Dar es Salaam. Hii ni sehemu ya tatu na ya mwisho ya mahojiano maalum kati ya The Chanzo na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 27, 2021.
Kwenye sehemu hii, Mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini anaeleza tathmini yake ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika ambayo kilele cha maazimisho ya sherehe hizo yatafanyika Disemba 9. Zitto anasema kwamba juhudi nyingi katika kipindi hiki cha miaka 60 zimeelekezwa kwenye kujenga nchi badala ya kujenga taifa.
Anadai kwamba miaka 60 ya uhuru bado kuna wananchi nchini Tanzania wana hali zile zile za maisha walizokuwa nazo wakati nchi ikijipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Zitto pia anagusia changamoto ambazo Kituo cha Demokrasia Tanzania, ambacho yeye anakiongoza kama Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, kimeshindwa kufanikisha kuandaa mkutano wake wa haki na maridhiano ambao licha ya kupangwa ufanyike Oktoba na kupelekwa mbele mpaka Novemba mkutano huo bado haujafanyika.
Mwanasiasa huyo pia anafunguka kuhusu hatua yake tata ya kuweka ukomo wa watu wanaoweza kujibu kwenye machapisho yake anayoyaweka kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, kufanya kwamba wale tu anaowafuatilia kwenye mtandao huo ndiyo wanaoweza kujibu kwenye machapisho hayo.
Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya The Chanzo na Zitto Kabwe.
The Chanzo: Watu wanasema unampenda Rais Samia [Suluhu Hassan].
Zitto Kabwe: Simchukii Rais Samia.
The Chanzo: Lakini kama kiongozi wa nchi anakukosha?
Zitto Kabwe: Simchukii Rais Samia.
The Chanzo: Sawa. Tunaenda kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru, tarehe 9 Disemba 2021. Ni miaka 60 ya mambo mengi tangu tuondokane na ukoloni wa Waingereza. Unaitathimini vipi hii safari ya uhuru wewe kama kiongozi wa kisiasa, hususani linapokuja suala la wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe?
Zitto Kabwe: Kwanza, ni dhahiri kwamba tulipata uhuru, tulimwondoa mkoloni. Tunajitawala wenyewe hata kama watawala waliopo hatuwapendi lakini tunajitawala wenyewe. Mifumo yetu ya kidemokrasia, pamoja na kwamba kinadharia inatupa uhuru wa kufanya mabadiliko ya kiungozi, lakini kiuhalisia Tanzania haijaweza kufanikiwa kufika huko kama ambavyo wenzetu nchi za Kiafrika wamefika.
Zambia wamefika. Malawi wamefika. Kenya wamefika. Lakini sisi ni kama ilivyo Namibia, kama ilivyo Zimbabwe ni kama ilivyo Afrika Kusini. Huwezi kusema kama Uganda kwa sababu wao mabadiliko yamekuwa ni ya mtutu wa bunduki. Lakini safari yetu bado ya watu kuwa na uhuru-, kwa sababu uhuru ni zaidi ya mtu mwenye ngozi kama yako kukuongoza. Uhuru ni pamoja na hali ya mtu unaweza ukasema hawa mimi siwataki, hawanipeleki kama Mtanzania au kama Mtanganyika nawabadilisha nawaweka hawa. Hiyo hali bado hatujaweza kufikia. Kwa hiyo, unaweza kusema Not Yet Uhuru.
La pili, kuna nchi tulikuwa nazo sawa wakati tunapata uhuru. Korea Kusini tulikuwa nao sawa, na kiuhalisia tulikuwa na kipato cha mtu mmoja mmoja kikubwa kushinda Korea Kusini. Malaysia tulikuwa nao sawa. Singapore tulikuwa nao sawa. Leo wenzetu wamepiga hatua kubwa sana. Sisi kuna watu ndani ya Tanzania wako vile vile kama ilivyokuwa mwaka 1961.
The Chanzo: Nini kilitokea?
Zitto Kabwe: Kwa sababu hatujaweza kutumia uhuru wetu kuleta maendeleo ya taifa letu. Mara nyingi ukisikia watu wanaeleza mafanikio ya uhuru watakuelezea zaidi ujenzi wa nchi, sio ujenzi wa taifa. Ujenzi wa nchi ndio mabarabara, madaraja, majengo na kadhalika. Ujenzi wa taifa ni kulifanya taifa lilostaarabika, taifa ambalo lina wananchi ambao wameelimika na wanatumia elimu yao kukabiliana na mazingira yao kufanya taifa lao liwe na maendeleo zaidi.
Kwa hiyo unaweza kusema ujenzi wa taifa ni software na ujenzi wa nchi ni hardware. Na sijui, labda wanasayansi na watafiti wanaweza wakalitafiti hili, labda sisi [Watanzania] ni wapenzi wa vitu vinavyoshikika zaidi kuliko vitu visivyoshikika. Yaani ni wapenzi wa hardware [kwamba] uone daraja ulishike, uone barabara uishike na sio wapenzi wa vitu ambavyo huwezi kuvishika.
Taifa ambalo limeelimika hulishiki utasema, lakini hushiki, na taifa liloelimika hata vitu vya kishenzi shenzi huwezi kuviona. Sasa ukitazama maendeleo ya wenzetu na sisi unajiuliza nini kilitokea? Sio kwa Tanzania tu ni kwa Afrika. Je, ni tatizo la uongozi? Kwa sababu mimi naamini kiwango cha umaskini kilichopo kwenye nchi zetu ni chaguo la viongozi na sio laana ya Mungu au Mungu amependa. Ni tumechagua kuwa maskini. Kwa sababu wenzetu ambao hawakuchagua wamepiga hatua na hamna rocket science.
Ukitazama Singapore maendeleo yao ni kwa kupitia biashara, na kwetu sisi Zanzibar ina nafasi kubwa ya kufanikiwa kupitia biashara kuliko hata hiyo Singapore kwa sababu wao [Singapore] hawana bara, sisi tuna maziwa makuu yote ambayo wangeweza kutumia jiografia yetu kwa mafanikio yao. Ukiangalia leo Malaysia ni kilimo, kilimo chenyewe cha mawese, mawese yenyewe mbegu wamezichukua Tanzania miaka ya 1960s lakini leo Malaysia wapo mbali sana.
Kwa nini sisi kilimo hakijatuinua, wao [Malaysia] hawana korosho, sisi tuna korosho. Hawana chai, sisi tuna chai. Hawana kahawa, sisi tuna kahawa. Hawana pamba, sisi tuna pamba. Kwa hiyo tunacho walichonacho na zaidi ya mara nne ya ambavyo sisi tunavyo wao hawana. Sasa ni nini kimetokea? Kwangu mimi ni uongozi, ni uongozi tu. Ni aina gani ya uongozi tunauhitaji? Ni kitu ambacho bado Watanzania hatujaweza na kwa hali ilivyo tunaweza kuwa hivi hivi miaka 60 ijayo.
The Chanzo: Asante sana tumalizie. Nini kimekwamisha mkutano wenu wa Haki na Amani ambao Kituo cha Demorasia Tanzania (TCD) ambacho nyie ACT-Wazalendo mnakiongoza kwa sasa na mlitangaza mkutano utafanyika Oktoba lakini ikapita, Novemba imeisha hiyo. Nini kimekwamisha?
Zitto Kabwe: Wala Novemba hautafanyika, wala Disemba hautafanyika labda kuna uwezekano ukafanyika Januari [2022]. Kwa sababu mara baada ya sisi kutangaza mkutano, Msajili wa Vyama [vya Siasa Francis Mutungi] alitangaza mutano wake na zikagongana tarehe. Baadaye tukaona kwamba tumpishe, busara inataka tumpishe afanye wake sisi tuandae wetu baadaye, akashindwa kufanya wake.
Sasa juhudi zetu, unajua TCD ni chombo kinachoongozwa na muafaka na Mwenyekiti wa TCD hana nguvu za kiutendaji, yeye anatekeleza maamuzi ya kikao cha TCD kinachojumuisha vyama vyote CCM, CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na sisi ACT-Wazalendo. Lakini kitu ambacho kama TCD tuliamua tufanye kwanza ni tukamilishe michakato ya ndani ya mabadiliko ya TCD. Nadhani unafahamu kwamba tunaajiri Mkurugenzi Mtendaji na tunatengeneza mpango mkakati. Tulikuwa tunafanya ukaguzi maalumu wa fedha za TCD ili Mkurugenzi Mtendaji mpya aweze kukuta kila kitu kipo mezani aweze kuanza kufanya kazi bila kuangalia nini kilitokea wapi. Tukaona kwamba tumpe nafasi Msajili kufanya anachojaribu kufanya kwa sababu hatutaki kushindana. Sisi tunaona kama TCD sio mshindani wa Baraza la Vyama [vya Siasa] bali inajazilishia kazi ambazo Msajili anapaswa kuzifanya ili kuhakikisha kuna demokrasia na ajenda za viongozi kwenye TCD ni nyepesi sana, turudi kwenye utaratibu wa demokrasia, vyama vifanye shughuli zao za kisiasa bila bughuza. Viongozi wa kisiasa ambao wana kesi za kubambikiwa ziondolewe mahakamani ili viongozi waweze kukaa, twende mezani, ajenda zetu ni hizo tu.
Turudi mezani. TCD ni chombo cha mazungumzo. Ni chombo cha majadiliano. Naamini mara baada ya kuwa shughuli za Msajili Vyama kuwa zimekamilika tutaweza kuendelea na shughuli zetu. Nazungumza na wenzangu mara kwa mara. Hivi leo tunavyoongea kamati ya ufundi ya TCD wapo Dodoma kuna kazi ambayo wanaifanya. Kwa hiyo, shughuli bado zinaendelea lakini tumeona mkutano huu ili uwe na maana ni lazima uwe kweli ni mkutano ambao utaleta watu pamoja ili tuweze kurudi kwenye njia ya demokrasia ambayo ndio njia sahihi ya kuweza kufanya.
The Chanzo: Kaka Zitto mimi nakushukuru sana.
Zitto Kabwe: Umeacha swali moja ulinambia utaniuliza. Kwa nini nimeondoa chagua la watu kukujibu kwenye ukurasa wangu wa mtandao wa kijamii wa Twitter?
The Chanzo: Ndiyo, tumalizie na hilo. Nimesahau mambo ni mengi unajua. Ni swali muhimu sana maana wewe ni kiongozi wa kiasa na umewahi kuwa mbunge na inafahamika wewe ni mmoja wa viongozi wachache mnaotambua namna mitandao ya kijamii inavyoweza kuwasogeza wananchi na viongozi wao iwe kwenye uwasilishaji wa malalamiko au uwajibishwaji wakati mwingine. Sasa kipindi cha hivi karibuni nimeona kitu kwenye machapisho yako unayoweka kwenye mtandao wa Twitter umezuia wengine kujibu ila wale tu ambao umefuata kurasa zao. Hii hatua imechochewa na kitu gani?
Zitto Kabwe: Kwanza wewe unafahamu kwamba mimi nashiriki sana kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter toka nimeingia zaidi ya miaka 10 sasa kutoa taarifa ambazo zingine hazipo kwenye kikoa cha umma nilipokuwa bungeni hata nje ya Bunge. Lakini pili, nimekuwa nikitumia kupata mawazo ya watu, kuona nchi inafikiri nini angalau kwa hilo kundi la watu ambao wapo Twitter ambao nadhani unafahamu watumiaji wa Twitter walio hai ni takribani laki tano. Ni sampuli ya kutosha kuona namna gani nchi inaenda na kadhalika. Nimekuwa si mtu tu ninayetuma machapisho yangu lakini pia najihusisha kwenye vitu vya watu wengine, nina unga mkono kampeni za watu wengine, nina toa maoni hata kwenye machapisho ya kawaida ya michezo, burudani na kadhalika bila tatizo lolote.
Lakini pia ni vizuri watu kufahamu mimi ni binadamu. Licha ya mimi kuwa kiongozi, mimi ni mwanadamu. Kuna nyakati unaona kitendo cha kujiweka karibu sana na watu kwenye mitandao ya kijamii kinatumika vibaya, na inafanyika makusudi kabisa. Sasa una machaguo, eidha uondoke kama alivyofanya Rais [wa Kenya Uhuru] Kenyata au ubaki kwa kuweka kikomo [kwa baadhi ya watu]. Mimi kuondoka naona sio sahihi, nina watu milioni moja na laki nne ambao wananifuata, nadhani ndio mwanasiasa ninayefuatwa na watu wengi zaidi kuliko mwanasiasa yoyote nadhani, sijatazama takwimu.
Mara ya mwisho nadhani baada ya Rais [wa awamu ya nne Jakaya] Kikwete mimi ndio nilikuwa nafuata kwa idadi ya watu waliokuwa wananifuata. Kwa hiyo, nilisema nikiondoka nitakuwa siwatendei haki hawa walionifuata, na wamenifuata kwa sababu mbalimbali. Sasa unafanyaje, unajua ukiachia wazi kuna watu watakuja watakutukana tu, watakukebehi hata kwa vitu ambavyo havina msingi. Ndio, unaweza ukavumilia lakini kuna mambo unaweza usivumilie.
The Chanzo: Si unaweza ukaacha usisome?
Zitto Kabwe: Tatizo langu mimi ni kwamba napenda kusoma. Hata ukijaribu kutosoma kuna wakati unasoma na unafadhaika kweli kweli. Kwa hiyo, Zitto kama binadamu wa kawaida ameweka kikomo kwa watu wanaoweza kujibu machapisho yake kwenye ukurasa wa Twitter.
The Chanzo: Kwa nini unadhani huu ni uamuzi sahihi?
Zitto Kabwe: Naamini unanipa amani. Sio kila chapisho la Twitter nafanya hivyo, kuna ambayo naachia mtu yoyote anaweza akajibu. Kuna machapisho ambayo naweka kikomo kwa niliowafuata tu ndio wanaweza kujibu, na kuna machapisho niliowataja tu ndio wanaweza kujibu. Kwa hiyo, hayo ni machaguo yaliyopo kwenye Twitter na mimi nayatumia kwa amani. Nadhani Khalifa utafurahi kushirikishana na kiongozi ambaye ana amani kuliko mwenye msongo wa mawazo.
Nafahamu watu ambao wameathiriwa sana kisaikolojia na namna mitandao ya kijamii inavyowajibu. Sio jambo la ajabu kuwa watu wanaozuia watu kabisa kwamba sitaki nione huyu mtu anacho kiandika. Nimekuwa najaribu hivyo. Nimekuwa njisikia vibaya kuwazuia kabisa watu, kuna watu niliwazuia nimeenda kuwaondolea hilo zuio kwa sababu sijisikii vizuri kwa sababu nimefuatwa na watu zaidi ya milioni moja na laki nne kwa hiyo sio watu wote hawa wananipenda, wengine wanataka tu kuona nimeandika nini.
The Chanzo: Ni kweli. Kwa sababu kama ulivyosema ni kwa sababu huwa unasoma mpaka ukafikia huo uamuzi wa kuweka kikomo cha watu wanaojibu machapisho yako. Unadhani hayo matusi yanakuwa yanachochewa na nini?
Zitto Kabwe: Mimi sijui, hilo ni jambo lakuuliza wanaotukana. Lakini wewe unajua, na bahati nzuri mimi ni mzoefu kwenye mitandao ya kijamii, sihangaishwi sana na matusi sababu mimi nilishatukanwa sana sana. Sidhani kama kuna mwanasiasa nchi hii ametukanwa sana kama mimi na bado nasonga mbele. Muda mwingine unatukanwa na watu unaowaheshimu, unajua ni kupishana kimtazamo tu. Lakini kuna wakati unaona kabisa kuna lengo hapa, sasa kwa nini uwape watu nafasi ya kufanikisha lengo lao kupitia wewe.
The Chanzo: Lengo gani?
Zitto Kabwe: Sijui, lakini unaona kabisa hapa kuna lengo. Sasa kuna njia nzuri, ndio maana Twitter wameweka hayo machaguo. Sababu pia ni muhimu kufahamu lile ni eneo langu la faragha.
The Chanzo: Nina shauku sana ya kujua wanakulenga kwa sababu gani. Au ni kwa sababu ya madai huko Twitter kwamba wewe ni kibaraka wa Chama cha Mapinduzi?
Zitto Kabwe: Hayo ni madai ambayo nimekuwa nikipewa kwa muda mrefu sana na wala hayanisumbui kwa sababu ni madai ambayo hayana msingi wowote. Ni maneno tu ambayo watu wanayatoa. Ni kitu ambacho hakinisumbui kabisa. Kwa sababu kwanza si kweli, kwa sababu rekodi yangu ya kazi ni dhahiri na watu wanaiona sihitaji kujisema katika hilo. Lakini pia ni kawaida mwanasiasa kupewa majina sio jambo linaloweza kunisumbua.
Mimi nimedhani kwa ajili ya amani ya akili yangu nimeamua kuweka hiko kikomo. Kuna wakati watu watakuwa na uhuru wa kujibu wanachotaka katika kitu nimekiandika na kuna wakati nitataka hiki kisijibiwe na mtu yoyote nataka tu niandike mawazo yangu watu wasome, anayetaka kusoma asome asiyetaka asisome. Lakini pia watu wana uhuru wa kunizuia, wasione ninachochapisha sababu pia simlazimishi mtu kusoma ninachoandika au mtu kuja kujibu ninachokitaka.
Lakini mimi nashirikishana na watu, nawajibu watu, natania watu, nacheka ana watu. Kwa hiyo, mtu ambaye anadhani hahitaji anaweza akaniwekea kikomo pia.
The Chanzo: Unasema haya madai hayana msingi wowote lakini unadhani yanaweza kuwa yamepunguza kwa kiwango chochote ushawishi ulionao kwenye jamii labda na kwenye siasa zetu za nchi?
Zitto Kabwe: Ninajuaje sasa? Jana tu jambo ambalo nimelipigana sana limefanywa [la watoto wanaolazimika kuacha masomo kwa sababu ya ujauzito wanaendelea na masomo kupitia mfumo rasmi]. Maana ushawishi kwenye siasa ni pale ambapo vitu ambavyo umekuwa ukivisimamia wale wenye uwezo wa kufanya eidha ndani ya Serikali au nje ya Serikali wanafanya.
Mimi naamini ushawishi wangu wa kisasa sahizi ni mkubwa sana kuliko wakati wowote ule. Ninachosema kinasikilizwa na ninaona kinafanyiwa kazi. Nafikiri nina ushawishi mkubwa zaidi. Usisahau naongoza chama cha siasa ambacho upande wa pili wa muungano kiko sehemu ya Serikali [ACT-Wazalendo ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar].
The Chanzo: Huwa unazingatia hasa kwenye mtandao wa Twitter kama mtu mwenye wafuasi milioni moja, unachapisha kitu ndani ya saa moja unakuta kimependwa na watu sitini, unazingatia hiko kama kipimo cha ushawishi wako?
Zitto Kabwe: Hapana nenda kwenye kipengele cha shuhuli za ukurasa wangu, angalia watu wangapi wanasoma, wangapi wanashiriki kwenye hayo machapisho. Kwa hiyo, kuna watu wanadhani utapima ushawishi wako Twitter kwa kuangalia wangapi wamependa chapisho lako au wameshirikisha wengine chapisho lako, hapana. Unapima kwa kuangalia namba za takwimu, nenda kwenye kipengele cha shughuli za ukurasa ambazo unaweza kuziona wewe tu, na hili ni somo linalotakiwa kufahamika na wengi.
The Chanzo: Unadhani watu wanakuangalia sawa sawa siku hizi ukilinganisha na walivyokuwa wanakuangalia zamani, Zitto yule?
Zitto Kabwe: Mimi sijui, sio jambo la msingi kwangu kujua. Muhimu mimi naamini ninachokifanya ni sahihi. Siku nikipata mashaka na kusema ninachofanya sio sahihi, huo ndio muda ambao nitabadili mwelekeo wangu. Lakini mimi naamini kuna muda kiongozi lazima ajitokeze, na anaweza akarushiwa kila aina ya mambo na ndio maana kuna kitu napenda kusema mara kwa mara kwamba usipoongoza?
The Chanzo: Utaongozwa.
Zitto Kabwe: Kiongozi anapaswa kuongoza. Kiongozi anatakiwa kuja mbele ya watu na kuna wakati utaenda mbele za watu na watu wasikutambue. Kwa hiyo, kuna nyakati nimefanya makosa, na kuna wakati nimepatia. Kwa hiyo, unajifunza kupitia hivyo. Kwa hiyo, kuondoa kwangu uwezo wa watu kujibu machapisho yangu hakuna uhusiano wowote na namna gani watu wananitazama. Zaidi zaidi kuna uhusiano na afya yangu ya akili.
The Chanzo: Afya ya akili, utulivu.
Zitto Kabwe: Hicho ni kitu muhimu sana.
Fuatilia pia:
Zitto Kabwe: Taasisi za Kimataifa Zina Nguvu Sana Tanzania Kuliko Watanzania