Arusha. Takriban asilimia 77 ya wanawake Watanzania wanaojihusisha na siasa nchini wameacha, au kusimama kwa muda, kutumia mitandao ya kijamii kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni unyanyasaji wa kijinsia uliokithiri ambao wanawake hao wamebainisha kupitia kwenye majukwaa hayo.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia inayojishughulisha na uhamasishaji wa matumizi sahihi na salama ya mitandao ya kijamii yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, Tanzania ijulikanayo kama Women at Web Tanzania na kuchapishwa Januari 17, 2022.
Utafiti huo uliopewa jina la Tathmini ya Unyanyasaji wa Kijinsia Mitandaoni Miongoni mwa Wanawake Walio Kwenye Siasa, ulilenga kubainisha changamoto ambazo wanawake wanasiasa wanazipitia pale wanapotumia mitandao ya kijamii pamoja na kupendekeza njia za kupambana na changamoto hizo.
Asilimia 79 ya wanawake waliohojiwa kwa ajili ya utafiti huo walikiri kuwahi kukutana na unyanyasaji wa kijinsia wakati wanatumia mitandao ya kijamii huku asilimia 47 wakisema hawana uhakika kama wameshawahi kukutana hali hiyo ama la.
Wengi (asilimia 41.7) kati ya wale waliokiri kukutana na unyanyasaji wa kijinsia mitandaoni walisema wameacha kabisa kutumia mitandao hiyo kama njia ya kutatua changamoto hiyo huku asilimia 34.9 wakisema wameacha matumizi kwa muda.
Kwa mujibu wa utafiti huo pia, wanasiasa wengi wanawake (asilimi 43.6) wanataja WhatsApp kama mtandao wa kijamii wanaoupenda zaidi, na wengi wao (asilimia 99.9) wanautaja kama mtandao wanaoutumia mara nyingi kuliko mingine.
Aina kubwa za unyanyasaji ambazo wanawake wanasiasa wamezitaja kwa mujibu wa utafiti huu ni uchokozi wa mtandaoni (asilimia 77), kukera kwa makusudi (asilimia 61), kumvunjia heshima (asilimia 47) na udhalilishaji wa kimwili (asimilia 43).
Ripoti hiyo inawataja wahusika wakuu wa utekelezaji wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia mitandaoni kuwa ni watu wenye ushawishi wanaojulikana kama influencers
Baadhi ya watu hawa, kutokana na kuwa na wafuasi wengi wanaowafuatilia mitandaoni, wamekuwa wakiwalenga na kuwashambulia wanawake wanaojihusisha na siasa kwa sababu ya kutofautiana kimtazamo au itikadi, utafiti huo unabainisha.
Wanasiasa wanawake 394 wahojiwa
Asha Abinallah ni moja kati ya viongozi wa Women At Web Tanzania aliyeieleza The Chanzo kwamba iliwachukua takriban miezi mitano kufanya utafiti huu ambapo jumla ya wanawake wanasiasa 394 walifikiwa na kuhojiwa kama sehemu ya utafiti huu.
“Tulijikita zaidi kuangalia na kuelewa ni kwa nini wanawake wengi ambao wapo katika siasa wanasita kutumia mitandao ya kijamii na ni wachache sana mitandaoni hasa katika ulimwengu ambao leo hii mwanajamii anaweza kuwasiliana kwa wepesi na kwa urahisi na viongozi wake katika mitandao ya kijamii,” anasema Abinallah.
“Sababu nyingine ni kuweza kufahamu na kuhamasisha wanawake ambao wapo katika siasa umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii na ni namna gani wanaweza wakashirikiana ama kuwasiliana na wananchi wao,” ameongeza Abinallah, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Media Convergency, kampuni inayojihusisha na masuala ya ushauri wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano iliyopo Dar es Salaam, Tanzania.
Doricas Matuku ni Katibu wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Chuo cha Bandari Dar es Salaam ambaye licha ya kwamba hajawahi yeye binafsi kupitia vitendo hivyo anadhani ni muhimu kwa mamlaka husika kama vile Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwachukulia hatua watu wanaohusiaka na kuwadhalilisha wanawake mitandaoni, akisema hiyo itawapunguzia hamasa watu wengine kufanya vitendo hivyo.
“[Wadhalilishaji] wanachukulia kama mwanamke ni mtu myonge, kwamba hawezi kufanya lolote hata akifanyiwa nini,” anasema Matuku. “Ndiyo maana watu kama TCRA wanatakiwa kuingilia kati. Lakini elimu pia itolewe [kwa wanasiasa wanawake]. Unakuta wengine hawana elimu [ya namna bora ya kukabiliana na hali kama hii].”
Ukosefu wa elimu
Wanasiasa wanawake wengi (asimilia 73.1) waliohojiwa kwenye utafiti huo walikiri kutokuwa na mafunzo stahiki ya kuwawezesha kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia mitandaoni, huku asilimia 76.9 wakisema wako tayari kupokea mafunzo hayo.
Careen Masawe ni mwanaharakati wa masuala ya kijinsia ambaye anahusisha unyanyasaji wa wanawake wanasiasa mitandao na kasumba waliyonayo baadhi ya watu kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi.
“Mwanamke anaonekana hawezi kusimama kusema jambo mbele ya umma kwa sababu tumeshaonekana kwamba sisi ni viumbe dhaifu kulingana na mtazamo potofu wa Kiafrika,” anasema Massawe.
“Hii inaenda mpaka huko kwenye mitandao ya kijamii. Na inasikitisha kidogo ukizingatia kwamba wanawake wengi sasa hivi wameendelea, wamesoma, na wana mtazamo chanya lakini bado kuna namna jamii haitaki kukubaliana na mabadiliko hayo,” anaongeza.
Akipendekeza namna bora ya kuweza kubadilisha mitazamo hii hasi katika jamii, Massawe anasema ni lazima juhudi zianzie katika ngazi ya famili.
“Mtu asipotengenezwa, asipoona thamani ya jinsia nyengine kuanzia kwenye ngazi ya familia inakuwa ni changamoto kuja kumbadilisha huyo mtu ukubwani,” anasema. “Kwa hiyo ni muhimu juhudi zikaanzia katika ngazi ya familia. Lakini hata shuleni, masomo kama haya yanatakiwa kutiliwa mkazo huko pia.”
Licha ya kwamba utafiti huu unaonesha kwamba zipo sheria na kanuni zinazo simamia na kuratibu shughuli za mitandaoni nchini Tanzania, sheria hizi nyingi hazijagusa moja kwa moja suala la unyanyasaji wa kijinsia mitandaoni.
Hii ndiyo sababu utafiti huu unawataka watunga sera na wadau wengine mbalimbali kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwepo na sheria pamoja na usimamizi madhubuti wa sheria hizo zinazohusiana na unyanyasaji wa kijinisa mitandaoni moja kwa moja.
Iman Hemed ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Arusha, anapatikana kupitia rashidiman377@gmail.com.
One Response
Sawa, Sheria na kanuni za kusimamia maswala ya mtandaoni ni sehemu muhimu ya ku address unyanyasaji wa wanawake mitandaoni, lakini kubwa zaidi ni mabadiliko ya kifikra na mitazamo kwa wote Me na Ke. Ni vema wanawake wakatumia ujasiri zaidi wa kupambana na maovu haya kutoka kwa Me na ambayo hayatumii physical strength. Wanawake wajitokeze na wapambane kwa kujibu mapigo pia.