The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Viti Maalumu Vishindaniwe Kwa Wananchi

Ni muhimu kuanzishwe mfumo mpya utakaofanya wanawake wa vyama mbalimbali wapambane kutafuta kura kwa wananchi moja kwa moja kuliko mfumo wa sasa ambapo viti hivyo vinaonekana kama fadhila au hisani za viongozi  kwa wanawake kuliko stahili yao iliyotokana na uwezo.

subscribe to our newsletter!

Hivi karibuni ilichapwa makala ya kitaaluma na Dk Victoria Lihiru, mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria cha Dar es Salaam iliyojaribu kuonesha udhaifu uliopo katika mfumo wa kuwapata wagombea wa viti maalumu vya wanawake ambao kwa kiasi fulani umechangia kuibuka kwa mgogoro unaoendelea juu ya uhalali wa wabunge 19 waliokuwa wakilisha CHADEMA bungeni ambao wamekanwa na kuvuliwa uanachama na chama chao hicho.

Kwa mujibu wa sheria,mtu hawi mbunge pasi kuwa na chama, lakini Spika wa Bunge aliyepita Job Ndugai, alipuuza uamuzi wa CHADEMA na kuamua kuendelea kuwatambua wabunge hao. Hoja ya Dk Lihiru ni kuwa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imeshindwa kuandaa mfumo unaofanana utumike kwenye vyama vyote na uliowazi wa namna ya kuchagua wabunge wa viti maalum, kama ambavyo  Ibara ya 81 ya Katiba ya mwaka  1977 inavyotaka.

Ibara hiyo ya 81 ya katiba inasema: “Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, Tume ya Uchaguzi yaweza kuweka masharti yanayofafanua utaratibu utakaotumiwa na vyama vya siasa kwa ajili ya kuchagua na kupendekeza majina ya Wabunge wa aina iliyotajwa katika ibara ya 66(1) (b).”

Kwenye chapisho lake hilo, Dk Lihiru anasema kushindwa huko kwa NEC kumefanya vyama vianzishe njia zao za kuchagua viti maalum ambazo hazikidhi viwango vya kimataifa vya Hatua Maalum za Muda Mfupi (TSM). Hali hiyo, anasema imepelekea kushuka hadhi kwa viti hivyo, kuwepo kwa ubaguzi dhidi ya wabunge hao na dharau kwa mfumo huo na hatimaye kuchelewesha kuhitimu kwao kwenda viti vya kawaida.

Alipozungumzia viwango vya kimataifa, Dk Lihiru alikuwa akirejelea Ibara ya 4(1) ya Azimio la Kimataifa la Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) la mwaka 1979 isemayo kuwa hatua za nchi kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake hazitazingatiwa kama ubaguzi wa kijinsia na hatua hizo zitakoma malengo yakishafikiwa.

Pia, alirejea ibara ya 9 ya Makubaliano ya Afrika juu ya Haki za Bianadamu  kuhusu Haki za Wanawake (Azimio la Maputo) ambayo yanataka Serikali zichukue hatua chanya za makusudi kukuza ushiriki wa wanawake katika siasa bila kubaguliwa katika ngazi zote za uchaguzi na wanakuwa wenza wa wanaume katika katika maendeleo na utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo.

Lengo zuri ambalo tija yake inaponzwa na mfumo

Nimesoma makala hiyo ya Dk Lihiru aliyoiita kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, Mgogoro wa mwaka 2020 wa Viti Maalum  Chadema nchini Tanzania: Je Tume ya Uchaguzi Inafuata Sheria, kwa umakini kwa sababu nami huwa nalitafakari jambo hilo mara kwa mara. Katika tafakuri yangu, nilishawishika kuamini kuwa viti maalumu vimeletwa kwa lengo zuri lakini mfumo wa utekeklezaji wake hauleti tija na faida tarajiwa.

Kutokana na kusoma kwangu hapa na pale, ikiwemo makala hii nzuri ya Dk Lihiru, ni wazi kuwa uanzishwaji wa viti maalum ilikuwa ni hatua ya muda iliyolenga kuondoa tofauti kubwa ya uwakilishi kati ya wanaume na wanawake katika vyombo vya maamuzi na pia kuwajengea uwezo wakinamama ili baadae waweze kupambana katika viti vya kawaida vya uwakilishi.

Hatua kama hizi zimewekwa katika maeneo mengine kadhaa, mathalan uteuzi wa wanafunzi kwenda shuleni na vyuoni ambapo ukomo wa chini wa alama za kupitishwa kwa wasichana huwa chini ukilinganisha tofauti na za wanaume. Kadhalika inafanyika hivyo kwenye baadhi ya ajira.

Ni maoni yangu kuwa, kwenye suala hili la viti maalumu bungeni na katika mabaraza ya madiwani, ni muhimu kuanzishwe mfumo mpya utakaofanya wanawake wa vyama mbalimbali wapambane kutafuta kura kwa wananchi moja kwa moja kuliko mfumo wa sasa ambapo viti hivyo vinaonekana kama fadhila au hisani za viongozi  kwa wanawake kuliko stahili yao iliyotokana na uwezo.

Ukiangalia sana, mfumo uliopo wa kuwapata wabunge wa viti maalum, kama alivyoeleza Dk Lihiru, sio tu unaleta migogoro, kama huu wa CHADEMA bali pia huzaa ufisadi. Sio mara moja tumesikia wabunge fulani wa viti maalum wakinasibishwa nafasi walizopata na uhusiano wao aidha wa damu au wa kimapenzi na viongozi wa vyama. Tetesi kama hizi zinashusha hadhi ya hivyo viti mbele katika mtazamo wa umma wa watu.

Michakato ya uteuzi haiko wazi

Tetesi hizi hakika zina mashiko kwa sababu michakato ya kuteua wagombea hawa kwenye baadhi ya vyama haiko wazi. Aghlabu uamuzi wa mwisho wa nani anaenda bungeni hufanywa na vikao baada ya matokeo ya uchaguzi, sio orodha iliyotolewa awali.

Pia, kwa upande mwingine, mfumo wa kuteuana ndani ya chama kwa hakika hautoi mazoezi ya kutosha kumuandaa mwanamke aweze kupambana na wanaume katika uchaguzi wa viti vya kawaida.

Kwa taratibu za vyama vyingi, huchukua kikao kimoja tu cha ndani kuamua nani wanakuwa wabunge wa viti maalum. Kisha, mteule huzunguka na wagombea kwenye kampeni na akipewa dakika tano za kusalimia na kukiombea kura chama.

Mfumo huo,  haufanani kabisa na uzito halisi wa kampeni halisi zinazojumuisha mipango, mikakati, na mfululizo wa mikutano ya kuomba kura kwa wananchi ambapo watamtahmini mgombea moja kwa moja na kuamua kumpa au kumnyima kura.

Hapo tunaona tena umuhimu wa kuwa na wabunge na madiwani wa viti maalumu wanaochaguliwa moja kwa moja na wananchi. Kukiwa na mfumo huo, kampeni anazofanya mwanamke, akipambana na wenzake, zinampa somo kubwa hata kama hatashinda. Na kiuhalisia, hata akishindwa, harakati za kumkomboa mwanamke zimeshinda kwa sababu aliyepita ni mwanamke.

Kwa nini tushindanishe viti maalum?

Mwanamke aliyepata ushindi wa namna hii anajiamini na hawezi kujisikia msindikizaji wa wanaume kwa sababu naye alipambana katika mfumo wa ushindani, akaweza kushawishi wapiga kura na kuwashinda wenzake. Mshindi huyu si kama yule  aliyetegemea  vikao vya chama  vilivyotawaliwa na wanaume kumpa fursa kwa sababu anacheka nao vizuri.

Pia, tusisahau kuwa mwanamke aliyepita kuomba kura uchaguzi mmoja, anakuwa tayari kashajulikana katika uchaguzi ujao kwa wananchi. Si mgeni tena, na anaweza hata kugombea katika viti vya kawaida akapokelewa, kama wananchi walimuelewa.

Kwa upande mwingine, viti maalum kwa mfumo wa sasa hautendi haki kwa wananchi ambao kodi zao zinalipa uendeshaji wa bunge. Kwa mfumo huu, wananchi  hawana fursa ya kuamua moja kwa moja nani aende bungeni miongoni mwa hao wanawake badala yake watu wachache ndani ya chama huamua.

Vilevile, mfumo wa kushindania viti moja kwa moja kwa wananchi unasaidia kuhakikisha ubora wa wale wanaokwenda bungeni. Ni ukweli mchungu kuwa baadhi ya wabunge wa viti maalum ni dhaifu mno, hawana mchango wowote bungeni ukilinganisha na wanawake wengi wenye uwezo ambao wangeweza kwenda kuwakilisha maslahi ya wanawake.

Baadhi huwasikii wakitajwa kuchangia si kwa hotuba wala maandishi. Hii ni kwa sababu hawakuwahi kujaribiwa katika majukwaa ya wazi, mbele za wananchi na mifumo ya uteuzi katika chama si mizuri.

Ushindani utaondosha dharau

Kutokana na udhaifu nilioutaja katika mfumo wa teuzi za wabunge wa viti maalum, nafasi hizi zimedharaulika. Hata neno lenyewe viti maalum, kama ambavyo Dk Lihiru ameonesha pia lina walakini lakini niongeze kuwa pia kwa sasa kijamii lina maana hasi – yaani nafasi za upendeleo, za kubebwa kwa kazi iliyofanywa na wengine.

Katika michezo, Simba akicheza vizuri mashindano ya vilabu vya Afrika, Tanzania ikiongezewa nafasi za ushiriki, hizo nafasi zinaitwa viti maalum katika kuzikoga timu nyingine, hususan watani wao Yanga. Hapa neno viti maalum linamaanisha udhaifu unaohusishwa na mwanamke anayestahili  nafasi za  bila kuzifanyia kazi, za kubebwa.

Njia pekee, kwa maoni yangu, ya kuvipa heshima viti maalumu ni kuvifanya vigombewe nje kati ya wagombea wa vyama na vyama, jaji akiwa ni mwananchi kwenye sanduku la kura. Undani wa namna ya kufanyikisha hilo, nina hakika Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuja na njia.

Ikifanyika hivyo, lengo la kuongeza uwakilishi wa wanawake litafikiwa kama ilivyo sasa, kwa sababu ni nafasi za wanawake na wanashindana wao kwao wao. Lakini muhimu zaidi, wanawake wataonja ladha halisi ya kupigania kiti na kupata mazoezi maridhawa. Nina hakika, katika mfumo huo, wabunge wengi zaidi wanawake wanaweza kuamua kujingiza kwenye kinyang’anyiro cha viti vya kawaida kwa sababu ya mapito magumu waliyopitia yaliyowakomaza kisiasa.

Naamini pia, kwa mfumo huo wabunge wanawake kupitia hivyo watakuwa bora zaidi kwa sababu washajaribiwa. Tukiangalia takwimu, tunaambiwa kuwa kuanzia mwaka 1965 hadi 1980, hakuna mwanamke aliyechaguliwa moja kwa moja kutoka kwenye jimbo. Mwanamke wa kwanza kushinda ilikuwa mwaka 1985, kisha wanawake wawili 1990, na ikiongezeka hivyo taratibu hadi nane mwaka 1995,  12 mwaka 2000, 17  mwaka 2005, 21 mwaka 2010, 25 mwaka 2015.

Hivi sasa miaka 60 baada ya uhuru, na miaka 36 baada ya kuanzishwa kwa viti maalum, wanawake wanaochaguliwa moja kwa moja kutoka majimboni ni chini ya asilimia 10, licha ya viti hivyo kuanzishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Makala nzuri sana. Inaelimisha naomba ingesomwa na wahusika hao ingesaidia sana kuweka wazi utaratibu wa kuchagua badala ya kuteuliwa.
    Nashukuru sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts