Kutokana na mazoea, wengi tumekuwa tukiamini kuwa lugha ndiyo chombo pekee cha mawasiliano. Ndiyo maana hata tukiwa shuleni, masomo ya lugha hupewa kipaombele kwani husadikika kuwa ni nyenzo muhimu katika kujifunza na pia, katika maisha baada ya shule.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba lugha si chombo pekee cha mawasiliano. Ili kufikisha ujumbe, binadamu hushirikisha alama, ama ishara, zisizo za kiisimu (lugha) ili kufikisha ujumbe. Mambo haya si mageni, bali tumekuwa tukiyapuuza kwani mengi hufanyika kwa mazoea.
Alama, au ishara, kama kukonyeza, kurusha mikono, miluzi, kukunja sura, kutoa sauti ama milio kuashiria jambo fulani, ni mambo ya kawaida sana, hufanyika wakati wote tukiwa tunawasiliana.
Ukiacha haya tunayofanya kwa kutumia viungo kwenye miili yetu, kuna vitu kama rangi (rejea taa za barabarani, mathalani), michoro, picha, harufu, ladha nakadhalika. Kwa maneno mengine, lugha ni chombo kimojawapo tu cha mawasiliano katika kundi kubwa la njia alama ama ishara zitumikazo katika kuwasiliana.
Makala haya yanaangazia zaidi eneo lililosahaulika, yaani, mawasiliano yanayofanyika pasipo kutumia lugha kwa kuhusisha na hali ya sasa ya maendeleo na utandawazi.
Mawasiliano ni utamaduni
Kuna usemi maarufu kutoka kwa mwanaanthropolojia na mtaalamu wa maingiliano ya tamaduni Edward T. Hall usemao, “Mawasiliano ni utamaduni na utamaduni ni mawasiliano.” Usemi huu unatukumbusha kuwa ili mawasiliano yaweze kufanyika kwa ufanisi, utamaduni haupaswi kupuuzwa.
Tazama kisa cha hivi karibuni ambapo msanii Naseeb Abdul Juma Issack, maarufu kama Diamond, alizua tafrani miongoni mwa Waamerika weusi baada ya kuonekana akiwa amepiga picha na bendera inayowakumbusha wahusika madhila ya utumwa na ubaguzi.
Ikumbukwe Diamond hakuongea,hakutumia lugha kuwasilisha ujumbe tajwa, bali ni rangi tu za bendera zilitosha kufikisha ujumbe husika. Pengine, msanii huyu hakufahamu utamaduni wa wahusika.
Kufahamu ama kutofahamu utamaduni Waamerika weusi si sehemu ya mjadala huu. Sisi tujikite katika kile tulichokiona, ama kusikia, kuwa wenye utamaduni wao, hawakufurahishwa.
Pia, katika vita inayoendelea huko nchini Ukraine, tulimsikia Rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelenskyy, akiwasihi baadhi ya wananchi wa Ujerumani walioandika/chora alama Z katika maeneo ya viunga vya miji yao. Kwake Zelenskyy, alama hii inaashiria kuunga mkono uvamizi wa Urusi huko Ukraine.
Alama hii inatumiwa na majeshi ya Urusi kuashiria ushindi na pengine kuhalalisha uvamizi wao huko Ukraine. Hali ni hiyohiyo kwa alama mashuhuri ya kinazi, Swastika.
Leo hii, huwezi kuvaa nguo yenye alama hii, ama kuonesha alama hii, mbele ya Wayahudi kwa kuwa huwakumbusha madhila waliyoyapata kutoka kwa askari katili wa kinazi kutoka Ujerumani.
Yote haya yanathibitisha kauli yangu ya hapo juu kwamba mtu unaweza usitumie lugha kabisa, ukatumia alama, ama ishara, tofauti kabisa kufikisha ujumbe. Katika zama hizi za utandawazi, hali imebadilika zaidi katika mawasiliano kuanzia umbo au namna ujumbe unavyosukwa hadi mahali ama njia za kufikisha ujumbe.
Simujanja na urahisi wa kuwasiliana
Wakati tulizoea kuwasiliana ana kwa ana, ama maandishi kama barua, magazeti pamoja na runinga na redio, siku hizi mambo yote haya yanapatikana kwa simujanja (smartphone) kupitia mitandao ya kijamii.
Sekunde chache zinatosha kusambaza ujumbe kutoka Dar es Salaam na kuwafikia wakazi wa Chicago, Marekani. Kimsingi, watu wamepunguza kuongea na kuandika, wengi tunatumia mchanganyiko wa njia mtambuka kuwasiliana.
Tazama, kwa mfano, mtangazaji mashuhuri nchini, Zamaradi Mketema, alipomtakia heri mpenzi wake siku ya wapendanao. Bango lenye picha ya mhusika na maandishi machache yalitosha kutikisa kitaifa na kimataifa.
Kama ilivyo lugha, alama hizi nyingine pia huathiriwa na utamaduni. Kwa hiyo, ni vyema tukawa na uelewa wa alama fulani kabla ya kuzitumia—picha, ishara, michoro yaweza kuwa na maana fulani kwenu, ikawa tofauti kwa wengine au kinyume chake.
Je, katika zama hizi za maendeleo na utandawazi, Watanzania tuna uelewa kiasi gani wa alama zitumikazo mitandaoni ama uga wa mawasiliano kwa ujumla?
Sina uhakika kama vibonzo/alama (emojis) zote zitumikazo kwenye simujanja, kwa mfano, zinaakisi utamaduni wa jamii zote ulimwenguni kwa pamoja.
Utandawazi unatulazimisha kutumia alama zenye tafsiri za kigeni. Sawa na lugha, huku nako kuna athari za kitamaduni zinazojitokeza. Kwa mfano, mtoto anaekulia zama za simujanja, ni rahisi kujifunza utamaduni wa kigeni kupitia alama mbalimbali.
Watengenezaji wa vibonzo, ama alama, hizi wanajua nguvu ya mawasiliano haya. Ukichunguza kwa makini, vitu kama mikono ama sura za watu, zimewekwa katika rangi tofauti zinazowakilisha watu wa matabaka tofauti, yaani, mtu Mweupe, Mweusi na rangi nyingine. Lakini, zipo alama nyingine ambazo zinatokana na utamaduni wao na hasa nchi zilizoendelea.
Vilevile, alama ama ishara nazo hubadilika kutokana na wakati au muktadha sawa na lugha. Katika utawala wa Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere, kuitwa bepari ilikuwa ni kama tusi, leo bepari ina sura chanya. Tumeona hata mchekeshaji Mpoki akijiita Bepari wa Kihaya.
Upinde wa mvua na kampeni za LGBTQ
Kwenye alama na ishara nyingine pia hali hii ipo. Kwa mfano, alama maarufu ya upinde wa mvua (rainbow). Kwa miaka mingi alama hii imekuwa ikihusishwa na hali ya hewa na pia ilitumika kuwasilisha dhana nyingi zenye mtazamo chanya ama tumaini jema.
Lakini, kwa miaka ya hivi karibuni, rangi ama bendera ya upinde wa mvua inawakilisha watu wenye kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja, waliobadili jinsi, wenye jinsi mbili na makundi yanayohusiana nayo kwa pamoja ambayo hufahamika kama LGBTQ.
Hivi karibuni kuna makasha ya kutunzia simu (phone covers) yenye rangi hii ya upinde wa mvua zimejaa mtaani. Wateja wake wengi wakiwa ni akina dada. Nimechunguza hata bidhaa kama mikoba pia hupakwa rangi hizi. Sina hakika kama watumiaji wa kifaa hiki wanajua ujumbe uliomo kwenye makasha haya.
Sina hakika pia kama kinachowakilishwa pale ni LGBTQ ama la. Lakini, uki–google maneno “LGBTQ phone cover” utakutana na makasha yenye rangi inayojadiliwa hapa.
Umuhimu wa kujifunza
Ni vyema ukafahamu matumizi ya alama, picha, rangi mbalimbali ili usijikute matatizoni kama Diamond au kujikuta unatuma ujumbe ambao hukukusudia.
Kujifunza tafsiri au fasili za alama hizi pia ni muhimu kwani zaweza kuleta mtafaruku unaoweza kuzuilika kama ungekuwa na uelewa. Ni muhimu tukawa na ufahamu wa nini haswa tumeshika mikononi mwtu au tumevaa kwenye miili yetu.
Mambo yote ambayo huweza kutazamika, kuonjwa, kuguswa, kusikizwa ama kunuswa ni nyenzo muhimu sana kwa mawasiliano. Usishangae marashi/manukato/uturi tu ukakusababishia balaa ambalo hutoamini katika maisha yako.
Vitu hivi vinawasilisha taarifa kwa watu wengine kulingana na utamaduni wao. Hivyo, ni vyema kufahamu umebeba ujumbe gani, hasa katika zama hizi za utandawazi kwa sababu mawasiliano ni utamaduni na utamaduni ni mawasiliano.
Abdulkarim Mhandeni ni mhadhiri kutoka Idara ya Masomo ya Lugha kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. Anapatikana kupitia amhandeni@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
14 Responses
Nmejifunza kitu kikubwa sana leo.
Lakini nina swali dogo kwenye makala hiii
Je?Kuna tatizo gani Endapo alietengeneza alama au ishara fulani akaiuza kwenye jamii ya watu wasioelewa maana ya iyo alama au kuzingatia iyo maana kunakuwa na madhara gani kwa mtengenezaji pamoja na mtumiaji??
Hakuna madhara ya moja kwa moja kusema labda utadhurika kwa kushika ama kutumia bidhaa yenye alama hizo. Changamoto zake ni za muda mrefu, mosi, utakuwa unatangaza kitu usichojua. Unaweza kwenda mahali ambapo alama hiyo inafahamika,mapokeo yake yanaweza kuwa chanya ama hasi kutegemea na jamii utakayokuwepo. Umeona Qatar (Waarabu) jinsi wamewaka baada ya kuwepo tetesi za “kupromote” hilo kundi kwenye kombe la dunia? Umeona kilichomtokea Diamond? Wengi tunaamini hakufahamu athari za hiyo bendera ya Confederation.
Aidha, jamii yetu kwa mfano, wengi hawakubaliani na harakati za LGBTQ. Sasa mnapoitangaza kwa kutojua, kesho wakihamia hatua nyingine hamtoona kama ni kitu kigeni. Hii ni changamoto kwa watoto wadogo zaidi ambao wao hujengwa kifikra kwa kuona ama kusikia. Kwahiyo, athari ni za kitamaduni zaidi, na hivyo itategemea mitazamo kulingana na mnachoamini ama mnachothamini.
Mtazamo wangu ni vyema ukafikiria kwanza asili yako wewe, Kwa dhana ya kukiuliza maswali kama nini hasa asili yangu, napaswa kuishi kwenye misingi ipi, nafasi yangu kwenye maisha halisi ni ipi na ninapaswa niitendee vipi nafasi yangu nadhani utapata mwanga wa jibu la swali lako 🇬🇳🇹🇿
Nmejifunza kitu kikubwa sana leo.
Lakini nina swali dogo kwenye makala hiii
Je?Kuna tatizo gani Endapo alietengeneza alama au ishara fulani akaiuza kwenye jamii ya watu wasioelewa maana ya iyo alama au kuzingatia iyo maana kunakuwa na madhara gani kwa mtengenezaji pamoja na mtumiaji??
Nimeelewa kwa kina zaidi
Nimejifunza meng kwa hili naomba ufafanuzi wa alama nyngne
Ahsante sana mwandishi kwa kutufungua vichwa na kutuongezea maarifa.
Ubarikiwe sana kaka Ticha Mhandeni
Nimejifunza kitu kikubwa sana. Na nimeelewa kwa kina. Asante sana kwa makala hii yenye mafunzo adhimu.
Thank you presenter for this shocking revelation.i think the perpetrators of this should come out clean instead of hiding behind these symbols to make a fool of themselves.
My advice for youngsters,is that we should always try to educate ourselves to avoid these atrocities,I don’t know where the world is heading to…but we need to be cautious and may God bless us all,for the end is near.
Daaah! Kiukweli umenifumbua akili , tunapaswa kuwa makini sana
Thanks presenter it’s a good message
Be blessed brother asee Kwa ufupi huu mdahalo ndo maisha halisi nje na maisha tunayoyaishi. Swali langu ni hili, KWANINI watu wamekuwa wavivu kitambua asili zao na kama ni utandawazi basi nimejijibu
Aisee,,”rainbow” nimejifunza kitu mkuu asante na nitaendelea kufatilia zaidi juu ya rainbow, lakini niulize kitu , umesema alama,ishara sio lugha, hakika sijaelewa kwani kuna mda tunasema lugha ya picha na lugha za alama ambazo zinasaidia kufikisha ujumbe kwa hadhara husika!?
Mna jua kusomesha ila ongezeni alama zenu