Dar es Salaam. Watanzania kadhaa waliokuwa wakikabiliwa na kesi za ugaidi katika Mahakama mbalimbali za Tanzania wameachiwa huru ndani ya siku za hivi karibuni baada ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kujitoa kwenye kesi hizo ikisema kwamba haina nia ya kuendelea nazo tena.
Watanzania hao, wengi wao wakiwa ni Masheikh wa dini ya Kiislamu, wamekuwa wakiendelea na kesi hizo kwa miaka mingi, huku kesi hizo zikipangiwa tarehe mpya kila mara zilipokuwa zikipelekwa mahakamani kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
Ili kufahamu hatua hii kwa undani, The Chanzo imefanya mahojiano maalum na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye amekuwa akifuatilia jambo hili kwa ukaribu sana.
Hapa, Sheikh Ponda anaanza kwa kueleza ni nini haswa kimetokea ndani ya siku za hivi karibuni:
Sheikh Issa Ponda: Ni kwamba hawa watu walikamatwa kwa muda mrefu sana, toka kipindi cha Rais [wa awamu ya nne] Jakaya Kikwete, [na] toka kipindi cha Rais [wa awamu ya tano] John Magufuli.
Ukamataji wa hawa watu ulichukua sura ya kidini kwa sababu walikuwa wanakamatwa watu wa dini moja na wakituhumiwa kwa kesi ya ugaidi. Kwa hiyo, taasisi za Kiislamu, kwanza Shura ya Maimamu, ilijihusisha kushughulikia suala hili kisheria na kuwahudumia watu hawa kwa sababu jambo lilichukua sura ya kidini.
Sasa, mtazamo wa awali wa Shura ya Maimamu ulikuwa ni kwamba hili jambo litakwenda katika mkondo wa kisheria, kwa maana kwamba baada ya watuhumiwa hawa kukamatwa na kupelekwa mahakamani, basi upande wa Jamuhuri utapeleka ushahidi.
Sasa, kilichotokea ni kwamba kwa muda wote huu wa miaka karibuni – kuna baadhi yao wamekuwa na miaka minane, wengine miaka saba, wengine miaka sita – upande wa Jamuhuri umekuwa haupeleki ushahidi mahakamani. Kwa hiyo, kumekuwa na malalamiko makubwa sana katika jamii.
Hatimaye, mwaka jana [wa 2021] na mwaka huu baadhi ya mashauri yalianza kuzungumzwa na katikati ya mashauri yale yaliyoanza kuzungumzwa hayakufika mwisho upande wa Jamuhuri wakaamua kujitoa kwa maelezo kwamba hawana haja ya kuendelea na mashauri.
Kwa hiyo, kuna utokaji wa kwanza huo kwa baadhi ya mashauri ambayo yamezungumzwa. Utokaji wa pili ndio huo ambao unaendelea sasa hivi ambapo upande wa Jumuhuri hawakuwasilisha ushahidi mahakamani lakini wameamua kutokuendelea na hayo mashauri.
The Chanzo: Kwa hiyo, mpaka hivi sasa wameachiwa watu wangapi?
Sheikh Issa Ponda: Hiyo ni takwimu ambayo inahitaji utulivu. Lakini naweza nikakueleza haraka haraka kidogo tu. Kama kutakuwa na makosa basi yatakuwa ni machache ya hapa na pale. Nakumbuka Arusha watu waliokuwa gerezani walikuwa 59 ambapo mpaka sasa taarifa ni kwamba wametoka 28, huku 31 wakiwa wamebakia magerezani.
[Mkoa wa] Pwani walikuwa 81, wametoka 57, kwa hiyo wamebaki 24. Dar es Salaam walikuwa kwanza 220 wakatoka 34. Halafu wamekuja tena kutoka 15. Kwa hiyo, nafikiri waliobaki watakuwa ni 171.
Tanga walikuwa 68 lakini sikumbuki vizuri mpaka niangalie waliotoka lakini walikuwa kama 30 hivi. Shinyanga walikuwepo 11 wametoka wanne. Kwa hiyo, watakuwa wamebaki saba. Mwanza pia. Lakini mpaka niangalie vizuri na Mtwara pamoja na Mbeya.
The Chanzo: Unauzungumziaje uamuzi huu wa Serikali kuwafutia mashtaka baadhi ya hawa watu waliokuwa wakishikiliwa sehemu mbalimbali nchini?
Sheikh Issa Ponda: Ni uamuzi mzuri kwa sababu tunachukulia kile kitendo cha kuwarejesha, kuwapatia watu haki yao ya kurudi kuwa katika jamii. Lakini kuna sehemu ya pili ya haki kutendeka kwa sababu hawa watu wamekamatwa bila ushahidi. Sasa, wakamataji wanasema wamefanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Sasa, hapa kuna mambo mawili. Yaani, ikiwa tumekuwa na sheria ambayo imeruhusu kumakamata mtu bila ushahidi, hiyo ni sheria mbaya. Ni sheria ya ukandamizaji na haikupaswa kabisa kuwepo nchini.
Na ikiwa watu wameamua kutumia mamlaka yao kuwakamata watu na kuwaweka ndani miaka tisa, halafu wakawaambia hatuna haja ya kuendelea na kesi, hiyo ni ukandamizaji mkubwa sana ambao unaidhalilisha nchi yetu na unavunja haki za raia.
Kwa hiyo, hili jambo kwa ujumla linaidhoofisha sana Serikali yetu na kuionesha kwamba ni Serikali ambayo haitendi haki kwa raia.
The Chanzo: Umegusia hapo kwamba bado kuna Masheikh ambao wanashikiliwa mpaka hivi sasa sehemu mbalimbali nchini. Tumesikia pia viongozi wa dini hapo jana, Machi 2, 2022, wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan atumie busara kumaliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe. Labda unadhani hatua hii ni muhimu kiasi gani, Sheikh?
Sheikh Issa Ponda: Tunachozungumzia ni kuwa na taifa ambalo linatenda haki. Taifa ambalo linatenda haki kwa maana ya kufuata sheria. Huwezi kumakamata mtu halafu ukamuweka ndani wakati huna ushahidi kwamba huyu mtu kafanya uovu.
Kinachopaswa kutangulia huwa ni uchunguzi. Ule uchunguzi ndio unakupa matokeo kwamba huyu mtu ni mtuhumiwa au ni mtu mhalifu au sio mhalifu.
Sasa, hili lililofanyika kwa hawa Masheikh ni jambo ambalo ni baya na tulichotarajia ni kwamba hawa watu waachiwe mapema iwezekanavyo. Waachiliwe huru na taifa litafakari juu ya haki za hawa watu za kuwekwa ndani na kuondolewa kwenye jamii na wengine wameteswa sana.
Kuna watu wameteswa [na] wamepata madhara makubwa. Wamepata vilema vya kudumu wakati wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Kwa hiyo, tulichokuwa tunasema ni kwamba [walioko kwenye mamlaka] wajue kwamba wananchi wanapolalamika wana haki ya kulalamika na wao [kama viongozi] wanapaswa kupima kuangalia kama kuna ukweli au la.
Kwa hiyo, yale yaliyozungumzwa na viongozi wa dini [juu ya matumizi ya hekima kwenye kuachiwa kwa Mbowe na wenzake], Serikali inapaswa kupima ule ukweli na ichukue ile hatua ambayo ni muafaka.
The Chanzo: Asante, na labda kwa kumalizia tu ni upi wito wako wa ujumla sasa kwa Serikali, hususan linapokuja suala la kusimamia haki nchini?
Sheikh Issa Ponda: Kuna haja ya kupitia utendaji wa watu waliopewa dhamana ya uongozi, hasa kwa watawala. Lakini vile vile, kupitia ule mfumo wetu wa kisheria.
Huko nyuma, wakati wa [Serikali ya] awamu ya tatu, wakati wa Rais Benjamin Mkapa, aliwahi kuunda Tume ya Jaji Nyalali kwa ajili ya kuchunguza mfumo wa kisheria na tume ilikuja na ripoti kwamba kuna sheria nyingi za ukandamizaji.
Hizo sheria hazikuondolewa. Kwa hiyo, kuna haja ya kuupitia ule mfumo wetu wa kisheria. Lakini pia kuangalia ule utendaji wa hawa watu waliopewa dhamana ya usimamizi wa sheria.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.