The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Inachoweza Kufanya Zanzibar Kuhakikisha Watoto Wanaorudishwa Skuli Hawarudi Mitaani

Ubunifu unahitajika sana katika ufundishaji wa watoto hawa ili kuwawezesha watamani kubaki madarasani badala ya kurudi mitaani.

subscribe to our newsletter!

Penye nia pana njia. Huu ni msemo maarufu wa wahenga unaokusudia kushajihisha juhudi binafsi katika kuliendea na kulikamilisha jambo lenye manufaa, ama kwa mtu binafsi au kwa jamii na hata taifa kwa ujumla.

Nia ya dhati ya kuimarisha sekta ya elimu Zanzibar imeanza kuoneaha nuru yake tangu awamu ya nane ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kuingia madarakani, chini ya uongozi wa Rais Hussein Ali Mwinyi.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imekuwa kinara katika kufanya juhudi kadhaa zinazolenga kubadilisha na kuimarisha utendaji wake ili kukidhi mahitaji ya elimu kwa raia wote. Moja kati ya juhudi hizo ni mradi unaoendelea hivi sasa wa kuwarudisha masomoni wanafunzi waliyoacha skuli kwa sababu mbalimbali.

Sababu hizi ni pamoja na hali ngumu ya maisha, utoro wa makusudi, ufuatiliaji hafifu wa wazazi na walezi na hata muamko mdogo wa baadhi ya wanajamii linapokuja suala la kuhimiza umuhimu wa elimu wa watoto wao.

Watoto wanaolengwa kwenye mradi huu wapo kwenye makundi mawili. Kuna wale wenye umri kuanzia miaka saba mpaka 14. Watoto hawa huingizwa kwenye darasa maalum linaloitwa Darasa la Mbadala ambapo wanadumu kwa jumla ya miezi mitatu kabla ya kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa elimu.

Kundi jengine la watoto wanaolengwa kwenye mfumo huu ni lile la watoto wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao huingizwa kwenye mfumo wa elimu ya amali. Watoto hawa huorodheshwa na kupangwa madarasani na kusaidia vifaa vya kujifunzia kama vile madaftari, vifaa vya kuandikia na kuchorea, sare, mabegi nakadhalika.

Mpaka sasa, inaonekana mpango huu wa Serikali umefanikiwa. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Elimu Mbadala ambayo inaendesha zoezi hilo, wanafunzi zaidi 700, ambacho ni kiwango kilichotarajiwa, wamerejeshwa skuli.

Watoto kurudi mitaani

Hata hivyo, imebainika kwamba muda mchache tu baada ya watoto hawa kurudishwa skuli, hutoroka tena madarasani na kurudi mitaani. Maswali ambayo yanaendelea kuwaumiza vichwa watunga sera wa Zanzibar ni pamoja na ni kwa namna gani watoto hawa wanaweza kurudishwa skuli na kuendelea kubaki hapo badala ya kurudi mitaani?

Kwa bahati nzuri mamlaka husika zimeliona hili na zimeanza kuchukua juhudi stahiki. Wizara ya Elimu, kwa mfano, imeamua kuandaa mafunzo maalumu kwa walimu wa wanafunzi hao yatakayowawezesha kuyafanya madarasa hayo kuwa vutizi kwa wanafunzi ili wapende kusoma na kubaki darasani.

Bila shaka hii ni hatua nzuri ya kuanzia.

Hata hivyo, nadhani ni muhimu kwa mamlaka husika kufikiria kuongeza ubunifu katika kuwfundisha watoto hawa, kama vile kufikiria matumizi ya visaidizi vya kufundishia (teaching aids), njia za kiteknolojia, michezo, maigizo na simulizi za kuvutia ambazo zinaweza kusaidia sana katika kuwaweka wanafunzi hao kwenye njia ya utayari na shauku ya kuendelea kujifunza.

Ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi, hasa wa aina hii, uegemee zaidi katika vitendo kuliko nadharia. Muda wa kufurahi na kupumzika uwe wa kutosha ili kuokoa hali ya kuchoshwa na kukata tamaa. Hizi zote ni njia za kiubunifu katika ufundishaji na ujifunzaji ambazo zinaweza kutumika ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu.

Ujifunzaji wa nje ya darasa

Pia, walimu pia wanaweza kufikiria mbinu ya ujifunzaji wa nje ya darasa (outdoor learning). Kwa mfano, mada zinazohusiana na sayansi jamii, na nyengine zinazoweza kusawiri mazingira nje ya darasa, ni vyema walimu wakawatoa mara kwa mara wanafunzi hawa nje ya madarasa na kuwapeleka katika mazingira husika yatakayowafurahisha na kuimarisha uwelewa wao.

Kuwatoa wanafunzi nje ya darasa kutarahisisha kujifunza kwa kuona na kugusa. Kujifunza kwa kuona na kugusa kutaimarisha mapenzi yao ya kujifunza na kusahau maisha ya mitaani.

Saikolojia ya kutosha pia inahitajika kwa walimu waliopangwa kusomesha watoto hawa wanaorudishwa skuli baada ya muda mwingi kuwa nje ya madarasa. Saikolojia hii itajumuisha kufuatilia historia na maendeleo ya watoto hao kuanzia maisha ya familia zao na mahusiano yao mitaani.

Hii itasaidia kuwatambua wanafunzi hao katika makundi maalumu kwa kule kutafautiana kwao katika sababu za kuacha masomo.

Ni muhimu kufahamu kwamba wanafunzi hawa wameacha masomo kwa sababu mbalimbali. Kuwatambua vizuri kwa makundi kwa kunasibiana na sababu hizo kutasaidia sana katika kubuni na kuibua njia sahihi za kuwasaidia kisaikolojia katika kuwatoa kutoka katika mazoea ya kuishi mitaani na kuwarudisha katika hamu ya kubaki skuli.

Vivyo hivyo, saikolojia itasaidia sana katika kutambua matatizo yanayowakabili kisaikolojia, kimaisha na hata kifikra na kung’amua njia bora za utatuzi wake.

Mahusiano ya kirafiki kati ya walimu na wanafunzi

Hii pia inahusisha uwepo wa mahusiano ya kirafiki kati ya walimu na wanafunzi hawa kwani wanafunzi hawa ni mahususi na hivyo ni vyema kwa walimu wakavaa joho la ulezi na uzazi zaidi kuliko ilivyozoeleka katika mahusiano ya kawaida ya walimu na wanafunzi.

Kwa mfano, utolewaji wa adhabu kwa wanafunzi hawa wanapokosea uwe katika umakini sana. Vyenginevyo tutawapoteza. Urafiki, ucheshi, na ishara za upendo muda wote vinahitajika sana.

Mathalan, mwalimu anaweza wakati wa kuwafundisha kufanya vitu tafauti vitakavyowafanya wahisi kuthaminiwa zaidi. Kwa mfano, kuwashika, kuwaita kwa majina, kuwasifu, kutabasamu na kufurahi nao, kuwapongeza na kuwazawadia ni miongoni mwa mambo yatakayojenga urafiki na mahusiano bora kati yao.

Wanafunzi hasa wa aina hii wanatakiwa kuwaheshimu walimu wao kwa kuwapenda zaidi kuliko kwa kuwaogopa. Hii haimaanishi kwamba wanafunzi wadekezwe kupita kiasi. Tunacholenga ni kupunguza uwezekano wa hofu na hisia ya kujihisi vibaya. Lengo ni kuwavutia wabaki skuli ili malengo ya wizara na taifa yatimie.

Lakini haya yote yanaweza yasifanikiwe endapo kama maslahi ya walimu hayatapewa kipaumbele. Kwa hiyo, ipo haja pia kwa Serikali, na hata wadau wengine wa maendeleo ya elimu Zanzibar, kuwawezesha walimu wa madarasa hayo kwa kuwapatia vifaa maalumu vya kufundishia kisasa pamoja na stahiki zao kuongezwa.

Pia, wazazi, jamii na walezi wanapaswa kushirikiana kwa pamoja katika kuwaweka karibu watoto hawa na kushirikiana na walimu wao ili kuwaongezea hamu ya kupenda kusoma na kusaidiana katika juhudi za kufikia malengo.

Kunatakiwa kuwe na nia ya dhati na ya makusudi ya kuhakikisha linafanywa kila linalowezekana, tena kwa kiwango cha mwisho wa uwezo wetu, kuwasaidia watoto hawa.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *