Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wamelaani vikali hatua ya Jeshi la Polisi Zanzibar kumshikilia mwandishi wa habari Yasser Mkubwa wa kituo cha RSV Online TV visiwani humo kwa makosa ya uhalifu wa mtandao, wakitaka Serikali ya Rais Hussein Mwinyi kuheshimu misingi ya uhuru wa habari kwa kumuachia mwandishi huyo mara moja.
Vyama vya ACT-Wazalendo na CHADEMA pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kwa nyakati tofauti, hapo Jumanne vimesema kuendelea kushikiliwa kwa mwandishi huyo wa habari kuna jenga hofu miongoni mwa waandishi wenzake, hali yenye athari kubwa kwa uhuru wa habari visiwani humo na Tanzania kwa ujumla.
Mkubwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Juni 20, 2022, katika kituo cha polisi Madema kilichopo Mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutenda makosa ya kimtandao kwa kushirikiana na aliyekuwa kada wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) Baraka Shamte.
Kwenye mahojiano hayo, Shamte alitoa maoni yake kwamba hadhani Rais Mwinyi anastahili kuwa Rais wa Zanzibar baada ya mwaka 2025, akisema Rais huyo wa nane wa Zanzibar ameshindwa kuonesha sifa za kiongozi bora.
Moja kati ya sababu alizoainisha za kuamini hivyo ni hatua ya Dk Mwinyi kutoa kwa wawekezaji visiwa vidogo kadhaa, hatua ambayo Shamte na wakosoaji wengine wameitafsiri kama “kuiuza Zanzibar kwa mlango wa nyuma.”
Siku chache baada ya kutoa kauli yake hiyo, Shamte alivamiwa na kupigwa na watu walioelezewa kama “mazombi” huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikimfukuza uanachama baada ya kumshutuma na kumdhalilisha Rais Mwinyi hadharani.
Tayari polisi visiwani humo inachunguza tukio la kushambuliwa kwake, huku Shamte mwenyewe akiomba radhi kwa kilichokuwa chama chake akisema hakupaswa kutoa kauli aliyoitoa.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mwandishi wa habari [Yasser Mkubwa] bila ya masharti yoyote,” ilisema taarifa ya TEF iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa jukwaa hilo linalowakilisha wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari Tanzania.
Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma wa chama cha ACT-Wazalendo Salim Bimani amesema kwenye taarifa yake iliyotolewa kwa umma kwamba Jeshi la Polisi linapaswa kuondosha nia yake ya kumpeleka mahakamani mwandishi huyo ikiwa ni pamoja na kuacha kujiingiza katika shughuli za kisiasa.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kundosha mara moja nia yake ya kumpeleka mahakamani ndugu Yasser Mkubwa,” Bimani amesema kwenye taarifa hiyo. “Na kuacha kuliingiza Jeshi la Polisi katika shughuli za kisiasa badala yake wafanye kazi zao kwa misingi, weledi na maadili ya kazi zao.”
Chama cha upinzani CHADEMA nacho kimelaani kukamatwa kwa mwandishi huyo, kikiagiza kuachiwa kwake mara moja.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika ameulezea uamuzi wa kukamatwa kwa mwandishi huyo wa habari kama “uvunjaji wa sheria na ukiukaji wa haki.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.