The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mwalimu Mbaroni Kwa Kujihusisha Kimapenzi na Mwanafunzi Wake

Ni mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Chipanga, wilyani Bahi aliyebainika akijihusisha na mapenzi na mwanafunzi wake wa kidato cha tatu.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Polisi wilayani Bahi jijini hapa wanasubiria maelekezo kutoka kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya hatua gani wachukue dhidi ya mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Chipanga anayedaiwa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka shule hiyo.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Bahi Idd Ibrahim ameieleza The Chanzo kwamba polisi wilayani humo ilishakamilisha uchunguzi dhidi ya mwalimu huyo aliyefahamika kwa jina la Philipo Lebabu na kwamba ngazi iliyofuata ni kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushauri hatua stahiki za kuchukuliwa.

“[Taarifa za tukio hilo] zilitufikia na [mtuhumiwa] aliwekwa mahabusu [lakini] akapata dhamana,” alisema OCD Ibrahim, akisema kosa la mtuhumiwa linadhaminika. “Jalada limepelekwa kwa [Ofisi ya] Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya maamuzi.”

Taarifa za mwalimu huyo kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 20 ambaye jina lake tunalihifadhi ziliibuka takriban wiki mbili zilizopita baada ya mmoja kati ya watu waliokuwa karibu na suala hilo kuitaarifu The Chanzo kuhusiana na jambo hilo, akitaka The Chanzo iingilie kati akidai kuna dalili za haki kutotendeka dhidi ya binti huyo.

Mdau huyo alidai kwamba kulikuwa na dalili za ‘mchezo’ kutaka kuchezeka kwenye sakata hilo wenye lengo la kumuondolea mshukiwa hatia na hivyo kumnyima mwanafunzi huyo haki anayostahiki.

Mnamo Septemba 7, 2021, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu alibainisha kwamba jumla ya walimu 285 kati ya walimu 10,115 walifikishwa katika Tume ya Utumishi wa Ualimu (TSC) kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi na wanafunzi katika kipindi cha miaka minne, akiahidi “kutomvumilia mwalimu yoyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo.”

Kwa mujibu wa maelezo ya mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma kidato cha tatu, Lebabu alikuwa “akimfukizia” kwa siku nyingi mpaka alipokuja mkubalia mnamo Juni 2021. Kuanzia kipindi hicho, binti huyo anasema kwamba alianza kwenda nyumbani kwa mwalimu wake na kulala huko huko pamoja na kufanya mapenzi. 

Lebabu alikuwa akimtunza binti huyo kwa kumnununulia baadhi ya mahitaji yake ya msingi kama vile mafuta, sabuni pamoja na mahitaji mengine, binti anadai.

“Mimi nilikuwa nakaa kwa shangazi yangu,” anasimulia binti huyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo. “Nilikuwa natoka usiku naenda kwake [kwa mwalimu Lebabu] narudi kwa shangazi. [Shangazi] alikuwa anajua maana nilikuwa naomba simu ya shangazi kuwasiliana na mwalimu.”

Hata hivyo, binti huyo anadai kwamba hakufanya kitendo hicho kwa kulazimishwa, na alifanya kwa utashi wake, ingawaje anafahamu kwamba alitenda kosa. Anaiambia The Chanzo: “Mimi naona tu nilikosea maana nilienda mwenyewe. Namaanisha sikulazimishwa. Na kusema ukweli bado tu ninampenda [mwalimu Lebabu].”

Hilda Mwaluko ni mama mzazi wa mwanafunzi  huyo anayesema kwamba alimpeleka binti yake kuishi kwa mjomba wake kutokana na umbali wa shule uliokuwepo. Anasema  alienda kwa kaka yake na kumuambia kuwa binti yake anahitaji kuishi pale na ndipo kaka yake alimkubalia kuishi pale.

“Roho yangu inaniuma,” Mwaluko anasema kwa masikitiko baada ya kupewa taarifa za mahusiano ya kimapenzi ambayo binti yake alikuwa akijihusisha na mwalimu wake. “Mtoto anaingia kidato cha mwisho ina maana [huyu mwalimu] amemuharibia. Ninatamani mwanangu aendelee kusoma. Natamani kuona mwalimu anapata adhabu yake ya kufungwa.”

Songora Mganga, baba mzazi wa mtoto, alikuwa na haya ya kusema kufuatia kadhia hiyo: “Mimi kama mzazi kwa kweli limeniumiza hata nguvu sina. [Hili jambo] limeniumiza sana. Mimi nimejitoa kumsomesha toka darasa la kwanza na kumfikisha mpaka sekondari. Nilikua na furaha tu. Lakini baada ya kupata hizi taarifa nimenyong’onyea kweli. Mimi sina mamlaka zaidi lakini naiomba Serikali inisaidie.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *