Search
Close this search box.

Suala Siyo Kuondoka Ngorongoro Bali Namna Zoezi Hilo Linavyotekelezwa

Je, anayeondoka ni kweli ametaka kuondoka au kwa sababu kuna vikwazo vikubwa ambavyo vimewekwa ambavyo mwisho wa siku vinaweza kumfanya yeye na familia yake kuona kwamba njia pekee iliyobaki ni kuondoka?

subscribe to our newsletter!

Katika kile kinachotokea Ngorongoro hivi sasa, naweza kusema tu kinachoendelea kwa sasa ni uhamaji wa hiari. Kwa sababu Serikali imeweza kuja na hoja kwamba hifadhi hiyo inaharibika kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, makazi yaliyotawanyika pamoja na idadi ya mifugo kuongezeka.

Kwa hiyo, kama Serikali imeamua kwamba sasa wananchi ni lazima wapungue kwenye hifadhi hiyo ili basi waweze kuhifadhi vizuri, au waweze kupungua kwa sababu hatuwezi kuendelea kuishi kwa namba hiyo, binafsi sina tatizo na hilo na sidhani pia kama Wamaasai wenzangu wana tatizo na hilo.

Kwa yeyote yule ambaye hana nia nyingine mbaya niseme tu kwamba, tatizo lipo katika ile haki kwenye zoezi zima. Tunatazama katika haki au maana halisi ya kujitolea kuhama kwa hiari.

Huyu mtu ambaye anajitolea kuondoka, anaondoka kwa sababu gani? Anaondoka kwa sababu kweli ametaka kuondoka au kwa sababu kuna vikwazo vikubwa ambavyo vimewekwa ambavyo mwisho wa siku vinaweza kumfanya yeye na familia yake kuona kwamba njia pekee iliyobaki ni kuondoka?

Kwa mfano, sasa suala la kilimo haiwezekani ndani ya Ngorongor. Suala la biashara za bodaboda haliwezekani. Suala la biashara ya machinga haiwezekani. Masuala mengine mbalimbali ya biashara hayawezekani kwa sababu ile ni hifadhi. Moja kwa moja vitu kama hivyo vinaweza vikamfanya mtu aweze kusema sasa mimi bora niondoke.

Suala la kupewa fidia

Lakini lazima niipongeze Serikali kwa suala zima la kusema wale ambao wanataka kuondoka kwa hiari yao watafidiwa. Na kimsingi ukiangalia kwa mujibu wa sheria zetu za nchi, sheria zetu za ardhi, kuna sheria mbalimbali, lakini sheria moja wapo ambayo ni muhimu sana ni hiyo sasa ya fidia ya haraka na ya haki ambayo inatakiwa mwananchi anapokuwa anaondolewa katika eneo lake apewe fidia ya haki na kwa wakati.

Niseme tu kwamba hiyo sasa ndiyo msimamo wetu sisi kama asasi ya kiraia. Kwamba tunatamani kuona kwamba kwa wale ambao wanaondoka kwa hiari tunawapongeza kwa sababu tunahitaji hifadhi yetu iendelee kuwepo. Lakini mwisho wa siku wapewe fidia ya haki.

Fidia ya haki haimaanishi kujengewa nyumba nzima na vitu kama hivyo. Hapana. Fidia ya haki inamaanisha mambo mengi, ikiwemo kuangalia vitu vyote ambavyo vinaweza kuendelea kuhusika kama binadamu.

Lakini pia kama nilivyopata kusema sehemu nyengine, kama nchi yetu inaweza kuingia kwenye mikopo ya fedha ili mwisho wa siku waweze kuendesha miradi, sio mbaya pia wakifikiria namna ya kupata namna nzuri kwa ajili ya wananchi hawa ambao wanasubiri kuondoka ili basi kama wakiondoka wasiende kupata matatizo kule wanakokwenda.

Lakini pia niseme kwamba mimi nimeendelea kuona, ukitembelea Handeni, wanajenga nyumba na vitu vingine. Lakini niseme tu kwamba ni jambo zuri kwa sababu kumuondoa mtu na kumuonesha pa kwenda ni jambo ambalo ni la muhimu sana na ni la muhimu sana. Niseme tu kwamba kwa hapo niipongeze Serikali yetu.

Wanasiasa kuingilia mchakato

Lakini naomba tu niendelee niseme kwamba kuna tabia zingine mbaya sana ambazo unakuta watu wanatumia siasa kwa ajili ya kuwaumiza wananchi. Unakuta kwamba watu wanadai kwamba eti wanawasaidia wananchi lakini mwisho wa siku kuna maslahi binafsi ambayo yanakuwa yanatunzwa, kwa mfano maslahi ya kisiasa.

Unakuta kwamba mtu anawaambia wananchi msiongee na Serikali, kwamba hakuna sababu ya kuongea na Serikali. Lakini mwisho wa siku yeye mwenyewe anaishi Karatu. Yeye mwenyewe anaishi Arusha. Yeye mwenyewe anaishi Dar es Salaam.

Lakini mwisho wa siku watakaoumia ni hawa wananchi wa kipato cha chini. Watu maskini. Watu ambao hawajasoma. Na ndiyo maana mimi niendelee kusisitiza kwa Serikali yetu tukufu ambayo naelewa kwamba inapenda wananchi wake.

Kwamba Wamaasai, au wananchi wa kawaida, wasije wakaumizwa kwa namna yoyote ile kwa sababu wengi wao kwanza hata Kiswahili hawaelewi. Kwa hiyo, hawaelewi hizi siasa zinazozunguka. Hata kusoma na kuandika hawaelewi kinachoendelea kwenye mitandao.

Na inawezekana hata tafsiri wanayoipata kuhusiana na hizo harakati kwa ajili ya kuokoa hifadhi au urithi inawezekana inapotoshwa na watu wachache ambao wanamaslahi yao ya kisiasa.

Na niseme tu wanasiasa wekuwa mstari wa mbele kuwapotosha wananchi na kuwakataza wananchi kujua ukweli na kuwakataza Serikali na wananchi wasiweze kukaa pamoja na kujadiliana na kuweza kufikia katika muafaka mzuri.

Kwa hiyo, niseme tu kwamba niombe na vyombo vya habari. Moja, taarifa zitoke kwa usahihi bila kuwepo kwa upotoshaji. Waandishi wa habari wasipotoshe umma kwa sababu wakipotosha inakuwa ni kama vile wanachochea moto kwa kumimina mafuta ya petroli. Hiyo itakuwa siyo poa sana.

Niseme tu kwamba mwisho wa siku niliona kwenye kamati ambayo imeundwa kisiasa, ambayo kimsingi kamati hiyo inasema inaandika mawazo, sijui mawazo ya nini na inaandika bila kuwashirikisha wananchi, bila kuwashirikisha wadau.

Wanasiasa wanaamua kusema tunaandika andika. Kwa hiyo, naamini hata hiyo ripoti kwa sababu wananchi hawajui muktadha wake bado naweza nikasema siyo ya wananchi.

Siyo ya wananchi kwa sababu wananchi hawajapitisha na kama ingekuwa ni ya wananchi mpaka sasa tungekuwa tumeshaona muktadha wake kabla haijapelekwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kwa hiyo, natumia nafasi hii kumwambia Waziri Mkuu pamoja na timu yake serikalini hiyo ripoti muiangalie kwa umakini sana kwa sababu ripoti hiyo siyo ya wananchi.

Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu sijui mkutano wowote wa wananchi uliopitisha hiyo ripoti baada ya kuandikwa. Nniseme tu wanasiasa wanatumia tatizo hili la wananchi, ambalo kimsingi ni kwa sehemu kubwa amelitengeneza yeye mwenyewe, kwa sababu ya kisiasa kujaribu kujinufaisha yeye mwenyewe.

Wito

Serikali ijitahidi iwe makini tu, wananchi wa kawaida wasije wakaumia kwa sababu tu ya maslahi ya watu wachache. Niseme wananchi hawana shida kwa vyovyote vile. Wanahitaji elimu.

Wananchi wanahitaji Serikali yao iongee nao polepole, wanahitaji majadiliano ya pamoja mezani ambayo yatakuwa ni ya huru ambapo kimsingi wangeweza kuongea na Serikali yao.

Na ninaamini kwamba Serikali siyo korofi kwa sababu imeendelea kutunza tunu yetu ya amani, imeendelea kutunza wananchi wa Ngorongoro na wananchi wa maeneo yote mengine. Lakini mwisho wa siku ijitahidi kuelewa vizuri wananchi wake ni wa hadhi ya namna gani.

Vyombo vya habari na asasi za kiraia tuendelee kusisitiza elimu. Lakini pia tuendelee kusisitiza kwamba ni muhimu Serikali itafute milango ya kuwafikia wananchi wa kawaida kabisa.

Iachane na wanasiasa ambao kimsingi wao wanaishi Dar es Salaam, wengi wao wanaishi Arusha na maeneo mengine ambao wao wanakuwa pazia la kukinga wananchi na kuwanyima wasione ukweli na mwisho wa siku watakuja kuumia wananchi wa kawaida wakiwa wao wapo Dar es Salaam na maeneo mengine.

Kwa hiyo, hilo tu ndio matazamo wetu sisi kama asasi na matandao wetu na sisi ni zaidi ya mashirika 136 kwa sababu Tanzania Pastoral Community Forum (TPCF) ni mtandao mkubwa ambao umetapakaa Tanzania nzima. Tunawanachama na mashirika mbalimbali na tulikwisha kutoa tamko letu na msimamo wetu ndiyo huo.

Hatuna maslahi yoyote sisi kwa namna nyingine yoyote ile. Tunachotaka sisi sheria zifuatwe. Wananchi waheshimu sheria na Serikali iheshimu sheria na sisi kama asasi ambao tunakuwa tunakaa tunatazama tu kinachoendelea na mwisho wa siku tunakosoa bila kuogopa pale inapobidi.

Joseph Parsambei ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Wafugaji Tanzania (TPCF).  Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *