The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dar es Salaam ya Uwanja wa Vita Baridi na Paradiso ya Wapigania Uhuru

Dar es Salaam ulikuwa mji wa kipekee miongoni mwa miji iliyokuwa uwanja wa vita baridi duniani kwani  vuguvugu la ukombozi dhidi ya ukoloni duniani lilikuwa limebaki na kushika kazi  zaidi barani Afrika

subscribe to our newsletter!

Katika kipindi cha nusu ya pili ya karne ya ishirini baada ya Vita ya Pili ya Dunia, mwenendo wa siasa za ulimwengu ulijikuta ndani ya wigo wa mambo mawili: Mosi, ni  siasa za Vita Baridi kati ya kambi ya Mataifa ya Magharibi yanayofuata mfumo wa kibepari wakiongozwa na Marekani dhidi ya kambi ya Mataifa ya Kikomunisti yanayofuata mfumo wa kijamaa wakiongozwa na Shirikisho la Jamhuri ya Kisoshalisti ya Kisovyieti (USSR). 

Pili, ni wimbi la vuguvugu la ukombozi lilokuwa likiendelea dhidi ya ukoloni na ubeberu karibia kona zote za dunia: Asia, Amerika Kusini na Afrika. Ingawaje vuguvugu la ukombozi lilikuwepo tangu siku ukoloni ulipoingia, harakati za kujikwamua na jinamizi hilo zilishika kasi zaidi baada ya Vita ya Pili ya Dunia na kupata  hamasa zaidi baada ya Mapinduzi ya China ya mwaka 1949 yaliyofanywa na wakulima masikini wa pembezoni mwa nchi hiyo. Mapinduzi hayo yalitoa mfano kwa watu wa nchi nyingine waliokuwa bado chini ya utawala wa mataifa ya nje.

Mwanahistoria George Roberts katika kitabu chake cha Politics, Decolonisation, and the Cold War in Dar es Salaam anaeleza kwamba katika mwelekeo huo wa siasa za ulimwengu ndipo kulipotokea miji ambayo ilijikuta kuwa uwanja wa mapambano ya Vita Baridi kati ya pande mbili zinazo ongozwa na Marekani na USSR. 

Miji kama Berlin, barani Ulaya, Mexico City bara la Amerika na Dar es Salaam barani Afrika, kwa umuhimu wake kisiasa, iligeuka uwanja wa propaganda za Vita Baridi, migongano ya kidiplomasia, na hujuma za kijasusi baina ya pande mbili za wahusika wakuu wa vita hiyo.

Kati ya miji mingi iliyokuwa uwanja wa vita baridi wakati huo, Dar es Salaam ulikuwa ni mji wa kipekee kwani  vuguvugu la ukombozi dhidi ya ukoloni duniani lilikuwa limebaki na kushika kasi  zaidi barani Afrika kuanzia miaka ya 1950s. Vile vile, mwaka 1963 Dar es Salaam ilichaguliwa kuwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi iliyoundwa na Umoja wa Afrika (OAU) mwaka 1963.

Kwa umuhimu huu wa kisiasa na mahusiano ya kimataifa, Dar es Salaam ikajikuta uwanja, ama front kwa kimombo, mpya wa mapambano ya Vita Baridi baina ya wakubwa hao wa dunia kwani hatima ya mataifa mengi ya Kusini mwa Afrika yaliyokuwa bado chini ya ukoloni ilionekana ipo Dar es Salaam. 

Ndio, ni Bongo Dar es Salaam hii hii kama tupendavyo kuiita vijana wa kizazi kipya. Jiji lenye watu takribani millioni sita kwa sasa kutokea watu 3,000 miaka ya 1860s wakati Sultani wa Zanzibar, Sayyid Majid bin Said Al-Busaid alipoanza mradi wa kujenga St. Petersburg yake pembezoni mwa kijiji cha Mzizima mahali penye eneo la bandari asili na tulivu mwambao wa Afrika Mashariki. Mwambao ambao una historia  ya kuwa na miji mashuhuri kwa karne nyingi zilizopita.

Katika mwambao huu wa Afrika Mashariki, tangu karne nyingi zilizopita, kumekuwa kukiibuka miji mashuhuri ambayo historia yake ni pamoja na kuwa kitovu cha mahusiano ya kiuchumi na kisiasa baina ya watu wa mataifa ya mbali na jamii za Waafrika zilizokuwa zikiishi maeneo ya bara na pwani. 

Kati ya karne ya kumi mpaka karne ya kumi na tisa iliwahi kuibuka miji kama Lamu, Kilwa, Mombasa, Bagamoyo na Sofala ambayo kwa nyakati tofauti ilikuwa kiungo muhimu baina ya jamii za watu walio ishi Afrika Mashariki na Kati na wageni kutoka Mashariki ya Mbali, Mashariki ya Kati na Ulaya. 

Vivo hivyo, kwa Dar es Salaam, katika kipindi cha nusu ya pili ya karne ya ishirini, hususani kuanzia miaka ya 1960s, mji huu ulikuwa kitovu cha siasa za ukombozi wa bara la Afrika na hivyo kuvutia shughuli za wakubwa wa dunia zilizokuwa zikiendelea kushawishi mataifa ya Afrika kutumikia pande zao zilizokuwa zikihasimiana.

Dar kama makutano ya mikakati ya kisiasa

Hata kabla ya Dar es Salaam kufanywa kuwa makao makuu ya Kamati ya ukombozi kusini mwa bara la Afrika mwaka 1963, tayari wapigania uhuru kutoka maeneo mbalimbali walishaanza kuwasili na kuifanya Dar es Salaam maskani yao. 

Wapigania uhuru wa Afrika Kusini, wakiwemo baadhi ya wanachama na viongozi wa ANC, SACP na PAC, na wapigania uhuru kutoka Msumbiji wa vyama vya MANU, UDENAMO na UNAMI walioungana na kuunda chama cha FRELIMO Juni 25, 1962, tayari kwao Dar es Salaam ilikuwa ni Paradiso ndogo baada ya kukimbia mateso ya nchi zao zilizokuwa bado ziko chini ya ukoloni na ubaguzi wa rangi.

Mwandishi wa habari kutoka Poland, Ryszard Kapuściński wakati akifanya kazi zake hapa Afrika Mashariki kati ya mwaka 1962 na 1965 anasema kwamba halikuwa jambo la kustaajabisha ukiwa kwenye kilabu cha pombe au mgahawa  ukajikuta meza ya pembeni yako watu wakijadili mambo kuhusu kuikomboa nchi yao au wakijitahmini na wakipanga mikakati ya vita vya ukombozi kwenye nchi zao. 

“Unaweza ukajikuta umeketi meza moja na [Eduardo] Mondlane kutoka Msumbiji, [Keneth] Kaunda kutoka Zambia, [Robert] Mugabe kutoka Rhodesia [sasa Zimbabwe],” anaandika Kapuściński kwenye kitabu chake The Shadow of the Sun, My African Life. “Au wakati mwingine ukajikuta umeketi na [Abeid Amani] Karume kutoka Zanzibar, [Dunduzu] Chisiza kutoka Malawi na [Sam] Nujoma kutoka Namibia.”

Hiyo ndio Dar es Salaam ya miaka hiyo ambayo mitaa kama ya Nkrumah ndipo ilipokuwa ngome ya vyama vya ukombozi kwani ndipo zilizopopatikana ofisi za FRELIMO, ANC, ZANU, ZAPU na SWAPO. 

Kilomita tano kuelekea magharibi nje kidogo ya mjini kuna vilima vinavyotazama jiji, hapo ndipo kilipojengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho miaka hiyo kilikuwa ndio kitovu cha minyukano ya  kifikra ya wasomi kuhusu siasa za ulimwengu na hatma ya Afrika. 

Chuo hiki kilikusanya wasomi wakimaendeleo, au progressive scholars kama wanavyojulikana kwa kimombo. Walikuwa wakitoka pande mbalimbali za dunia, wakimwemo Walter Rodney, Yash Tandon, Milton Santos, John Ilife nakadhalika. Minyukano hii ya kifikra hapo UDSM ilitoa hamasa sana kwa vuguvugu la ukombozi lilokuwa likiendelea wakati huo.

Siasa za Vita Baridi na msimamo wa Nyerere

Vyama vingi vya ukombozi kusini mwa Afrika vilipata uungwaji mkono kutoka nchi za Kikomunisti zaidi tofauti na nchi za magharibi ambazo nyingi zilikuwa na maslai ya moja kwa moja na makoloni yaliyokuwa Afrika. 

Kitendo hiki kiliwapa hofu kambi ya nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani kuhofia mataifa ya Afrika kujiunga na kambi ya nchi za Kikomunisti. 

Hii ilipelekea  Dar es Salaam, ambako ndio yalikuwa makao makuu ya harakati za ukombozi, kuangaliwa kwa jicho la kipekee na mataifa yote ya magharibi na ya kikomunisti. Mfano, mwandishi George Roberts anaeleza kuwa mwaka 1965 wakati balozi mpya wa Marekani alipokuwa akipewa maelezo kwa ufupi kabla ya kuelekea Tanzania kama balozi mpya wa Marekani, Shirika la Ujasusi la nchi hiyo CIA lilimweleza balozi huyo kuwa kipaumbele chao cha juu katika bara la Afrika ni kuongeza idadi ya maafisa wa ujasusi na shughuli za ukusanyaji taarifa nchini Tanzania. 

Pia mwandishi Roberts anaeleza, kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali za Shirika la Ujasusi la Shirikisho la Kisovyieti KGB, shirika hilo lilikuwa bingwa wa kuchapisha vipeperushi feki kama njia ya kueneza propaganda dhidi ya mahasimu wao Marekani na washirika wake, na baadae dhidi ya China. 

Vitendo hivi vinadhihirisha ni kwa kiwango gani kulikuwa na minyukano ya kijasusi na kidiplomasia baina ya wakubwa hao katika jiji la Dar es Salaam. 

Hii ndio hali ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla ilivyokuwa. Kwa upande mmoja mashirika kama CIA, MI16, KGB na STASI yalikuwa yakiendelea na minyukano yao, upande mwingine nchi ilikuwa hatarini dhidi ya hujuma na mashambulizi kutoka kwa Makaburu, Wareno na Walowezi wa Zimbabwe ambao waliiona Tanzania kama adui kwa kuwa ilihifadhi wapigania uhuru.

Hata hivyo, minyukano ya wakubwa hao, pamoja na hatari yote ya kuhifadhi wapigania uhuru, haikudhohofisha msimamo wa kiongozi wa nchi zilizokuwa mstari wa mbele, Julius Nyerere na msimamo wa Tanzania kwa ujumla. 

Mathalani, wakati fulani Tanzania na vyama vya ukombozi viliposhutumiwa kutumiwa na kambi ya nchi za Kikomunisti katika vita baridi kwa sababu tu ya misaada waliyopata toka nchi hizo, Nyerere alimwandikia Rais wa 38 wa Marekani Gerald Ford barua kuelezea msimamo wa Waafrika kwamba, vyama vya ukombozi vinapokea silaha na misaada kutoka nchi za Kikomunisti ni kwa sababu ndiko wanakoweza kupatiwa silaha kukomboa nchi zao. 

Mwalimu Nyerere alieleza  kwamba nchi za magharibi hazija wapa silaha na hazina mpango wa kuwapa silaha wapigania uhuru, kwa nini sasa wakatae misaada kutoka nchi zilizo tayari kuwasaidia katika mapambano yao ya ukombozi? Huo ndio ulikuwa msimo wa Tanzania ambao kwa kiasi kikubwa ulitokana na diplomasia ya ukombozi iliyokuwepo wakati huo na msimamo wa kutofungamana na upande wowote.

Rumourville

“Ukiwa mjini Tabora watu wanajadili zao la tumbaku na bei katika soko. Ukienda Mwanza, wanajadili zao la pamba na bei zitakuwaje sokoni. Ukienda Mtwara wanajadili korosho […] lakini ukija hapa Dar es Salaam watu wanajadili watu.” Haya ni maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akihutubia wananchi Uwanja wa Taifa mwezi Aprili 1964, akionya hatari ya propaganda na habari za majungu zilizokuwa zimekithiri Dar es Salaam katika kuhatarisha amani na maendeleo ya taifa.

Matukio ya vipeperushi vya propaganda kusambazwa mitaani vikimshutumu kiongozi fulani kula njama au nchi fulani kula njama dhidi ya Serikali lilikuwa jambo la kawaida sana kwa Dar es Salaam. 

Wakati mwingine sio tu vipeperushi, hata vyombo vya habari hususani magazeti wakati huo, yalikuwa sehemu ya wachapishaji wa visa na mikasa hiyo katika jiji lilokuwa linafukuta vuguvugu la siasa za ukombozi, propaganda za vita baridi na minyukano ya kisiasa ya ndani ya chama cha TANU ambacho ndio kilikuwa kinaongoza nchini Tanzania wakati huo.

Dar es Salaam haikuwa imepoa kama tusemavyo vijana wa sasa. Jiji halikuisha visa vya wanasiasa, watumishi wa umma na watu mashuhuri kurushiana vijembe kimkakati. Hilo ilikuwa jambo la kawaida, huku wananchi jioni kwenye mabaraza yao hawakuisha kujadili yaliyojiri kila uchwao.  

Au ndio tuseme  moja ya vitu vinavyoitambulisha Dar es Salaam hivi sasa, kama vile kukithiri kwa habari za udaku, kiki, majungu na kujadili watu badala ya masuala ni moja ya athari za kihistoria za jiji hili?

Joel Ntile ni Mwanamajumuhi wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @NtileJoel. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts