The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Buku la Biubwa Amour Zahor Limefunua Chano Hadharani

Ni kitabu cha Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi kilichozinduliwa Dar es Salaam mnamo Novemba 13, 2021.

subscribe to our newsletter!

Labda kwangu mimi, kama si kwa Dk Harith Ghassany kunitia katika utafiti wa kitabu chake, kinachoitwa Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru, nisingejua mengi katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kubwa katika kitabu cha Dk Ghassany ni kufichua moja ya siri kubwa sana katika historia ya mapinduzi, nayo ni kuwepo kambi ya mamluki wa Kimakonde wakata mkonge waliokuwa Kipumbwi, kijiji kidogo cha wavuvi maili chache kutoka Tanga na jirani ya Pangani. Wamakonde hawa walikuwa waajiriwa wa shamba la mkonge la Sakura.

Mnamo Novemba 6, 2021, katika hoteli ya Golden Tulip huko mjini Zanzibar kulikuwa na uzinduzi wa kitabu, kiitwacho Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi, kilichoandikwa na mwanahabari mashuhuri Zuhura Yunus.

Mapinduzi ya ‘amani, utulivu na upendo’

Mwanzoni mwa kitabu tu, Biubwa, ambaye ndiye muhusika mkuu wa kitabu hicho, anaeleza kwenye utangulizi wa kitabu cha maisha yake kwamba kashiriki katika mapinduzi na mengi aliyofanya yameleta “amani, utulivu na upendo.” Maneno mazito hayo yanayohitaji tafakuri pana!

Niliposoma sentensi hii iliyopo kwenye kurasa za mwanzo wa kitabu hicho nilijua kuwa hiki si kitabu chepesi. Hii ikanikumbusha tamthilia ya Macbeth iliyoandikwa na William Shakespeare ambapo mwandishi huyo mashuhuri wa tamthilia za Kiingereza anafungua kitabu chake na sentensi inayosema,  “The Three Weird Sisters.”

Kama hilo halikutosha, nyuma ya kitabu katika blurb yameandikwa maneno “mapinduzi matakatifu.” Asubuhi na mapema, al fajr baada ya uzinduzi, nikawa nimetambua kuwa haitakuwa rahisi kwangu kufanya pitio la kitabu hiki.

Narudia tena kusema kuwa kama na hili halikutosha kila nilipofungua kurasa kusoma, (na hapa nikiri kuwa hiki ni fast book, yaani ni kitabu kinachokwenda kasi) nakutana ndani ya kitabu majina ya watu ambao nawafamu kwa karibu na kwa mbali kwa njia moja ama nyingine na wote wamo katika dramatis personae ya mapinduzi.

Hili ni tatizo kubwa kwangu. Hii inahitaji makala yake pekee inayojitegemea. Kitabu hiki kinahitaji kufanyiwa pitio na mtu asiyeijua historia ya Zanzibar. Lakini mtu huyo hii leo utamtoa sayari gani, nani asiyejua historia ya Zanzibar?

Ubaguzi na mikasa ya mapenzi

Kitabu hiki kupitia maisha ya Biubwa kimeeleza ubaguzi katika uhalisia wake. Yawezekana kuwa historia ya Biubwa ni isolated case isiyowezekana kujenga hoja madhubuti?

Kitabu kinaeleza yaliyotokea kwenye uchaguzi wa Juni 1961 na kitu cha kufikirisha sana ni kwamba vurugu kama hizo zimekuwa zikirejea kila pafanyikapo uchaguzi Zanzibar, nusu karne baada ya mapinduzi kutokea.

Wazanzibari bado wanauliwa katika kila uchaguzi. Lakini Biubwa anasema mapinduzi ambayo yeye ameshiriki yameleta “amani, utulivu na upendo.”

Kitabu hiki ni kamusi ya visa vya kusikitisha vya mapenzi yaliyomkuta binti mdogo wa miaka 18 akihangaika na uzito wa kutafuta faraja mahali pasipo na faraja ila ukame katika mapambano baina ya chama cha Afro-Shirazi (ASP) na Zanzibar Nationalist Party (ZNP), au Hizbu kama kinavyoitwa muda mwengine.

Fikiria, Unguja ya  miaka hiyo, Biubwa msichana wa Kiarabu, mtoto mdogo wa miaka 18, tena bado mwanafunzi, anawaletea wazee wake mchumba Mzungu?  Maneno ya posa anapeleka nani, nani mpokeaji? Na tujaalie posa imekubaliwa, na mchumba kasilimishwa, akdi [ndoa] inafungiwa wapi?

Waingereza wangesema, sheer spectacle!

Vichekesho!

Lakini hata alipotokea kutaka kuolewa na Mzanzibari mwenzake, kijana msomi, daktari muhitimu wa Chuo Kikuu cha Makerere, Dk Hassan Kingwaba, kasoro ikawepo. Rangi ya Dk Kingwaba. Lakini huyu si Muislam? Kwani Uislam unajali rangi? Ataolewaje na Mwafrika ilhali yeye ni Mwarabu?

Biubwa asimulia upande wake wa hadithi

Wengi kwa miaka mingi sana wamemuhukumu Biubwa kwa historia yake katika mapinduzi ya mwaka wa 1964, mapinduzi ambayo yalisababisha baba yake mwanachama wa Hizbu kuuliwa akiwa jela.

Katika kitabu hiki, Biubwa kajipa mwenyewe haki ya kusikilizwa kwani mahakama ilimuhukumu bila ya kumpa nafasi ya kujieleza.

Inawezekana labda kwa yeye sasa kujieleza baada ya nusu karne, hakimu ataelewa yaliyomfika hadi kufikia pale alipofika akawa amebeba bunduki katika vichochoro vya Stone Town wakati Waarabu ndugu zake wamejifungia majumbani mwao kwa kuogopa kuuliwa na askari wa John Okello.

Kama nilivyosema hapo awali, mbali na jambo zito ambalo Dk Ghassany kalieleza katika kitabu chake cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru nililolitaja katika utangulizi wa makala haya, lipo jambo lingine lililoelezwa na mwandishi huyo kwenye kitabu chake hicho, jambo ambalo linasadikishwa na maelezo ya Biubwa. Jambo hilo ni uhusika Myahudi mmoja  katika mapinduzi ya 1964.

Dk Ghassany kaeleza uhusiano uliokuwapo baina ya Myahudi Moshe Finsilber na Karume na uongozi wa ASP. Dk Ghassany hakugusia hata kwa mbali kuwa Moshe Finsilber alikuwa na uhusiano na Julius Nyerere.

Kitabu cha Biubwa kinasema kuwa Nyerere akifahamiana na Myahudi huyu na ndiye aliyempa amri Finsilber kuwapeleka Karume, Kassim Hanga na Abdulrahman Babu Zanzibar siku ya pili asubuhi baada ya mapinduzi. Kwa kuelezwa haya, Biubwa kamsadikisha Dk Ghassany kwa mengi.

Tusome zaidi ili kuelewa

Msomaji anachotakiwa kufanya ni kuunganisha yale ya Wamakonde wa Kipumbwi, Wayahudi ndani ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika chini ya Julius Nyerere ili kupata picha kamili ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964.

Labda utajiuliza, wako wapi Makomredi na nini nafasi yao katika haya yote ya kupinduliwa Serikali ya Sheikh Mohammed Shamte?

Hashil Seif kaandika kitabu kinachoitwa Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar (2019).

Ipo pia makala ya marehemu Salim Msoma iliyo na jina Zanzibar the Agony of its History (2016).

Kitabu cha Biubwa kimefunua ukurasa mwingine ambao unahitajika kusomwa.

Mohamed Said ni mwanahistoria na mwandishi wa kitabu cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968): Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati Za Waislam Dhidi Ya Ukoloni Wa Waingereza Katika Tanganyika. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mohamedsaidsalum@gmail.com au kupitia akaunti yake ya Facebook ambayo ni @Mohamed Said. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *