Ni Kwa Namna Gani CHADEMA Inaenda Kudai Katiba Mpya?

Je, mbinu ya mazungumzo ambayo CHADEMA imesema inaiongeza kwenye orodha yake ya mbinu itakazotumia kudai Katiba Mpya itawezesha upatikanaji wa nyaraka hiyo muhimu kabla ya mwaka 2025?
Lukelo Francis25 March 20225 min

Dar es Salaam. Kuna njia mbili kuu ambazo chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA kinaweza kuzitumia kufanikisha dai lake la kufufuliwa kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya kabla ya mwaka 2025: kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan na kumshawishi kuhusiana na suala husika au kwenda kwa wananchi na kuwashajihisha waishinikize Serikali kufufua mchakato huo.

Haya yalikuwa ni maoni ya wadau na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa hapa nchini wakitoa mtazamo wao juu ya swali la ni kwa namna gani CHADEMA itaendeleza harakati za kudai Katiba Mpya katika mazingira ambayo chama hicho chenye itikadi ya mrengo wa kati kwenda kulia kimesusia michakato inayoendelea ya kuifanyia tathmini demokrasia ya vyama vingi nchini inayofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na Baraza la Vyama vya Siasa.

Mnamo Machi 18, 2022, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe aliushirikisha umma wa Watanzania maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho yaliyohusu kususia kile kinachoitwa Mkutano wa Haki, Amani na Maridhiano unaotegemewa kufanyika kati ya Aprili 1 mpaka Aprili 5, 2022, jijini Dodoma, akisema mchakato huo umelenga kukwamisha dai la kupata Katiba Mpya, dai ambalo ni kipaumbele cha CHADEMA.

“Sisi hatushiriki kwenye vikao vya TCD kwa sababu hatuioni nia njema ya kutibu kiu ya Watanzania kuhusu neno Katiba [Mpya],” alisema Mbowe. Mkutano huo wa Dodoma unafanyika chini ya TCD. “Hapa [kwenye hivi vikao] hatuoni ufumbuzi wa kuipata Katiba ya nchi yetu.”

Mgawanyo wa mageuzi yanayohitajika

Michakato ya kufanyia mageuzi mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini inayoendeshwa chini ya TCD na Baraza la Vyama vya Siasa imeyagawa mageuzi yanayopaswa kufanyika kwa kuweka mageuzi ya muda mfupi, mageuzi ya muda wa kati na mageuzi ya muda mrefu.

Mageuzi ya muda mfupi yanahusu vyama vya siasa kuweza kufanya shughuli zao bila bugudha yoyote, kama vile kuweza kufanya mikutano yao ya ndani na ile ya hadhara bila kuingiliwa na vyombo vya dola. Tayari mchakato wa kuandaa kanuni zitakazoviwezesha vyama vya siasa kujisimamia wenyewe katika hili umeanza.

Kwa upande wa mageuzi ya muda wa kati, ambayo yanahusu, maboresho ya mfumo wa uchaguzi, mabadiliko makubwa yamependekezwa kufanyika kwenye Sheria ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa. Maboresha haya yanategemewa kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Suala la Katiba Mpya limewekwa kwenye sehemu ya mageuzi ya muda mrefu, huku kikosi kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuratibu maoni ya wadau kuhusiana na namna bora za kuendesha siasa za vyama vingi nchini ikitaka mchakato wa kuandika Katiba Mpya uanze baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Demokrasia kutoka chini

Dk Aikande Kwayu ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya kisiasa ambaye ameieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba kilicho muhimu kwa kiongozi wa upinzani kama Mbowe ni uwezo wa kuwashawishi wananchi kufanya kitu badala ya kuwashawishi watawala.

Kwayu anasema kwamba ni kazi ya CHADEMA kwenda mashinani na kuongea na wananchi kuhusiana na umuhimu wa Katiba Mpya kwani hiyo itazalisha demokrasia inayotoka chini kwenda juu badala ya demokrasia inayotoka juu kwenda chini.

“Kwa sababu mwisho wa siku tunachotaka sisi ni kuona msukumo wa Katiba Mpya unatoka chini kwenda juu na siyo vinginevyo,” anaeleza Dk Kwayu. “Lakini kinachofanyika hivi sasa ni kama vile Katiba Mpya italetwa na Rais. Sisi hatutaki hivyo. Hatutaki demokrasia inayotoka juu kuja chini. Tunataka demokrasia inayotoka chini kwenda juu.”

Haijulikana mbinu anayoipendekeza Dk Kwayu inaweza kufanikiwa kwa kiwango gani sasa ukizingatia namna ilivyoshindwa huko nyuma.

Itakumbukwa kwamba Mbowe alikamatwa na kupewa kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi katikati ya kuendesha vuguvugu la mashinani la kudai Katiba Mpya. Serikali ilifuta mashitaka dhidi yake mnamo Machi 4, 2022, baada ya kusota rumande kwa siku 226.

Huko nyuma pia CHADEMA ilijaribu kutumia nguvu ya wananchi kwenye kushinikiza baadhi ya matakwa yake kwa kuwashajihisha wananchi kushiriki kwenye maandamano lakini kwa bahati mbaya wasichokitarajia ndicho kimekuwa kikitokea: ushiriki hafifu wa wananchi.

Hali ilikuwa hivyo kwenye maandamo ambayo CHADEMA waliyapa jina la UKUTA kwa lengo la kupambana na ‘udikteta’ wa Rais wa awamu ya tano John Magufuli. Ikajirudia tena pale walipoitisha maandamano ya nchi nzima yasiyo na ukomo yaliyolenga kuishinikiza Serikali kutisha uchaguzi wa marudio wa 2020 baada ya kugomea matokeo yaliyompa ushindi Magufuli.

Mtanziko wa kimkakati

Hali hii ya uwezekano wa mavuguvugu ya mashinani yanayoandaliwa na CHADEMA kushindwa kutimiza malengo yake na msimamo wa chama hicho kususia michakato ya mazungumzo inayofanyika chini ya TCD na Baraza la Vyama vya Siasa ndiyo mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dastan Kweka anaiita kama “mtanziko wa kimkakati” unaoikumba CHADEMA.

“Kama ushajihishaji wa kutosha unaoweza kubadili hali ilivyo kwa sasa nchini hauwezekani (hali ambayo inaonekana kuwa hivyo),” aliandika Kweka kwenye andiko lake la Disemba 30, 2021, lililochapishwa kwenye safu hii, “ushirikishaji wa kimkakati ndiyo njia sahihi ya kuchukua, hususan pale fursa muhimu, kama vile mdahalo wa hivi karibuni, zinapojitokesa.”

Kweka alikuwa akizungumzia mkutano ulioitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini uliofanyika Disemba 2021 na ambao CHADEMA na NCCR-Mageuzi walisusia. Ni mkutano huu uliozaa kikosi kazi kilichowasilisha ripoti yake ya awali kwa Rais Samia hapo Machi 21, 2022.

Kutatua “mtanziko wake wa kimkakati,” Kweka alishauri kwamba CHADEMA ibadili mbinu zake kuakisi utawala wa Rais Samia, mabadiliko ambayo hata hivyo aliona yanaweza kupingwa na baadhi ya wana-CHADEMA wenye msimamo mkali.

Kwa ufupi, Kweka anashauri CHADEMA iyape kipaumbele mazungumzo badala ya mavuguvugu ya mashinani. Na inaonekana ushauri wa Kweka umepata usikivu kutoka kwenye masikio ya Mbowe.

Je, mazungumzo yatazaa Katiba Mpya?

Wakati ni ukweli kwamba Mbowe hajasema kama hataendelea na makongamano ya kudai Katiba Mpya, kiongozi huyo wa upinzani aliweke wazi namna CHADEMA inavyokwenda kupigania Katiba Mpya katikati ya wao kususia michakato inayoendelea chini ya TCD na Baraza la Vyama vya Siasa.

“Sasa hatuwezi kuendelea na hatua ambayo tunajua itatupeleka kwenye kuikosa Katiba, kwa hiyo tumekubali kuongezea kipengele cha mazungumzo,” alisema Mbowe kwenye mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu atoke jela.

“Kwamba mapambano ya Katiba embu yatupeleke kwenye mazungumzo,” aliongeza Mbowe. “Mazungumzo haya yakishindikana basi tutatafuta mbinu nyingine. Lakini vita ya Katiba, harakati za Katiba, ni harakati za kudumu hadi tuipate Katiba ya nchi yetu.”

Hata hivyo, baadhi ya wadau wana wasiwasi kwamba haijalishi ni mbinu gani CHADEMA inaenda kuitumia, ni vigumu sana kwa mazingira ya sasa ya Tanzania kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya mwaka 2025.

Mhadhiri wa siasa na utawala wa umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Richard Mbunda, kwa mfano, anaona ipo haja kwa CHADEMA kuendelea kupitia upya mikakati yake kwa namna ambayo itawawezesha kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 bila ya kuwa na Katiba Mpya.

Wasiwasi wa Dk Mbunda ni kwamba haijalishi ni mbinu gani CHADEMA wataitumia ni ngumu sana kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya kabla ya 2025 ukizingatia namna maoni ya wadau wa msingi yalivyogawanyika kwenye suala husika.

“Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, kwa mfano, ajenda yake ni Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba Mpya,” anasema Dk Mbunda. “Kikosi Kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kinataka mchakato wa Katiba Mpya uanze baada ya 2025. Na Rais Samia anaonekana kwenda kwenye muelekeo huu. Sioni ni kwa namna gani CHADEMA inaenda kuipata Katiba Mpya kwenye mazingira kama hayo.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Lukelo Francis

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved