The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jaji Mathew Mwaimu: Tanzania Kuwa na Katiba Mpya ni Jambo Jema

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora anasema kwamba Serikali ilianzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwa sababu ilioni hatua hiyo ni muhimu kwa taifa na hivyo haina budi kuukamilisha mchakato huo.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Jaji (Mstaafu) Mathew Mwaimu ameuita mchakato uliokwama wa kuandika Katiba Mpya ya nchi “matakwa ya wananchi” na kwamba kwa Tanzania kuwa na Katiba Mpya “ni jambo jema.”

Jaji Mwaimu, aliyetueliwa kwenye nafasi hiyo mnamo Oktoba 2019 na aliyekuwa Rais wa Tanzania John Magufuli, alibainisha hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Dodoma hivi karibuni.

“Ninachoweza kusema ni kwamba kwa sababu suala hili [la Katiba Mpya] lilianzishwa na Serikali, nafikiri kwamba, kwa mawazo yangu, kwamba muelekeo ule pengine ungeweza kukamilishwa,” anasema Jaji Mwaimu kwenye mahojiano hayo. “Hata kama siyo kwa leo lakini nafikiri kuwa na Katiba Mpya ni jambo jema.”

Jaji Mwaimu anasema kwamba kwa sababu Serikali yenyewe tangu mwanzo iliona kwamba hatua ya kuandika Katiba Mpya ni hatua sahihi basi ifike wakati mamlaka za nchi zione umuhimu wa kukamilisha mchakato huo.

Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo kati ya The Chanzo na Jaji Mwaimu yaliyofanyika Februari 21, 2022, na hapa anaanza kwa kutoa tathmini yake ya hali ya kuheshimiwa kwa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini Tanzania kwa sasa. Endelea …

Mathew Mwaimu: Kwa sasa naweza kusema Tanzania inaheshimu haki za binadamu. Kwa sababu ukiangalia tulikotoka huko nyuma, unaweza kuona kwamba kwa ujumla wake ni kwa kiasi gani kuheshimiwa kwa haki za binadamu na utawala bora kumeimarika Tanzania.

Ukilinganisha na nchi nyingine pia, Tanzania nafikiri haki za binadamu zinatekelezwa vizuri. Hatukatai kwamba zipo changamoto, lakini changamoto hizi ni za kawaida. Lazima zipo lakini zinatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine kutokana na mazingira ya kila nchi.

The Chanzo: Ni masuala gani ya  msingi unayoyaona nchini Tanzania  kwa sasa ambayo yanakupa hofu kwamba  yanatishia haki za binadamu na utawala bora nchini?

Mathew Mwaimu: Naweza kusema kwa sasa siyaoni sana. Ingawaje unaweza kusema kwamba labda hapo nyuma kidogo zilikuwepo changamoto. Kama vile kuna haki ambazo zilikuwa hazielekei kutekekezwa. Kulikuwa na malalamiko kwamba haki ya kukusanyika kwa ajili ya kufanya shughuli za kiasiasa ambapo ilikuwa inasemwa kwamba wananchi walikuwa wanazuiliwa wasishiriki kufanya mikutano na kadhalika.

Lakini vile vile kulikuwa na changamoto ambayo ilikuwa inalalamikiwa kuhusu haki ya kupata taarifa. Baadhi ya wananchi walikuwa wanalalamika kwamba ukienda katika ofisi za Serikali basi kupata taarifa ilikuwa ni jambo gumu kidogo. Hayo ndio mambo ambayo yalikuwa yanaonekana hivyo.

Lakini ukiangalia mwelekeo wa siku za hivi karibuni unaona kwamba kuna vitu vingine vinabadilika. Kwa mfano, malalamiko hayo ya baadhi ya sheria, kwa sababu sheria ndio zilikuwa zinalalamikiwa kwamba zimeweka mazingira magumu kwa ajili ya watu kuweza kushiriki kwenye shughuli za kisiasa, kukusanyika na vile vile kupata habari stahiki.

Lakini siku za karibuni utaona kwamba mazingira yanakuwa yanabadilika. Kwa mfano, kulikuwa na vyombo ambavyo viliwahi kufungiwa. Lakini kwa sasa hivi vimefunguliwa. Lakini vile vile siku za karibuni unaona kwamba Baraza la Habari Tanzania (MCT)  limepata fursa pia ya kukaa na kujadili sheria mbalimbali ambazo wanaona kwamba zinaweza kuwa zinazuai haki ya kupata habari.

The Chanzo: Vipi haya madai ya vyama vya siasa kwamba Jeshi la Polisi linajihusisha na siasa, kitu ambacho vyama vya siasa vinalalamikia kwamba kinawanyima haki na uhuru wao wa kufanya kazi?

Mathew Mwaimu: Ni kweli hayo malalamiko yamekuwepo hasa kwenye kipindi hiki. Nafikiri naweza kusema kwa kipindi cha karibu miaka minne, mitano iliyopita, yamekuwepo malalamiko ya namna hiyo. Na nafikiri sababu kubwa ni kwamba malalamiko ni kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likizuia mikutano yao, ama ya hadhara ama ya ndani.

Na mara nyingi wamekuwa wakitaka kufanya basi unakuta labda Jeshi la Polisi linafika. Au wanaweza wakawa wametoa taarifa polisi lakini wakati wanataka kufanya mikutano yao, basi tayari unakuta askari au polisi wanakuwa wameshafika na kuelekeza kutawanyika na kuacha kufanya mkutano.

Lakini wakati mwingine wanapoomba vibali huwa wanaambiwa kwa sababu za kisualama hawawezi kufanya mikutano hiyo. Kwa hiyo, hayo malalamiko yamekuwepo katika siku za hivi karibuni. Na malalamiko hayo yamekwenda mbali sana mpaka kumekuwa na baadhi ya taasisi za kimataifa zimekuwa zikitoa taarifa, kama vile Amnesty International na Human Rights Watch.

The Chanzo: Je, tume inadhani sasa ni muda muafaka kwa Jeshi la Magereza  kuruhusu vyombo vya habari na Asasi za Kiraia kuwa na uwezekano wa kuingia magerezani na kutathmini  hali ya magereza na jinsi wafungwa wanavyofanyiwa ili kupunguza malalamiko kwamba magereza  na mahabusu yatumika kama vyumba vya mateso?

Mathew Mwaimu: Suala la kila mtu kungia gerezani naweza kusema ni suala nyeti. Kwa sababu magereza wanakaa kwanza wafungwa ambao wameshahukumiwa kwamba ni wakosaji.

Lakini magereza pia ni eneo ambapo wanakaa mahabusu, hawa watu wanaosubiri kesi zao kusikilizwa. Ni wale ambao tayari Mkurugenzi wa Mashtaka anakuwa ameshapeleka mashtaka mahakamani dhidi yao. Lakini kesi zao ama bado upelelezi unaendelea kufanyika ama kesi zao zinasubiri kusikilizwa. Sasa hawa hawajahukumiwa. Kwa hiyo, ni sehemu ambayo wanahifadhiwa watu  wenye changamoto za kisheria.

Siyo kila mtu anaruhusiwa kuingia katika magereza. Kwa sababu, sababu nyingine zinatolewa ni za kiusalama.  Kwa sababu magereza wanakaa watu wa aina nyingi. Na magereza mengine wanakaa wahalifu sugu, ni wahalifu ambao wamesha hukumuwa na adhabu ya vifungo virefu.

Lakini zipo taratibu ambazo zinaongoza namna ya kutembelea magereza na namna ya kuyafanyia ukaguzi. Na jukumu hilo [la kufanya ukaguzi] lipo kwa walinzi wa amani. Kwa mujibu wa sheria, kuna watu wanaitwa walinzi wa amani ambao ndio wanajukumu la kutembelea magereza. Na unapozungumzia walinzi wa amani maana yake ni Jaji wa Mahakama Kuu hata Mahakama ya Rufaa. Lakini anaweza akawa hakimu. Wanaitwa walinzi wa amani.

Lakini kuna maafisa wengine kwenye kazi zao kama Mkuu wa Wilaya nafikiri na wenyewe wanaweza kuwa na fursa ya kuingia huko. Sasa kwenda kule haijaruhusiwa kila mtu kuingia na kufanya ukaguzi kuna taratibu zake. Na mimi binafsi kwa sababu nimekuwa nikifanya kaguzi mara kwa mara ninafahamu kuna taratibu nyingine za kiusalama ambazo lazima ziangaliwe.

Kwa maana hiyo, si kila mtu anaweza kuruhusiwa kuingia mule. Na sababu kubwa kwa nini si kila mtu anaruhusiwa kuingia mule? Ni kwa sababu, kwa mfano, taasisi zisizo za kiserikali kama AZAKI wakati mwingine huwezi kujua hasa kinachowapeleka mule kwa uhakikika kwamba wanataka kwenda kuangalia nini?

Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba hawa wanaoitwa walinzi wa amani ambao wameruhusiwa  kuingia mule wamekuwa wanaandaa taarifa na hizo taarifa zimekuwa zinafikishwa katika vyombo husika kwa madhumuni ya kuweza kuboresha mazingira ya hayo magereza.

Kwa hiyo, kwa  utaratibu wa Tanzania ndivyo ulivyo. Na kama nilivyo tanguliwa kusema kuna mazingira ya kiusalama ambayo yanasababisha magereza yasikaguliwe na kila mtu. Kwa sababu ukaguzi wa magereza unafanyika kwa mujibu wa  sheria na kuna watu ambao wameruhusiwa kuingia gerezani kukagua na si kila mtu.

Lakini kama  unawazo kwamba kila mtu aweze kuingia mule labda pengine mfanye ushawishi. Kwamba kizuizi hicho kiondolewe ili kila mtu aweze kuingia gerezani kwenda kuona gereza likoje. Lakini kimsingi kabisa, na hili liko katika nchi nyingi, ni kwamba gereza si mahali ambako kila mtu anaweza kwenda kuingia na kufanya ukaguzi.

The Chanzo: Mtazamo wa tume kuhusu madai ya Katiba Mpya ni upi?

Mathew Mwaimu: Sasa suala la Katiba Mpya nadhani hili siyo la tume peke yake. Kwa sababu tume ni taasisi. Na swali kwamba iwapo kunahitajika Katiba Mpya au la haliwezi kuamriwa na tume kama taasisi.

Lakini ni mawazo ambayo yanasemwa na kila mtu na kila mtu anaweza kuwa na maoni yake. Na tume haijakaa na kusema kwamba wana mtazamo gani kuhusu kutungwa kwa Katiba Mpya.

Lakini labda mimi niseme kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni matakwa ya wananchi yanayotokana na wananchi. Lakini vile vile ni mambo yanayoweza yakaanzishwa na Serikali yenyewe. Kama utakumbuka mchakato huu ambao uliwahi kufanyika hapo nyuma ulianzishwa na Serikali.

Na ulikwenda mpaka ngazi ya kufikia hatua ya Bunge la Katiba. Ambalo pia Bunge la Katiba lilijadili rasimu ile ya Jaji Warioba na kutoka na rasimu. Lakini kwa mujibu wa sheria ya mchakato ule ilikuwa imetaka sasa, baada ya rasimu hiyo kufikia hatua hiyo, ingepaswa kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kwa hiyo, mchakato ulifika hatua ile lakini baada ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliuanzisha alipomaliza muda wake wa kutawala, ulipoingia utawala wa Hayati John Magufuli aliona vipaumbele vingine tofauti na hilo. Aliliacha hilo kwa kipindi chake na sasa baada ya yeye kufariki, Rais Samia Suluhu Hassan naye ameshika hatamu za uongozi.

Na yeye katika kipindi chake viongozi mbalimbali wa siasa na baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakilizungumzia hilo kwamba mchakato huu uanzishwe tena. Nafikiri utakumbuka Rais Samia alisema suala hilo lipo lakini aliomba kwamba kwa sasa aachiwe kujenga uchumi wa nchi na baada ya hapo suala hili linaweza kuendelea.

Lakini utakumbuka kwamba bado baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, baadhi ya wanazuoni na baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu na wengine bado wanaona jambo hili linahitaji kufanyiwa kazi.

Sasa hili nafikiri mimi siwezi kulitolea uamuzi kwa sababu kuna mawazo mchanganyiko ya watu. Lakini ninachoweza kusema ni kwamba kwa sababu suala hili lilianzishwa na Serikali, nafikiri kwamba, kwa mawazo yangu, kwamba muelekeo ule pengine ungeweza kukamilishwa hata kama siyo kwa leo lakini nafikiri kuwa na Katiba Mpya ni jambo jema.

Kwa sababu Serikali yenyewe toka mwanzo iliona kwamba linafaa. Kwa hiyo, labda pengine Serikali ifike mahali ione umuhimu wa kukamilisha mchakato ule. Kwa sababu kwa sasa hivi kuna wengine wanaosema Katiba Mpya, wengi siwasikii wakisema uendelezwe ule uliokuwepo mpaka ulipofikia kwamba sasa twende kwenye kura ya maoni au wanataka mchakato huo uanze upya?

Sijasikia watu wakisema chochote kuhusu hili. Kwa hiyo, wengi wanasema Katiba Mpya, lakini tunaanzia wapi? Tunaanzia tulipoishia? Au tunaanza mwanzo? Hakuna watu wanaosema hicho.

Lakini haya yote ni mambo ambayo yanahitaji tafakuri ya wadau wote kukutana na kuzungumza. Kwa sababu kwa manufaa ya nchi ni vizuri wote tukazungumza kwa pamoja na kuona kipi kinaweza kuisaidia nchi yetu.

Lakini kwa mawazo yangu ni kweli kwamba kuwepo kwa katiba hiyo ni wazo jema na kwa sababu lilianzishwa na Serikali yenyewe nafikiri si vizuri kutolipa umuhimu. Lakini kama nilivyotangulia kusema, Rais [Samia] amezungumzia kuhusu kuomba kwamba kwanza ajenge uchumi halafu masuala hayo mengine yatafuata baadae.

The Chanzo: Unatoa wito gani kwa Tanzania kama nchi linapokuja  suala la kuheshimiwa kwa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini?

Mathew Mwaimu: Wito kwa taifa letu kwa ujumla wake, kuanzia viongozi na wananchi kwa ujumla, ni kwamba sisi kama Watanzania na Serikali yetu tulikubali kuridhia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu. Hii ni mikataba ya kimataifa, mikataba ya kikanda lakini vile vile tulikubali kuridhia mikataba hiyo kwa kuingiza katika Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mazingira kama hayo kwa sababu nchi yetu imeridhia na kuweka kwenye katiba haki hizo na kuweka mifumo ambayo inasaidia kulinda  na kukuza haki hizo. Basi ni dhahiri natoa wito kwamba ni vizuri kuenzi vitu ambavyo Serikali yenyewe imevikubali.

Lakini kwa wananchi pia ni vizuri wakafahamu haki zao kupitia vyombo mbalimbali.

Lakini pengine jambo la msingi kabisa ambalo ni muhimu sana, wakati wananchi wakifurahia haki zao wanapaswa pia kujua kwamba haki hizo zinakwenda na wajibu. Hakuna haki ambayo ni uhuru kwamba unaifurahia bila ya kujua kwamba haki hizo unapozifurahia kuna wajibu pia.

Na wajibu mkubwa katika kufurahia haki ni pamoja na kujua kwamba wakati unafurahia haki yako pale inapoishia haki yako kuna haki ya mtu mwingine inaanzia. Kwa hiyo, usipokuwa na wajibu basi maana yake haki hizo zinaweza zikafika mahali badala ya kuwafanya watu wafurahie haki wakawa wanakwazika nazo.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *