Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

Kwa sababu wao ndiyo waajiri wa Serikali, wananchi wanapaswa kuhakikisha Serikali yao inafanya mambo yanayokidhi maslahi na matakwa yao, na siyo vinginevyo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze amesema kwamba ni wajibu wa wananchi kuhakikisha kwamba Serikali yao inafanya mambo kwa uwazi ili kuchochea uwajibikaji hali inayoweza kuchangia kuboresha hali zao za maisha kiuchumi na kijamii.

Eyakuze, ambaye shirika lake linafanya kazi zake nchini Tanzania, Uganda na Kenya kuchochea uwazi na uwajibikaji serikalini, alitoa kauli hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake hapo Julai 8, 2022.

“Hii Serikali inakutumikia wewe, wewe si mtumishi wa Serikali,” alisema Eyakuze, ambaye pia ni Mwenyekiti-mwenza wa Open Government Partnership, mpango wa kidunia unaopigania uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji serikalini. “Wewe ndiyo mwajiri wa hiyo Serikali.”

Eyakuze alisema kwa msingi huo, ni wajibu wa wananchi kuhakikisha Serikali ina wajibika, akisisitiza umuhimu wa wananchi kulinda haki zao ambazo kama hawatakuwa makini zinaweza kupotea muda wowote.

“Hizi haki ambazo tunazichukulia poa leo hii zinaweza zikatoweka ndani ya sekunde moja,” alisema Eyakuze kwenye mahojiano hayo maalum. “Je, tuko na utayari gani wa kuzilinda na kuzipa nguvu zaidi kwa kuzisimika kwenye mifumo ya utawala wetu?”

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo. Endelea …

The Chanzo: Tunashukuru sana kuwa na wewe. Na ningependa kuanza moja kwa moja kwenye suala naweza kusema pengine ni binafsi, hivi unajisikiaje kuwa mwenyekiti, au kiongozi, wa mpango ambao Serikali yako sio mwanachama?

Aidan Eyakuze: Sasa hapo najisikia kidogo kama kuna upungufu kwa kiasi fulani. Lakini pia kwangu mimi ni motisha ya kujaribu kuirudisha, [au] kuirejesha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie kwenye mpango huu wa Open Government kwa sababu tuliijiunga mwaka 2011 tokajitoa mwaka 2017.

Na hapa katikati mambo mengi yamefanyika tangu mwaka 2017, ndipo hapo mimi nimechaguliwa kuwa mwenyekiti-mwenza kwa wakati huu pamoja na Serikali ya Italia. Nikaona labda hii itakuwa motisha moja wapo katika kutumikia mfumo mzima wa Open Government Partnership kujaribu kuirejesha Tanzania kwenye partnership yenyewe hii.

Kwa hiyo, hii ni changamoto kwangu mimi, ni motisha kwangu mimi, japokuwa kuna kaugumu fulani pale, nimekaweka pembeni, nimesema sisi tuifanyie kazi tuone kama kweli tutaweza kurejea kama taifa kwenye Open Government Partnership.

The Chanzo: Na kwa tathimini yako, kwa mfano, kama mtu ambaye umejitolea, mtu ambaye unavutiwa sana na suala zima la uwazi na uwajibikaji serikalini, kwa tathimini yako unadhani Serikali ya Tanzania inafanya shughuli zake kwa uwazi kiasi gani?

Aidan Eyakuze: Unajua Serikali ya Tanzania kuna sehemu ambapo inajitahidi kufanya mambo kwa uwazi. Kwa mfano, kutoa zile ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) – zamani zilikuwa hazitoki hizo – na kuonesha madudu yanayofanyika na rasilimali za umma. Kwa kiasi hicho nadhani inafanya mambo kwa uwazi.

Zamani – sasa labda sijui wameacha, sasa wamesitisha – kututangazia yale mapato ya Mamlaka ya Mapato (TRA) waliokusanya kwa kila mwezi. Lakini inasitisha kwa sasa. Kwa hiyo, ni mifano kidogo ya kufanya mambo kwa uwazi ili wananchi wapate kujua michango yetu, au kodi zetu, zinatumikaje au zinakusanywa kwa kiwango gani na zinafanya kazi gani.

Kwa hiyo, mambo mengine kidogo nadhani wanafanya mambo kwa siri na wanaweza wakasema kwamba mambo mengine lazima yafanywe kwa siri. Lakini siyo kila kitu. Nadhani wananchi na wao wana haki ya kupata taarifa nyingi zaidi na zaidi haswa pale ambapo Serikali inawagusa moja kwa moja.

Kwa mfano, kwenye Serikali za mitaa, halmashauri za mikoa na za miji na vitu kama hivyo. Na zile halmashauri za wilaya. Hapo wananchi wanahaki ya kwenda kuomba kupewa taarifa ya matumizi ya bajeti zilizopangwa wajue je, utekelezaji wenyewe ukoje, uko kwa hali gani?

Unajua lakini mara nyingi unategemea kiongozi ndio afike pale, asomewe risala, aulizwe masula magumu, halafu ndiyo wananchi waseme ndiyo huyo hafanyi hiki na kile. Lakini siyo lazima pawepo na kamera, pawepo na kinasa sauti, pawepo na kiongozi wa ngazi za juu ndiyo haya mambo yaweze kufanyika kwa uwazi kila siku ya Mungu kule tunapoishi sisi kule mitaani.

Sasa kwa hapo hapo sio dhana ya Serikali lakini ni mazoea ya watendaji kwamba naficha hiki kitu ili nisiibuke, au nitumie kwa manufaa yangu na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, ndiyo kuna sehemu ambapo siyo lazima tufungue siri zote za nchi lakini ule utendaji wa watendaji wa kawaida unaweza ukawa ni uwazi zaidi shirikishi zaidi ya wananchi unaowajibika zaidi kwa wananchi wa pale pale.

The Chanzo: Na umefanya nikuulize, unadhani hili linasababishwa, yaani kwa mfano, kuna miuundo ambayo ipo mahali inazozifanya hizo mamlaka kutokuwa wazi au ni uamuzi tu watendaji kwa mfano?

Aidan Eyakuze: Mimi nadhani ni uamuzi wa watendaji. Kwa sababu kuna mifumo yetu ambayo inasema, kwa mfano kidogo tu, ni lazima kila robo ya mwaka pawepo na mkutano wa mtaa, au wa kijiji, wananchi wasomewe mapato na matumizi yanayoingizwa eneo lile, wajadili, watoe maoni yao yafanyiwe kazi.

Hii ipo kwenye mfumo lakini mara ngapi inafanyika? Kwenye wilaya zipi? Kwenye Serikali zipi za mitaa inafanyika? Nadhani utakuta ni mara chache sana. Sisi tumewahi kufanya utafiti mmoja tu, miaka imepita kidogo, nadhani ilikuwa kama miaka mitano sita, kuna sheria hii ya upatikanaji wa habari, tukasema hebu tuone kama kweli inatekelezwa au maoni ya watendaji wa Serikali kuhusu suala hili yapoje. Ndiyo wanalipokea hili jambo au hawalipendi na hawalitekelezi.

Tukaona kweli halmashauri, nadhani kama thelathini hivi, tukawatuma watu wetu tukawaambia nyie nusu nendeni mkadai hizi taarifa kama haki yenu tuone kama mtapewa, nusu tukawaambia nendeni pale mkawaombe watu kwamba naomba mnifanyie fadhila kwamba jamani kuna ndugu yangu anahitaji nijue bajeti tuone wapi na yupi atapata taarifa.

Hawa waliokwenda kuomba kama fadhila walipata taarifa, hawa wanaoenda kudai haki yao ndio wakakwamishwa, yaani mara nyingi sana. Kwa hiyo, utakuta kwamba hata mfumo uliopo, sera zipo, sheria ipo lakini utekelezaji unatofautina kidogo kulingana na namna yule mtendaji wa pale analichukuliaje suala husika.

Halafu hakuna adhabu, hakuna chochote kile ambacho kitamfanya, kitamsukuma, afanye hiyo kazi ya kutoa taarifa kwa sababu hata asipotoa kwani nani atamshugulikia? Hakuna mtu. Kwa hiyo, na wananchi wanasema ya nini nionekana kwamba mimi ni tatizo, nina kiherehere, ni msumbufu na mimi nitaacha hayo. Kwa hiyo, nabaki nakaa nyuma.

Mwisho matokeo yake ni kwamba wengi serikalini hawatendi, hawafanyi kazi ipasavyo. Hawawatendei wananchi haki yao. Pili, wananchi wanasema hii ni usumbufu. Mimi nitakaa pembeni. Kwa hiyo, hata hiyo nguvu ya kukuletea maendeleo, kusukuma gurudumu la maendeleo, yenyewe inafifia, inabaki hapo hapo. Maisha hayaendi, hayawi mazuri kama yale ambayo tungeweza kuyapata tungejikita tena katika utawala wa mambo yetu.

The Chanzo: Sasa inafikirisha kwa sababu unaona kwamba hii tabia ya kufanya mambo kwa siri au gizani haisababishwi na mifumo lakini hulka. Sasa hiyo tunabadilisha vipi hiyo hali kwa mtazamo wako wewe? Yaani tunafikaje kwenye hali ambayo kuna hiyo, kwa mfano, kama sasa hivi mtu anautashi wa kufanya mambo kwa siri, tunafikaje kwenye hali ambayo mtu anakuwa na utashi kufanya mambo kwa uwazi?

Aidan Eyakuze: Kumsaidia mtu, kumpa [mtu] utashi ni kazi ngumu sana. Hiyo ni kazi ya viongozi wetu wa dini, kumfanya mtu awe na utashi wa kutotenda dhambi. Kwa hiyo, siyo lazima umfanye mtu awe na utashi. Labda [kinachotakiwa] ni kujenga [au] kuimarisha ile mifumo ambayo italazimisha sasa ama atoe taarifa, awashirikishe wananchi, awajibike kwa wananchi.

Ni kwa kuwalazimisha kimfumo, au kuwahamasisha, kuwapa ule utashi yaani leo na kesho awe amebadilika hilo siyo lengo letu. Siyo lengo letu kumfanya mtu awe na utashi huo. Lakini mifumo inaweza ikatengenezwa ambayo inamsukuma, inamlazimisha, afanye kazi vile au Serikali itembee ifanye kazi zake kwa uwazi na kwa ushiriki na uwajibikaji.

Nadhani sehemu moja ni kuonesha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya utendaji kazi wa aina hii na kuboresha maisha ya wananchi husika. Kuonesha kwamba wananchi wakiruhusiwa, wakipewa nafasi ya kuhoji, au kuweka vipaumbele vyao vinavyowasumbua, yanaweza yakafanyiwa kazi na maisha yao yakawa bora zaidi.

Nikupe mfano. Tunafanya kazi kama hii wilaya ya Pangani kule na kuna kijiji kimoja ambapo walikuwa wao wana tatizo la maji. Ilikuwa wazi kwamba visima vilikuwa vichafu havijafunikwa wala nini. Kwa hiyo, hali ya usalama wa yale maji ilikuwa ni mbaya.

Tukakaa, tukawahamasisha wananchi wakapewa wahamasishaji wa jamii pale wakawa wanasema unajua sisi pale ni kweli tuna hili tatizo la maji ndiyo, kuna visima vyetu siyo salama. Lakini ngoja nikwambieni kitu, kuna tatizo moja sugu zaidi. Kuna danguro hapa. Kuna mama anafanya kazi hii ambayo ni haramu, haifai, hilo jambo kwanza ndiyo kipaumbele chetu.

Wakaenda sasa kuna mtu nadhani kulikuwa kuna polisi pale ambaye yeye alikuwa anajaribu hilo tatizo lakini jamii ushirikiano wa wazi na yule mwenye danguro ndio alikuwa mwenye nguvu. Sasa lakini jamii ilipoambiwa hivyo kwa uwazi yule polisi akasema sasa nimepata nguvu na ushirikiano wa wazi wa wananchi nitalishughulikia hili jambo na amelishughulikia danguro limefungwa.

Baada ya hapo sasa tukasema sasa turudi kwenye suala la maji. Sasa unaona utofauti kwamba tayari wananchi walikuwa na kipaumbele chao lakini walikuwa hawana sehemu ya kulisemea likafanyiwa kazi na walikuwa hawajiamini kwamba hili jambo litafanyiwa kazi.

Waliposimama, wakaongea, wakasikilizwa likafanyiwa kazi na huyo na wenzake huyo polisi wakasema sasa kumbe tuna nguvu hii ya kujiamulia na kuwashirikisha dola tukalitatua hili tatizo tutaendelea mambo mengine. Kwa hiyo, nikuonesha kwamba upo uwezekano kabisa katika ushiriki huu, ushirikishwaji huu wa wananchi na asasi za kiraia na Serikali tukatatua matatizo, tukaenda mbele.

Nadhani hio ndio itaweza kuonesha watu kwamba huu mfumo huu uwe si shirikishi tu lakini uwe wa kweli uwe na uzito fulani, upewe uzito fulani na upande mmoja ni muhimu sana ikupe uzito ni Serikali kwamba sawa tupo tayari kuwasikilizeni nyinyi, kuwashirikisheni nyinyi wananchi na kuwajibika kwenu nyinyi ili twende kule wote twende pamoja.

Utashi huo wa Serikali, au kuweka mifumo ambayo itailazimisha Serikali kufanya mambo kama hayo, itaihamasisha. Unajua Serikali hazipendi kulazimishwa? Itaihamasisha Serikali kusema sisi tunalenga hili na tumelifanyia kazi na tumepata matokeo haya hapa, ndiyo mpango mzima wa uhamasishaji wa Open Government Partnership.

Serikali zote siyo tu Tanzania, Serikali zote duniani [zinasema] tupo hapa kwa ajili ya wananchi. Sasa fanyeni kwa vitendo. [Wanasema] sisi ni Serikali sikivu, basi fanyeni. Huu mfumo wa Open Government Partnership ndio unahakikisha kwamba yale ambayo mnayasema, yale malengo ambayo mmeyaweka hadharani, zile ahadi mnazotoa, zitekelezwe na kama kuna vikwazo tunatatua wote wawili, watatu tuendelee mbele. Lakini msiseme moja mkafanya lingine. Huo ni uongo.

The Chanzo: Unajua umegusia suala la watu kama nyinyi au watu kama sisi kama waandishi, asasi za kiraia na nini kwenye kuhamasisha, maana umesema Serikali haipendi kulazimishwa, kwenye kuihamasisha Serikali kufanya mambo kwa uwazi, moja kati ya mbinu ambayo tunaweza tukaifanya ni kuonesha uhusiano uliopo kati ya uwazi na maendeleo. Na mimi naamini kwamba inaweza ikawa ni ngumu kwa wananchi kuuona huo uhusiano lakini kwa watendaji? Ni lazima huo uhusiano wanauona siyo? Yaani si kitu ambacho wanapaswa kuambiwa jamani kufanya mambo kwa uwazi kunaleta maendeleo?

Aidan Eyakuze: Ni kweli unachokisema kwa watendaji hilo ni tatizo, ni changamoto na nisikupe mfano wa hapa Tanzania. Kuna mfano wa Uingereza ambao ndiyo waanzilishi wa Open Government Partnership. Uingereza mwaka 2010 [au] 2011 walisema sisi ndani ya Serikali tulipata wakati mgumu sana kuhamasisha wenzetu kwa sababu walisema yaani nyinyi mnataka kuanika madudu yetu yote hadharani ili wananchi kule wapoteze imani yao na sisi?

Wakasema jamani tujaribu basi angalau kitu kidogo. Tuoneshe kwamba tumefanikisha mipango hii, nadhani walikuwa wanazungumzia mipango ya afya, tumefanikisha mipango hii wanapata huduma za afya zaidi lakini tumefanya makosa haya pia na hayo makosa tusiyafiche chini ya kapeti tuyaweke ili takwimu wazione.

Kilichotokea ni kwamba baada ya muda wenzake wanasema kumbe ulikuwa sahihi wanasema kwa nini, tumeambiwa na wananchi wetu kwamba kwa sababu tupo tayari kuonesha madudu yenu, makosa yenu, sisi imani yetu kwenu nyinyi imeongezeka kwa sababu tumeona mko tayari kuwa wazi na makosa na sehemu ambazo mmepata changamoto mmeweka wazi, tuko tayari kuwa na imani kubwa zaidi kwa yale ambayo mnatwambia, mmefanya vizuri. Kwa hiyo, unaona hilo yaani ni kitu cha kushangaza.

Kwa hiyo, uwazi kwamba mema pamoja na mapungufu yanamuongezea yule ambaye yupo wazi Serikali tendaji imani kwa wananchi. Unajua sisi ni binadamu, tunajua kwamba tuna mapungufu. Kwa nini mtu akikuambia kila siku kwamba yeye ni mtakatifu na hakosei na kila kitu anachokifanya ni kizuri nitakuwa kidogo nina mashaka ya uwazi huo.

Unaweza ukaongeza imani ya wananchi kwa Serikali na nimalizie kwa kusema kwamba changamoto kubwa sana ya Serikali zote – si ya Marekani ya Uingereza na hata hapa Tanzania – ni wananchi kukosa imani na Serikali zao, kukata tamaa kwamba Serikali ipo hapa kwa ajili ya manufaa yangu mimi na familia yangu na maisha yangu. Sehemu nyingi sana, nchi za Uarabuni, nchi hizi ambazo zimeendelea na nchi zetu za Afrika hiyo imani ya wananchi kwa Serikali yao inafifia kwa kasi kubwa sana.

The Chanzo: Mimi nakuaamini kwa sababu mimi binafsi nilitafutwa na kaka yangu Sammy Awami, akasema bwana unajua kuna hii sheria ya haki ya kupata taarifa kutoka serikalini, kuna hili jambo nataka tuijaribu hii sheria, twende tukaombe hizi taarifa kutoka serikalini kwa wahusika na sikumpa ushirikiano yeye Sammy kwa sababu siamini kwamba watakuwa tayari kutupatia zile taarifa. Kwa hiyo, nimekuamini kabisa. Lakini mimi nimekuwa najiuliza, na hapo umenifafanulia vizuri, nilikuwa najiuliza kama imethibitika kisayansi na kiuzoefu kwamba uwazi serikalini unaathari ya moja kwa moja na maendeleo ya wananchi au kwenye jamii …

Aidan Eyakuze: Ni uwazi, ushiriki na uwajibikaji. Hivi vitu vitatu viende pamoja.

The Chanzo: Kabisa, kama kuna huo ushahidi, kwa hiyo, nikawa najiuliza kwa nini sasa viongozi wetu wanakuwa wagumu kukubali kufanya haya mambo kwa uwazi, kwa nini wanapenda kufanya mambo kwenye giza au gizani? Wewe umeelezea sababu moja kwamba kwa uzoefu wa Uingereza kwamba watendaji wanahofia madudu yao kuonekana. Labda unadhani kunaweza kuwa na sababu nyingine ukiachana na hiyo ambayo inapelekea hii hali?

Aidan Eyakuze: Sababu nyingine kubwa sana ni rushwa. Ni rushwa. Vile vikundi ambavyo vinaiteka Serikali au sehemu za Serikali kujinufaisha vyenyewe kama vikundi fulani na hili suala la rushwa na ubadhirifu wa mali za umma ni kila sehemu zinatokea sio Ukraine, sio Marekani, [ni] kila sehemu.

Sasa hivi vikundi vina nguvu za kuweza kushawishi, au wakati mwingine kulazimisha watendaji serikalini, wafanye vitu gizani, watoe tenda gizani, wafanye malipo ambayo yapo nje ya mifumo. Vitu kama hivyo.

Sasa hapo ndiyo tunahitaji kusema lazima tumulike sasa tochi kwenye maeneo kama hayo. Ukraine, tuzungumzie Ukraine kidogo. Ukraine wanarais wao mmoja ambaye maarufu sana alikuwa anaitwa Viktor Yanukovych. Wananchi walikuwa hawamuamini mpaka wakasema sasa basi wakaenda wakaandamana akakimbia.

Sasa sisemi kwamba ubadhirifu Ukraine umeisha kabisa lakini moja wapo ya sababu ya wananchi kuandamana huyu rais alikuwa amejilimbikizia mali nyingi sana. Sasa wamemwondoa wakasema tukae kama asasi za kiraia na hawa vijana ambao ni watundu kwenye masuala ya teknolojia ya mawasiliano na programu mabalimbali.

Wakasema kwa nini tusitengeneze mfumo wa manunuzi wa Serikali ambao upo wazi ili kila mtu aone kila kitu? Kwa hiyo, wakatengeneza mfumo huo. Huo mfumo umewasaidia mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza kwenye manunuzi wameokoa zaidi ya dola bilioni moja. Kwa nini? Kwa sababu watu na makampuni mengi zaidi wakatafuta kwa nini mfumo huo ni wazi na una haki wakaweka tenda pale.

Wengi zaidi wakaweka biashara ndogo ndogo zikawa zinapata tenda za Serikali, bei zikashuka za bidhaa na huduma ambazo Serikali ilikuwa inanunua. Kwa nini? Kwa sababu ya mfumo huo. Umesaidia sana, umeokoa hela nyingi sana kwenye taifa kama Ukraine.

Hiyo ni nchi moja, Afrika Kusini wanamfumo unaoonesha hela zetu zinatumikaje na hiyo inasaidia. Kwa hiyo, kuna nchi ambazo zinatumia mfumo wa manunuzi kwa uwazi, open contracting, kwa uwazi ndiyo mfumo ambao umesaidia tumejifunza Open Government Partnership.

Kwa nini tusiulete huo mfumo hapa Tanzania kwa mfano ili tupunguze mianya ya watafunaji wa fedha na mali za umma? Kwa hiyo, kuna uhusiano huo ni uwazi, ushiriki na uwajibikaji.

Mimi nina wasiwasi ninaposikia kwamba tufanye haraka katika masuala ya zabuni ili mambo yaende haraka. Kwenye huo uharaka unaweza ukajikuta unajikwaa kwa sababu watundu wataingia hapo watafanya ya kwao kuharakisha mambo.

Kwa hiyo, mathalani mnataka mfanye haraka basi wekeni kila kitu wazi, hadharani hakuna kuchapisha tumia tovuti basi kila mtu aweke zabuni yake pale mimi na wewe kama mwandishi wa habari naweza nikasema hii zabuni ya bidhaa fulani au ya jengo fulani ni watu hawa wamefanya zabuni zao, bei zao ni hizi, aliyeshinda ni huyu, atafanya kwa kipindi hiki ili tuweze kufuatilia mambo kwa uwazi.

Uganda wamefanya hivyo, Uganda hawapo kwenye Open Government Partnership lakini wanao huo mfumo ambao unaweka mambo yake hadharani na watu wanajua, ni mambo kama hayo.

Kwa hiyo, kwa kujibu swali lako la msingi kuna Serikali, au dola, kwa kiwango kidogo ambazo zinatekwa, zinazungukwa na hao wabadhirifu wamo ndani na nje ya Serikali ambao wanataka kujilimbikizia mali na utajiri.

Afrika Kusini wameliona hilo hata wakati Open Government Partnership walikuwa wanachama wa Open Government Partnership nisiseme kwamba Open Government Partnership ni aina fulani ya chanjo dhidi ya ubadhirifu, hapana. Lakini inaweza ikaonesha njia zaidi ya kujikinga kwa kiwango kikubwa na mambo kama hayo kabisa.

The Chanzo: Sijui kama Zanzibar wana mfumo huo ambao umeuzungumzia huko Uganda kwa mfano au Afrika Kusini au Ukraine. Lakini naona kuna namna ambayo mimi kama mwananchi naweza nikaona watu ambao Serikali imeingia nao mikataba, hususani kwenye hizi pesa za UVIKO-19. Kwamba nakwenda pale kwenye ile tovuti naona kumbe Serikali imetumia hizi pesa kujenga shule hii na aliyepewa hii zabuni ni huyu hapa na si maelezo ni mkataba kabisa upo umechanganuliwa, umewekwa pale unaona mtu huyu aliyesaini kwa upande wa Serikali ni huyu aliyesaini kwa upande wa kampuni hi huyu. Nadhani hicho ni kitu kizuri.

Aidan Eyakuze: Kitu kizuri sana. Sasa wajibu wa Serikali ameshautimiza yeye, amekuwa muwazi. Sisi kama wananchi inabidi, kama wewe ni mchambuzi uende ukachambue pale ufuatilie uende kwenye ile shule upige pige picha pale unasema kweli walichokisema kinatekelezwa kwa kiwango hiki kwa ubora huu unawahoji wananchi unaonaje hicho kitu hapo Serikali inafurahi kwamba wamekuwa wazi halafu wanapata ushirikiano mzuri wa wananchi.

Lakini wakiweka na hilo ni kosa au niseme ni fundisho tulilolipata kama Open Government Partnership kimataifa tangu mwanzoni ile awamu ya kwanza miaka ya kwanza ya pili ya tatu Serikali nyingi zilipokuwa zinajiunga ziliweka taarifa nyingi sana zikawa wazi kwenye tovuti taarifa za wazi ndio ilikuwa Serikali ya uwazi lakini haitoshi kwa sababu kuweka taarifa wazi ni kama kumnywesha mtu maji lakini kwa lile bomba kubwa lile sasa watu hatuna huo uwezo wa kuzichakata na kuzielewa kuzitumia kuiwajibisha Serikali.

Sasa kidogo tumejifunza, tumefanya mambo sio lazima iwe Serikali ya uwazi lakini kuna manunuzi ya wazi, mikataba ya wazi ili watu wapate kujua maana ya hizi tunazoambiwa ni nini katika maisha yangu moja kwa moja.

Kwa hiyo, huo mfano wa Zanzibar nadhani ni mzuri sana na je, Zanzibar inaweza ikaiambukiza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ili kila wilaya, kila halmashauri wawe wanafanya vitu kama hivyo? Mimi nadhani inawezekana. Ni utashi. Ni kama mifumo haimlazimishi basi hatafanya, atasema ni kazi za ziada nisijisumbue na haya mambo.

The Chanzo: Hudhani kwamba kukabiliana na tatizo kama la kwangu mimi la kutokumpa ushirikiano mwezangu ambaye alikuwa anataka kutafuta taarifa fulani kutoka serikalini, kuifanyia majaribio ile sheria iliyowekwa, hudhani kwamba kukabiliana na tatizo kama hili kuna uhusiano pia na namna viongozi wetu wanavyopatikana au namna tulivyounda mfumo wetu wa kiutawala?

Nitakupa mfano. Tanzania tuna Mwenyekiti wa Kijiji ambaye anachaguliwa na wananchi lakini tuna Mtendaji ambaye hachaguliwi na wananchi na yeye ndio mwenye nguvu. Juzi tu hapa sisi The Chanzo tumechapisha habari Wenyeviti wa Serikali za vijiji huko Mtwara na Lindi wanalalamika kwamba Watendaji wanakwamisha kazi za Wenyeviti na hiyo ni ngazi ya kijiji. Kwenda kwenye Kata ndio hivyo hivyo, Diwani anatoka kwa wananchi lakini sijui ni nani anaitwa hatoki kwa wananchi.

Aidan Eyakuze: Kuna Mkurugenzi nadhani kwenye ngazi ya wilaya.

The Chanzo: Ndiyo. Kwenye ngazi ya wilaya ambapo pia kuna Mkuu wa Wilaya na una Meya ambaye anatoka kwa Madiwani, ambao wanatoka kwa mwananchi, lakini hana nguvu. Mimi binafsi nitakwambia kwa sababu na mimi ni mwananchi hii mimi inanifanya nakosa nguvu, yaani kwa sababu naona kama mtu ambaye mimi nimemchagua, nimeenda kumpigia kura sio ambaye anahatma ya mwisho ya kuamua kilichosahihi kwangu.

Mtu ambaye ameletwa na Rais, hata kama Rais nimemchagua mimi, lakini huyu mtu anayeletwa huku ngazi ya kijiji, ngazi ya kata, ngazi ya wilaya na hata ngazi ya mkoa ndio mwenye nguvu, anakuja kumwakilisha Rais pale na yeye ndio mwenye nguvu Diwani hana nguvu, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa hana nguvu.

Hii unadhani inaweza ikawa inachangia kwa kiasi gani kwa mfano wananchi kukosa hiyo hamasa ya kwenda kuomba hizo taarifa au kukosa hamasa ya kuiwajibisha Serikali yao kwa sababu wanaona mwisho wa siku siwezi kufanya kitu, yaani mimi si mtu ambaye nimemuweka mimi siwezi kumfanya kitu. Anaweza akafanya kitu ambacho kinaniumiza mimi lakini akabaki ofisini, anaweza akaja akafanya kitu ambacho kimemuudhi aliyemteua ndio akatoka hata kama – tumeona miaka sita iliyopita – kitu alichokifanya ni kwa maslahi ya wananchi lakini aliyemteua hakukipendelea anaondoka. Hiyo huoni inaweza ikawa inapelekea tatizo?

Aidan Eyakuze: Ndiyo, ni kweli. Kwamba huo mfumo kidogo nadhani unaleta huo mgongano. Ukiangalia suala la utawala likawa ni suala la mabishano na mafarakano na mgongano wa kila wakati.

Kwa hiyo, inategemea pia na sisi wenyewe kama wananchi sisi labda tatizo letu, changamoto yetu ni kwamba tunauona mfumo wa utawala kama ni mashindano fulani hivi kati ya huyu na yule aliyeteuliwa na aliyechaguliwa. Saa nyingine nadhani hapo ndiyo tunapokosea. Inabidi tuwe na ushirikiano kati ya waliochaguliwa na wananchi na walioteuliwa na mamlaka husika ambayo na yenyewe hatimaye ilichaguliwa na wananchi.

Kwa hiyo, inabidi sisi tubadilishe. Na nikupe mfano mwingine wa huko huko Pangani kijiji kingine. Kulikuwa na suala hilo hilo kwamba wananchi wanasema hawa walioletwa kama Serikali ya mtaa wameletwa sio wa kwetu sisi, sisi hatukuwachagua, kwa hiyo hatuwapi ushirikiano wowote ule. Kwa hiyo mambo yakakwama, maendeleo yakakwama, mitaro ikakwama, yaani maendeleo yakakwama kabisa.

Walipohamasishwa na wale waliochaguliwa, au walioletwa na Serikali, kwa kusema na sisi tunaomba radhi, ni kweli lakini tupo hapa tunaomba ushirikiano wenu, tunaomba radhi kama tumekuwa tumewadharau, tumewakwaza. Wakasema sawa kwa kuwa mmekiri hilo kosa tutashirikiana kwenye mambo kadhaa yanayotaka maendeleo.

Kwa hiyo, hili ni jambo la siasa na wananchi linahitaji ukomavu fulani kwamba tusiwapinge hawa kwa sababu hizi nyingine, tujaribu kushirikiana nao kwa uwezo wetu ili tujiletee sisi maendeleo na utakuta kwamba hata Mtendaji, hata Mkurugenzi hataki matatizo kila siku yamuandame, lazima hata yeye ananataka aishi maisha kidogo ya amani, aishi vizuri na watu wanaomzunguka, lakini akipewa hiyo fursa ya kushikiriana na wananchi na hiki kitu nimelikuta sehemu nyingi Mbogwe na nini, kama Twaweza.

Wakipewa hiyo fursa wakiona kwamba kweli wananchi wanajituma, kweli wananchi wana matatizo ya msingi na mimi nina uwezo wa kutatua hayo matatizo basi tushirikiane tufanye hicho kitu.

Tushirikiane lakini kwa upande wa wananchi inabidi na wao wawe na utayari wa kushirikiana na kwa upande wa uongozi na viongozi aidha, waliochaguliwa au walioteuliwa, na wao wawe na utayari wa kuwa wanyenyekevu fulani hivi na wasikivu kwa wananchi ili mambo yaende. Lakini ukileta ubabe hapo watu watagongana, watakwama.

The Chanzo: Asante sana kaka Aidan na labda pengine kwa kufupisha, unajua sitaki mwananchi ambaye anatuangalia akawa pengine anapoteza mwelekeo, kwa hiyo kwa kufupisha, labda bibi yangu kwa mfano kule kijijini akiwa anaangalia haya mahojiano na anaweza akawa anajiuliza kwa nini mimi mwananchi wa kawaida nijali kuhusiana na Serikali kufanya mambo yake kwa uwazi, yaani mimi ni kwa nini nijali?

Aidan Eyakuze: Kwa sababu nadhani ya msingi ni kwamba wewe kama mwananchi, hata kijijini kwako, nchi hii ni ya kwako. Hii Serikali inakutumikia wewe, wewe si mtumishi wa Serikali. Wewe ndiyo mwajiri wa hiyo Serikali.

Una haki za msingi zilizoandikwa kwenye Katiba na kwenye sheria nyingi ambazo Serikali inapaswa ikupe wewe, moja wapo ikiwa ni huduma bora za afya. Kama afya yako kidogo inaukakasi na matatizo una haki ya msingi ya kupata siyo huduma tu au bora huduma, unapaswa kupata huduma bora za afya.

Kwa hiyo, una kila nafasi, kila fursa ya kwenda kudai hayo. Na kuzungumza na kulalamika na pale ambapo unapata huduma bora ni kupongeza na kushukuru kwamba kweli nimepata huduma lakini ni haki yako ya msingi ya kibinadamu.

Kwa hiyo, ni bora kujali nadhani hiyo ndio changamoto kubwa ambayo sisi kama AZAKI, waandishi wa habari, ni kujaribu kuwahamasisha wananchi kwa kuwaambia nchi ni ya kwako, ni ya kwenu, sio Serikali. Nyinyi ni waajiri wa Serikali, Serikali ni waajiriwa wenu. Kwa nini mnalipa kodi? Ni kwa sababu si kodi hiyo inaenda kuwalipa mishahara inawapa marupurupu? Nchi ni ya kwenu.

The Chanzo: Tangu aingie madarakani hapo Machi 19, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kiasi kikubwa amekuwa akichukua hatua mbalimbali ambazo ukiziangalia zinalenga kutoa mwelekeo tofauti wa Tanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Na kusema ukweli kwenye matamko yake, na kwenye matamshi yake mbalimbali kwenye ziara za nchi na kwenye ukaguzi wake mbalimbali amekuwa akitoa matamko ambayo yanaashiria uelewa wake wa dhana hii ya uwazi na uwajibikaji, hususan kwenye suala zima la ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwenye hizi idara za Serikali.

Lakini bado Tanzania haijarudi kama mwanachama wa Open Government Partnership. Unadhani ni nini kinaweza kuwa kimekwamisha kurejea kwa Tanzania licha ya kuwepo kwa mwelekeo huu mpya ambao kusema ukweli lazima tukiri ni wa tofauti na mwelekeo ambao ulikuwepo miaka mitano, au sita, iliyopita?

Aidan Eyakuze: Huu mwelekeo ni kweli kama ulivyosema unatia moyo kwa vitendo na kwa matamko yake Mheshimiwa Rais ameonesha utayari wake kuwa muwazi kushirikisha wananchi na kuiwajibisha Serikali kwa wananchi.

Nadhani siyo tatizo la kukwama kwa sababu amekuwa madarakani mwaka mmoja na miezi kama minne [au] mitano. Niseme pia kwamba huo mwaka wa kwanza wa kwake wa kwanza hiyo miezi ya kwake ya kwanza nadhani hata sisi kama AZAKI, kama Twaweza, tulikuwa tunaangalia muelekeo upoje na kadri tunavyoona kwamba ndio unaelekea huko ambapo tunapapenda huko pazuri.

Basi tumechukua jukumu kama Mwenyekiti mwenza wa Open Government Partnership nimeweza kuwashawishi wenzangu wa Serikali ya Italia tuandike barua rasmi ya kuikaribisha Serikali ya Tanzania irudi, irejee kwenye mpango wa  Open Government Partnership. Sasa hiyo barua tumeipeleka mwezi wa nne tu mwaka huu.

Kwa hiyo, wanaifanyia kazi hiyo nimeambiwa leo [Julai 8] na ngazi za juu za Serikali kwamba wanaifanyia kazi kati ya wizara moja ya Mambo ya Nje na Ikulu yenyewe kwa sababu tulipojitoa Open Government Partnership ilikuwa imewekwa Ikulu na ndio ilikuwa taasisi ambayo ilikuwa inasukuma juhudi hizo.

Kwa hiyo, wanaangalia tena inakuwa kuwaje hapa tumefika wapi tunahitaji vigezo vipi tuvifikie ili tuweze kurejea kwenye Open Government Partnership, inafanyiwa kazi. Niseme hilo na sisi tupo tayari kuisaidia Serikali pale popote ambapo wanahitaji msaada wa kiufundi ili tuweze kurudi haraka iwezekanavyo.

Kwa nini nimehamasika na huo mwelekeo wa Mheshimiwa Rais, nimehamasika na utayari wa Open Government Partnership kwenye ngazi za juu kuialika Tanzania kurudi. Kwa hiyo sasa ni kuifanyia kazi.

The Chanzo: Aidan mimi nakushukuru sana, kusema ukweli nikiangalia hapa nina maswali mengi sana ya kuendelea kukuuliza lakini kwanza sitaki nikuchukulie muda wako mwingi lakini pia naona jua linaanza kukupiga hapo kwa hiyo nitakuuliza swali la mwisho ambalo nilianza kukudadisi kabla hata hatujaanza kurekodi.

Swali hili ni la kidunia, linatokea kwenye nchi za ulimwengu wa kwanza, ulimwengu wa pili na ulimwengu wa tatu na ni suala ambalo linahusiana na kutoweka au kupotea kwa zile haki ambazo zamani watu walikuwa wanajua kama ni haki zetu na haziwezi kwenda popote lakini unakuta tayari zimetoweka.

Ukiangalia kinachotokea Marekani, ukiangalia kinachotokea India lakini hata kwa hapa kwetu Afrika ukiangalia, kwa mfano, kinachotokea ukanda wa Afrika Magharibi, mapinduzi ya kijeshi, haya mambo tulikuwa tunaona tumeshayaacha nyuma miaka sitini, labda sabini lakini ni mambo ambayo yanaonekana kupata nguvu na kasi.

Kwa kiasi gani haya mambo yanakuhuzunisha na unadhani haya yanaweza yakawa na athari hasi gani kwenye harakati zenu kama Open Government Partnership kuweza kuhakikisha uwazi, ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji wa Serikali?

Aidan Eyakuze: Umegusia jambo ambalo ni la msingi sana sana. Kwamba kutoweka kwa hizi haki za msingi ambazo tumechukua muda mrefu sana kuzipigania ili zipatikane. Lakini unajua hata ukiangalia kihistoria kusema ukweli ni kipindi kifupi ambapo tumesema tumefika kweli.

Tangu mwaka 1989 mpaka hivi sasa miaka ya 2020, miaka thelathini sio kipindi kirefu. Baada ya hapo hata takwimu zetu za Open Government Partnership zinaonesha hata nchi wanachama wa Open Government Partnership na wao wameanza kurudi nyuma, hiyo Marekani iwe Canada iwe Uingereza na wao wanapitisha sheria ambazo zinabana haki zinawafungia watu.

Kwa mfano, haki ya kuandamana, hata Uingereza imezungumzia hebu ngoja tupunguze hizi haki, wanatumia visingizio vya UVIKO-19 imekuwa ni kisingizio, wanatumia kisingizio cha ugaidi. Kwa hiyo, wanatumia vitu hivyo, wanatutisha halafu wanaminya ule uhuru.

Kwa hiyo, unachokisema ni kweli kabisa inatupa sisi kama wananchi nje ya Open Government Partnership inatuonesha sisi kwamba hizi haki ambazo tunazichukulia poa leo hii zinaweza zikatoweka ndani ya sekunde moja.

Je, tuko na utayari gani wa kuzilinda na kuzipa nguvu zaidi kwa kuzisimika kwenye mifumo ya utawala wetu? Kwa hiyo, hata hapa Tanzania kwa mfano sheria nyingi zimepitishwa na awamu iliyopita ambazo inabidi zirudiwe upya ama zirekebishwe ili uhuru huu tuliouchukua uwekwe sawa.

Na katika ngazi ya kimataifa tuseme tunafanya mpango mkakati mpya wa Open Government Partnership kwa sababu tumeliona hili kama ni jambo la msingi tutawezaje kuhamasisha jamii ya mataifa na jamii ya Serikali za mitaa na jamii ya wananchi kusimama na kuzipigania hizi haki za msingi.

Kwa hiyo, hilo ndio swali moja kubwa ambalo linatusukuma. Kwangu mimi binafsi imenitia hamasa kubwa. Sasa hii wanaita ni kama ile tunasema huu ndio dhima ya maisha ya mtu ni kuhakikisha kwamba hili wimbi kubwa na la giza angalau tunalipunguza mwendo halafu tunalisimamisha halafu tunalirudisha.

Sasa hiyo ni kazi ya kizazi sio kimoja, ni la vizazi viwili, vitatu huko mbele ni mipango. Na hiyo ndio mpango tunauchukulia kama mipango hapa Tanzania tunafanya hizo kazi na juhudi za kimataifa kwa ajili ya Open Government Partnership na kwingineko ni kujaribu kusimamisha hilo wimbi la giza hilo ambalo linakuja kutunyang’anya haki zetu za msingi za binadamu.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Lukelo Francis. Stephen Gimbi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahiri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts