Mvutano Mkali Bungeni Madai ya Serikali Kuwahamisha Wamaasai

Ni kati ya Mbunge Ole-Sendeka na Serikali kuhusiana na mpango wa Serikali kupandisha hadhi mapori tengefu kadhaa kuwa mapori ya akiba, hali inayozuia hofu juu ya hatma ya wenyeji wa maeneo hayo.
The Chanzo Reporter20 June 202213 min

Dar es Salaam. Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson leo Jumatatu, Juni 20, 2022, alilazimika kuingilia kati mvutano uliokuwa unaendelea bungeni kati ya Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole-Sendeka (Chama cha Mapinduzi – CCM) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja kuhusiana na madai kwamba Serikali imepanga kuwahamisha Wamaasai kwenye maeneo yao ya asili.

Katika mchango wake juu ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Ole-Sendeka, yeye mwenyewe akitokea kwenye kabila hilo la Wamaasai, alidai kwamba mpango wa Serikali wa kupandisha hadhi mapori tengefu huko kaskazini mwa Tanzania kuwa mapori ya akiba utapelekea uhamisho “wa asilimia mia moja” kwa Wamaasai walioshio kwenye maeneo hayo.

Akiwasilisha taarifa ya bajeti ya wizara yake bungeni mnamo Juni 3, 2022, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana alisema kwamba Serikali inakusudia kupandisha hadhi mapori tengefu ya Ziwa Natron, Kilombero, Loliondo, Lolkisale, Longido, Mohowesi, Umba River, Mto wa Mbu, Simanjiro, Ruvu Maasai, Ruvu Same, Kalimawe, Misitu ya Litungandyosi na Gesi Mazoa kuwa mapori ya akiba.

Tofauti kati ya pori tengefu na pori la akiba ni kwamba shughuli za binadamu, kama vile ufugaji, zinaruhusiwa kwenye mapori tengefu. Shughuli hizo, hata hivyo, haziruhusiwi kwenye mapori ya akiba.

Wasiwasi wa Ole-Sendeka ni kwamba kwa kuwa eneo takriban lote linalokaliwa na ambalo Wamaasai hufanyia shughuli zao kwa sasa linaangukia kwenye mapori tengefu, kuyapandisha hadhi maeneo haya na kuwa mapori ya akiba ni kuwahamisha Wamaasai hawa kwenda sehemu zisizojulikana.

“Mheshimiwa Spika jambo hili, kwa vigezo vyovyote vile, haliwezi kukubalika,” alitamka Ole-Sendeka ambaye amekuwa Mbunge wa Simanjiro tangu mwaka 2010 huku akihimiza ushirikishwaji zaidi wa wenyeji wa maeneo hayo ufanywe na mamlaka za nchi kabla ya kuendelea na mpango wake huo.

Akiendelea kuchangia, Ole-Sendeka aliongeza: “Lakini Mheshimiwa Spika, kugeuza wilaya zote hizo za Maasai – nasema za Maasai maana Wamaasai wana wilaya hizo nne ndiyo wengi wao wako – [na] kuyageuza kuwa mapori ya akiba yanatutwisha mzigo [Wamaasai] wa kujiuliza dhamira yake ni nini?”

Hata hivyo, akisimama kutolea taarifa kauli hiyo ya Ole-Sendeka, Masanja alisema kwamba dhamira ya Serikali kupandisha hadhi mapori tengefu kuwa mapori ya akiba yatahusisha yale maeneo ambayo hayana vijiji vya wananchi.

“Kwa hiyo, maeneo yanayokwenda kupandishwa hadhi, kutoka mapori tengefu kuwa mapori ya akiba ni yale maeneo muhimu tu kwa ajili ya uhifadhi na hayana wananchi ndani yake,” alisema Masanja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka CCM.

Baada ya Spika Tulia kumuuliza Ole-Sendeka kama anapokea taarifa hiyo, Mbunge huyo alikataa kupokea taarifa hiyo, akisema kauli ya Masanja “haina hadhi ya [kuwa] taarifa.” Ole-Sendeka aliitaka Wizara ya Maliasili “mujitafakari, mupitie maamuzi yenu, [ni] lazima yajenge haiba nzuri kwa taifa letu.”

Dk Tulia akamuinua tena Masanja, mara hii akimtaka afafanue kauli yake kwamba maeneo yatakayopandishwa hadhi kutoka mapori tengefu kuwa mapori ya akiba hayana wananchi.

Masanja alisema kwamba maeneo hayo ni maeneo ambayo yalikuwa ni mapori tengefu ambayo kwa asilimia kubwa tayari yana wawekezaji, wakiwemo wawindaji wa kitalii.

“Tunapoona yana sifa ya kuhifadhiwa, ili wananchi wasiyasogelee, tunayapandisha hadhi: pori tengefu inakuwa pori la akiba na pori la akiba linakuwa hifadhi ya taifa,” aliongeza Masanja. “Sasa tumeona haya maeneo yana hadhi ya kupanda kutoka mapori tengefu kwenda mapori ya akiba. Na hayana wananchi.”

Alipoombwa afafanue hoja yake kwamba “asilimia mia” ya wenyeji wapo hatarini kuhamishwa kutokana na mpango huo wa Serikali, Ole-Sendeka alieleza kwamba mapori tengefu yanayolengwa na mpango huo yalishafutwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2009.

Hata hivyo, alipoelekezwa kutaja kifungu cha sheria hiyo kilichoyafuta mapori hayo tengefu, Ole-Sendeka alishindwa kufanya hivyo, kitu kilichompelekea Spika Tulia kufanya hitimisho la mvutano huo kama ifuatavyo:

“Nilitaka nikurahisishie [Ole-Sendeka] ili kama huna uhakika na hicho unachokisema, [hili jambo] tuliachie hapa,” alisema Dk Ackson. “Kama unao uhakika, nitataka wewe uniletee ushahidi na [Naibu] Waziri aniletee ushahidi. Mheshimiwa Ole-Sendeka, nakupa hiyo nafasi.”

“Mheshimiwa Spika,” alifunga Ole-Sendeka, “kwa sababu hapa tunazungumza habari ya tafsiri ya sheria, na mimi siyo bingwa kwenye eneo hilo, ninaomba niondoe hoja hiyo katika sura hii.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com. 

The Chanzo Reporter

One comment

  • Akech

    20 June 2022 at 7:44 PM

    Masanja said “the areas were formerly forested areas that largely already had investors, including tourist hunters.”

    This means foreign HUNTERS And INVESTORS ARE WELCOMED, NOT MAASAI

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved