Tembo wa Zawadi Kutoka kwa Nyerere Kwenda kwa Rais wa Ireland Alivyoibua Mzozo wa Kidiplomasia

Ireland yagoma kuirejeshea Tanzania fedha ilizotumia kumsafirisha tembo kwa ndege kwenda Ireland, licha ya Tanzania kudai kwamba Ireland iliahidi kulipia gharama hizo.
Na Mwandishi Wetu30 December 20211 min

Dar es Salaam. Mahusiano kati ya Tanzania na Ireland yaliingia dosari baada ya Serikali ya Ireland kugoma kulipia gharama za usafiri wa ndege kwa ajili ya tembo ambaye Rais Julius Nyerere alikuwa amemzawadia Rais Patrick Hillery wa Ireland wakati huo.

Hii ni kwa mujibu wa nyaraka za kidiplomasia zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland kwenda kwenye Idara ya Nyaraka ya taifa hilo la Ulaya.

Nyerere alimzawadia Hillery tembo huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu aliyepewa jina la Mimi kama zawadi mwaka 1979 wakati Hillery alipotembelea Tanzania, vyombo mbalimbali vya nchini Ireland vimeripoti.

Mimi alisafirishwa mpaka Dublin, mji mkuu wa Ireland mnamo mwaka 1980, na moja kwa moja alipelekwa Dublin Zoo, ambayo ni nyumba ya kuangalia wanyama, nyaraka hizo zinadai.

Lakini utata ulikuja pale Tanzania ilipoanza kudai kurejeshewa gharama ilizotumia kumsafirisha kwa ndege tembo huyo na hatua ya Serikali ya Ireland kugoma kulipa deni hilo.

“Ubalozi [wa Ireland nchini Tanzania] utakumbuka kwamba Serikali ya Ireland ilibeba jukumu la kulipia gharama za usafiri wa ndege wa tembo mmoja aliyehai aliyekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Ireland kama zawadi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” nyaraka hizo zinamnukuu afisa wa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania akiueleza Ubalozi wa Ireland.

“Ni kutokana na ukweli huo kwamba Wizara inayo heshima ya kuomba kurejeshewa jumla ya Sh66,063, kama gharama za kumsafirisha kwa ndege tembo huyo aliyehai aliyetajwa hapo juu,” afisa huyo alimalizia.

Hata hivyo, nyaraka hizo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Ireland zinasema kwamba maafisa ubalozi wa Ireland walishindwa kujua kama kweli Serikali yao iliahidi kulipia gharama hizo au la.

Maafisa hao walilisogeza jambo hilo kwa Wizara ya Mambo ya Nje ambayo nayo ililisogeza kwa Idara ya Taoiseach, ambayo unaweza kusema kama ni Serikali Kuu.

Idara hiyo, hata hivyo, iligoma kulipa fedha hizo, ikisema kwamba haina fedha kwa ajili ya jambo hilo.

Nyaraka hizo hazielezi ni kwa namna gani jambo hili lilirekebishwa na Serikali za nchi hizo mbili.

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved