Mahakama Uingereza Kusikiliza Kesi ya Raia 10 wa Kitanzania Dhidi ya Barrick

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mnamo Februari 2020 na Watanzania saba ambapo watatu wengine walijiunga kwenye kesi hiyo dhidi ya Barrick mnamo August 2020.
Na Mwandishi Wetu16 March 20223 min

Dar es Salaam. Mahakama Kuu nchini Uingereza hapo Machi 17, 2022, inategemewa kusikiliza shitaka lililowasilishwa mahakamani hapo na wananchi wapatao 10 kutoka mkoa wa Mara dhidi ya kampuni tanzu za kampuni ya madini ya Barrick Gold kwa tuhuma za mauaji na mateso kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2019.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza mnamo Februari 2020 na Watanzania saba ambapo watatu wengine walijiunga kwenye kesi hiyo dhidi ya Barrick mnamo August 2020.

Kesi hiyo ni dhidi ya Barrick Tanzania Limited, ambayo inamilikiwa kwa ubia wa kampuni ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania. Barrick Tanzania Limited ilikuwa ikijulikana kama Acacia Mining.

Miongoni mwa kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu ambazo wananchi hao wamewasilisha mahakamani ni pamoja na kisa kilichotokea Julai 19, 2018, cha baba mmoja ambaye binti yake mwenye umri wa miaka tisa aligongwa na kuuliwa na gari iliyokuwa inamilikiwa na mgodi huo na bila kuhudumiwa vizuri.

Kisa kingine kinamuhusisha kijana mmoja aliyedai kushambuliwa kwa risasi kutokea mgongoni na kupigwa na askari walioajiriwa na mgodi kipindi akiwa na umri wa miaka 16. Visa vingine vinahusisha familia zinazolalamikia kuuliwa kwa baba zao kulikofanywa na askari wa mgodi.

Wahanga hao walisaidiwa na RAID, shirika lisilo la kiserikali lenye makao makuu yake nchini Uingereza linaloangazia ukiukwaji wa sheria na maadili unaofanywa na makampuni, pamoja na MiningWatch Canada, shirika lisilo la kiserikali linaloangazia athari zitokanazo na uchimbaji wa madini duniani.

Mashirika haya mawili yamekuwa yakifanya tafiti kwenye mgodi wa North Mara tangu mwaka 2014. Watanzania hao 10 wanawakilishwa mahakamani na wanasheria kutoka kampuni ya uwakili ya Hugh James iliyopo nchini Uingereza.

Madai ya muda mrefu

Mgodi wa North Mara, unaopatikana kando kabisa ya mkoa wa Mara, umekuwa ukikumbwa na madai ya uvunjifu wa haki za binadamu tangu ulipochukulia na Barrick kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2006.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Mark Bristow amewahi kunukuliwa huko nyuma akikiri kwamba “Acacia imekuwa ikifanya biashara zake bila kuwepo uwajibikaji,” na kwamba mgodi “haukuwa ukiendeshwa vizuri.”

Endapo kama Watanzania hao wataibuka washindi kwenye kesi yao hiyo dhidi ya Barrick, hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa wahanga wa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu wanaoishi pembezoni mwa migodi kuibuka washindi ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

Mnamo Mei 2021, kwa mfano, kampuni ya uchimbaji madini ya Petra Diamonds inayomiliki mgodi wa Williamson, maarufu kama mgodi wa Mwadui, uliopo Shinyanga, ilikubali kulipa shilingi bilioni 14 kwa wahanga 71 wa uvunjifu wa haki za binadamu wanaoishi maeneo ya karibu ya mgodi huo, hatua iliyotokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Uingereza.

Hatua hiyo ilikuja baada ya miaka kadhaa ya mapambano yalioendeshwa na wakazi na wanaharakati wa maeneo yanayouzunguka mgodi wa Mwadui yaliyokuwa na lengo la kukomeshwa kwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu uliokuwa unafanywa na walinzi wa mgodi huo pamoja na askari polisi wa Tanzania.

Ukiukwaji bado unaendelea

Licha ya Barrick kukabiliana na kesi hiyo, uchunguzi wa RAID wa hivi karibuni umebaini kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu bado unaendelea kwenye mgodi wa North Mara.

Kwenye taarifa yake iliyotolewa Machi 14, 2022, RAID ilibainisha kwamba angalau watu wanne wameuwawa na 7 wengine kujeruhiwa vibaya mgodini hapo tangu Barrick ichukue tena uendeshaji kamili wa mgodi huo.

“Madai ya Barrick kwamba imetatua ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa North Mara yanaonekana hayana ukweli,” taarifa hiyo ilimnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa RAID Anneke Van Woudenberg akisema.

Van Woudenberg alikuwa akizungumzia kauli ya Barrick kwamba kampuni hiyo imerekebisha kwa kiasi kikubwa mahusiano yake na jamii zinazouzunguka mgodi wake. Barrick ilitoa maelezo hayo kwenye ripoti yake ya haki za binadamu ya mwaka 2020.

“Bodi [ya wakurugenzi] ya Barrick pamoja na wawekezaji wake wanapaswa kuhakikisha wanakomesha mahusiano yaliyopo kati ya askari wa mgodi huo na Barrick,” aliongeza Van Woudenberg. “[Barrick pia] inapaswa kuanzisha uchunguzi huru na wa kuaminika kuhusiana na shutuma zilizoelekezwa kwake.”

Wakijibu swali la RAID kuhusiana na taarifa za hivi karibuni za mauaji yaliyoripotiwa katika mgodi wake, Barrick ilisema: “Itakuwa siyo sahihi [kwa upande wetu] kujadili shutuma hizi zilizoibuliwa na RAID nje ya kesi ya kesi inayoendelea Mahakama Kuu ya Uingereza.”

Na Mwandishi Wetu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2023 © All Rights Reserved