Nimesikia azma ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria kikao cha kazi cha tatu cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi kitakachofanyika kati ya Agosti 30 na Septemba 1, 2022, katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS) kilichopo Moshi, Kilimanjaro.
Ninashawishika kama raia kugusia machache juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi kwa azma ya kushawishi mabadiliko ya kiutendaji ya kweli, mabadiliko ambayo yatatizama kwa umakini na kwa dhati ndani ya Jeshi la Polisi badala ya kusaka na kutisha wananchi wasio na hatia.
Eneo la kwanza linalohitaji mageuzi ndani ya Jeshi la Polisi ni kwa jeshi hilo kuanza kukiri kwamba lina tatizo. Udhaifu wa kiutendaji katika Jeshi la Polisi si suala ngeni. Nadiriki kusema kuwa hakuna mwananchi aliyepita kwenye kituo cha polisi asichefuliwe kama si na aliyetendewa basi na aliyeyashuhudia.
Wakati Jeshi la Polisi limeapa kulinda raia na mali zao na kutii sheria za nchi, mara nyingi sheria zinawekwa pembeni na ubabe unatumika hata pale pasipo na haja ya kutumia nguvu. Imekuwa kawaida kuwasweka watu ndani kwa makosa ambayo si ya kuwekwa mtu kizuizini.
Imekuwa kawaida kutoruhusu watu kujidhamini wakati sheria inaruhusu watu kujidhamini hasa pale pasipo na tishio la wao kutoroka au kudhuru wengine. Tatizo ni kuwa askari wa Jeshi la Polisi wanaamua wao sheria inataka nini na inamhusu nani.
Ole wake mwananchi atakayeonesha kujua haki zake au kutaka ufafanuzi wa vifungu vinavyotumika kumuandalia mashtaka. Huu unatizamwa kama usaliti wa juu na mwananchi huyo atakomeshwa tu kama kilivyothibitisha kisa alichotoa ushuhuda mtoto wa Marehemu Kinguge Ngombare Mwiru aliposhambuliwa na polisi aliyemkosea heshima mke wake.
SOMA ZAIDI: Lini Polisi Iliahidi Hadharani Kutekeleza Ushauri Kutoka Chama cha Upinzani?
Nchi za wenzetu ndani ya Jeshi la Polisi kunakuwa na kitengo cha kupeleleza polisi waovu, wakorofi, sumu, waliooza na kuhatarisha kuharibu wenzao. Waovu hawa wakilalamikiwa wanachunguzwa ndani kabla mamlaka nyingine hazijashirikishwa.
Ni sawa na kuwa na wakaguzi wa mahesabu wa ndani wanaofuatilia mambo na kutahadharisha balaa kabla halijatokea. Hivyo, ni muda sasa Jeshi la Polisi liwe na kitengo, au idara, inayohusika na nidhamu, maadili na weledi wa watumishi wake na kitengo hiki kiwe huru kinapofanya kazi zake.
Watumishi wake ingawa wanatoka katika Jeshi la Polisi wateuliwe na kuajiriwa kwa masharti tofauti na wengine kutokana na unyeti wa kazi yao.
Kufanya kazi kwa uwazi
Kumekuwa na shutuma nyingi siku za hivi karibuni kuhusu uvunjaji wa sheria, tena wa wazi, unaofanywa na watendaji na askari katika Jeshi la Polisi. Miongoni mwa shutuma hizi ni pamoja na kupiga na kutesa watu, kuwasakazia kesi na kudai rushwa.
Njia moja Jeshi la Polisi linaweza kuondokana na tuhuma dhidi yake ni kujiweka wazi katika utendaji wake. Hili linawezekana kwa kuweka CCTV camera katika vituo vya polisi, hususan kwenye kaunta wanapofika raia kwa sababu mbalimbali.
Kadhalika gari za polisi zinazofanya mawindo ziwekwe dashboard camera ili ziwe zinanasa matukio moja kwa moja. Utamaduni huu umesaidia kugundua ubaguzi na uhujumu unaofanywa dhidi ya watu wenye asili ya Afrika pamoja na watu masikini nchini Marekani na Ulaya.
SOMA ZAIDI: Sintofahamu Mahakamani Polisi Wakizuia Watu Kuingia na Simu Kwenye Kesi ya Mbowe
Hakuna sababu ya msingi kwa nini hapa kwetu haiwezi kuanziswa hata kwa majaribio tukianza na vituo vyenye malalamiko mengi ya uvunjwajwi haki za raia.
Ni muhimu pia kwa Jeshi la Polisi kuacha kujifanya ndiyo Mahakama na kutoa maamuzi wasiyokuwa na upeo nayo. Shauri nyingi zinaharibiwa vituo vya polisi kwa sababu askari wanajigeuza kuwa Mahakama.
Badala ya kutimiza kazi yao ya kuandaa maelezo na ushahidi wa awali wao wanaamua kama kuna kesi au hakuna kesi, kuna kosa au hakuna kosa, ushahidi unafaa au haufai na mara nyingi hufanya uamuzi huu bila ya kuzingatia sheria inasema nini.
Binafsi nimetoa taarifa toka Februari 2022 kuhusu shambulio na vitisho dhidi yangu na mpaka leo ninazungushwa. Miongoni mwa maelezo kwa nini kesi yangu haijapelekwa mbele ni kuwa kaka yangu amekwenda kuondoa kesi na niliyemshtaki amekwenda kusema tumemalizana.
Nilipouliza sheria gani inaruhusu hilo nimebaki kuzungushwa kuwa sasa jalada inakosa mara hiki mara kile. Cha kushangaza mimi sijatakiwa kufanya la ziada na polisi na wala hawajataka kuhakiki upande wangu. Jalada limekaliwa kwa sababu kuna askari kaamua kumlinda mhalifu wangu.
Hivyo kesi yangu imesikilizwa na kuamuliwa kituo cha msingi cha polisi na wala si mara ya kwanza. Limekuwa jambo la kawaida, ukihoji unatishiwa kuwekwa ndani kwa kufanya fujo.
Polisi waache visingizo
Jeshi la Polisi linatoa visingizio vingi kwa kukosa kuwajibika kwa mujibu wa viapo vyao lakini ukweli utabaki ni huo, ni visingizio na vingi havina msingi. Kisingizo kikuu kinachonyima wengi haki zao ni cha ushahidi kutokamilika wakati hakuna jitihada za kweli, au za dhati, kutafuta na kuchukua ushahidi.
Labda nikuulize ndugu Inspekta kwa nini Jeshi la Polisi (na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka) wanakazia sana suala la DNA kama vile hakuna ushahidi wa alama za vidole au aina nyingine ya utambulisho hasa pale utambulisho wa mhusika hauna shaka?
SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?
Au katika enzi hizi za kidijitali ambapo mna vifaa vya kugeza mwendo kwa nini msiwe na kamera za kuchukua ushahidi wa matukio? Iweje wanakuja watu wamepigwa na wenzi wao msichuke picha za majeraha yao mnasubiri mpaka apone aende mahakamani halafu ajaribu kuonesha Mahakama kuwa mwezi uliopita alikuwa kavimba au kapasuka sehemu fulani?
Ushahidi upo wa aina nyingi lakini hata unapokuwepo polisi wanakuwa hawana haja nao. Hata ukiwapa wanaukataa. Mimi nitasimama popote kwa ushahidi kuonesha namna polisi inaendelea kupuuza ushahidi nilioutoa kwa makusudi ili kusiwe na ushahidi wa kumbana mlalamikiwa.
Jeshi la Polisi pia liache kupoteza muda wa wananchi na rasilimali za nchi. Wananchi wengi wanalalamika kuhangaishwa wakienda polisi. Nenda rudi zimekuwa nyingi. Unatakiwa uache taarifa zako nyingi, ikiwemo kitambulisho na simu lakini kamwe hivi havitumiki kukutafuta mpaka wewe uende kituoni.
Unaweza kutumia rasilimali zako kupeleka wapelelezi sehemu ya tukio kutoa photocopy ya nyaraka na isiwe lolote. Ingawa nimegusia kutoa taarifa polisi toka Februari 2022 nina mashauri mengine polisi ya zaidi ya miaka 20 na mpaka leo hakuna lililofanyika.
Nimepoteza muda mwingi kufuatilia kipindi kimoja mwaka na nusu lakini kila ngazi ninayofika nachezeshwa danadana na kuzungushwa bila hatua ya maana kuchukuliwa. Kubwa nabadilishiwa watendaji wa kunisikiliza lakini hakuna utatuzi. Nyaraka nilowasilisha nyingi zimepotezwa.
SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania
Kuhusu uwajibikaji, askari wamekuwa wanapokea mishahara ya bure. Wanapoteza rasilimali za nchi kwa kutokuwa na ufanisi kazini au katika matokeo yao ya kazi. Nimeshawahi kuwekwa polisi kutwa bila ya kupatiwa matibabu wakati nikivuja damu na mwisho wa siku askari walishirikiana na wahalifu kuharibu kesi.
Mwaka wa 10 huu sijaweza kutetea haki yangu kwa sababu Jeshi la Polisi wameshiriki kuhujumu haki na uwezekano wa kukomesha uovu uliotendwa. Badala ya kupunguza matukio ya uvunjaji sheria, mwenendo/hulka za Jeshi la Polisi zinasaidia kushamiri kwa uvunjaji sheria kwani mhalifu anajua nikijua kuongea au kiasi cha kutoa sina haja kujibu kwa uovu niliotenda.
Badala yake nitamkomesha anayethubutu kutetea haki yake. Athari ya kutamalaki kwa hali hii ni Tanzania kuwa na sifa ya kutoheshimu sheria na haki yaani kuwa nchi yenye impunity na siyo utawala wa sheria.
Pengo kati ya ahadi, utendaji
Kuna pengo kubwa sana kati ya ahadi za Jeshi la Polisi za kusimamia sheria na haki za watu na utendaji halisi. Mrundikano mkubwa wa mahabusu ni ushahidi wa hali hii lakini pia mashauri ya watu kama yangu ambayo yamekosa kushughulikiwa na Jeshi la Polisi kama inavyostahili ni ushahidi mwengine.
Unapokwenda polisi kutoa taarifa ya tukio la uhalifu utaambiwa mkamate umlete mhalifu kituoni. Polisi hao hao watasema usichukue sheria mikononi lakini wanategemea mhalifu atakubali kwa wepesi tu kupelekwa kituoni?
Usalama wangu mnauzingatia mnaponipa amri kama hiyo? Tuseme mhalifu kafika kituoni changamoto inayofuata ni kupata mpelelezi wa kuandika maelezo yako yanayokisi kilichotokea na kukusanya upelelezi wa kutosha ambao ni zaidi ya maelezo ambayo yanaweza yakatolewa mahakamani.
SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania
Ushauri wangu kwa Jeshi la Polisi ni kwamba waombe taasisi husika, ikiwemo Bunge, liwaondolee jukumu la kufanya uchunguzi kwa kupendekeza watu waweze kufanya uchunguzi na hatimaye mashtaka binafsi, yaani private prosecution hasa kwa kesi za kawaida ili nyinyi mshughulike jinai kubwa tu.
Hii itasaidia sana kukusanya ushahidi kwa wakati na pia kushughulikia matukio kwa wakati madhali moja ya sababu zenu za kuchelewa kushughulikia makosa ni kuwa hamna watendaji wa kutosha au hawana ujuzi wa kutosha.
Kama suala la lindo limeweza kubinafsishwa kwa nini hili lisibinafsishwe pia? Nina kesi mbili za watu, mmoja yupo Kilimanjrao na mwengine yupo Morogoro hawajaletwa Dar es Salaam kujibu mashitaka eti ninavyoambiwa kituoni hakuna mtu wa kuwasindikiza.
Miaka 10! Kila rai unayotoa haikubaliki kama siyo kula sahani moja na wahalifu niamini ni nini?
Kujiandikia maelezo
Jeshi la Polisi pia linaweza kuweka utaratibu wa wananchi wanaojua kusoma na kuandika waandae maelezo yao. Najua kuwa polisi hujitetea kuwa maelezo ni ya kitaalamu lakini hoja hii haina mashiko maana kesi nyingi zinatupwa nje ya Mahakama kutokana na maelezo mabaya yasiyo na mashiko kisheria yanayoandaliwa na polisi.
Ni sababu hii pia iliyopelekea mashtaka kuwa mikononi mwa Mwendesha Mashtaka au Wakili wa Serikali lakini kwa vile polisi kesha koroga mambo kurekebisha mwisho inakuwa kazi.
Zamani jamii kubwa ilikuwa haijui kuandika wala kusoma. Leo wananchi wengi wanajua kusoma na kuandika tena kuliko hao polisi wanaopewa jukumu la kuandika maelezo. Kubwa zaidi mara zote nimelazimishwa kuandikiwa maelezo nimegundua kwamba polisi hawako makini na kazi zao.
SOMA ZAIDI: Tito Magoti: Barua ya Wazi kwa Rais Samia Kuhusu Hali ya Haki Jinai Tanzania
Akili zao zipo kwengine mara anasikilza radio call mara anajibu lile. Wanaandika wanavyojua wao na kukuweka masaa kituoni uchoke hata wakimaliza wanahakikisha unaweka sahihi uondoke maana ushapoteza muda mwingi hapo. Bora maelezo yako uandike mwenyewe, ujinyonge mwenyewe.
Kwa leo haya yanatosha. Nia ni kujenga na kutengeneza. Ifike wakati mwananchi wa Tanzania aone usalama na amani akienda polisi, asikie faraja akishughulikiwa na polisi, awe na imani kuwa atatendewa haki.
Kwa vile vigezo havifikiwi si halali wala haki kudhulumu watu uhuru, stahili na haki zao kwa vile tu mnavaa magwanda ya polisi. Kufanya hivi ni kuwapoka watu haki zao za asili, za msingi na kisheria na ni kuwatia unyonge wa kutopata ulinzi na hifadhi katika taifa leo.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mwandishi wa makala haya amejitambulisha kama Mtanzania mpenda haki ambaye hakupenda jina lake lichapishwe kwa sababu binafsi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamao wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kwa maelezo yetu kupitia editor@thechanzo.com.