The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kijana Mlemavu Mwenye Ndoto ya Kuwa Rubani Afaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kwa Kupata Daraja la Kwanza

Augustino Ilomo, kijana mwenye ulemavu wa kuongea na ambaye viungo vyake vya mwili havina uwezo wa kufanya kazi, amefaulu daraja la kwanza, alama 12, huku akifanya vizuri zaidi kwenye masomo ya Kiingereza na Hesabati kwa kupata daraja A.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Unamkumbuka yule kijana mwenye mahitaji maalum Augustino Ilomo ambaye The Chanzo ilichapisha simulizi yake hapa mnamo Disemba 15, 2021, ambapo licha ya kuwa hana uwezo wa kuongea na viungo vyake vya mwili havina uwezo wa kufanya kazi ana ndoto za kuja kuwa rubani hapo baadaye?

Basi kijana huyo anayeishi Tabata jijini hapa yuko mbioni kukamilisha ndoto yake hiyo baada ya kufaulu mtihani wake wa Kidato cha Nne ambao matokeo yake yametoka Januari 15, 2022, ambapo Augustino aliweza kuwashangaza ndugu, walimu, jamaa na marafiki baada ya kupata daraja la kwanza.

“Una furaha kama ile niliyokuwa nayo mimi?” mwalimu wake Augustino, Sylvia Ruambo, alimuuliza mwandishi wa habari mnamo Januari 17, 2022, baada ya kupiga simu akiwa na shauku ya kutaka kuwasilisha habari hizo njema kuhusiana na kufaulu kwa mwanafunzi wake kwa mwandishi.

The Chanzo ilifika nyumbani kwa akina Augustino, 22, mnamo Disemba 9, 2021, kwa ajili ya kufanya mazungumzo naye na wazazi na walimu wake baada ya kupata taarifa za uwepo wa kijana huyo ambaye licha ya hali yake ya kimwili ameamua kuvunja miiko na desturi hasi za kijamii kwa kuamua kujiendeleza kimasomo.

“Tunamshukuru Mungu,” alisema Mwalimu Sylvia wakati wa maongezi hayo mafupi na mwandishi wa habari hii katikati ya kilio cha furaha. “Augustino amefaulu kwa kupata daraja la kwanza. Tunamshukuru Mungu.”

Kwa ufaulu huo, Augustino anakuwa moja kati ya wanafunzi wachache waliofaulu kwa daraja hilo kwenye mtihani huo unaodaiwa kuzalisha zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi wenye ufaulu wa daraja la nne.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk Godfrey Msonde alitangaza mnamo Januari 15, 2022, kwamba kati ya watahiniwa 422, 388, waliopata daraja la nne walikuwa 248, 966 sawa na asilimia 51.46.

Akisomea Shule ya Sekondari Kimanga, Augustino amefaulu kwa kupata daraja la kwanza, alama 12, huku akifanya vizuri zaidi kwenye masomo ya Kiingereza na Hesabati kwa kupata daraja A.

“Nimefurahi, nimefurahi sana” mama mzazi na Augustino, Faraja Kambanyuma, alisema wakati akiongea na The Chanzo kufuatia matokeo hayo.

Mwalimu Sylvia Ruambo, ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha Augustino anapambana na kushinda changamoto mbalimbali ili kupata elimu bora kama watu wengine, anaamini kwamba matokeo hayo yametokana na utayari wa Augustino kuendelea kujitafutia elimu licha ya hali yake ya kimwili.

“Nia aliyokuwa nayo lakini pia utayari wa kusoma na ushirikiano wa walimu,” anabainisha Mwalimu Sylvia ambaye pia ni mtaalamu wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu. “Mimi ninachukulia kuwa chanya kwamba hakuna kisichowezekana mradi nia ipo. Nia ilikuwepo na ndio maana kila kitu kikawezekana tunamshukuru Mungu.”

Ni mategemeo ya walimu na wazazi wa Augustino kwamba matokeo ya kijana wao yatafungua njia ya kujengeka kwa mtazamo chanya dhidi ya watu wenye mahitaji maalum na kuwafungulia njia ya kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Augustino aliiambia The Chanzo mnamo Disemba 9 mwaka jana kwamba yuko mbioni kukamilisha kitabu chake alichokipa jina la The Real Love ambapo ndani yake kinabeba maudhui mbalimbali yanayoihusu jamii zetu.

Baadhi ya mambo aliyoieleza The Chanzo kuwa ameyaangazia katika kitabu chake ni suala zima la walemavu kukataliwa katika jamii zetu lakini pia suala la watoto yatima pamoja na changamoto wanazokumbana nazo.

Inaonekana ni kama vile Augustino amepata msukumo zaidi wa kuendelea kuandika kitabu hicho ambacho kinatarajiwa kutoka Januari mwaka huu.

Lakini kwa sasa, kipaumbele cha Augustino na familia yake ni maandalizi ya kuhakikisha anajiunga na elimu ya juu ya sekondari wakati muhula wa masomo kwa mwaka 2022 utakapoanza.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *