Serikali Afrika Mashariki Zatakiwa Kutunga Sheria Kali Dhidi ya Bidhaa za Plastiki

Ripoti hiyo iliyochapishwa Februari 10, 2022, inatoa mapendekezo sita ambayo wanamazingira wanaamini kwamba kama yatatekelezwa vizuri yataifanya EAC kuwa katika viwango vya kimataifa juu ya ulindaji wa mazingira.
Na Mwandishi Wetu16 February 20222 min

Dar es Salaam. Ripoti mpya juu ya uchafuzi wa mazingira unaofanywa na bidhaa za plastiki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imezitaka Serikali za nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutunga sheria na kanuni kali zitakazoangazia siyo tu uzalishaji, uingizaji, matumizi na mauzo ya bidhaa za plastiki bali pia bidhaa zisizo muhimu za plastiki zinazotumiwa mara moja na kutupwa.

Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa kwa pamoja na mashirika ya mazingira ya Flipflopi, ALN Kenya, na Sustainable Inclusive Business inabainisha kwamba EAC inakosa sheria na kanuni zinazoweza kusaidia nchi wanachama wake kudhibiti kwa pamoja bidhaa za plastiki kwenye maeneo ya utekelezaji, malengo ya wazi, viwango na lugha ya kutumia.

Ripoti hiyo iliyochapishwa Februari 10, 2022, inatoa mapendekezo sita ya namna EAC inavyoweza kutatua mapungufu hayo, mapendekezo ambayo wanamazingira wanaamini kwamba kama yatatekelezwa vizuri yataifanya jumuiya hiyo kuwa katika viwango vya kimataifa juu ya ulindaji wa mazingira.

Mapendekezo hayo ni pamoja na haja ya kuanzishwa kwa mfumo wa kisheria wa kudhibiti uzalishaji, uingizaji, matumizi na mauzo ya bidhaa za plastiki; kuuwezesha mfumo na msaada wa kifedha na kiufundi; na kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji utakaorekodi maendeleo na kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa.

Mapendekezo mengine ni uanzishwaji wa miundombinu sahihi ya usimamizi wa taka; kuhamasisha matumizi ya bidhaa endelevu na zinazoweza kutumiwa zaidi ya mara moja; pamoja na kuanzishwa kwa kampeni za kukuza ufahamu miongoni mwa walaji wa bidhaa za plastiki, wazalishaji na wadau wengine muhimu.

“Ni pale tu tutakapoamua kufanya maamuzi sahihi kwa pamoja kuelekea dira moja kwa ajili ya Afrika Mashariki ndiyo tutaweza kuona maendeleo [dhidi ya kupambana na bidhaa za plastiki] ambayo tunayahitaji sana,” inasema sehemu ya ripoti hiyo yenye kurasa 49.

Mnamo mwaka 2019, Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku matumizi ya bidhaa za plastiki, takriban miaka kumi baada ya Serikali ya Zanzibar kuchukua uamuzi kama huo. Lakini wakati ripoti hiyo inabainisha kwamba kumekuwa na matokeo chanya juu ya marufuku hiyo, taarifa za kuonesha ni kwa kiwango gani marufuku hiyo inatekelezwa zimekuwa hazipatikani.

Hali hii wanamazingira wanaamini inachochewa na kukosekana kwa uratibu wa pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki katika kutekeleza marufuku kama hizo. Mashirika hayo yanasema kwenye taarifa yao kwa waandishi wa habari: “Ni muhimu kuwepo kwa sheria moja na hatua shirikishi kwenye kupambana na bidhaa hizi.”

Inakadiriwa kwamba jumla ya tani milioni 300 za bidhaa za plastiki huzalishwa kila mwaka ulimwenguni kote, ambapo nusu ya bidhaa hizo hukusudiwa kwa matumizi ya mara moja kabla ya kutupwa. Angalau tani milioni 14 za plastiki huishia baharini kila mwaka, hali inayopelekea madhara mengine siyo kwa uzalishaji wa samaki tu bali hata afya za binadamu.

Ripoti hiyo ya Flipflopi na wenzake imetolewa kabla ya kikao cha sita cha Mkutano wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa unaotegemewa kufanyika kati ya Februari 28 na Machi 3, 2022, katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Mkutano huu hutoa fursa kwa Serikali kuelezea dhamira zao juu ya uanzishwaji wa mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya uchafu wa mazingira unaofanywa na bidhaa za plastiki ambao wanamazingira ulimwenguni kote wamekuwa wakipigia kelele uanzishwaji wake.

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved