Dodoma. Wakati mazungumzo kuhusu Mapinduzi Manne ya Viwanda, yanayohusiana na mapinduzi ya kidijitali, yakiendelea kushika kasi ulimwenguni, waandishi wa habari nchini Tanzania wametakiwa kufuatilia kwa ukaribu mabadiliko hayo na kutumia mbinu za kisasa za kidijitali katika kufanya kazi zao za kila siku.
Wadau wa sekta ya habari na vyombo vya habari ulimwenguni kote wamekuwa wakibainisha umuhimu wa wahariri na waandishi wa habari kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
Hoja kubwa imekuwa ni kwamba kushindwa kufanya hivyo kutawafanya waandishi wa habari kushindwa kuendana na kasi ya karne ya 21 inayoambatana na mabadiliko mengi na ya haraka kwenye namna watu wanafanya kazi zao mbalimbali.
Akiongea na The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwa njia ya simu hivi karibuni, Mtaalam wa Mawasiliano ya Umma na Mratibu wa Programu ya Women In News Tanzania Dk Joyce Bazira alisema kwamba ifike mahala waandishi wa habari wa Tanzania waone fursa zilizopo kwenye mapinduzi ya kidijitali yanayoendelea kutokea duniani, ikiwemo kuibuka kwa mitandao ya kijamii na fursa zinazoambata na mabadiliko hayo.
“Hii simu unayotumia inaweza ikatumika kukufanyia vitu vingi sana,” Dk Bazira anasema. “Ndio ofisi sasa hivi hii. Sasa hivi huhitaji kwenda ofisini ndio uweze kutafuta habari. Unaweza ukatumia hii hii mitandao [ya kijamii] ukapata habari.”
Akizungumzia namna mitandao ya kijamii inavyoweza kuwa ya manufaa kwa mwandishi wa habari, Dk Bazira anasema kwamba si tu mitandao inaweza kumsaidia mwandishi wa habari kupata mawazo ya habari bali pia inaweza kukuza brand yake kama mwandishi wa habari.
“Unaweza ukawa unachapisha vitu vya manufaa,” anasema. “Kwa mfano, sasa hivi watu wote tunahangaika kupata taarifa sahihi kuhusu janga la UVIKO-19. Sasa mtu ambaye anatuchapishia hizi taarifa, mambo mazuri mazuri kuhusu yanayoendelea kwenye hilo eneo, lazima atapata watu wanaomfuatilia. Na watu wakimfuatilia wengi ina maana brand yake inakuwa.”
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uhalisia, au relevance, ya mwandishi wa karne ya 21 unakuja kwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendana na karne hiyo. Kushindwa kuendana na kasi hiyo, si tu kunatishia kazi za waandishi wa habari bali pia inatishia tasnia nzima ya habari.
Wakiongea na The Chanzo kwa nyakati mbalimbali, waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wameonesha uelewa wao juu ya umuhimu wa kwenda na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na nini mabadiliko hayo yanamaanisha kwenye kazi zao za kila siku.
Seleiman Kodima ni mwandishi wa habari na mtangazaji wa kituo cha Dodoma Redio: “Mitandao ya kijamii inatupa wanahabari uwanda mpana kwa ajili ya kufikisha kazi zetu kwenye jamii. Pia, inatuongezea nguvu zaidi ya kupaza kile ambacho ni kusudio la wananchi juu ya matatizo ambayo yanawakabili.”
Winifrida Ngasa ni mwandishi wa habari na mtangazaji wa Redio Joy mkoani Kigoma: “Mitandao ya kijamii hutusaidia kupata mawazo mbalimbali ya habari. Kwa mfano, leo hii wewe ulikuwa umezoea kutangaza kwa maneno yako fulani lakini kupitia mitandao kuna vitu umejifunza kupitia watu wanaotangaza, [na] namna watu wanavyoandika habari. Kwa hiyo, hivyo ni vitu ambavyo mimi naona kama fursa kwa upande wetu sisi waandishi wa habari.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dodoma. Anapatikana kupitia jackline@thechanzo.com.