Mbeya Katikati ya Mtanziko wa Kulinda Maslahi ya Kiuchumi na Kujikinga na Ajali za Barabarani

Ni kuhusu katazo dhidi ya mabasi ya “Hakuna Kulala” kwa kuhatarisha usalama wa abiria. Lakini katazo hilo linaonekana kuathiri uchumi wa mkoa huo.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Mamlaka mkoani hapa, kwa kushirikiana na Serikali za mikoa ya jirani, zinafikiria namna bora ya kuondokana na mtanziko uliopo kati ya kulinda maslahi ya kiuchumi ya mikoa hiyo na haja ya kulinda uhai wa wananchi dhidi ya ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiripotiwa kutokea sana nchini Tanzania kwa siku za hivi karibuni.

Kilichopo katikati ya mtanziko huo ni mabasi yanayosafirisha abiria kutoka Mbeya kwenda maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwemo jijini Dar es Salaam, yanayofanya shughuli zake wakati mabasi mengine ya abiria yakiwa yamesitisha kufanya hivyo. Yakijulikana kwa jina maarufu la “Hakuna Kulala,” mabasi hayo mara nyingi hufanya safari zake usiku.

Lakini kuna wasiwasi kwamba utaratibu huo unayaweka rehani maisha ya Watanzania wanaotumia usafiri huo. Hofu hizi zimeshamiri zaidi hivi karibuni baada ya basi moja la “Hakuna Kulala” kugonga lori lililokuwa limeharibika karibu na eneo la Changarawe, Mafinga mkoani Iringa na kupelekea vifo vya watu 16.

Kufuatia ajali hiyo mbaya iliyotokea usiku wa kuamkia Juni 10, 2022, mamlaka mkoani Iringa zilipiga marufuku usafiri huo kupita mkoani hapo,  huku Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga akisema Serikali haiwezi kuendelea kupoteza uhai wa raia wake “kwa sababu zisizoeleweka.”

Athari za kiuchumi

Lakini katazo hilo linatajwa kuwa na athari ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa mingine ya jirani, wakiwemo wajasiriamali wadogo ambao wameieleza The Chanzo kwamba tangu Serikali ianze kusimamia katazo hilo, biashara zao zimeathirika kwa kiwango kikubwa, hali inayoathiri ustawi wao kama wananchi.

Neema Bobu, kwa mfano, ni mjasiriamali kutoka eneo la Uyole ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa anategemea abiria wa mabasi ya “Hakuna Kulala” kama wateja wake wa msingi. Tangu zuio hilo liwekwe, hata hivyo, Bobu anasema hali imekuwa ngumu sana kwenye biashara yake.

“Nina wiki tatu sasa hivi sijauza chochote,” Bobu alilalama wakati akiongea na The Chanzo. Mimi nina familia nyumbani na kazi ya kudanga sijazoea, nimezoea niuze nipate posho watoto nikalishe.”

Bobu, mama wa watoto sita anayewalea peke yake baada ya kudai kutelekezwa na aliyekuwa mume wake, anaeleza kwamba kabla ya zuio alikuwa anauwezo wa kuuza mifuko ya viazi mviringo ndoo za lita 20 tano ambapo kwa siku alikuwa anapata faida ya Shilingi 40,000.

Lakini sasa hata kumaliza mfuko mmoja wa ndoo tano ili apate faida ya Shilingi 10,000 ni changamoto.

Ni sauti kama hizi za akina Bobu ndizo zilizoisukuma Serikali ya mkoa wa Mbeya kushawishi Serikali za mikoa ya jirani ili kuona kwamba katazo hilo lililowekwa dhidi ya mabasi ya “Hakuna Kulala” linaondolewa na badala yake kutaka mabasi ambayo yangependa kufanya safari hizo kupata kibali maalum kutoka polisi.

Katazo laondoshwa

Akizungumza katika Kongamano la Nishati na Madini lililofanyika mkoani hapa mnamo Juni 27, 2022, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera alitangaza kuondosha zuio hilo dhidi ya mabasi ya “Hakuna Kulala,” akitaja sababu za kiuchumi kama msingi wa uamuzi huo.

Uamuzi wa Homera ulikuja takriban wiki moja baada ya kuwaeleza wafanyabiashara wa Mbeya kwamba angefanya mazungumzo na mamlaka za mikoa ya jirani pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuona mabasi ya “Hakuna Kulala” yanaendelea na shughuli zao bila kuathiri uchumi na uhai wa watu.

“Magari ya ‘Hakuna Kulala’ lakini yana uhitaji na watu wanayahitaji,” alisema Homera. “Lakini lazima tukae chini kati ya hao wenye hayo magari ya ‘Hakuna Kulala’ pamoja na Jeshi la Polisi ili tujiridhishe maana wafanyabishara wengi wanasafiri usiku wanawahi Dar es Salaam, yaani akiondoka hapa saa 4 usiku [au] saa 1 jioni, asubuhi anaingia Dar es Salaam.”

Baraka Mwasambamba ni moja kati ya madereva wanaojihusisha na usafirishaji wa mabasi kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam ambaye ameieleza The Chanzo kwamba haitoshi tu kwa Serikali kuondosha zuio hilo, akihimiza umuhimu wa kufanya maboresho ya mabasi hayo.

Madereva wawili

Moja kati ya eneo muhimu ambalo Mwasambamba anadhani Serikali inapaswa kulisimamia kwa umakini zaidi ni kuhakikisha ndani ya mabasi haya kuna kuwa na madereva wawili ambao watakuwa wanapokezana ili kuepusha ajali za barabarani zinazosababishwa na uchovu.

“Kwa hizi Costa za ‘Hakuna Kulala’ wangeboresha zingekuwa labda na madereva wawili,” Mwasambamba aliiambia The Chanzo. “Kwa sababu dereva mmoja anaweza akawa amechoka na safari za usiku akalala halafu mwisho wa siku ndiyo yakatokea mambo ya ajali.”

Homera pia anaona umuhimu wa kuboresha mabasi haya ili yawe salama zaidi kwa wanayoyatumia kwenye safari zao.

“Tunachohitaji ni kwamba hatutaki ajali za barabarani. Ninachotaka kusisitiza ni kwamba magari ya ‘Hakuna Kulala’ yale yatakuwepo, lakini yatakuwa na vibali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,” anasema Homera. “Lakini tunapendekeza zaidi mabasi makubwa [ndiyo yatumike], siyo haya madogo. Haya madogo uwezo wake wa kuhimili safari ndefu siyo nzuri sana. Tunahitaji usalama zaidi wa mwananchi.”

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts