Jeshi Sudan Siyo Taasisi Tu, Bali Dola Ndani ya Dola

Yanayotokea Sudan yanadhihirisha wazi kwamba jeshi la nchi hiyo halina nia ya kubaki kama taasisi ya ulinzi wa taifa.

Sudan imerudi tena  kugonga vichwa vya habari baada ya jeshi la nchi hiyo ya Kaskazini-Mashariki mwa Afrika kumkamata Waziri Mkuu wa Serikali ya kiraia Abdullah Hamdok na maafisa kadhaa wa ngazi ya juu na kutangaza limefanya mapinduzi. 

Matukio hayo  yamezusha  upya maswali juu ya mustakbali wa Bara la Aafrika, hususan katika eneo la utekelezaji wa misingi ya kidemokrasia na utawala bora. Wakati miaka  ya 1990 ilifungua mlango wa matumaini kutokana na kile kilichoitwa “upepo wa mabadiliko,” baada ya  karibu miongo miwili na nusu gurudumu la maendeleo ya kidemokrasia barani humo limeanza kurudi nyuma. Mtindo wa wanajeshi kutwaa madaraka, umerudi tena.

Katika kipindi cha zaidi kidogo ya mwaka mmoja, kumetokea mapinduzi matatu, mawili nchini Mali na moja nchini Guinea. Pia, kulifanyika jaribio lililoshindwa nchini Niger. Kuna wanaosema kwamba matukio nchini Chad baada ya  kuuwawa kwa Rais Idris Deby yalikuwa ni mapinduzi. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Chad, Spika wa Bunge ndiye aliyepaswa kushika hatamu za uongozi kwa kipindi cha mpito hadi pale Rais mpya atakapokuwa amechaguliwa. Lakini jeshi lilijiingiza haraka na kumpa madaraka mwanawe Deby ambaye pia ni mwanajeshi.

Sasa yamerudi tena Sudan

Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na mji  wa pili kwa ukubwa wa Omdurman, mara baada ya habari kuvuja kwamba Hamdok pamoja na maafisa wengine wamekamatwa na wanajeshi wa ulinzi, ambao walimpeleka Hamdok mahala pasipojulikana.

Mapinduzi hayo yanafuatia jaribio la mwezi uliopita la baadhi ya wanajeshi ambalo sasa linaashiria lilikuwa ni kujaribu tu kupima joto litakuaje. Inawezekana lile tangazo kwamba jeshi lilikandamiza jaribio hilo, ilikuwa ni sehemu tu ya njama iliokuwa imepikwa, pakisubiriwa wakati muafaka.

Mapinduzi nchini Sudan yamefanyika wakati jeshi likitarajiwa kukabidhi uongozi wa baraza la pamoja la kugawana madaraka wiki chache tu zijazo. Utaratibu huo unafuatia makubaliano yaliofikiwa kwamba jeshi liongoze kwa kipindi cha miaka miwili na baadae baraza hilo liongozwe na raia, makubaliano yaliofikiwa baada ya kuangushwa Rais Omar Hassan al-Bashir mnamo Aprili 2019 kufuatia vuguvugu la upinzani wa umma kupamba moto.

Ni dhahiri Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Jeshi la Sudan na ambaye amekuwa akiliongoza taifa hilo katika kipindi chote hiki cha mpito, hakuwa tayari kwa hilo. Jenerali huyo amejiunga na makundi ndani ya Sudan yaliyojitokeza kuikosoa Serikali ya Waziri Mkuu Hamdok  kwamba imeshindwa kuyashughulikia matatizo sugu ya taifa hilo, ikiwepo rushwa, uchumi mbovu na hali ngumu ya maisha. 

 

Serikali ya mseto ya mchanganyiko wa raia na wanajeshi haikuwa na madaraka ya kuamuwa. Kutokana na hayo, haikuweza kuongoza ipasavyo. Kwa upande mwengine,  raia waliokuwemo ni wawakilishi wa vyama mbali mbali vya kisiasa, wanaharakati na asasi za kiraia, kila upande ukiwa na masilahi yake.

Miaka miwili tangu yalipopatikana makubaliano mnamo Agosti 2019, paliwekwa lengo la hatimaye kufanyika uchaguzi Julai  2023 utakaoirejesha Sudan katika utawala kamili wa kiraia, Serikali ya Hamdok imeandamwa na mivutano baina ya wajumbe wake wa kiraia kwa upande mmoja na kati yao na wanajeshi kwa upande wa pili.

Jenerali al-Burhan amelivunja baraza la mpito lililopewa jukumu la kuilinda Katiba, umma wa Sudan na demokrasia. Amesema sasa itaundwa Serikali ya wataalamu na siyo wanasiasa kuiongoza nchi hiyo na  kwamba jeshi linabakia kuwa mdhamini wa kipindi cha mpito cha taifa hilo kuelekea utawala wa kiraia. Wengi wanaitilia mashaka kauli ya Jenerali al-Burhan kwani ameshasema ni yeye atakayeendelea kuuongoza mchakato huo.

Jeshi limefanikiwa kuigawa jamii

Jamii ya Wasudan imegawika kati ya wanaopigania mabadiliko ya haraka na utawala kamili wa kiraia na wale wanaoliunga mkono jeshi, ambao waliandamana  wiki iliyopita na kuweka kambi nje ya kuta za Ikulu anakoishi Jenerali al-Burhan. Kuna tetesi kwamba baadhi yao ni wafuasi wa kiongozi wa zamani Omar Hassan al-Bashir na huenda ni maandamano yalioandaliwa kama chachu ya hatimaye jeshi kufanya ilichokifanya. 

Wanajeshi wanaungwa mkono pia na makundi yenye silaha  katika wilaya tafauti yakiwemo yale ya jimbo la magharibi la Darfur. Kwa mfano, watu kutoka kabila la Beja walioanza maadamano ya karibuni kuipinga Serikali ya Hamdok kuwa imeshindwa kurekebisha hali mbaya ya kiuchumi, wanadaiwa kupewa usafiri hadi Khartoum.

Raia wanaoyapinga mapinduzi hayo wamekula kiapo kuendelea na vuguvugu  lao, lakini haielekei kama kasi itakuwa sawa na ile  ya Desemba 2018 iliyo sababisha hatimaye al-Bashir kun’goka madarakani miezi minne baadaye. Sababu kubwa ni kwamba jeshi limefanikiwa kuigawa jamii na kuwa na kisingizio cha kuhalalisha hatua yake ya kurudi madarakani. 

Umoja wa Afrika hadithi ni ile ile

Umoja wa nchi huru za Afrika kama kawaida umetoa wito wa kupinga yanayoendelea kutokea nchini Sudan na  kuwataka wanajeshi kumuachia huru Waziri Mkuu Hamdok na maafisa wengine waliokamatwa. Hatua hii ya AU haishangazi kwani huo ndio umekuwa mtindo wa kawaida yanapotokea mapinduzi. Umoja wa Afrika umeshindwa kuchukua hatua za kivitendo, zaidi ya kauli tu kwamba wahusika watasusiwa na kuwekewa vikwazo kama hawatorejesha utawala kwa raia.

Halikadhalika, nchi na jumuiya za kimataifa, kama Marekani na Umoja wa Ulaya, zimetoa taarifa kupinga mapinduzi hayo. Ni mtindo wa kawaida na hapatarajiwi kubwa la kuigeuza hali ya mambo. Wafadhili kwa sehemu kubwa wameshindwa kuisaidia Serikali ya Hamdok kurekebisha hali mbaya ya kiuchumi. Huenda kuwemo kwa wanajeshi kilikuwa kikwazo, pamoja na ahadi alizopewa Hamdok.

Hata hivyo, matokeo ya Sudan ni pigo kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Dk Abiy Ahmed ambaye  alitoa mchango mkubwa kufanikisha mapatano ya kugawana madaraka kati ya jeshi na raia, na kufungua njia ya  kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi. Abiy binafsi anakabiliwa na mtihani katika  mkoa wa Tigray ambako kuna  harakati za kutaka kujitenga, zilizosababisha vita vinavyoendelea kati ya waasi na Serikali Addis Ababa.

Historia ya Sudan kisiasa imegubikwa na mapinduzi ya kijeshi. Miaka 65 tangu uhuru, wanajeshi wametawala vipindi vitatu ambavyo kwa pamoja vimedumu miaka 50. Hivyo ni pamoja kile cha Jaffar Nimeiri na Omar Hassan al-Bashir. Yanayotokea Sudan yanadhihirisha wazi jeshi la nchi hiyo halina nia ya kubaki kama taasisi ya ulinzi wa taifa.

Jenerali Abdulfatah al-Burhan  amerudi kufuata nyayo za wajina wake, jirani yake wa kaskazini Abdulfatah al-Sisi wa Misri. Haitoshangaza pindi al-Burhani naye atajivua sare za kijeshi na kugeuka mgombea wa kiraia, kama alivyofanya al-Sisi baada ya kumpindua Rais aliyechaguliwa na umma Mohammed Morsi, au kama alivyofanya Omar Hasasan al-Bashir. 

Kama vuguvugu jipya la kupinga hatua ya jeshi kutwaa tena madaraka kamili litazaa matunda, ni jambo la kusubiri na kuona.

Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Mohammed AbdulRahman

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved