Serikali, Wakulima Mbeya Waumiza Vichwa Kushuka kwa Bei ya Parachichi

Vita ya Ukraine yanyooshewa kidole; Serikali yataka wakulima wajiunge na ushirika.
Asifiwe Mbembela24 June 20224 min

Mbeya. Wakulima wa parachichi na Serikali mkoani hapa wameendelea kuumiza vichwa juu ya namna nzuri ya kukabiliana na mporomoko wa bei za zao hilo la biashara, huku sababu mbalimbali za hali hiyo zikitajwa pamoja na mapendekezo ya kukabiliana nayo.

Wakulima mkoani hapa, kama ilivyo kwa wakulima wenzao kutoka mikoa mengine ya nyanda za juu kusini nchini Tanzania, wamekuwa wakijihusisha na kilimo cha parachichi kwa siku nyingi za hivi karibuni ili kujikwamua kimaisha.

Utafiti mdogo uliofanywa na The Chanzo mapema mwaka huu ulibaini kwamba parachichi iko mbioni kulipoteza zao la kahawa, ambalo kwa miaka mingi ndiyo limekuwa utambulisho wa ukanda huo.

Manufaa yaliyokuwa yanatokana na parachichi yalikuwa ni yenye kuwaridhisha sana wakulima kiasa cha kuligeuza jina zao hilo na kuliita “dhahabu ya kijani.”

Hata hivyo, baada ya bei ya kilo moja ya parachichi – ambayo inakuwa ni kama maparachichi manne – kushuka kutoka Shilingi 2,000 mpaka Shilingi 500 au Shilingi 800, wakulima wengi mkoani hapa wameieleza The Chanzo kwamba wanahisi kuchanganyikiwa, huku wakiwa hawajui nini cha kufanya.

Vilio

“Kwa kweli tunaiomba Serikali itusaidie kutafuta soko,” anasema Baraka Mwalukwe ambaye ni mkulima wa parachichi wa siku nyingi. “Kinachotusumbua ni soko la uhakika. Ili bei ipande, Serikali tunaomba itusaidie. Itufutie soko.”

Mwalukwe anawakilisha vilio vya wakulima wengi wa parachichi ambao walikuwa wakitekeleza kilimo hicho kwa bidii, wakidhani kwamba mkombozi wa maisha yao waliyekuwa wanamsubiria kwa siku nyingi tayari amewadia.

Mdororo huu wa bei umekuwa ukiendelea kwa takriban miezi minne sasa. Na ingawaje yenyewe isingependa kuangushiwa mzigo wa kuwajibika na halii, wadau wa zao la parachichi wanashindwa kujizuia kuinyooshea kidole vita inayoendelea kati ya mataifa mawili ya Mashariki mwa Ulaya, Urusi na Ukraine.

Moja kati ya wadau hawa ni Edward Kabuje, Meneja Rasilimali Watu kutoka kampuni ya Kuza Africa Limited, kampuni ambayo inajihusisha na kulima na kununua parachichi wilayani Rungwe.

Ni vita ya Ukraine

“Hii vita ya Urusi na Ukraine imechangia kwa sehemu kubwa hali hii,” Kabuje anaieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum.

“Kwa sababu baadhi ya meli zinazosafirisha mzigo wetu ni meli zinazomilikiwa na Urusi,” anaongeza. “Kwa hiyo, wakati mwingine baadhi ya nchi ambazo zimeiwekea vikwazo Urusi kunakuwa na ugumu kidogo wa namna ya kuingiza mzigo kwenye nchi hizo.”

Vita hiyo ambayo imekuwa ikiendelea ilianza hapo Februari 24, 2022, baada ya vikosi vya Urusi kuvamia sehemu ya Ukraine kwa kile ilichodai ni mpango wake wa kutokemeza “Unazi” nchini humo.

Ukraine, hata hivyo, imeendelea kupambana, ikikataa kutii shinikizo la Urusi linaloitaka kuweka silaha zake chini, hali inayofanya vita hiyo kuendelea na athari zake kuonekana ulimwenguni kote.

Ingawaje Kabuje anataja sababu nyengine zinazoweza kuwa zimepelekea kushuka kwa bei ya parachichi – “kumekuwa na kushuka kwa uhitaji wa matunda” – hoja ya vita ya Ukraine inagoma kufa.

Watu kama Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera na hata Mwenyekiti wa Chama wa Wakulima wa zao la Parachichi (UWAMAMBO) Anyingulile Angetile Msyani pia wameendelea kuipigia chapuo hoja hii.

Lakini Homera amesema kwamba hii haimaanishi kwamba Serikali haichukui hatua zozote zinazolenga kukabiliana na hali hiyo.

Akizungumza kwenye kwenye hafla ya Baraza la Biashara la mkoa wa Mbeya hivi karibuni, Homera amesema Serikali ya mkoa huo imekuwa ikifanya kila linalowezekana kuwapunguzia machungu wakulima unaotokana na mdororo huo wa bei.

Wakulima na ushirika

Lakini, kwa mujibu wake, kuna changamoto moja. Alisema Homera: “Tumeongea na watu kama Avo Afrika [mnunuzi wa parachichi]. Huyu anataka kununua. Lakini hataki kununua kiholela. Yeye anachotaka ni kwenda kununua kwenye chama cha msingi. Sasa watu wetu wengine hawataki ushirika. Sasa hili ni tatizo.”

Ushirika nchini Tanzania una ladha mbaya miongoni mwa wakulima na wazalishaji, wengi wao bado wakiwa na kumbukumbu hai za namna ushirika, hususan kipindi cha utawala wa Rais wa kwanza Julius Nyerere, ulivyosaidia kufukarisha wakulima badala ya kuwatajirisha.

Lakini Homera anaamini kwamba kama wakulima na wazalishaji wadogo kweli wamedhamiria “kutoboa” basi hawawezi kukwepa ushirika.

“Sisi tunasema anayetaka kuuza kiholela akauze,” alifafanua Homera. “Anayetaka kwenda kuuza chama cha msingi, akauze. Lakini anayetoka chama cha msingi ndiyo atafanikiwa zaidi na bei itakuwa iko vizuri.”

Kama Mwenyekiti wa chama wa wakulima wa parachichi, ni yapi maoni ya Anyingulile Angetile Msyani? The Chanzo ilimtafuta mzee huyo kupata mtazamo wake.

“Tukiwa pamoja, tunaweza kutafuta masoko ya maparachichi,”  Msyani alianza kwa kueleza. “Nikiwa pekee yangu muda mwingine siwezi kujua nikauze wapi maparachichi yangu. Pia, mimi nikiwa kwenye ushirika tunaweza kupata madawa ya kutibu maparachichi na kupewa elimu.”

Umoja ni nguvu

Msyani anaeleza kwamba mara nyingi wataalamu wa kilimo wanakuwa wagumu kumfuata mtu mmoja mmoja na kumpatia elimu juu ya kilimo cha zao la parachichi, changamoto inayoweza kutatuliwa vizuri kama wakulima wataungana kwenye ushirika.

Msyani anaongeza pia kwamba ushirika ndiyo chanzo cha kufanikiwa kwa wakulima wa parachichi, husasan wale wenye mitaji midogo kwani huwafanya wakulima kuwa na sauti moja yenye nguvu inayoweza kuwasaidia kwenye majadiliano na Serikali pamoja na wanunuzi.

Kama wakulima watashawishika na hoja hizi na hivyo kuamua kujiunga na ushirika au la hilo ni suala la muda kuamua.

Kwa sasa, kinachosubiriwa kwa hamu na wakulima wa parachichi mkoani hapa ni thamani ya “dhahabu ya kijani” kuongezeka, wakitaka angalau bei ya parachichi wanazozalisha irudi kwenye bei iliyokuwepo kabla ya vita hiyo ya ndugu wawili wa Ulaya kuibuka.

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com

Asifiwe Mbembela

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved