The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Shangwe la ‘Mlete Mzungu’ Lina Harufu ya Ubaguzi wa Rangi

Jaribu kuwaza iwapo tukio la aina hiyo lingefanywa na Wazungu katika nchi zao kwa mchezaji wa Kiafrika? Dunia ingepasuka.

subscribe to our newsletter!

Kibwagizo cha  Mlete Mzungu kilichoasisiwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally alipokuwa akimtambulisha mchezaji wao mpya mgeni, Dejan Georgijević hapo Agosti 8, 2022, siku ya tamasha la klabu hiyo lililofanyika uwanja wa Benjamin William Mkapa, kimepata umaarufu mkubwa siku za hivi karibuni.

Umaarufu wa kibwagizo hicho umechagizwa na utani wa jadi kati ya klabu hiyo na Dar Young Africans ambao walikitumia kumcheka na kumkejeli Ally, kwa waliochokiona kama ni kukosa umahiri katika ushereheshaji na kithembe katika matamshi yaliyompelekea kutamka mdhungu badala ya mzungu.

Kibwagizo hicho kikaenea zaidi katika jamii na kunoga zaidi baada ya uwezo wa mchezaji huyo kuonekana ni wa kawaida kuliko ilivyotarajiwa.

Utani pembeni, ndani ya kibwagizo hiki kuna ubaguzi wa rangi uliojificha, licha ya utetezi unaoweza kutolewa kuwa lengo halikuwa kumbagua Georgijević.

Ubaguzi uliojificha katika kibwagizo cha Mlete Mzungu katika sakata la Georgijević, raia wa Serbia, upo katika walau maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kule kutajwa na kutambulishwa kwa rangi yake badala ya jina lake halisi na sifa yake ya uchezaji.

Hili linamuhusu zaidi Ally, aliyefanya utambulisho. Katika hili, nitajenga hoja pia kwamba siyo tu tumembagua Georgijević lakini pia ni mwendelezo wa tabia ya Waafrika kujidharau na kutukuza uzungu ikiwa ni athari ya ukoloni.

Eneo la pili tunapoona ubaguzi dhidi ya Georgijević, ikiwa ni zao la kumtambulisha kwa rangi yake, ni hii hali ya kutathmini uwezo wa mchezaji huyo kwa vigezo vya rangi ya ngozi yake. Huu ni ubaguzi uliopo katika jamii nzima, bila kujua.

Ukitaka kuelewa kuwa kuna walakini katika namna Georgijević alivyotambulishwa, jaribu kuwaza iwapo tukio la aina hiyo lingefanywa na Wazungu katika nchi zao kwa mchezaji wa Kiafrika. Unadhani dunia ingejibuje?

Nadhani ingekuwa habari kubwa duniani na matamko ya kulaani tukio hilo yangetolewa kutoka kila kona – kwa wanaharakati, wanasiasa, viongozi wa michezo na kila mwenye sauti ya kusikika. Labda mhusika hata angelazimishwa kujiuzulu!

Kisa cha Demba Ba

Ukitaka kujua namna Waafrika tunavyokuwa wakali kwa kutajwa kwa rangi zetu, rejea tukio lililomuhusisha mchezaji wa klabu ya Basaksehir ya Uturuki, Demba Ba, aliyemvaa kamisaa wa mchezo wa timu hiyo dhidi ya timu ya PSG ya Ufaransa kwa kutumia lugha hiyo. Mchezo huo ulifanyika Disemba 8, 2020.

Katika tukio hilo, Demba Ba alimshutumu afisa huyo aliyekuwa akisimamia mchezo huo kwa kumtaja Kocha Msaidizi wa timu hiyo ya Uturuki, Pierre Webo, kwa maneno, “Yule mtu mweusi.” Mechi hiyo ilibidi iahirishwe katika dakika ya 14 kwa sababu ya mzozo huo.

Uchunguzi uliofuatia tukio hilo ulipelekea uamuzi wa kufungiwa kwa afisa huyo raia wa Romania Sebastian Coltescu hadi mwisho wa msimu na kuamriwa ahudhurie kozi maalum kabla Juni 2021. Refa msaidizi wa mchezo huo, Octavian Sovre, naye alipewa onyo katika uamuzi huo ulitangazwa Machi 8, 2021.

Kama ni haramu tukio kama hilo kufanywa Ulaya kwa mchezaji Mweusi, lawezaje kuwa sahihi likifanywa dhidi ya Mzungu huku kwetu Afrika?

Kibwagizo cha Mlete Mzungu ni dhahiri kilikuwa ni cha kibaguzi, kama vibwagizo vingine tunavyovitumia kubagua baadhi ya makabila kama vile Wamaasai au Waasia, tukijificha nyuma ya pazi la utani au kudai tunataka kuwatambulisha kutoka kundi la watu.

Hata yule afisa mwamuzi wa Kiromania kimsingi alikuwa akijaribu kumtambua Webo kutoka kundi la watu lakini utetezi wake ni wazi haukukubalika.

Siku ile ya tamasha la Simba, wachezaji wote walitambulishwa kwa majina na sifa zao za umahiri wa uchezaji kasoro Georgijević ambaye aliitwa kwa kibwagizo cha Mlete Mzungu jambo ambalo halikuwa sahihi.

Athari za ukoloni

Kwa upande mwingine, ukikichambua kibwagizo kile unaona athari ya ukoloni iliyotupelekea Waafrika kutukuza Uzungu na kujidharau sisi wenyewe. Kwetu sisi, Uzungu, ikimaanisha rangi nyeupe, ni ufanisi, umahiri, ubora, uimara, akili, ujanja, utaalamu, kipaji na ustaarabu.

Ndiyo maana kwa mtambulishaji ilitosha kusema Mlete Mzungu kutambulisha umahiri wa Georgijević na kuwatishia watani zake Yanga!

Nimeeleza hapo juu kuwa kutawaliwa muda mrefu kumetuondolea kujiamini hadi kufikia kudhani Uzungu ndiyo umahiri. Labda nikupe mifano zaidi ya kuonesha namna tulivyoathirika kwa fikra hizi.

Katika nyakati tofauti, niliwahi kuwasikia wachambuzi katika vipindi vya michezo wakikosoa na kuponda baadhi ya mambo eti kwa sababu Ulaya, ambako ndiyo rejeo lao la namna bora ya kufanya mamvo, hawafanyi.

SOMA ZAIDI: Kutweza Kiswahili ni Ishara ya Kujidharau, Kutojiamini

Miongoni mwa vitu walivyokosoa ni pamoja na uwepo wa wasemaji (wahamasishaji) katika vilabu vyetu vya michezo. Jingine walilokosoa ni haya matamasha ya vilabu kila mwanzo wa msimu.

Walikosoa siyo kwa sababu wanaona tatizo, au hasara, za uwepo wa hayo mambo mawili bali kwa sababu tu Wazungu hawafanyi! Hivi sisi tutaendelea kupokea tu ubunifu wa wengine? Lini wenzetu watatuiga kama hatuthamini ubunifu wetu?

Ukiniuliza, ntakwambia kwamba mambo haya mawili – wasemaji wa vilabu na matamasha yanayoongezeka kila mwaka – yameleta faida kubwa katika kutangaza na kuhamasisha michezo yetu, husan soka. Huhitaji utafiti wa kisayansi kulijua hili.

Hii hali ya kuukubali unyonge watafiti wa mambo ya ubaguzi wa rangi walishaiona na kuipa jina la ‘internalised racism,’ ikimaanisha hali ambapo kundi la watu wa rangi, au kabila, fulani linalobaguliwa kuikubali imani, au mitazamo, ya kibaguzi dhidi yao.

Kwa maana nyingine kuukubali unyonge wao. Hii unaweza kuiona katika imani kuwa Mzungu, kwa Uzungu wake tu, ana faida ya kuwa mahiri zaidi. Hii internalised racism ni matoleo ya ukoloni.

Matarajio makubwa kwa Georgijević

Athari za kibwagizo cha Mlete Mzungu sasa ndiyo zinaonekana. Kwa kuwa kwetu Mzungu si kiumbe wa kawaida, jamii imemtolea macho Georgijević aoneshe kuwa yeye kweli ni Mzungu! Matarajio kama haya ndiyo huzaa maneno mengine ya kibaguzi zaidi kama ‘Mzungu pori’ nakadhalika.

Matarajio ni makubwa mno kwake kwa sababu anaangaliwa na kutathminiwa kwa vigezo vya Uzungu wake hadi namuonea huruma. Hii si haki hata kidogo. Kushindwa kwetu sisi Watanzania ni ishara ya walakini katika Uzungu wake!

Georgijević amekuwa mhanga wa kejeli za kila aina kutoka kwa mashabiki wa timu yake wasiomtaka na kutoka kwa timu pinzani, hususan watani wao wa jadi Yanga. Ukosoaji wote kwake unaambatanishwa na rangi yake!

Mshabiki mmoja wa Simba, baada ya kufungwa na watani wao Yanga, akasema: “Yule siyo Mzungu ni mzungukaji.” Nao mashabiki wa Yanga wakachukua mdoli wa dukani na kuubeba huku wakiimba Mlete Mzungu. Binafsi, ningekuwa Georgijević, nisingeweza kuishi Tanzania katika mazingira haya.

Wanazuoni waliotafiti ubaguzi wa rangi hii wanaita ‘racial microaggression,’ ambayo ni aina nyingine ya ubaguzi ikijumuisha maneno, au vitendo, vinavyolenga mtu, au kundi la wachache, aghlabu kwa dhihaka na aghlabu bila wafanyaji kujua.

Wameita micro kwa sababu hutokea katika mazungumzo madomadogo ya watu lakini athari yake ni kubwa kwa wapokeaji. Kauli kama ya yule ni mzungukaji siyo Mzungu inaingia humo kwa sababu inahusianisha umahiri wa kucheza mpira na rangi.

Bahati mbaya sana, hata vyombo vyetu vya habari vimeingia katika mtego huu wa ubaguzi. Baadhi ya radio maarufu zimechukua kibwagizo cha Mlete Mzungu kufanyia dhihaka.

Watanzania wenzangu, tuwe makini katika kauli zetu. Kubaguliwa kunauma mno, kuwe kwa waziwazi, kwa chinichini, au hata kwa utu wako kufanyiwa dhihaka na kituko.

Wanaharakati mpo wapi? Semeeni hili.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *