote hii iliyoko hapa hali ya hewa inaruhusu kulima mazao gani? Je, yanafanana na mazao yanayotakiwa yalimwe kanda ya ziwa inawezekana si kweli?

Halafu baada ya mipango hiyo iliyotokana na muafaka wa kitaifa mwisho nasema Katiba na iandikwe. Hatua kwa hatua hadi hapo tunaposema kwamba Katiba iandikwe. Sasa hapo inawezekana Rais Samia atakuwa ameshaona hali inavyokwenda nchini. Mjadala unaendelea, unaendelea kwa kasi katika kila kikao kikikutana suala la Katiba linajadiliwa na watu wa eneo hilo wanasema mahitaji yangu mimi kama mwananchi wa kisiwa cha Mafia hayawezi kufanana na mahitaji ya mtu wa Kondoa, kwa sababu mazingira yake ya uzalishaji na maisha yake yote ni tofauti na mahitaji yangu na maisha yangu mimi nikiwa kama mtu wa kisiwa cha Mafia.

Lakini yote hiyo inachukuliwa pamoja kwamba ni sehemu ya mjadala wa kitaifa na kwamba kukubaliana kama taifa haina maana kwamba tunafanana. Hatufanani, kuna maeneo tunatofautiana sana. Kuna maeneo ambapo ili uonekane wewe ni tajiri lazima uwe na ng’ombe 5,000. Niambieni, kule wapi, hapa Rungwe, ng’ombe 5,000 itawezekana? Lakini Simanjiro inawezekana. Kwa hiyo, mahitaji ya Rungwe na mahitaji ya Simanjiro pamoja na kwamba wote ni Watanzania kuna tofauti kubwa sana.

Tukishazungumza hayo yote ndio sasa tunasema tutaandika Katiba na bila shaka katika Katiba hiyo kipengele kimoja wapo muhimu ni kwamba haitakuwa inawezekana tena kwa mtu ambaye maisha yake yote ni Simanjiro akachaguliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Rungwe kwa sababu tu bwana mkubwa fulani Dodoma au Dar es salaam kampenda sana kwamba huyu mtu wa Simanjiro aende kufanya kazi ya kuleta maendeleo wilayani Rungwe. Hiyo ndio maana yake.

Sisi tuendelee kuongea. Tuendelee kujadili. Mjadala huu [juu ya Katiba Mpya] uendelee na uwe mpana na unawezekana usiishe kesho, miaka mitano inawezekana haitoshi kuufanya mjadala huu. Lakini uendelee mpaka hapo utakapofika mahala tukasema kwamba sasa ama kwa ridhaa ya wakubwa wa nchi hii ama bila ridhaa yao, sisi wananchi tumeamua tunaanzisha Katiba yetu kwa njia moja au nyingine ili tuweze kusema kama inavyotakiwa iseme Katiba kwamba, We the People.

Asanteni!

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *