The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Haya ni Lazima Yazingatiwe Ili Upangaji, Upanguaji Safu Katika Sekta ya Elimu Zanzibar Uweze Kuzaa Matunda

Hatua hizi zinazoendelea kuchukuliwa kuboresha sekta ya elimu Zanzibar hazitazaa matunda endapo kama wale wanaopewa dhamana hawatachukua jitihada za makusudi katika kurekebisha vikwazo vilivyopo ili changamoto za sekta ya elimu kutatuliwa ipasavyo.

subscribe to our newsletter!

Kuna msemo mmoja adhimu sana usemao: Watu hujenga ufalme wao kwa elimu na mali; ufalme haujengwi kwa ujinga na ufakiri. Maana yake ni kwamba bila ya kuandaa wananchi waliyoelimika na wakatumika ipasavyo katika taaluma zao, taifa kamwe haliwezi kusonga mbele kwa kasi na kwa mafanikio zaidi.

Juhudi za dhati za Serikali ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa mara tu baada ya Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Rais Hussein Ali Mwinyi kuingia madarakani. 

Juhudi hizi zinajumuisha kukutana na wadau wa elimu na kusikiliza changamoto na kupokea mapendekezo; kubadilisha baadhi ya mambo katika mitaala; na kurudisha darasa la saba. 

Nyingine ni kushirikiana na wahisani na wadau wa elimu katika kutoa mchango wa hali na mali kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji; kuwawezesha watoto waliyokimbia shule kurudi masomoni; pamoja na kufanya mabadiliko ya teuzi mbalimbali kwa watendaji wa taasisi na idara za Wizara ya Elimu.

Pamoja na juhudi hizo zinazokusudia kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu Zanzibar, ni wajibu wetu kuzua mjadala chanya ambao utachochea hamasa ya mabadiliko hayo. Ni muhimu kuuliza, kwa mfano, ni kwa namna gani kutenguliwa na kuteuliwa kwa watendaji wapya kwenye sekta ya elimu Zanzibar kunaweza kuchagiza mabadiliko husika yanayotafutwa?

Upangaji safu Wizara ya Elimu

Mnamo Februari 3, 2022, Rais Mwinyi alifanya mabadiliko kadhaa kwa watendaji wa taasisi na idara za wizara mbalimbali, zikiwemo za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali. Tarehe 4, siku moja baadaye, yalitangazwa mabadiliko ya wenyeviti wa bodi, wakurugezi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali. 

Wengine wakiziba nafasi zilizotenguliwa na wengine wakibadilishana taasisi au idara. Katika mabadiliko hayo, nafasi 12 zilihusishwa. Wizara ya Elimu iliguswa zaidi kwa kufanyiwa mabadiliko ya nafasi tisa kati ya 12, sawa na asilimia 75 ya mabadiliko yote.

Uteuzi Mpya wa Bodi, Idara na Taasisi za Wizara ya Elimu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali.

Mwenyekiti wa Baraza la Elimu.

Mkurugenzi wa idara ya Elimu Msingi na Maandalizi.

Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani la Zanzibar.

Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni na Michezo Wizara ya Elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Zanzibar (ZIE).

Mkurugezi wa Idara ya TEHAMA.

Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya Ualimu.

Mkurugenzi wa Idara Ukaguzi wa Elimu.

Hali halisi ya elimu Zanzibar

Kwa kutumia kigezo cha matokeo ya mitihani, kiwango cha ufaulu Zanzibar kinaonekana kupanda ukilinganisha na mwaka uliyopita, kama ilivyobainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Sekondari, wakati akitoa taarifa ya tathmini ya matokeo ya kidato cha nne 2021 Zanzibar. 

Taarifa hiyo inabainisha kupanda kwa ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne kwa asilimia 8.59 kutoka asilimia 57.5 kwa mwaka 2020, hadi kufikia asilimia 66.09 kwa mwaka 2021. Hata hivyo, asilimia 33.91 ya watahiniwa wameshindwa katika mitihani yao kwa mwaka 2021. 

Kiwango hiki bado ni kikubwa mno kinacholazimisha kuinamisha kichwa cha masikitiko na tafakuri juu ya idadi kubwa ya watoto wa Kizanzibari kushindwa hata kupata cheti cha kidato cha nne. Hatua za dhati zinapaswa kuchukuliwa ili kutokomeza sababu za maafa haya.

Sekta ya elimu Zanzibar inakabiliwa na changamoto za kila aina ambazo kwa hakika nyingi ya changamoto hizo ni marudio. Miongoni mwazo hugusa masuala kama vile maslahi duni ya watumishi wa sekta ya elimu; utoro wa wanafunzi; muamko hafifu wa jamii; ushirikiano mdogo wa wadau wa elimu; na uhaba na udhaifu wa mikakati pamoja na utekelezaji wake. 

Nyingine zinaweza kuwa ni kukosekana kwa ubunifu wa kutosha wa walimu katika ufundishaji; vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi; umasikini na ukosefu wa ufanisi katika usimamizi; na utekelezaji na ufuatiliaji. 

Wakati mwengine kisingizio cha bajeti hutumiwa kama sababu. Dhana ya ubunifu kulingana na mazingira halisi haitiwi maanani litajwapo suala la ufinyu wa bajeti. Hizi ni baadhi tu ya changamoto kuu zinazoikumba sekta ya elimu Zanzibar.

Wadau pia wanataja nidhamu mbovu ya kiutendaji; upoeo hafifu wa watendaji na watekelezaji; athari za kukosekana kwa nia ya dhati katika utekelezaji; uzembe na kutowajibika; ubinafsi na urasimu usio wa lazima kama vikwazo vingine vinavyoikabili sekta ya elimu Zanzibar.

Vikwazo hivi na ambavyo havikutajwa ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu. Jambo ambalo huziwia vigumu juhudi na hatua za kuimarisha elimu Zanzibar kufikia malengo yake kama yanavyotarajiwa.

Kinachotarajiwa kwa wateule wapya

Utenguzi na uteuzi mpya uliyofanywa na Raisi Mwinyi katika taasisi na idara za Wizara ya Elimu hautakuwa na maana kama wateule hao hawatachukua jitihada za makusudi katika kurekebisha vikwazo vilivyopo ili changamoto za sekta ya elimu kutatuliwa ipasavyo. 

Matarajio ni kwamba wateule hawa watazingatia sana mambo yafuatayo ili utenguzi na uteuzi huo mpya uwe chachu ya mabadiliko ya sekta ya elimu Zanzibar.

Wateule ni lazima wawe waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao. Nia safi na ya dhati, haki, utu, uwajibikaji, uzalendo, ari na nidhamu ya kiutendaji ni miongoni mwa viungo imara na viashiria thabiti vya kiwango cha uadilifu katika upangaji, utekelezaji na usimamiaji wa mipango mikakati ya kuenua sekta ya elimu.

Kukosekana kwa uadilifu kwa watendaji na watumishi wa umma kumekuwa kikwazo kikubwa sana katika maendeleo ya sekta nyingi za Serikali, ikiwemo sekta ya elimu.

Utenguzi na uteuzi mpya unatarajiwa kuondoa kabisa urasimu usio na faida, uzembe na kutowajibika, uvivu wa tafakuri na utendaji, ubinafsi na uzoroteshwaji wa mipango yenye nia njema na endelevu.

Kupitia uteuzi mpya, tunatarajia kushuhudia kasi kubwa ya mabadiliko itakayochochewa na upeo mkubwa wa kufikiri, kupanga na kufanya maamuzi. Tunatarajia tutafurahia ubunifu wa kipekee kupewa kipaumbele katika uendelezaji wa sekta ya elimu ili kutoa matunda yanayotarajiwa. 

Tafiti, ushirikishwaji upewe kipaumbele

Ili kufikia matarajio haya, tafiti za kina katika sekta ya elimu zipewe kipau mbele. Kupitia tafiti za uhakika ndipo tutagundua hasa changamoto zinzoikabili sekta ya elimu, misingi na vyanzo vya changamoto hizo pamoja na ufumbuzi wake. 

Tafiti za kina na zinazokusudia kurekebisha na kujenga misingi imara ya kielimu bado hazijapewa nafasi stahiki. Ama hazifanywi, hazifanyiki ipasavyo au ripoti zake hazitiliwi maanani.

Pia, ushirikishwaji wa wadau waliyokaribu na sekta ya elimu uimarishwe. Tena kwa nia ya dhati na kwa kiwango stahiki. Mtu ni watu. Msemo wa wahenga unaosisitiza umuhimu wa ukweli kwamba maendeleo ya sekta au jambo lolote hutegemea ushirikishwaji wa wadau husika. 

Ni muhimu kwa wasimamizi na watendaji wakuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuvaa kwa ukamilifu joho la unyakanga wa sekta ya elimu, vazi linalowalazimu. 

Ni jukumu letu pia kama wadau kuwasimamia na kuwasaidia kwa karibu manahodha waliyoteuliwa katika kupindua tanga ili tuipate bandari, kabla ya gharika ya mkondoni.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *