The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mange Kimambi, Naomba Tuzungumze Kidogo

Inasikitisha kuona umechagua watu wakukumbuke kwa mabaya badala ya wema.

subscribe to our newsletter!

Mpendwa Mange Kimambi, dada wa taifa – kama ambavyo mwenyewe hupenda kujiita – binafsi nilianza kukufuatilia kipindi cha awamu ya tano kutokana na ujasiri wako wa kuwasemea Watanzania wenzako kwa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa haki, hususan ule unaofanywa na Serikali.

Naikumbuka siku ya Alhamisi, Aprili 26, 2018, siku ambayo itaendelea kujulikana kama Siku ya Maandamano ya Mange Kimambi, jinsi ulivyoitikisa Serikali na vyombo vyake vya dola kwa kuwahamasisha wananchi waingie barabarani kupinga dhuluma mbalimbali wanazofanyiwa na Serikali yao.

Wengine wanaweza kusema maandamano yale yalifeli, hitimisho ambalo mimi nisingependa kufikia. Mimi naamini yalifanikiwa. Yalifanikiwa kwa kuifanya Serikali ionyeshe rangi zake halisi kwa Watanzania na dunia kwa ujumla. Nikiri kwamba siyo jambo dogo kwa mtu mmoja kufanikisha kitu kama hicho.

Ni bahati mbaya kwamba hata wewe binafsi ni mmoja kati ya watu wanaoamini kwamba maandamano yale yalifeli, imani iliyokupelekea kuamua kuachana na uanaharakati wa kisiasa kabisa kabisa. Mbadala wake, hata hivyo, nauona ni wa hatari zaidi, siyo kwako tu binafsi bali kwa suala zima la ustaarabu wa kibinadamu.

Huu mradi ulioibuka nao wa kutumia app ya simu ya mkononi – Mange Kimambi App – kuchapisha picha za ngono ni mradi unaokwenda kinyume na misingi yote ya ustaarabu iwe ni ya kiutu, kidini au kiutamaduni. Nitajaribu kukishirikisha baadhi ya sababu zinazonipelekea mimi binafsi niamini hivyo.

Waathirika ni wanawake

Jambo moja lililowazi ni kuwa zinapochapishwa picha za utupu mitandaoni, aghlabu ni wanawake ndiyo wanaodhalilika, wanaokashifika, wanaoaibika na wanaotukanika. Video za wanaume zinapovuja, kijamii, huonekana ni sifa, badala ya aibu, kwa kuwa zinaonesha ukidume wao. Inasikitisha lakini hivyo ndivyo jamii yetu inavyofikiri.

Huu ndiyo msingi wa kwa nini, kwa mfano, Mange Kimambi App, mtandao unaotumia kuchapisha picha za ngono za watu mashuhuri, wahusika wote ni wanawake. Walaji wa maudhui haya, kwa upande mwengine, ni wanaume. Sina takwimu rasmi lakini hisia zangu zinanituma kuhitimisha kwamba hakuna mwanamke anayependa kuona mwanamke mwingine picha zake za utupu zikichapishwa mitandaoni – isipokuwa wewe labda.

Zipo fikra kwamba kuvuja kwa hizo picha za uchi za wanawake ni makosa yao. Fikra hizo siyo sahihi. Wengi kati ya wanawake hawa hawakutaka kurekodiwa, na hata kama walirekodiwa kwa ridhaa na kujirekodi wenyewe, haikuwa kwa ajili kuonesha hadharani.

Ninacholenga kukueleza hapa dada yangu ni kwamba hawa wanawake unaovujisha picha zao za utupu ni wahanga. Na lawama hapa zisielekezwe kwa wanawake ambao picha zao za uchi zimevuja bali kwa wavujishaji. 

Ni kwa namna gani wewe binafsi unaweza kushiriki kwenye kusambaza picha hizi za uchi za wanawake wenzako, zilizochukuliwa kinyume na ridhaa ya wahusika, tena kwa malengo ya kupata fedha, ni swali ambalo limekuwa likinisumbua sana bila kupata majibu. Labda utanisaidia!

Hatari zilizopo

Ni jambo la kusikitisha sana kwamba wewe Mange unaweza kununua picha hizo za uchi zilizochukuliwa bila ya ridhaa ya wahusika na kuziweka kwenye app yako na kuziuza kwa walaji. Naona hatari mbili kubwa sana ambazo zitasababishwa na huu mradi uliokuja nao.

Hatari ya kwanza ni kwamba wanaume wataanza – au huenda washaanza– kurekodi wanawake kwa ajili ya tamaa ya kujipatia pesa kutoka kwako. Pili, wanaume wanaweza kutumia nafasi hii kuwakomoa wanawake pale wanapoachana, jambo ambalo siyo sawa. Je, uko tayari kuwajibika kwa kusababisha hatari hizo?

Mange dada yangu ni muhimu ukakumbuka kwamba wewe ni mama. Umeshafikiria ni taswira gani unajijengea kwa watoto wako? Hatari ninayoiona ni kwamba mradi wako wa picha za ngono unawatengenezea watoto wako maadui wasiokuwa wao na kuwafanya waishi maisha ya wasiwasi.

Ni muhimu ukakumbuka pia kwamba wanawake unaochangia kwenye kuwaumiza ni ndugu wa watu. Wana mama na baba. Wana kaka na dada. Wana wapenzi na marafiki. Umejaribu kujiweka kwenye viatu vyao na kufikiria maumivu unayowasababishia?

Mchango chanya

Ni ushauri wangu kwamba bado hujachelewa kuelekeza ushawishi wako kwenye kuchagiza mabadiliko chanya kwenye jamii zetu. Siyo lazima urudi kwenye harakati za kisiasa. Jamii yetu ya Kitanzania ina changamoto lukuki zinazonyima watu wake fursa za kuishi maisha yaliyo bora. Unaweza kuchagua iliyo karibu na moyo wako.

Mange, ni muhimu ukafahamu kwamba mtu hukumbukwa kwa mema yake aliyoyafanya akiwa hai. Nisingependa kuwasemea, ila sidhani kama watoto wako wangependa sana kujivunia rekodi yako kama muuza picha za ngono zilizochukuliwa bila ya ridhaa ya wahusika. 

Nina wasiwasi sana kuwa usipozingatia haya ipo siku utaingia kwenye majuto makubwa pale utakapomuabisha mtu dhaifu kihisia, akajidhuru mwenyewe kwa kushindwa kubeba aibu! Majuto ya kusababisha kifo cha mtu dada yangu siyo mzigo mdogo kuubeba moyoni.

Nimalizie makala haya kwa kutoa wito kwa wateja wako: acheni kuchukulia picha hizi za utupu kama burudani. Hawa wadada maarufu wana wazazi, kaka, watoto, ndugu, jamaa, marafiki, na wana biashara zao. Wanastahiki heshima, staha, na haki ya kufurahia faragha zao. 

Leo unaweza kufurahia picha za uchi za mtu mashuhuri huyu au yule, kesho – nani anaweza kujua? – tunaweza kukuta dada zetu, wake zetu, shangazi zetu, binamu zetu au hata mama zetu katika nafasi hii ya kuaibishwa. Hakuna mtu anaweza kufurahia kadhia hiyo ikitokea kwa mtu wake wa karibu.

Sisi Waislamu, Mtume Muhammad aliwahi kutuasa kwa kusema: “Haamini mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake [kile] akipendeleacho nafsi yake.” Kama katika nafsi yako unapenda ndugu zako wa kike waheshimiwe, waenziwe utu wao, hali ni hiyo kwa binadamu wengine, hata kama huwajui!

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Nasaha nzuri saana kwa dadayetu. Mange pamoja.na yoote ayafanyayo bado ni dadayetu ktk imani na ni Mtanzania mwenzetu,hivyobasi;ANAHITAJI NASAHA NJEMA NA KWA AJILI YA ALLAH. HAKUNA MKAMILIFU! SISI SOTE NI WAKOSAJI. MBORA NA MKAMILIFU NI ALLAH(S.W) PEKEE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *